Je, uokoaji wa mateka wa Israel huko Gaza ulifanyikaje?

Hargari

Chanzo cha picha, AFP

Mateka wanne wameokolewa na jeshi la Israel kutoka katikati mwa Gaza, katika operesheni ambayo ilipangwa kwa wiki kadhaa.

Kwa Waisraeli ilileta sherehe na utulivu. Kwa Wapalestina ilileta mateso zaidi, huku hospitali zikisema makumi ya watu - ikiwa ni pamoja na watoto - waliuawa katika uvamizi wa kambi ya Nuseirat yenye wakazi wengi.

Operesheni hiyo iliyopewa jina la "Seeds of Summer", ilifanyika kwa njia isiyo ya kawaida wakati wa mchana - Jeshi la Ulinzi la Israel linasema lilitaka uvamizi huo wa kushutukiza kuwaacha wengi na mshangao.

Majira ya saa za asubuhi yalimaanisha kuwa mitaa ilikuwa na shughuli nyingi na watu kufanya ununuzi kwenye soko la karibu.

Pia ilimaanisha hatari kubwa kwa vikosi maalum vya Israel, sio tu kuingia, lakini haswa kutoka nje.

Afisa mmoja wa kikosi maalum alijeruhiwa na kufariki akiwa hospitalini, polisi wa Israel walisema.

Soma pia:
tt

Chanzo cha picha, Getty Images

"Ilikuwa kiwango cha operesheni ya Entebbe," kulingana na Msemaji Mkuu wa IDF Admiral Daniel Hagari akiashiria uokoaji wa Israeli wa mateka 100 nchini Uganda mnamo 1976.

Kwa kuzingatia taarifa za kijasusi, baada ya kuingia Gaza kutoka Israel, makomandoo wenye ujuzi wa hali ya juu walivamia kwa wakati mmoja vyimba viwili vya makazi huko Nuseirat ambapo mateka hao walikuwa wakishikiliwa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika ghorofa moja kulikuwa na mateka Noa Argamani mwenye umri wa miaka 26. Wengine walikuwa Shlomi Ziv mwenye umri wa miaka 41, Andrey Kozlov mwenye umri wa miaka 27 na Almog Meir Jan, 22.

Bw Hagari alisema hawakuwa kwenye vizimba bali katika vyumba vilivyofungwa vilivyozingirwa na walinzi.

Alisema makomando wa Israel, baada ya kuingia ndani kwa nguvu, waliwakamata mateka hao wakijikinga karibu nao ili kutoa ngao kabla ya kuwaingiza kwenye magari ya kijeshi yaliyokuwa yakisubiri nje.

Walipoondoka alisema walikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa Kipalestina.

Bw Hagari alisema wanajeshi wa Israel walikuwa wamepanga uvamizi huo kwa kina, hata kujenga picha za mizaha za vyumba viwili vya mafunzo.

Marekani pia ilitoa usaidizi wa kijasusi kwa Israel kwa operesheni hiyo, kulingana na CBS News, mshirika wa BBC, ambayo iliwataja maafisa wawili wa Marekani.

Video ya simu ya rununu kutoka eneo la tukio inaonyesha watu waking'ang'ana kujificha huku makombora yakidondoshwa kutoka angani na milio ya risasi ikisikika.

Picha za baadaye zilionyesha miili iliyotapakaa mtaani.

Nuseirat

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Muonekano wa Nuseirat baada ya shambulio la anga la Israeli siku ya Jumamosi

Ni wazi uvamizi hu ulihusisha nguvu kubwa. Madaktari katika hospitali hizo mbili katikati mwa Gaza walisema wamehesabu zaidi ya miili 70.

Bw Hagari alikadiria chini ya mia moja, huku ofisi ya vyombo vya habari vya Hamas ikisema zaidi ya 200 wameuawa.

BBC haijafanikiwa kuthibitisha idadi ya waliofariki.

"Nimekusanya viungo vya mwili wa mtoto wangu, mtoto wangu mpendwa" Nora Abu Khamees, anayeishi Nuseirat, aliambia BBC huku machozi yakimtiririka.

“Mtoto wangu mwingine yuko kati hali mahututi. Hata mume wangu na mama mkwe wangu, familia yetu yote imeangamizwa. Haya ni mauaji ya kimbari.”

Areej Al Zahdneh mwenye umri wa miaka kumi, akizungumza katika hospitali iliyo karibu, alituambia kulikuwa na mashambulizi ya anga, mizinga na risasi.

“Hatukuweza kupumua. Dada yangu Reemaz alipigwa na vipande kichwani mwake na dada yangu wa miaka mitano Yara pia alipigwa vipande vyangu.”

tt
Maelezo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi