Kwa nini Marekani inaipa Israel mfumo wenye nguvu wa kuzuia makombora?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Wizara ya ulinzi ya Marekani, imethibitisha kuwa inatuma mfumo wa kukabiliana na makombora wa anga ya juu unaoendeshwa na wanajeshi wa Marekani kwa Israel.
Maafisa wanasema mfumo uitwao Terminal High-Altitude Area Defense (Thaad) utaimarisha ulinzi wa anga wa Israel baada ya shambulio la kombora la Iran nchini humo mapema mwezi huu.
Rais Joe Biden amesema inalenga "kuilinda Israel", ambayo bado inatarajiwa kulipiza kisasi dhidi ya shambulio la Iran lililohusisha zaidi ya makombora 180 ya balistiki yaliyorushwa dhidi ya Israel tarehe 1 Oktoba.
Tayari kuna idadi ndogo ya vikosi vya Marekani nchini humo, lakini upelekaji huu mpya wa wanajeshi wapatao 100 ni muhimu kwani unaashiria kujiingiza zaidi kwa Marekani katika vita vya kikanda vinavyopanuka.
Israel bado haijaanza kulipiza kisasi shambulio la Iran, ambalo litakuwa " baya, sahihi na zaidi ya yote, la kushangaza" kulingana na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant.
Tehran ilisema iliifyatulia risasi Israel kwa sababu ilimuua Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hezbollah inayoungwa mkono na Iran, huko Beirut.
Bado haijafahamika iwapo kupelekwa kwa Thaad ni sehemu ya mpango wa dharura wa Marekani wa kuziba mapengo yaliyobainishwa katika ulinzi wa anga wa Israel, au kama inaashiria wasiwasi unaoongezeka huko Washington wa shambulio kali zaidi la Israel dhidi ya Iran.
Rais Biden amepinga mashambulizi yoyote dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, pamoja na miundombinu yake ya mafuta au nishati, huku kukiwa na hofu kwamba ingezua mzozo unaoendelea na kuathiri uchumi wa dunia.
Bila kujali uamuzi uliofikiwa awali, inaashiria hitaji zaidi la Israel kwa usaidizi wa kiulinzi wa Marekani huku kukiwa na ongezeko la vita vya Mashariki ya Kati.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Makombora ya balistiki kama Fattah-1 yaliyotumiwa na Iran mapema mwezi huu yalirushwa juu angani, ambapo yalibadilisha mwelekeo na kushuka kuelekea shabaha yao. Moja ya faida zake za kijeshi ni kasi yake kubwa ikilinganishwa na makombora ya cruise au ndege zisizo na rubani.
Mfumo wa Thaad una ufanisi mkubwa dhidi ya makombora ya balestiki, kulingana na mtengenezaji Lockheed Martin, mtengenezaji mkuu wa silaha wa Marekani.
Raytheon, kampuni nyingine ya silaha ya Marekani, inaunda rada yake ya hali ya juu.
Thaad inatafutwa sana na Ukraine ili kukabiliana na mashambulizi ya makombora ya Urusi.
Mashambulizi ya Iran ya tarehe 1 Oktoba dhidi ya Israel yaliua mtu mmoja huko Jeriko katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ambaye alipigwa na sehemu ya kombora ambalo inaonekana lilidunguliwa.
Israel ina mfumo wa ulinzi wa angani unaothaminiwa sana, uliotengenezwa na Marekani, ikijumuisha makombora ya Arrow 2 na Arrow 3 ya anga.
Ndege hizi huruka kwa kasi kubwa na zinaweza kurusha makombora ya balestiki angani. Wabunifu wa mfumo wa Israel walisema Arrow "ilifanya kama ilivyotarajiwa" na matokeo "ya ajabu" dhidi ya mashambulizi ya Iran.
Marekani iliunga mkono operesheni hiyo ya kujihami, ikifyatua vizuizi kutoka kwa mifumo miwili ya uharibifu ya majini mashariki mwa Mediterania, sambamba na usaidizi kutoka kwa baadhi ya nchi za Ulaya na Kiarabu.
Picha za satelaiti zilionesha uharibifu katika kituo cha Nevatim cha Jeshi la Wanaanga la Israel, ambacho kinahifadhi ndege za kivita za F-35, zikiwemo kreta kwenye njia ya kurukia.
Mashambulizi ya makombora ya Iran yalifuatia mauaji ya Israel dhidi ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh (mpatanishi katika mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka wa Gaza), Hassan Nasrallah mjini Beirut, mashambulizi ya anga ya Israel katika maeneo yenye wakazi wengi wa Beirut na uvamizi wake wa ardhini nchini Lebanon.
Israel ilisema imekuwa ikishambulia uongozi wa Hezbollah na kuharibu hifadhi yake kubwa ya makombora kutokana na miezi 11 ya kurusha roketi kuvuka mpaka ndani ya Israel.
Inasema shinikizo la kijeshi tu na uwezo wa kuharibu uwezo wa Hezbollah utahakikisha Waisraeli 60,000 wanaweza kurejea makwao kaskazini mwa Israel.
Pentagon inaelezea kupelekwa kwa Thaad kama sehemu ya "marekebisho makubwa ambayo jeshi la Marekani limefanya katika miezi ya hivi karibuni" kusaidia Israeli na kuwalinda wafanyakazi wa Marekani kutokana na mashambulizi ya Iran na vikundi vinavyoungwa mkono na Iran.
Inasema Thaad ilitumwa kusini mwa Israel kwa ajili ya mazoezi mnamo mwaka 2019, mara ya mwisho na ilijulikana kuwa huko pekee.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alionya Jumapili kwamba Marekani inaweka maisha ya wanajeshi wake "hatarini kwa kuwatuma kuendesha mifumo ya makombora ya Marekani nchini Israel".
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Seif Abdalla












