Uchaguzi Uganda 2026: Waganda wengi ni vijana – Watamchagua Mzee wa miaka 81?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Sammy Awami
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Iwe wamevaa rangi ya manjano ya chama tawala au wamevaa rangi nyekundu ya chama kikuu cha upinzani, vijana ndio wanaongoza miongoni mwa wafuasi katika kampeni za uchaguzi nchini Uganda.
Katika viwanja vya umma vilivyojaa watu na mikusanyiko ya kando ya barabara, wafuasi vijana wanaoimba nyimbo za chama na kupiga picha kwenye simu zao, ndio wengi kuliko watu wengine wote.
"Bobi Wine ni mtu mzuri. Akiingia madarakani, naamini ataipeleka nchi katika hatua fulani katika suala la maendeleo. Tunahitaji tu kumwamini na kumruhusu aoneshe uwezo wake," Steven Bagasha Byaruhanga ameiambia BBC katika mkutano wa hadhara uliojaa wafuasi wa upinzani katika kijiji kimoja kusini-magharibi mwa Uganda.
Ingawa Ndyasima Patrick anaunga mkono chama tawala, pia alikuwepo kwenye mkutano huo, labda ili kusikia kile Bobi Wine anachosema. Lakini Patrick hakushawishika.
"Namuunga mkono Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi huu kwa sababu ametuweka hai miaka hii yote. Huenda amekuwa madarakani kwa muda mrefu lakini hatujapata anayefaa bado. Bobi Wine anaonekana anafaa lakini huu sio wakati wake bado, labda 2031," anasema.
Uchaguzi wa rais wa Alhamisi ni marudio ya kinyang'anyiro cha 2021 ambapo Museveni mwenye umri wa miaka 81, aliye madarakani kwa miongo minne, akipambana tena na nyota wa zamani wa muziki, Bobi Wine mwenye umri wa miaka 43, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi.
Shauku kubwa katika kampeni hii ni ukumbusho kwamba katika nchi ambayo umri wa wastani ni miaka 17 tu, siasa husukumwa sana na vijana.
Miaka arobaini iliyopita, Ronald Reagan na Margaret Thatcher walipokuwa wanasiasa wenye ushawishi, Diego Maradona alipoinua Kombe la Dunia kwa ajili ya Argentina, Whitney Houston alitamba sana na kibao chake cha The Greatest Love of All na kiongozi wa waasi Yoweri Museveni alichukua madaraka nchini Uganda.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa Waganda wengi, watu hao wako tu katika kumbukumbu za wazazi wao lakini Museveni anabaki kuwa rais pekee wanayemjua.
Chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) kinafanya kampeni chini ya kauli mbiu "Kulinda Kilichopatikana," kikihimiza mwendelezo wa utulivu.
"Tazama Uganda - miaka 40 iliyopita, tulikuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa wakimbizi katika nchi zote jirani zinazotuzunguka. Hivi sasa, Uganda ndiyo inahifadhi wakimbizi wengi kutoka barani Afrika," msemaji wa NRM Emmanuel Lumala Dombo anaiambia BBC, huku akiorodhesha mafanikio ambayo chama chake kinayatetea.
Kwa upande mwingine, Chama cha National Unity Platform (NUP) cha Bobi Wine, kinavutia wapiga kura kwa kauli mbiu "Kura ya Maandamano," ujumbe unaosisitiza uharaka wa mabadiliko ya kizazi.
"Uchaguzi huu unahusu ukombozi, unahusu uhuru, unahusu watu kupaza sauti zao," anasema Bobi Wine, ambaye amekuwa mwanasiasa maarufu kwa vijana waliokata tamaa.
Miito ya vyama vyote viwili inalenga hadhira ile ile, vijana, lakini vinafikiria mustakabali wa Uganda kwa njia tofauti kabisa.
Museveni anatafuta muhula wa sababa mfululizo madarakani.
Uganda ni mojawapo ya nchi yenye vijana wengi zaidi duniani, lakini mfumo wake wa kisiasa unatawaliwa na viongozi walioingia madarakani miongo kadhaa iliyopita na hawajawahi kuondoka.
Mvutano huu si Uganda pekee

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika nchi nyingi Afrika, vijana wanatawaliwa na wazee ambao wamefanikiwa kuondoa ukomo wa madaraka kupitia katiba na kukwepa shinikizo la kisiasa la kujiuzulu.
Wingi wa vijana nchini Uganda ndio rasilimali kubwa na hatari inayobadilika-badilika.
Kila mwaka, maelfu ya vijana huingia katika soko la ajira, lakini wanashindwa kuajiriwa kutoka na uchumi mbovu.
Fursa za kubadilisha hali ya mambo, hukumbana na udhibiti. Maandamano mara nyingi hukumbana na kukamatwa, vitisho na vurugu - jibu ambalo limeongeza hasira badala ya kutoweka.
Kote barani Afrika, vijana hawana tena subra ya kimya kimya.
Katika nchi jirani ya Kenya, maandamano yanayoongozwa na vijana dhidi ya utawala na ugumu wa kiuchumi yametikisa taasisi za kisiasa.
Nchini Tanzania, ambayo kwa muda mrefu ilichukuliwa kuwa imedhibitiwa kisiasa, aina mpya za harakati zinaibuka na maandamano kuhusu uchaguzi wa mwaka jana yaliwaacha wengi wakiwa wamekufa.
Msumbiji imepitia machafuko yaliyochochewa na ukosefu wa ajira na ukosefu wa usawa.
Na huko Madagascar, jeshi lilichukua madaraka mwaka jana baada ya maandamano yaliyoongozwa na vijana kusababisha rais kukimbia.
Matukio haya yanafuatiliwa kwa karibu nchini Uganda, na wanaharakati vijana, na serikali iliyoazimia kuzuia machafuko kama hayo.
Kutokana na hali hii, waangalizi wengi wanaona uchaguzi wa Alhamisi si wa kutafuta uhalali wa kisiasa wa kukaa madarakani bali ni kama operesheni ya usalama inayolenga kudhibiti upinzani.
Wataalamu wanasemaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Fergus Kell, mtafiti katika taasisi ya fikra tunduizi ya Chatham House yenye makao yake makuu London, ameandika kuhusu siasa "zinazoendeshwa kijeshi" ambapo NRM imetumia "mifumo ya serikali kulinda mamlaka yake kwa kukandamiza vyama mbadala kutoshika madaraka."
Museveni anatarajiwa kushinda kwa wingi. Historia ya uchaguzi wa Uganda, waangalizi huukosoa mara kwa mara jinsi usivyokuwa huru na wa haki, na inaonyesha kwamba hakutokuwa na matokeo tofauti mwaka huu.
Wiki iliyopita, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema uchaguzi huo "utafanyika katika mazingira yaliyojaa ukandamizaji na vitisho dhidi ya upinzani, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wale wenye maoni tofauti."
Profesa kutoka Uholanzi, Kristof Titeca anasema “ushindani kwa njia za kidemokrasia" unaonekana lakini "matokeo yake tayari yamepangwa mapema."
Wengi wanadai kwamba uchaguzi wa mwaka huu umeshuhudia vurugu chache kuliko ule wa mwisho ambapo angalau watu 54 walifariki.
Sababu moja inaweza kuwa uchaguzi wa 2021 ulifanyika wakati wa janga la Covid-19, wakati huo serikali ilitekeleza vikwazo vikali zaidi.
Zaidi ya kambi mbili zinazoongoza, vyama kadhaa vidogo vya upinzani pia vinagombea, ingawa havina ushawishi mkubwa.
Miaka mingi ya mgawanyiko wa ndani imeviacha vyama hivi vikipambana, ingawa hakuna uwezekano wa kubadilisha matokeo ya kinyang'anyiro cha urais, vyama hivi vinaendelea ushindana katika matawi ya chini na bunge.
Hata hivyo, kwa wapiga kura wengi wachanga, vyama hivi vya upinzani vya kitamaduni vinaonekana kama sehemu ya enzi ya siasa za awali, haviwezi kuongoza uhitaji na makabiliano ya wakati huu ya vijana.
Baada ya Museveni

Chanzo cha picha, Reuters
Zaidi ya matokeo yanayotabirika, uchaguzi wa Januari unaangazia swali la msingi zaidi: Nini kitatokea baada ya Museveni?
"Hakuna jawabu moja la uhakika. Mambo mengi yanaweza kutokea," aliandika mmoja wa waandishi wa habari wenye uzoefu mkubwa nchini Uganda, Charles Onyango-Obbo, miaka mitatu iliyopita, alipokuwa akizungumzia enzi ya baada ya Museveni.
Uvumi kuhusu mipango ya kustaafu ya Museveni umeanza miaka 25 iliyopita.
"Tangu mwaka 2001. Lakini kila dalili ya kuondoka imefuatiwa na marekebisho ya katiba ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa mipaka ya mihula ya urais na mipaka ya umri - mageuzi ambayo yamemwezesha kubaki madarakani kwa muda usiojulikana," anasema mchambuzi wa siasa Monday Akol Amazima.
Katikati ya haya ni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mwanawe Museveni, ambaye umaarufu wake unaoongezeka na kuzusha maswali kuhusu mrithi wa Museveni.
Baada ya kuchukua uongozi wa vikosi vya nchi kavu mwaka 2021, kupanda kwa Jenerali Kainerugaba kuliongezeka kwa kasi.
Mwaka 2022, alizunguka nchi nzima katika mfululizo wa sherehe za "siku ya kuzaliwa" zilizopangwa kwa mtindo wa kipekee ambazo zilitumika kama mikutano ya kisiasa, kabla ya kuzindua chama cha Patriotic League of Uganda, chama ambacho kinaonekana ni kama uwanja wa majaribio kwa matarajio yake ya kisiasa ya siku zijazo.
Licha ya uvumi kwamba angombea urais mwaka huu, baadaye alitangaza kumuunga mkono baba yake. Hata hivyo, ujumbe wake unaendelea kumfanya awe kiongozi anayesubiriwa.
Matarajio hayo yalizidi kuwa makubwa Machi 2024, wakati Jenerali Kainerugaba alipoanzisha mabadiliko makubwa ndani ya vyeo vya juu vya jeshi.
Kwa kupanga upya muundo wa amri na kuboresha marupurupu ya kustaafu, aliashiria upanuzi wa mamlaka yake na juhudi za kuyalinda, akipunguza upinzani huku akiwapa wafuasi wake nafasi za kimkakati katika vyombo vya usalama.
Hata hivyo, msemaji wa NRM Dombo anapuuza mapendekezo kwamba Museveni anamlea mwanawe kama mrithi.
Anasisitiza kwamba chama kina michakato ya ndani iliyo wazi ya urithi wa uongozi, akiongeza kwamba ikiwa Jenerali Kainerugaba angeonyesha nia ya kugombea nafasi ya kisiasa kupitia NRM, angehitajika kufuata njia zilizowekwa.
"Ikiwa Jenerali Muhoozi angependa kutumia fursa kama kiongozi wa kijeshi, anapaswa pia kujua kwamba kuna mambo mengine ambayo lazima ayathibitishe," Dombo anasema.
Kwa upande wake, Bobi Wine bado ana shaka kwamba Museveni anajiandaa kujiuzulu.
Anafanana na Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe, ambaye aling'ang'ania madaraka hadi miaka yake ya 90 kabla ya kuondolewa madarakani na jeshi.
"Kama vile Mugabe, na madikteta wengine wote. Hatajiuzulu, naweza kukuhakikishia. Kwa sababu anaamini nchi hii ni yake na familia yake," kiongozi huyo wa upinzani anasema.
Kutokana na hali hiyo, uchaguzi umechukua umuhimu ambao unaenea zaidi ya wagombea binafsi.
Ni kama kura ya maoni kuhusu kulinda utaratibu ulioanzishwa unaotokana na mafanikio ya kihistoria au kujibu matakwa ya kizazi kipya kuhusu ujumuishaji, usawa na ushiriki wenye maana katika maisha ya umma.
Kinachoonekana wazi ni kwamba vijana wa Uganda si waangalizi tena.















