Mwaka mmoja wa mauaji umeipeleka Mashariki ya Kati kwenye ukingo wa vita vikubwa zaidi

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Vita vinatengeneza upya siasa za Mashariki ya Kati. Mashambulizi ya Hamas yaliuwa watu 1,200, wengi wao wakiwa raia wa Israel. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alimpigia simu Rais Joe Biden na kumwambia “Hatujawahi kuona ushenzi kama huu katika historia ya taifa hilo.”
Israel iliona mashambulizi ya Hamas kuwa tishio kwa uwepo kwake. Tangu wakati huo, Israel inashambulia Gaza. Takriban watu 42,000, wengi wao wakiwa raia wameuawa, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas. Sehemu kubwa ya Gaza ni magofu. Wapalestina wanaishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki.
Miezi kumi na miwili baada ya Hamas kufanya shambulizi hilo, sasa Mashariki ya Kati iko kwenye ukingo wa vita vibaya zaidi, vipana zaidi, na viharibifu zaidi.

Chanzo cha picha, EPA
Viongozi wa Marekani na Uingereza, na wengine, walikuwa wamejiaminisha kuwa Netanyahu, licha ya kupinga taifa la Palestina katika maisha yake yote ya kisiasa, angeweza kwa namna fulani kushawishika kukubali kukomesha vita.
"Mapatano makubwa" ya Rais Biden yalipendekeza kwamba Israeli itatambuliwa kamili kidiplomasia na Saudi Arabia, nchi yenye ushawishi mkubwa, kama malipo ya kuruhusu taifa la Palestina.
Mpango wa Biden ulikumbwa na kizingiti. Netanyahu alisema mwezi Februari kwamba nchi kwa Palestina itakuwa "malipo makubwa" kwa Hamas. Bezalel Smotrich, mmoja wa Mawaziri wenye misimamo mikali, “alisema itakuwa "tishio kwa Israel.”
Kiongozi wa Hamas, Yahya Sinwar, alijidanganya pia. Huenda alikuwa na matumaini kwamba "mhimili wa upinzani" ingejiunga, kwa nguvu zote, katika vita vya dhidi ya Israel. Alikosea.
Sinwar aliweka mipango yake ya kushambulia Israel tarehe 7 Oktoba siri sana. Aliwashangaza wengi. Vyanzo vya kidiplomasia viliiambia BBC Sinwar hata hakuwaambia mipango yake viongozi wa kisiasa wa shirika hilo walio uhamishoni nchini Qatar.
Iran iliweka wazi kuwa haitaki vita vikubwa zaidi na Rais Biden akaamuru vikosi vya wanajeshi wa Marekani kusogea karibu ili kuilinda Israel.
Badala yake, Hassan Nasrallah kupitia kundi lake la Hezbollah walifanya mashambulizi ya kiasi kwa makombora kwenda kaskazini mwa Israel, na wakasema wataendelea hadi mapigano yasitishwe Gaza.
Israeli ilihamisha zaidi ya watu 60,000 mbali na mpaka. Huko Lebanon, watu wengi zaidi walilazimika kukimbia makazi yao vilevile.

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kisha Israel ilizindua moja ya mashambulizi makali zaidi katika vita vya sasa. Ililipua na kuharibu mawasiliano ya Hezbollah na kuwaua viongozi wake. Katika siku yake ya kwanza Israel iliua takriban watu 600 huko Lebanon, wakiwemo raia wengi.
Tarehe 27 Septemba, shambulio kubwa la anga kwenye kitongoji cha kusini mwa Beirut lilimuua Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hezbollah na wengi wa manaibu wake wakuu.
Israel ilitoka kwenye vita vya mpaka na kuingia Lebanon. Ikiwa na nia ya kimkakati ya kuilazimisha Hezbollah kusitisha mapigano na kurudi nyuma kutoka kwenye mpaka.
Siku ya Jumanne tarehe 1 Oktoba, Iran iliishambulia Israel kwa makombora ya balistiki.
Viongozi wa Hamas hawakubali kwamba mashambulizi dhidi ya Israel yalikuwa ni makosa. Nchini Qatar, saa moja au zaidi kabla ya Iran kushambulia Israel tarehe 1 Oktoba, nilimhoji Khalil al-Hayya, kiongozi mkuu wa Hamas nje ya Gaza, wa pili katika shirika lao baada ya Yahya Sinwar.
Alikanusha kuwa watu wake waliwalenga raia - licha ya ushahidi mwingi - na alihalalisha mashambulizi kwa kusema ni muhimu kuyaweka masaibu ya Wapalestina kwenye ajenda ya kisiasa ya dunia.

Chanzo cha picha, Oren Rosenfeld
Israeli ilihisi pigo, tarehe 7 Oktoba, Benjamin Netanyahu alitoa hotuba akiahidi "kisasi kikubwa." Aliweka malengo ya vita kuwa ni kuwaondoa Hamas kama jeshi na vuguvugu la kisiasa na kuwarudisha mateka nyumbani.
Waziri Mkuu anaendelea kusisitiza "ushindi kamili" unawezekana, na ushindi huo hatimaye utawakomboa Waisraeli wanaoshikiliwa na Hamas kwa mwaka mmoja.
Wapinzani wake wa kisiasa, wakiwemo jamaa wa mateka, wanamshutumu kwa kuzuia usitishaji mapigano ili kuwaridhisha wana siasa wenye siasa kali za kizalendo katika serikali yake. Anashutumiwa kwa kuweka mbele uhai wake wa kisiasa badala ya maisha ya Waisraeli.
Uchambuzi wa picha za satelaiti kutoka kwa wasomi wa Marekani Corey Scher na Jamon Van Den Hoek unasema 58.7% ya majengo ya Gaza yameharibiwa.
IDF imeteua eneo la pwani - al-Mawasi - kusini mwa Gaza kama eneo la kibinadamu. Eneo hilo bado hupigwa mabomu. BBC imepata mashambulio 18 ya anga ndani ya eneo hilo.
Hakuna anayeweza kutilia shaka dhamira ya Israel ya kutetea watu wake. Hata hivyo, ni wazi kwamba vita hivyo vimeonyesha kwamba hakuna mtu anayeweza kujidanganya kuwa Wapalestina watakubali maisha ya kuishi milele chini ya uvamizi wa kijeshi wa Israel, bila haki na uhuru wao.

Chanzo cha picha, Maxar
Baada ya Hamas kushambulia Israel, hofu ilikuwa kwamba vita vitaenea. Polepole, na kisha haraka sana, vikaenea, baada ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Hezbollah na Lebanon.
Mashariki ya Kati iko ukingoni mwa vita vikubwa. Israel inakabiliana na Iran. Ninavyoandika Israel bado haijalipiza kisasi kwa shambulio la kombora la balistiki la Iran tarehe 1 Oktoba. Israel imebainisha kuwa inakusudia kutoa adhabu kali.
Iwapo Iran itajibu kulipiza kisasi kwa Israel kwa wimbi jingine la makombora ya balistiki huenda nchi nyingine zikaingia pia. Nchini Iraq, wanamgambo wa Iran wanaweza kushambulia maslahi ya Marekani. Wanajeshi wawili wa Israel waliuawa na ndege isiyo na rubani iliyotoka Iraq.
Kipaumbele cha wale wanaotaka kusitisha vita hivi kinapaswa kuwa usitishaji vita huko Gaza. Ni nafasi pekee ya kutuliza mambo na kutengeneza nafasi kwa diplomasia. Vita vilianza Gaza na vinaweza kuishia hapo hapo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












