Furaha na hofu: Hali nchini Iran baada ya kuishambulia Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Staff reporters
- Nafasi, BBC News Persian
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Siku ya Jumanne usiku, wakati anga ya Iran ilipong'aa kwa mwanga wa makombora yaliyorushwa kuelekea Israel, Wairani walikuwa na hisia mchanganyiko – wale walio furahi, wenye hofu, na kutokuwa na uhakika.
Ndani ya dakika chache, machapisho katika mitandao ya kijamii nchini kote yalipambwa na video za roketi zikipaa juu.
Mashambulizi hayo yameongeza mivutano iliyopo katika nchi ambayo tayari inakabiliana na matatizo ya kiuchumi, machafuko ya kisiasa na mgawanyiko wa kijamii.
Televisheni ya taifa ya Iran ilionyesha makundi ya watu wakishangilia barabarani, wakipeperusha bendera na kuimba “Kifo kwa Israel!”.
Lakini kwenye mitandao ya kijamii, hali ilikuwa tofauti - sio kila mtu aliunga mkono shambulio hilo dhidi ya Israel.
Baadhi ya watu walikuwa na wasiwasi juu ya uwezekano wa kuanza kwa vita vikubwa zaidi. Baadhi ya Wairani wanasema: "Mara hii hali ni tofauti."
Siku ya Alhamisi, hatua za kidiplomasia ziliendelea, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alikwenda nchini Qatar kwa siku mbili. Kwa mujibu wa ripoti, ujumbe wake kwa Marekani kupitia Qatar – ulibeba onyo kwamba Iran itaishambulia zaidi Israel iwapo kutakuwa na mashambulizi makubwa.
Kiongozi huyo wa Iran pia atakutana na maafisa mbalimbali wa Ghuba, akiwemo waziri wa mambo ya nje wa Saudia.
Furaha na hofu

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa wafuasi wengi wa serikali, shambulio hilo linawakilisha wakati wa kujivunia na kuonesha upinzani: “Heko kwa [Kiongozi Mkuu wa Iran Ali] Khamenei! Heko kwa Walinzi wa Mapinduzi!” Alisema mwanamke kijana kwenye video iliyosambaa.
Kwake yeye, mashambulio dhidi ya Israel ni onyesho la uwezo na nguvu ya Iran katika kanda.
Lakini hisia yaikuwa ya furaha pekee, kulikuwa na hisia nyingine ya hofu katika mtandao: “Tafadhali tofautisha kati ya watu wa Iran na Walinzi wa Mapinduzi; tuko chini ya shinikizo kubwa,” alisema mwanaume wa makamo katika video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Baadhi ya Wairani waliona shambulio hilo ni uchokozi usio wa lazima ambao utasababisha tu mateso kwao kuwa mabaya zaidi. Wanahofia hatua hii ya kulipiza kisasi itawaongezea matatizo ya kila siku yanayochangiwa na miaka ya vikwazo vya kiuchumi, mfumuko wa bei na kuporomoka kwa sarafu.
"Hatuna la kufanya ila kulinda nchi yetu, lakini sisi ndio tunapata madhara," mkazi wa mji mkuu, Tehran, alisema kwa wasiwasi.
Saa chache baada ya shambulio hilo, uvumi uliibuka kuwa Israel huenda ikajibu kwa kulenga miundombinu ya mafuta ya Iran, ambayo ni sehemu muhimu ya uchumi wa nchi hiyo.
Video ziliibuka zikionyesha vituo vya mafuta vikiwa vimesheheni watu, huku misururu mirefu ya watu wakikimbilia kujaza matangi yao, wakihofia uhaba wa mafuta.
Diplomasia yanafifia
Shambulio hilo la kombora limekuja wakati ambapo kumekuwa na matumaini kuhusu diplomasia. Kuchaguliwa kwa Masoud Pezeshkian kama rais mpya kumeleta matumaini miongoni mwa wale wenye misimamo ya wastani. Baadhi ya watu walimwona kama daraja la kupunguza mivutano ya kikanda.
Hata hivyo, mashambulizi ya makombora ya siku ya Jumanne yamepunguza matumaini ya diplomasia. "Shambulio hili ni hatua nyingine mbali na diplomasia, ni hatua ya kuelekea kwenye migogoro," alisema mtazamaji mmoja wa BBC Kiajemi.
"Ninahofu vita hivi vinaweza kutumika kama kisingizio cha kuzidisha ukandamizaji kwetu, wakati huu ambapo tunapigania uhuru," mwanaharakati kijana alisema - akimaanisha maandamano ya Mwanamke, Maisha, Uhuru ambayo yamebadilisha kwa kiasi kikubwa hali ya kijamii ya Iran.
Wengi wana wasiwasi kwamba mzozo mpya hauwezi tu kudhoofisha wito wa mageuzi, lakini pia kuipa serikali uwezo wa kukandamiza zaidi upinzani wa ndani.
Tofauti na mizozo ya huko nyuma, wakati huu kuna hofu ya uwezekano wa mashambulizi makubwa kutoka Israel. Wengi wanaamini uwezo wa hali ya juu wa jeshi la Israel unaweza kuleta uharibifu mkubwa ikiwa vita vikubwa vitazuka.
"Hakuna anayetaka vita, si watu wala viongozi," alisema mchambuzi kwenye mtandao wa kijamii.
Mabadiliko ya utawala au ulinzi wa taifa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Katikati ya mvutano unaoongezeka, baadhi ya watu wametoa wito wa mabadiliko ya utawala. "Njia pekee ya kuiokoa Iran sio kupitia vita, lakini ni kwa njia ya kuangusha utawala wa sasa," alisema mtazamaji mwingine wa BBC Kiajemi, na kuzitaka Magharibi kuunga mkono Wairani katika mapambano yao dhidi ya serikali.
Hata hivyo, wengi wanaamini mustakabali wa nchi hiyo unapaswa kuamuliwa ndani, bila kuingiliwa kati - ili kuepusha machafuko yanayoweza kusababisha kuingiliwa kutoka nje.
Mashambulizi ya makombora ya Iran dhidi ya Israel yamezidisha mgawanyiko ndani ya nchi hiyo. Upande mmoja ni wale wanaounga mkono hatua za serikali kwa fahari ya utaifa, huku upande mwingine ni wale wanaoogopa vita, kuporomoka kwa uchumi, na kukandamizwa kwa harakati za mageuzi ya ndani.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












