Nini kimewapata viongozi mashuhuri wa Hamas?

- Author, Raffi Berg & Lina Alshawabkeh
- Nafasi, BBC News, London & BBC News Arabic, Amman
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Tangu vita vilipoanza huko Gaza kufuatia shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, viongozi wake wamekuwa wakilengwa na Israel. Wengine wameuawa, wengine wamesalia kidete katika kuipinga Israel.
Huu hapa ni muhtasari wa kile kilichotokea kwa viongozi mashuhuri wa Hamas.
Ismail Haniyeh

Chanzo cha picha, Reuters
Ismail Haniyeh alizingatiwa sana kama kiongozi mkuu wa Hamas.
Aliuawa, katika shambulio la angani, kwenye jengo alilokuwa akiishi wakati wa ziara yake mjini Tehran tarehe 31 Julai, 2024. Iran na Hamas zimeilaumu Israel kwa shambulio hilo.
Mwanachama mashuhuri wa Hamas mwishoni mwa miaka ya 1980, Israel ilimfunga Haniyeh kwa miaka mitatu mwaka 1989 huku ikikabiliana na uasi wa kwanza wa Wapalestina.
Kisha alihamishwa mwaka 1992 hadi ardhi isiyomilikiwa na nchi yoyote kati ya Israel na Lebanon, pamoja na baadhi ya viongozi wa Hamas.
Baada ya mwaka mmoja alirudi Gaza. Mnamo 1997 aliteuliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kiongozi wa kidini wa Hamas, akiimarisha nafasi yake.
Haniyeh aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Palestina mwaka 2006 na Rais Mahmoud Abbas baada ya Hamas kushinda viti vingi zaidi katika uchaguzi za kitaifa. Lakini alifukuzwa kazi mwaka mmoja baadaye huku kukiwa na ghasia mbaya huko Gaza, na Hamas hatimaye kukiondoa chama cha Fatah cha Bw Abbas kutoka Ukanda wa Gaza.
Haniyeh alipinga kufukuzwa kwake kama "kinyume cha katiba", na Hamas iliendelea kutawala huko Gaza.
Alichaguliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa yenye nguvu zaidi ya Hamas mnamo 2017, na kumfanya kuwa kiongozi wa jumla.
Mnamo mwaka wa 2018, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilimtaja Haniyeh kuwa gaidi. Alikuwa ameishi Qatar kwa miaka kadhaa iliyopita.
Yahya Sinwar

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Yahya Sinwar ni kiongozi wa Hamas ndani ya Ukanda wa Gaza. Israel inaamini kuwa ndiye aliyepanga shambulio hilo ambalo halijawahi kutokea tarehe 7 Oktoba 2023.
Sinwar alizaliwa katika kambi ya wakimbizi ya Khan Younis huko Gaza mnamo 1962.
Mwaka mmoja baada ya Hamas kuanzishwa mwaka 1987, aliunda huduma yake ya usalama wa ndani, ambayo miongoni mwa mambo mengine ililenga wanaodaiwa kuwa ni Wapalestina wanaoshirikiana na Israel.
Sinwar alikamatwa na Israeli mara tatu. Alihukumiwa vifungo vinne vya maisha mwaka 1988 kwa kupanga utekaji nyara na mauaji ya wanajeshi wawili wa Israel na mauaji ya Wapalestina wanne.
Hata hivyo, mwaka 2011 alikuwa miongoni mwa wafungwa 1,027 wa Wapalestina na Waisraeli wa Kiarabu walioachiliwa na Israel kwa kubadilishana na mwanajeshi wa Israel aliyetekwa na Hamas kwa zaidi ya miaka mitano.
Sinwar alirejea katika nafasi yake ya kiongozi mashuhuri katika Hamas na aliteuliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya kundi hilo katika Ukanda wa Gaza mwaka 2017, na kumfanya kuwa kiongozi wa Hamas katika eneo hilo.
Mnamo 2015, Marekani ilijumuisha jina la Sinwar kwenye orodha yake ya "magaidi wa kimataifa".
Israel wiki jana ilitangaza kumuua Sinwar na kutoa video hii iliyoonyesha dakika zake za mwisho mwisho kabla ya mauti kumkumba
Mohammed Deif

Chanzo cha picha, Reuters
Mohammed Deif alikuwa mkuu wa Brigedi ya Izz al-Din al-Qassam, kitengo cha kijeshi cha harakati ya Hamas. Alikuwa mtu anayesakwa sana na Israeli kwa miongo kadhaa, na aliuawa katika shambulio la anga la Israeli mwezi uliopita, Israeli inasema. Hamas haijathibitisha hili.
Deif, mtu ambaye ni vigumu kujua aliko na shughuli zake, alijulikana kwa Wapalestina kama The Mastermind, na kwa Waisraeli kama Paka mwenye Maisha Tisa.
Mamlaka ya Israeli ilimfunga gerezani mwaka wa 1989 wakati wa intifada ya kwanza ya Wapalestina (maasi), na kumwachilia baada ya mwaka mmoja na nusu. Muda mfupi baadaye aliunda Brigedi ya al-Qassam, kwa lengo la kuwakamata wanajeshi wa Israel.
Pia alisaidia katika ujenzi wa mahandaki yaliyowawezesha wapiganaji wa Hamas kuingia ndani ya Israel kutoka Gaza.
Deif alishutumiwa na Israel kwa kupanga na kusimamia mashambulizi ya mabasi yaliyoua makumi ya Waisraeli mwaka 1996, na kuhusika katika kuwakamata na kuwaua wanajeshi watatu wa Israel katikati ya miaka ya 1990. Alikamatwa na Mamlaka ya Palestina mwaka 2000, lakini alitoroka miezi saba baadaye mwanzoni mwa intifadha ya pili.
Alikuwa mtu anayetafutwa sana na Israeli, lakini tangu wakati huo hakuna aliyejua aliko.
Majaribio makubwa zaidi ya kumuua yalikuwa mwaka wa 2002: Deif alinusurika lakini alipoteza jicho lake moja. Israel inasema pia alipoteza mguu na mkono, na tatizo la kuongea.
Israel ilijaribu na kushindwa tena kumuua Deif wakati wa shambulio la 2014 kwenye Ukanda wa Gaza, lakini ikaua mke wake na watoto wake wawili.
Deif alikuwa mmoja wa watu walioshutumiwa kupanga shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, 2023. Israel ilisema ilimuua katika shambulio la anga kwenye boma katika eneo la Khan Younis huko Gaza tarehe 13 Julai.
Marwan Issa

Chanzo cha picha, Media sources
Hamas haijathibitisha kwamba Marwan Issa, naibu kamanda mkuu wa Brigedi ya Izz al-Din al-Qassam, aliuawa katika shambulio la anga la Israeli mnamo Machi 2024, kama ilivyoripotiwa na Ikulu ya White House.
Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan alisema aliuawa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), kufuatia ripoti katika vyombo vya habari vya Israel kwamba alifariki katika shambulio kwenye eneo la handaki chini ya kambi ya wakimbizi ya Nuseirat.
Kamanda huyo mkuu pia anajulikana kama 'Shadow Man' na ametazamwa kama 'mtu wa mkono' wa Mohammed Deif.
Kabla ya ripoti za kifo chake, alikuwa kwenye orodha ya wanaosakwa zaidi na Israeli, na alijeruhiwa wakati Israeli ilipojaribu kumuua mnamo 2006.
Vikosi vya Israel vilimzuilia wakati wa intifada ya kwanza kwa miaka mitano kwa sababu ya shughuli zake na Hamas.
Mamlaka ya Palestina ilimkamata mnamo 1997, lakini aliachiliwa baada ya intifada ya pili mnamo 2000.
Ndege za kivita za Israel pia ziliharibu nyumba yake mara mbili wakati wa uvamizi wa Gaza mwaka 2014 na 2021, na kumuua kaka yake.
Haikujulikana anafanana vipi hadi 2011, alipoonekana katika picha ya pamoja iliyopigwa wakati wa mapokezi ya wafungwa waliobadilishwa.
Anafikiriwa kuwa na jukumu muhimu katika kupanga uvamizi ndani ya Israeli, ikiwa ni pamoja na wa hivi karibuni.
Khaled Meshaal

Chanzo cha picha, AFP
Khaled Meshaal, ambaye alizaliwa katika Ukingo wa Magharibi mwaka 1956, anachukuliwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa Hamas.
Chini ya maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, shirika la kijasusi la Israel la Mossad lilijaribu kumuua Meshaal mwaka 1997 alipokuwa akiishi Jordan.
Maafisa wa Mossad waliingia Jordan wakiwa na pasipoti ghushi za Canada na Meshaal alidungwa sindano yenye sumu wakati akitembea kando ya barabara.
Mamlaka ya Jordan iligundua jaribio la mauaji na kuwakamata maafisa wawili wa Mossad.
Marehemu Mfalme Hussein wa Jordan alimwomba waziri mkuu wa Israeli dawa ya ya kumtibu Meshaal kuzuia kifo chake kutokana na sumu aliyodungwa. Akikabiliwa na shinikizo kutoka kwa Rais wa wakati huo wa Marekani Bill Clinton, Bw Netanyahu alitoa dawa baada ya awali kukataa ombi hilo.
Meshaal, ambaye anaishi Qatar, alitembelea Ukanda wa Gaza kwa mara ya kwanza mwaka 2012. Alipokelewa na maafisa wa Palestina na umati wa Wapalestina ulijitokeza kumkaribisha.
Hamas ilimchagua Ismail Haniyeh kumrithi Meshaal kama mkuu wa ofisi yake ya kisiasa mwaka 2017, na Meshaal akawa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya kundi hilo nje ya nchi.
Mahmoud Zahar

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahmoud Zahar alizaliwa Gaza mwaka 1945 kwa baba Mpalestina na mama wa Misri. Anachukuliwa kuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa Hamas, na mwanachama wa uongozi wa kisiasa wa harakati hiyo.
Alienda shule huko Gaza na chuo kikuu huko Cairo, kisha akafanya kazi kama daktari huko Gaza na Khan Younis hadi mamlaka ya Israeli ilipomfukuza kwa msimamo wake wa kisiasa.
Mahmoud Zahar alishikiliwa katika jela za Israel mwaka 1988, miezi kadhaa baada ya kuanzishwa kwa Hamas. Alikuwa miongoni mwa wale waliofukuzwa na Israel hadi katika ardhi iliyomilikiwa na nchi yoyote mwaka 1992, ambako alikaa mwaka mmoja.
Pamoja na harakati ya Hamas kushinda uchaguzi mkuu wa Palestina mwaka 2006, Zahar alijiunga na Wizara ya Mambo ya Nje katika serikali mpya ya Waziri Mkuu Ismail Haniyeh kabla ya kutimuliwa.
Israel ilijaribu kumuua Zahar mwaka 2003, wakati ndege ilipodondosha bomu kwenye nyumba yake katika jiji la Gaza . Shambulio hilo lilimwacha na majeraha madogo, lakini lilimuua mwanawe mkubwa, Khaled.
Mwanawe wa pili, Hossam, ambaye alikuwa mwanachama wa Brigedi ya al-Qassam, aliuawa katika shambulio la anga la Israeli huko Gaza mnamo 2008.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












