Kwanini Marekani imeshindwa kupata makubaliano ya amani Mashariki ya Kati?

d
Muda wa kusoma: Dakika 5

Mwaka mmoja uliopita, baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 na kuanza kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza, Joe Biden alikua rais wa kwanza wa Marekani kuizuru Israel wakati wa vita.

Alikutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na baraza la mawaziri la vita huko Tel Aviv, na kuwaambia: "Hamuko pekee yenu.” Lakini pia aliuhimiza uongozi wa Netanyahu, kutorudia makosa ambayo Marekani iliyafanya baada ya 9/11.

Mwezi Septemba mwaka huu katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais Biden aliongoza wito wa kimataifa akitaka Israel na Hezbollah zijizuie kushambuliana.

Netanyahu alitoa majibu kwa kusema Israel ina mkono mrefu, na unaweza kufika popote katika eneo la Mashariki ya Kati.

Dakika tisini baadaye, marubani wa Israel walirusha makombora yaliyotolewa na Marekani kwenye majengo ya kusini mwa Beirut.

Shambulio hilo lilimuua kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah.

Diplomasia ya Biden ilikuwa ikizikwa katika magofu ya shambulio la anga la Israel kwa kutumia mabomu yaliyotolewa na Marekani.

Lengo kuu la diplomasia kama inavyoelezwa na utawala wa Biden ni kupata usitishaji wa mapigano kwa makubaliano ya kuwaachilia huru mateka wa huko Gaza.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka mmoja baada ya Hamas kuvunja uzio wa kijeshi kuelekea kusini mwa Israel – na kuua zaidi ya watu 1,200 na kuwateka nyara 250 - ikiwa ni pamoja na raia saba wa Marekani – mateka wengi wamesalia kifungoni, huku idadi kubwa ikiaminika kuwa wamekufa.

Huko Gaza, mashambulizi makubwa ya kulipiza kisasi ya Israel yamesababisha vifo vya takribani Wapalestina 42,000, kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, eneo hilo limeharibiwa, watu wanakimbia na limekumbwa na njaa.

Umoja wa Mataifa unasema idadi kubwa ya wafanyakazi wa misaada wameuawa katika mashambulizi ya Israel, huku makundi ya kibinadamu yakiishutumu mara kwa mara Israel kwa kuzuia upelekwaji wa misaada - jambo ambalo serikali ya Israel imekuwa ikilikanusha.

Wakati huo huo, vita vimeenea hadi Ukingo wa Magharibi na Lebanon. Wiki iliyopita Iran ilirusha makombora 180 kwenda Israel kulipiza kisasi mauaji ya Nasrallah, kiongozi wa kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.

Mafanikio na hasara

Maafisa wa Biden wanadai shinikizo la Marekani lilibadilisha "sura ya operesheni za kijeshi za Israel," wakirejelea operesheni za Israel huko Rafah, wanaamini ilikuwa na mipaka, hata kama sehemu kubwa ya mji huo ni kifusi na magofu.

Kabla ya uvamizi wa Rafah, Biden alisimamisha shehena moja ya silaha alipokuwa akijaribu kuizuia Israel kufanya mashambulizi makubwa. Lakini rais huyo alikabiliwa na upinzani kutoka Republicans huko Washington na kutoka kwa Netanyahu mwenyewe na tangu wakati huo ameondoa usitishwaji huo na hajarudia tena kusitisha.

Wizara ya Mambo ya Nje inadai shinikizo lake kwa Israel lilifanikisha kupelekwa msaada zaidi Gaza, licha ya Umoja wa Mataifa kuripoti uwepo wa njaa huko Gaza mapema mwaka huu.

Kazi nyingi za Biden zimefanywa na mwanadiplomasia wake mkuu, Anthony Blinken. Amefanya safari kumi Mashariki ya Kati tangu Oktoba katika duru za kidiplomasia na kazi ya siri ya CIA ya kujaribu kupata makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza kati ya Israel na Hamas.

Lakini safari hizo zilionekana kutofua dafu hasa baada ya Netanyahu kudai kuwa "amemshawishi" Blinken juu ya hitaji la kuweka wanajeshi wa Israel kwenye mpaka wa Gaza na Misri kama sehemu ya makubaliano.

Hilo lilivunja makubaliano na Hamas na Misri. Afisa mmoja wa Marekani alimshutumu Netanyahu kwa kujaribu kuhujumu makubaliano hayo. Mpango huo haukuenda popote.

Katika safari yake ya kumi katika eneo hilo mwezi uliopita, Blinken hakuitembelea Israel.

Diplomasia imefikia wapi?

Wakati Marekani inatoa wito wa kusitishwa vita huku ikiipa Israel silaha za thamani ya dola za kimarekani bilioni 3.8 kwa mwaka, na imekubali ombi la nyongeza ya silaha tarehe 7 Oktoba, inaonekana imeshindwa kutumia nguvu zake au inafanya undumilakuwili.

Wakosoaji wa Biden wakiwemo maafisa wa Marekani, wanasema upanuzi wa sasa wa vita kwa kweli unathibitisha undumilakuwili, kuliko kushindwa kwa sera ya kidiplomasia ya Marekani.

"Ni kweli Marekani imefanya diplomasia na mikutano mingi. Lakini haijafanya juhudi yoyote ya maana kubadili tabia ya mmoja wa wahusika wakuu - Israel,” anasema afisa wa zamani wa ujasusi Harrison J. Mann, Meja wa Jeshi la Marekani ambaye alikuwa akifanya kazi katika kitengo cha kijasusi cha Mashariki ya Kati na Afrika wakati wa shambulio la Oktoba 7.

Mann alijiuzulu mapema mwaka huu akipinga uungaji mkono wa Marekani kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza na idadi ya raia wanaouawa kwa kutumia silaha za Marekani.

Washirika wa Biden wanakataa ukosoaji huo. Wanatoa mfano upatanishi uliosababisha wa mwezi Novemba mwaka jana ambao ulishuhudia mateka zaidi ya 100 wakiachiliwa huru huko Gaza na karibu wafungwa 300 wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel wakiachiwa.

Maafisa wa Marekani pia wanasema utawala huo uliizuia Israel kuivamia Lebanon mapema zaidi wakati mzozo wa Gaza unaanza, licha ya kurushwa kwa roketi za Hezbollah kwenda Israel.

Seneta Chris Coons, muungaji mkono wa Biden ambaye hushiriki katika Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni na amesafiri kwenda Israel, Misri na Saudi Arabia mwishoni mwa mwaka jana, anasema ni muhimu kuipima diplomasia ya Biden na hali ya mwaka jana.

"Nadhani pande zote mbili zinahusika kwa kutopatikana kwa makubaliano, lakini hatuwezi kupuuza au kusahau kwamba Hamas ndio ilianzisha mashambulizi haya," anasema.

"Amefanikiwa kuzuia chokochoko za kichokozi za mara kwa mara kutoka kwa Wahouthi, na Hezbollah, na wanamgambo wa Shia nchini Iraq - na amewaleta pamoja washirika wetu wa kikanda," anasema.

Waziri mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Olmert anasema uungaji mkono wa Biden umekwenda katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, akiashiria kupelekwa kwa jeshi kubwa la Marekani, ikiwa ni pamoja na meli za kivita zinazobeba ndege na nyambizi ya nyuklia.

Lakini anaamini Biden ameshindwa kuushinda upinzani wa Netanyahu.

"Kila mara alipokaribia kufanikiwa, Netanyahu kwa namna fulani alipata sababu ya kutotii, hivyo sababu kuu ya kushindwa kwa diplomasia hii ni upinzani wa mara kwa mara wa Netanyahu," anasema Olmert.

imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhahiriwa na Seif Abdalla