Jinsi Israel ilivyompata na kumuua kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanajeshi wa Israel walikuwa wamemuwinda kwa zaidi ya mwaka mmoja kiongozi wa Hamas, ambaye alitoweka huko Gaza mara tu baada ya kupanga mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba.
Yahya Sinwar, 61, alisemekana alitumia muda wake mwingi kujificha kwenye vichuguu chini ya Ukanda huo, pamoja na kada ya walinzi na "ngao ya kibinadamu" ya mateka waliokamatwa kutoka Israeli.
Lakini hatimaye, inaonekana alikutana na mwisho wake katika kukutana na doria ya Israeli kusini mwa Gaza. Alikuwa na idadi ndogo ya walinzi. Hakuna mateka waliopatikana.
Bado taarifa zinaendelea kujitokeza, lakini hiki ndicho tunachokijua hadi sasa kuhusu mauaji ya Sinwar.

Chanzo cha picha, Getty Images
Doria ya kawaida
Jeshi la Ulinzi la Israel linasema kuwa kikosi cha 828 cha Biislamach Brigade kilikuwa kikishika doria Tal al-Sultan, eneo la Rafah, siku ya Jumatano.
Wanamgambo watatu walitambuliwa na walipambana na wanajeshi wa Israeli, na wote waliuawa.
Katika hatua hiyo hakuna kitu kilichoonekana kuwa cha kushangaza hasa kuhusu zima moto na askari hawakurejea eneo la tukio hadi Alhamisi asubuhi.
Hapo ndipo wafu walipokuwa wakikaguliwa, ndipo moja ya miili hiyo ilipopatikana ina mfanano wa kushangaza na kiongozi wa Hamas.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maiti hiyo hata hivyo ilisalia situ kutokana na kushukiwa kuwa na mitego ya vilipuzi na badala yake, sehemu ya kidole ilitolewa na kupelekwa Israel kufanyiwa uchunguzi.
Mwili wake hatimaye ulitolewa na kupelekwa Israeli baadaye siku hiyo kwani eneo hilo liliwekwa salama.
Daniel Hagari, msemaji wa IDF, alisema vikosi vyake "havikujua kuwa alikuwa huko lakini tuliendelea kufanya kazi".
Alisema askari wake waliwatambua watu hao watatu wakikimbia nyumba hadi nyumba, na kuwashambulia kabla hawajatengana.
Mtu huyo ambaye alitambuliwa kama Sinwar "alikimbia peke yake kwenye moja ya majengo" na aliuawa baada ya kupatwa na ndege isiyo na rubani.
Hakuna mateka hata mmoja ambaye Sinwar aliaminika kutumia kama ngao ya binadamu aliyekuwepo na msafara wake mdogo unaonesha kuwa alikuwa akijaribu kusogea bila kutambuliwa, au alikuwa amepoteza wengi wa wale waliokuwa wakimlinda.
Yoav Gallant, waziri wa ulinzi wa Israeli, alisema: "Sinwar alikufa wakati akipigwa, akiteswa na kukimbia, hakufa kama kamanda, lakini kama mtu aliyejijali mwenyewe. Huu ni ujumbe wa wazi kwa maadui wetu wote. "
Picha zilizotolewa na jeshi la Israel siku ya Alhamisi zilisemekana kuonesha dakika za mwisho za Sinwar kabla ya kuuawa.
Video hiyo inaonekana kupigwa kutoka kwenye ndege isiyo na rubani inayoruka kupitia dirisha lililo wazi la jengo lililoharibiwa zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sinwar 'aondolewa'
Israel ilitangaza kwa mara ya kwanza kuwa "inachunguza uwezekano" kwamba Sinwar aliuawa huko Gaza siku ya Alhamisi alasiri kwa saa za huko.
Ndani ya dakika chache baada ya tangazo hilo, picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha mwili wa mwanaume mwenye sura zinazofanana sana na kiongozi huyo wa Hamas, ambaye alikuwa amepata majeraha mabaya kichwani.
Hata hivyo, maafisa walionya "katika hatua hii" utambulisho wa yeyote kati ya watu watatu waliouawa haukuweza kuthibitishwa.
Muda mfupi baadaye, vyanzo vya Israeli viliiambia BBC "wanajiamini zaidi" kuwa wamemuua. Hata hivyo, walisema vipimo vyote muhimu lazima vifanyike kabla ya kifo kuthibitishwa.
Vipimo hivyo havikuchukua muda mrefu. Kufikia Alhamisi jioni, Israeli ilikuwa imetangaza kuwa imekamilika na kwamba Sinwar alithibitishwa "kuuawa".
Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa Israel, alisema "uovu" "umeshughulikiwa", lakini akaonya kuwa vita vya Israel huko Gaza havijakamilika.

Chanzo cha picha, IDF
Kitanzi cha kukaza
Sinwar alikuwa akikimbia kwa zaidi ya mwaka mmoja. Bila shaka alihisi shinikizo la Israeli likiongezeka wakati viongozi wengine wa Hamas, kama vile Mohammad Dief na Ismail Haniyeh, waliuawa, na wakati Israeli ikiharibu miundombinu aliyokuwa ametumia katika ukatili wa Oktoba 7.
Katika taarifa, IDF ilisema operesheni zake katika wiki za hivi karibuni kusini "zimezuia harakati za utendaji za Yahya Sinwar alipokuwa akifuatiliwa na vikosi na kupelekea kuondolewa kwake".
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












