Kwa nini ushirikiano wa Marekani na Israel unakumbwa na mzozo mbaya zaidi katika miongo kadhaa

Chanzo cha picha, AFP
Rais Joe Biden alibadilisha mojawapo ya uhusiano muhimu wa kimkakati zaidi ulimwenguni.
Hatua hiyo ilijiri wiki hii katika mahojiano ya runinga, alipoulizwa nini kitatokea iwapo Israeli itavamia Rafah, Biden alijibu: "Sitaisambazia silaha."
Kuipatia Israel silaha ndio msingi wa uhusiano kati ya Marekani na Israeli, kwa hivyo kwa mara ya kwanza katika miongo minne mgogoro wa kidiplomasia ulionekana.
Biden amekuwa chini ya shinikizo la kudumu nyumbani na nje ya nchi kusaidia kuzuia kuongezeka kwa vifo vya raia na kuzidisha mzozo wa kibinadamu huko Gaza.
Hatimaye alivuka kizingiti cha kuzuia shehena ya silaha kwa Israel, mshirika wa karibu wa kimkakati wa Marekani katika eneo hilo, hatua ambayo haijaonekana tangu urais wa Ronald Reagan katika miaka ya 1980.
Tangu kuanza kwa vita, Biden amekumbwa na mgawanyiko wa kisiasa kati ya Chama cha Republican kinachounga mkono Israel bila shaka na Chama chake cha Democratic kilichogawanyika sana, anasema Aaron David Miller, mchambuzi wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje na mpatanishi mkongwe wa amani Mashariki ya Kati.
Hadi sasa rais huyo ameonekana kusita kufanya lolote linaloweza kuharibu uhusiano kati ya Marekani na Israel, Miller anaongeza.
Kilichobadilisha hali hiyo ni mtazamo wa Biden kwamba Waisraeli walikuwa karibu kuivamia Rafah.
Wiki iliyopita, Israel ilisema vikosi vyake vya ardhini vinaanza "shughuli" mashariki mwa mji huo, na vifaru vya Israeli vilisemekana kupiga kambi karibu na maeneo yanayolengwa.
Wakazi waliripoti sauti za mara kwa mara za milio ya makombora na walisema hospitali ambazo hazifanyi kazi zilizidiwa na majeruhi.
Umoja wa Mataifa unaonyesha kuwa zaidi ya watu 100,000 wamekimbia mapigano na wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa makazi, chakula, maji na huduma za afya.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameapa mara kwa mara kuanzisha uvamizi wa ardhini dhidi ya mji huo wenye makazi ya zaidi ya Wapalestina milioni moja waliokimbia makazi yao.
Anasema operesheni kubwa inahitajika kuharibu vikosi vinne vilivyosalia vya Hamas vilivyojificha huko, na kwamba watafanya hivyo bila kujali iwapo mazungumzo ya kusitisha mapigano yanafanikiwa.
Washington imesisitiza mara kwa mara kutofanya hivyo, ikishinikiza "operesheni inayolengwa zaidi" huko Rafah dhidi ya Hamas. Miller anasema rais wa Marekani anahofia kwamba uvamizi wa Rafah "utadhoofisha kimsingi nafasi yoyote ya kupunguza vita na kuwaachilia mateka."
Afisa huyo wa zamani, ambaye alitumia miaka mingi kushauri tawala ambazo Biden alihudumu, anasema rais pia anataka kuepusha mzozo na nchi jirani ya Misri na kwamba kuna hatari kwamba uvamizi unaweza kusababisha uchungu na mgawanyiko zaidi katika Chama cha Democrats.
"Ndio maana kilituma ishara hii," Miller anasema.
Usitishwaji wa silaha wenye utata
Kabla ya mahojiano ya televisheni ya Biden, Marekani ‘’ilisitisha’’ usafirishaji wa silaha kwenda Israeli: Shehena ya mabomu ya kilo 900 na 230.
Afisa mkuu wa utawala aliniambia kulikuwa na wasiwasi fulani kuhusu "matumizi " ya silaha na athari ambazo zinaweza kuleta katika mazingira ya mijini, "kama tulivyoona katika maeneo mengine ya Gaza."
Mabomu hayo yenye uzito wa kilo 900 ni miongoni mwa silaha zenye uharibifu mkubwa katika ghala la kijeshi la Israel. Jeshi lake linashikilia kuwa mabomu haya ni muhimu ili kuangamiza Hamas.
Usafirishaji wa vifaa vya mashambulio ya moja kwa moja (JDAM) ambavyo hubadilisha mabomu yasiyodhibitiwa kuwa mabomu ya kuongozwa pia unaangaziwa upya afisa huyo wa Marekani alisema.
Siku ya Ijumaa, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilitoa ripoti iliyoagizwa na Biden mapema mwaka huu ambayo ilisema huenda Israel ilitumia, katika baadhi ya matukio wakati wa mashambulizi ya Gaza, silaha zilizotolewa na Marekani katika mashambulizi ambayo yalikiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.
Lakini ripoti hiyo ilisema haikuwa na "taarifa kamili" katika tathmini yake, ikimaanisha kwamba msaada wa kijeshi unaweza kuendelea

Chanzo cha picha, AFP
Kanali Joe Buccino, mshambuliaji wa zamani wa Jeshi la Marekani ambaye alipanda ngazi hadi kuwa afisa mkuu katika Centcom (kamandi ya jeshi la Marekani Mashariki ya Kati), anabainisha kuwa jeshi la Israeli linaweza "kuharibu" Rafah kwa silaha inazomiliki.
Washington inaipatia Israel msaada wa kijeshi wa dola bilioni 3.8 kila mwaka. Hivi majuzi bunge la Congress liliongeza dola bilioni 17 katika mifumo ya silaha na ulinzi: Israeli, kwa jumla, ndio mpokeaji mkubwa zaidi wa misaada ya silaha kjutoka kwa Marekani.
Kanali Buccino anasema usafirishaji uliositishwa ni "kitu kisicho na maana" kwa shambulio lolote dhidi ya Rafah.
"Ni aina ya mchezo wa kisiasa kwa raia wa Marekani ambao... wana wasiwasi kuhusu hili," anaongeza.
"Nadhani usitishwaji huo unachukiza kabisa," alisema Seneta wa Marekani Pete Ricketts, akizungumza nami nje ya mkutano wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni. "Rais kwa kweli hana haki ya kufanya hivi."
Nilipomwambia kuwa Israel bado ina mbinu za kutekeleza shambulio hilo, alijibu: "Hii ni kuhusu kumuunga mkono mshirika wetu Israel dhidi ya shirika la kigaidi."
Seneta mwingine wa chama cha Republican, John Barrasso, alisema Israel ina haki ya "kufanya chochote inachotaka kulinda uhuru wake." Kwake, hatua ya Biden ilionyesha jambo moja: "Udhaifu wa rais huyu."
Lakini ndani ya chama cha Biden mwenyewe, kumekuwa na mapokezi mazuri zaidi kwa mabadiliko hayo.
Wakati muhimu
Miezi kadhaa iliyopita, Seneta wa chama cha Democrats Chris Coons alitoa wito wa kuzuiwa kwa msaada wa kijeshi kwa Israeli ikiwa kungekuwa na shambulio huko Rafah bila mabadiliko makubwa katika jinsi raia wa Palestina walivyotendewa na kulindwa.
"Mgogoro wa Gaza umesababisha tafakari zenye uchungu kwa watu kama sisi ambao tumeunga mkono Israel, lakini pia tuna wasiwasi kuhusu mateso ya binadamu katika eneo hili," alisema.
Coons anaamini kwamba Rais Joe Biden amejaribu "tena na tena" kumzuia Netanyahu, lakini mvutano kati ya wawili hao umeongezeka kwa sababu nguvu ya waziri mkuu wa Israel inategemea kwa kiasi kikubwa uungwaji mkono wa watu wenye msimamo mkali wanaopinga misaada ya kibinadamu inayokwenda Gaza na wanataka kuwafukuza Wapalestina wote kutoka Ukingo wa Magharibi.
"Hii inaweza kuwa mara ya kwanza kwa uhusiano huo kuvunjika," Coons anasema.
"Hatua hii dhidi ya waziri mkuu wa Israel inatokea wakati mgumu wa kuweza kuafikia usitishaji mapigano ili kubadilishana na kuachiliwa kwa wale waliotekwa nyara na Hamas.
Katika mazungumzo hayo yaliyokuwa yakifanyika nchini Misri, makubaliano hayakufikiwa na yakafutiliwa mbali.
Baadhi ya wachambuzi wa Israel wamependekeza kuwa maamuzi ya hivi karibuni ambayo Biden ameyafanya yataathiri mazungumzo ya mateka na kwamba jaribio lolote la kusitisha shambulio kwenye kivuko cha mpaka cha Rafah ni kwa manufaa ya Hamas.
Lakini maelezo ya midahalo, hata hivyo, hayeleweki, na hivyo kufanya iwe vigumu kujua iwapo dhana hiyo ni sahihi. Tatizo kubwa ni kwamba Hamas inataka kukomesha vita huko Gaza, jambo ambalo Israel inapinga.
Uhusiano kati ya Biden na Netanyahu ulianza miongo mitano iliyopita na umekuwa wa misukosuko mara kwa mara.

Wakati wote wawili walikuwa vijana, Biden alitia saini picha ya Netanyahu, ambayo aliiweka kwenye meza yake, ambayo inasema: "Bibi, nakupenda, lakini sikubaliani na jambo hata moja unalosema."
Netanyahu amemsifu rais huyo wa Marekani kwa uungaji mkono aliouonyesha kwa Israel, lakini wawili hao wamekuwa na tofauti kubwa kuhusu masuala yanayowahusu Wapalestina.
Chini ya wiki mbili baada ya shambulio la Oktoba 7, Biden alielekea Israeli na kumkumbatia Netanyahu kwenye lami huko Tel Aviv.
Nilikuwepo wakati Biden alipotoka kutoka kwenye mkutano na kiongozi wa Israel na baraza lake la mawaziri la vita na kusimama kwenye jukwaa kuthibitisha uungaji mkono wake bila masharti kwa Israeli.
Lakini alikuwa na onyo: Tusirudie makosa tuliyofanya baada ya mashambulizi ya 9/11.
"Watu wa Palestina pia wanateseka sana na tunaomboleza kupoteza maisha ya Wapalestina wasio na hatia kama ulimwengu mzima," alielezea kwa kina.
Safari ya wakati wa vita ya Biden inachukua umuhimu mkubwa katika kutazama nyuma: mwanzo wa jaribio la kuepusha mpasuko ambao haujawahi kushuhudiwa katika uhusiano kati ya Marekani na Israeli, mapumziko ambayo yalikaribia kutokea wiki hii.
Siku ya Alhamisi, siku moja baada ya Biden kutangaza kusitisha usafirishaji wa silaha, Netanyahu alijibu. Waziri mkuu ameelewa kwa muda mrefu kwamba anaweza kutumia raslimali zake kupinga shinikizo la Marekani.
"Ikiwa tunahitaji kuwa peke yetu, tutakuwa peke yetu. Nimesema ikibidi tutapigana kwa kucha,” alisema.
Niliwasilisha taarifa ya Netanyahu kwa Chris Coons, seneta wa Democrat.
"Hawahitaji kupigana kwa kucha. Watapigana na lazima wapigane na mifumo ya kisasa ya silaha ambayo wameunda mara nyingi pamoja nasi, na ambayo mara nyingi tunawapa," seneta huyo alisema.
"Lakini wanapaswa kufanya hivyo kwa njia ambayo itapunguza vifo vya raia," alisema.












