Jinsi upelekaji wa mfumo wa ulinzi wa Thaad Israel unavyozidi kuiingiza Marekani katika vita kati ya Israel na Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani inaongeza ushiriki wake katika mzozo kati ya Israel na Iran.
Washington ilisema itapeleka mfumo wa kukabiliana na makombora na wanajeshi kwa Israeli kusaidia ulinzi wake wa anga baada ya nchi hiyo kushambuliwa kwa makombora na Iran mwezi Oktoba 1.
Taarifa ya Pentagon ilisema Rais Joe Biden ameamuru kutumwa kwa mfumo wa Ulinzi wa Anga wa Terminal High Altitude (THAAD) na jeshi kuuendesha ili "kuilinda Israeli."
Mwezi Oktoba 1, Iran ilirusha makombora 200 ya balestiki huko Israeli. Ingawa jeshi la Israel liliripoti kwamba mengi ya makombora hayo yalizuiliwa, baadhi yao yakipiga katikati na kusini mwa nchi hiyo.
Israel bado haijathibitisha jinsi itakavyojibu, lakini Waziri wake wa Ulinzi Yoav Gallant ametangaza kwamba jibu litakuwa "la mauti, sahihi na, zaidi ya yote, la kushangaza."
Tehran kwa upande wake imesema pia itajibu shambulizi la Israel.
Tangazo la Washington linakuja huku kukiwa na wasiwasi wa ongezeko hili.
Je, usafirishaji wa mfumo wa Thaad kwenda Israel una maana gani?
Pentagon ilisema kutumwa kwa Thaad "kunasisitiza dhamira isiyoyumbayumba ya Marekani ya kuilinda Israeli na kuwalinda Wamarekani huko Israeli dhidi ya shambulio lolote la ziada la makombora kutoka Iran."
Marekani ilikuwa tayari imetuma mfumo huo wa kujilinda na makombora Mashariki ya Kati baada ya shambulio la Hamas dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7. Mnamo 2019, ilituma mfumo huo kwa Israeli kwa zoezi la ulinzi dhidi ya ndege.
Mfumo wa Thaad ni nini na unatumika kwa nini?
Mfumo wa Thaad ni mfumo wa ulinzi dhidi ya ndege ulioundwa ili kunasa makombora ya masafa mafupi na ya kati katika awamu ya mwisho ya safari yao.
Unatumia teknolojia ya hit-to-kill, ambapo nishati ya kinetic makombora yanayowasili.
Ukiwa na uwezo wa kuruka hadi kilomita 200, makombora yake ya kukatiza yanaweza kusafiri umbali wa kilomita 150 / h.
Ulianza kufanya kazi tangu 2017, mfumo huo hapo awali ulikuwa umewekwa na Marekani huko Guam, Hawaii na Korea Kusini kama jibu la uwezekano wa shambulio la Korea Kaskazini.

Chanzo cha picha, Getty Images
Tulifikaje hapa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Iran imesema mashambulizi yake dhidi ya Israel ni kujibu mauaji ya kiongozi wa Hezbollah nchini Lebanon Hassan Nasrallah na kamanda mkuu wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran mjini Beirut na kiongozi wa Hamas huko Palestina Ismail Haniya mjini Tehran, yanayodaiwa kutekelezwa na Israel lakini serikali yake haijathibitishi wala kukanusha.
Israel imeongeza kwa kiasi kikubwa kasi ya mshambulizi yake dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon katika wiki za hivi karibuni, ikifanya mashambulizi mabaya kusini na mashariki mwa nchi hiyo, na pia katika mji mkuu, Beirut.
Israel na Hezbollah zimekuwa zikikabiliana tangu Oktoba mwaka jana, wakati wanamgambo wa Lebanon walipoanza kufyatulia risasi Israel kwa kile walichokionyesha kuwa wanaunga mkono Wapalestina huko Gaza.
Utawala wa Biden umeitaka Israel kujizuia katika mashambulizi yake ya kijeshi huko Gaza na kutaka kuwalinda raia wa Palestina, lakini wakati huo huo imesisitiza ahadi yake ya "haki ya kujilinda" ya Israel na imeendelea kutuma zana za kijeshi.
Marekani imekuwa na mzozo wa muda mrefu na Iran na ilisaidia kujibu shambulio la kwanza la Iran dhidi ya Israel mwaka huu.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












