Museveni akiri wanaharakati wa Kenya walikamatwa Uganda

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Uganda Yoweri Museveni kwa mara ya kwanza amekiri kwamba wanaharakati wawili wa Kenya waliotoweka nchini mwake kwa muda wa wiki tano walikuwa wamekamatwa.
Mwezi uliopita, mashuhuda waliripoti kuwaona Bob Njagi na Nicholas Oyoo wakilazimishwa kuingia kwenye gari na watu ambao waliovalia sare baada ya tukio la kisiasa ambapo walikuwa wakimuunga mkono kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine.
Habari za kutekwa kwao zilithibitishwa Jumamosi lakini hadi kufikia wakati huo mamlaka ilikuwa imekanusha kuwa wanazuiliwa.
Katika mahojiano ya moja kwa moja Jumamosi jioni, Museveni aliwataja wanaharakat hao wawili kama "wataalamu wa ghasia" ambao walikuwa wamefungiwa kwenye ''jokofu kwa siku kadhaa.''
Museveni alikuwa akijibu swali kuhusu maandamano yaliyoongozwa na vijana katika taifa jirani la Tanzania.
Rais huyo ambaye ameongoza Uganda kwa miongo minne aliyashutumu makundi ya kigeni kwa kuchochea ghasia na kusema "wale watakaofanya mchezo huo hapa Uganda watakiona cha mtema kuni".
Bila ya kutaja majina, aliongeza kuwa wanaharakati wawili wa Kenya waliachiwa huru baada ya kupigiwa simu na "baadhi ya viongozi wa Kenya" waliokuwa wakisinikiza kuachiwa kwao.
Siku ya Jumamosi, shirika la Vocal Africa lilithibitisha kuwa wanaharakati hao wawili walikuwa salama, na kwamba wako safarini kutoka Busia nchini Uganda kuelekea mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
"Wacha wakati huu uashirie mabadiliko muhimu katika udumishaji wa haki za binadamu katika eneo la Afrika Mashariki mahali popote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki," shirika hilo liliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram.
Pia unaweza kusoma:







