Kuwatafuta wapendwa waliopotea katika makaburi ya halaiki ya Gaza

Na Fergal Keane ,

BBC News, Jerusalem

h
Maelezo ya picha, Kareema Elras alipata mwili wa mwanawe, Ahmed, ambaye aliuawa Januari 25, katika hospitali ya Nasser.

Mama atamtafuta mtoto wake aliyepotea popote. Na ili mradi awe na nguvu, hataacha kamwe.

Haijalishi awe hai au amekufa.

Kwa siku nne Kareema Elras amepitia kelele, vumbi na harufu kali ya makaburi ya halaiki katika hospitali ya Nasser.

Ni mama yake Ahmed mwenye umri wa miaka 21, ambaye aliuawa tarehe 25 Januari katika mji wa Khan Younis, kusini mwa Gaza. Mwili wake umetoweka tangu wakati huo.

Siku ya Jumanne, Kareema alimpata mwanaye wa kiume.

"Nimekuwa nikija hapa wakati wote hadi sasa," alisema, "mpaka nilipopata mwili wa mwanangu, mwanangu Ahmed, mvulana mdogo mpendwa. Baba yake alifariki alipokuwa na umri wa miaka 12, nami nikamlea."

Katika eneo jirani naye, familia nyingine hutembea kando ya eneo la makaburi.

Ni tukio linalofadhaisha sana ambalo ni la kawaida katika maeneo ya vita kote duniani.

Tingatinga zinachimba ardhini ili kuwafikia wafu.

Wachimba makaburi wanaweka alama kwenye maeneo ambayo miili iliyofukuliwa itazikwa, huku familia zenye wapendwa wao waliopotea zikiwa na matumaini ya kuwapata wapendwa wao katika wafu.

g

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wafanyakazi wa Ulinzi wa Raia wa Palestina wanasema zaidi ya miili 330 imeopolewa kutoka katika uwanja wa hospitali ya Nasser
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hatahivyo taswira nzima ya tukio sio lazima iwe na maelezo sawa . Kila kaburi la watu wengi - iwe katika Balkan, Afrika ya kati, Mashariki ya Kati, au mahali pengine - ni matokeo ya hali yake ya ndani.

Katika vita ambavyo vimeripotiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya 34,000 kwenye ardhi yenye msongamano mkubwa wa watu , mazishi ya wafu yamekuwa kazi ngumu na mara nyingi ya hatari.

Baadhi ya makaburi yamejaa. Wengine hawawezi kufikiwa kwa sababu ya mapigano. Kwa sababu ya shinikizo hizi miili imezikwa katika uwanja wa hospitali ambapo majeshi ya Israeli yalisema yalipigana na Hamas.

Katika baadhi ya vita ambavyo nimeripoti iliwezekana kueleza kwa haraka kilichotokea kwa waathiriwa. Hii ni kwa sababu wachunguzi wa mahakama walikuwa kwenye eneo la tukio muda mfupi baadaye na waandishi wa habari waliweza kufikia eneo hilo na kupata taarifa mapema.

Katika hali ya sasa ya Gaza - huku Israeli na Misri zikiwazuia waandishi wa habari wa kimataifa kuingia katika nchi hizo , na mapigano yakitengeneza mazingira hatari sana kwa timu yoyote ya wachunguzi wa mahakama - ni changamoto kubwa kubaini ni lini na ni lini kila mwili wa wale wanaoopolewa kutoka kwenye makaburi ya hospitali ya El Nasser na pia hospitali ya al-Shifa hospital, kaskazini mwa Jiji la Gaza alifariki .

Je baadhi yao waliuawa na vikosi vya Israel, kama Hamas na waokoaji wa eneo hilo wanavyodai?

Au je, mamia ya waliokufa katika makaburi ya halaiki ndio waathiriwa wote wa mashambulizi ya anga na mapigano katika eneo la ndani na karibu na majengo ya matibabu, pamoja na waathiriwa wengine wa magonjwa na utapiamlo unaosababishwa na vita? Je, Waisraeli walihamisha miili kutoka kaburi moja hadi kaburi jipya?.

Je, tunajua nini kuhusu mazishi ya hospitali ya Nasser?

Na Shayan Sardarizadeh, BBC Verify

Kitengo cha BBC Verify kimethibitisha video zilizochapishwa mtandaoni tarehe 22 , 25 na 28 Januari, ambazo zinaonyesha Wapalestina wakizika miili katika maeneo mawili katika ua wa hospitali ya Nasser.

Kanda hiyo ya vídeo ilipangwa kwa kutumia mstari wa mitende miwili na kulinganisha majengo yanayoonekana kwa umbali wa kati.

Mazishi hayo ya muda yalifanyika huku wafanyakazi wa afya na raia walioyakimbia makazi yao wakiripoti mapigano makali katika eneo hilo na baada ya hospitali hiyo kusemekana kuzingirwa na vikosi vya ardhini vya Israel.

g

Chanzo cha picha, Google

Maelezo ya picha,

Hatuna njia ya kuthibitisha kwa usahihi ni miili mingapi ilizikwa kabla ya uvamizi wa Israel kuanza tarehe 15 Februari. Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema tarehe 27 Januari kwamba miili ya watu 150 ilikuwa imezikwa katika ua wa hospitali hiyo, lakini ni vigumu kuthibitisha idadi hiyo.

Tunaweza kuthibitisha kuwa picha zilizochapishwa katika siku za hivi karibuni , kufuatia kuondolewa kwa wanajeshi wa Israeli kutoka Khan Younis, zinaonyesha maeneo sawa ya mazishi. Mstari sawa wa miti na majengo ya jirani yanaweza kuonekana wazi.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa haki za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina, Ajith Sunghay, aliniambia lazima kuwe na uchunguzi huru wa kisayansi wa makaburi hayo.

Siku ya Jumanne, afisa mwingine wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa baadhi ya miili ilipatikana ikiwa imefungwa mikono.

Hii ilifuatia taarifa ya afisa wa Ulinzi wa Raia wa Palestina, kikundi kinachofanya shughuli za uokoaji , kwamba miili imepatikana ikiwa imefungwa pingu, huku wengine wakionekana kupigwa risasi kichwani, na wengine wamevaa sare za wafungwa.

Reem Zeidan alitumia wiki mbili kuutafuta mwili wa mwanaye Nabil, ambao ulipatikana Jumatano alasiri.

Reem anasema aliona miili iliyokuwa na dalili za mateso, huku mikono ikiwa imefungwa pingu. "Waliuawa. Wengine walifungwa pingu mikono na miguu pamoja na kunyongwa. Hii itaendelea hadi lini?"

Nilimuuliza Bwana Sunghay kama alikuwa ameona ushahidi thabiti wa miili iliyofungwa mikono.

“Bado hatuna ushahidi, tuna taarifa,” alijibu. "Na taarifa hizo zinahitaji thibitisho kutoka vyanzo tofauti. Na hiyo ndiyo sababu hasa tunahitaji uchunguzi huru wa kimataifa."

"Kile ambacho hatuwezi kuruhusu, katika hali hii ya sasa ambapo tumeona ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu huko Gaza, mwingi ukiwa ni uhalifu wa kivita, na ambapo tumeibua hofu ya uhalifu wa kikatili unaoweza kutokea, hilo linakuwa janga jingine. Ukiukaji huo umekithiri."

Bw Sunghay alisema ana timu zilizo tayari kupelekwa Gaza iwapo zitapewa ruhusa na kupita salama na Israel.

f
Maelezo ya picha, BBC Verify inathibitisha video kutoka matukio muhimu katika kituo cha afya cha Nasser Medical Complex huko Gaza

Jeshi al Israel, IDF, liliongeza kuwa miili ilitolewa na kuchunguzwa ili kuona kama iwapo kuna wale mateka waliokamatwa na Hamas na kupelekwa Gaza wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7 dhidi ya Israeli.

Taarifa hiyo ilisema: "Uchunguzi ulifanyika kwa uangalifu na hasa katika maeneo ambayo ujasusi ulionyesha kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa mateka. Uchunguzi ulifanyika kwa heshima huku ukidumisha hadhi ya marehemu."

Kazi ya kujaribu kutambua na kutoa mazishi ya heshima kwa wafu itaendelea kwa siku zijazo.

Upande wa Israel umekanusha kuwa ni kashfa madai kwamba ilizika miili katika hospitali hizo.

Katika taarifa yake, Jeshi la Ulinzi la Israel lilisema: "Madai kwamba IDF ilizika miili ya Wapalestina hayana msingi ."

g
Maelezo ya picha, Somaya al-Shourbagy alipiga magoti kando ya kaburi la mumewe Osama akiwa na binti yao mdogo, Hind.

Somaya al-Shourbagy aliuchukua mwili wa mumewe Osama katika hospitali ya Nasser na kufanikiwa kumpeleka kwenye kaburi ili kuzikwa karibu na familia yao yote.

Alipiga magoti kando ya kaburi lililochimbwa upya pamoja na binti wa wanandoa hao, Hind.

"Binti yangu mdogo aliniomba kuzuru kaburi la baba yake," Somaya alisema, "na ningemwambia mara tu tukimzika tutamtembelea, namshukuru Mungu, hali ni ngumu, lakini tunaweza kupata nafuu baada ya kumzika."

Hind, ambaye ana umri wa karibu miaka mitano, aanamkumbuka baba yake kwa kumbukumbu ya kitoto: "Alinipenda, na alikuwa akininunulia vitu, na alikuwa akinipeleka kutembea."

Unaweza pia kusoma:

Ripoti ya ziada na Alice Doyard, Haneen Abdeen na Nik Millard.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah