Netanyahu akabiliwa na wakati mgumu, Marekani ikihimiza mpango wa kusitisha mapigano Gaza

Antony Blinken anazuru Mashariki ya Kati kutafuta uungwaji mkono kwa mkataba mpya wa kusitisha mapigano Gaza na kuwaachilia mateka.

Chanzo cha picha, Reuters

Ikiwa wanadiplomasia wanahisi hakuna kilichobadilika licha ya juhudi zilizofanywa ndani ya saa 24, huenda Blinken alikuwa akihisi kuchoka wakati ndege yake ilipowasili Mashariki ya kati katika ziara yake ya hivi karibuni.

Ni ziara yake ya nane ya kidiplomasia katika eneo hilo katika muda wa miezi minane tangu mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana.

Siasa za kujaribu kufanya mazungumzo ya kusitisha vita huko Gaza na kubadilishana mateka wa Israel kwa wafungwa wa Kipalestina tayari zimekuwa ngumu.

Imekuwa hali ya kukanganya zaidi kuliko hapo awali ambapo kiongozi wa upinzani wa Israel Benny Gantz amejiuzulu kutoka kwa baraza la mawaziri la vita la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, pamoja na mshirika wake wa kisiasa Gadi Eisenkot. Wanaume hao wawili ni majenerali wastaafu walioongoza Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kama wakuu wa majeshi.

Kujiuzulu kwa Benny Gantz katika baraza la mawaziri la vita la Israel kunatoa changamoto nyingine kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Chanzo cha picha, Reuters

Bila Benny Gantz, Wamarekani wamepoteza mawasiliano yao katika baraza la mawaziri. Sasa amerejea upinzani, Bw Gantz anataka uchaguzi mpya, ndiye anayependwa zaidi na wapiga kura kuwa waziri mkuu ajaye, lakini Bw.Netanyahu yuko salama mradi tu anaweza kuulinda muungano unaompa kura 64 katika bunge la Israel lenye wabunge 120. .

Hiyo inategemea uungwaji mkono wa viongozi wa mirengo miwili yenye msimamo mkali. Hao ni Itamar Ben-Gvir, waziri wa usalama wa taifa, na Bezalel Smotrich, waziri wa fedha.

Hiyo ndiyo hatua ambayo ujumbe wa Waziri wa Mambo ya Nje, Blinken unagongana na siasa za Israel. Rais Joe Biden anaamini kuwa wakati umefika wa kumaliza vita huko Gaza.

Kazi ya Bw Blinken ni kujaribu kufanya hilo litokee. Lakini Ben-Gvir na Smotrich wametishia kuiangusha serikali ya Netanyahu ikiwa atakubali kusitishwa kwa mapigano yoyote hadi watakaporidhika kwamba Hamas imeondolewa.

Ni wazalendo wa Kiyahudi waliokithiri, ambao wanataka vita viendelee hadi kusiwe na athari ya Hamas.

Wanaamini kwamba Gaza, kama eneo lote kati ya Bahari ya Mediterania na Mto Yordani, ni nchi ya Kiyahudi ambayo inapaswa kukaliwa na Wayahudi. Wapalestina, wanahoji, wanaweza kuhimizwa kuondoka Gaza "kwa hiari".

Vita huko Gaza bado vinaendelea baada ya miezi minane

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Antony Blinken yuko Mashariki ya Kati kujaribu kusimamisha mpango wa hivi punde wa kusitisha mapigano usife. Maazimio matatu ya kusitisha mapigano katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yalipingwa na Marekani, lakini sasa Joe Biden yuko tayari kwa makubaliano.

Maazimio matatu ya kusitisha mapigano katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yalipingwa na Marekani, lakini sasa Joe Biden yuko tayari kwa makubaliano.

Tarehe 31 Mei, rais alitoa hotuba akiitaka Hamas kukubali kile alichosema ni pendekezo jipya la Israel la kumaliza vita huko Gaza.

Ulikuwa ni mpango wa sehemu tatu, ambao sasa umeungwa mkono na azimio la Umoja wa Mataifa, kuanzia na usitishaji vita wa wiki sita, "kuongezeka" kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza, na kubadilishana kwa mateka wa Israel kwa wafungwa wa Kipalestina.

Mpango huo utaendelea hadi kuachiliwa kwa mateka wote, "kusitishwa kwa uhasama" wa kudumu na hatimaye kazi kubwa ya kuijenga upya Gaza. Waisraeli hawapaswi tena kuogopa Hamas, alisema, kwa sababu haikuweza tena kurudia tukio la tarehe 7 Oktoba.

Rais Biden na washauri wake walijua kulikuwa na shida. Hamas inasisitiza kuwa itakubali tu kusitishwa kwa mapigano ambayo yatahakikisha kuwa Israel itaondoka Gaza na kumalizika kwa vita.

Uharibifu na vifo vya raia vilivyosababishwa na Israel katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat huko Gaza wakati wa uvamizi wa kuwaachilia mateka wanne wiki iliyopita vinaweza tu kuimarisha azimio hilo.

Mamlaka ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza inasema kuwa Wapalestina 274 waliuawa wakati wa uvamizi huo. IDF inasema idadi ilikuwa chini ya 100.

Bw Biden pia alitambua kuwa baadhi ya majeshi yenye nguvu nchini Israel yangepinga.

"Nimeutaka uongozi wa Israel kusimama kwenye mpango huu," alisema katika hotuba hiyo. "Bila kujali shinikizo lolote litakalokuja."

Benjamin Netanyahu sasa anategemea zaidi vikundi vya watu wenye msimamo mkali katika muungano wake unaoongoza

Chanzo cha picha, Reuters

Shinikizo lilikuja haraka, kutoka kwa Bw. Ben Gvir na Smotrich. Ni mawaziri wakuu wa serikali, wanaopinga vikali makubaliano ambayo Joe Biden aliwasilisha. Haikuleta tofauti kwao kwamba mpango huo uliidhinishwa na baraza la mawaziri la vita, kwani wao si wanachama.

Kama ilivyotarajiwa, walitishia kuuangusha muungano wa Netanyahu ikiwa atakubali makubaliano hayo.

Si Hamas wala Israel ambao wamejitokeza hadharani kuunga mkono makubaliano ambayo Rais Biden aliweka.

Hakuna dalili kwamba kiongozi wa Hamas huko Gaza, Yahya Sinwar, yuko katika hatua hiyo. Anaonekana kudhamiria kushikilia mkondo ambao ameufuata tangu 7 Oktoba.

Baadhi ya ripoti kutoka Gaza zilisema kuwa Wapalestina katika magofu ya kambi ya Nuseirat walikuwa wakiilaani Hamas pamoja na Israel kwa kutojali maisha yao.

BBC haiwezi kuthibitisha hilo, kama ilivyo kwa mashirika mengine ya habari ya kimataifa hairuhusiwi na Israel na Misri kuingia Gaza, isipokuwa kwa safari za nadra na zinazosimamiwa sana na jeshi la Israel.

Almog Meir Jan alikuwa mmoja wa mateka wanne wa Israel waliookolewa na wanajeshi wa Israel katika operesheni katikati mwa Gaza siku ya Jumamosi.

Chanzo cha picha, Reuters

Watazingatia ukweli kwamba mauaji ya Wapalestina zaidi ya 37,000, wengi wao wakiwa raia, kulingana na wizara ya afya huko Gaza, yameiletea Israel sifa mbaya.

Inakabiliwa na kesi ya madai ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa na ombi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya kutaka kukamatwa kwa Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant.

Kwa upande wa Israel, Waziri Mkuu Netanyahu amepoteza wajumbe wawili wa baraza la mawaziri la vita, Messrs Gantz na Eisenkot, ambao walitaka kusitishwa kwa vita ili kuruhusu mazungumzo kuwaachilia mateka.

Wizara ya afya ya Gaza imesema zaidi ya Wapalestina 270 waliuawa wakati wa operesheni ya kuwaokoa mateka wa Israel

Chanzo cha picha, Reuters

Pengine Antony Blinken atamsihi wafanye mpango huo na kuwaridhisha mamilioni ya Waisraeli wanaotaka mateka warudishwe kabla ya wengi wao kuuawa.

Bw Netanyahu basi anaweza kuwa hana jingine ila kuhatarisha serikali yake kwa kucheza karata kwenye uchaguzi.

Kushindwa kutaleta tume za uchunguzi ambazo zitachunguza kama anawajibika kwa kushindwa kisiasa, kijasusi na kijeshi kulikoruhusu Hamas kuingia Israel miezi minane iliyopita.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga