Kwa nini misukosuko ya ndege inaongezeka? Kuna suluhisho?

Chanzo cha picha, Getty Images
"Tuliona damu na uharibifu." Haya yalikuwa maelezo ya abiria mmoja kuhusu tukio la ndege ya Shirika la Ndege la Singapore kukumbwa na misukosuko mikali ilipokuwa ikipita kusini mwa Myanmar mwaka 2024.
Mapema msimu huu wa machipuo, ndege ya United Airlines Boeing 787 pia ilikumbana na msukosuko mkubwa ilipokuwa ikisafiri juu ya Ufilipino. Mhudumu wa ndege alitupwa, na kusababisha kuvunjika mkono.
Matukio ya msukosuko kama haya yanaongezeka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na binadamu. Hali mbaya ya hewa ambayo haionekani kwa satelaiti, rada na jicho la mwanadamu, imeongezeka kwa 55% tangu 1979 - pale rekodi za kuaminika za hali ya hewa zilipoanza, kulingana na utafiti wa Paul Williams, profesa wa sayansi ya anga katika Chuo Kikuu cha Reading.
Hali mbaya ya hewa inatarajiwa kuongezeka mara tatu duniani kote kufikia miaka ya 2050 na kuna uwezekano kuwa na athari kubwa kwa Asia Mashariki na Atlantiki ya Kaskazini.
Kuna suluhisho?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbali na misukosuko ya ndege kuwa hatari, pia hugharimu sekta ya usafiri wa anga pesa, na kusababisha uchakavu wa ndege na kuongeza muda wa safari za ndege huku marubani wakijaribu kukwepa hali mbaya ya hewa. Juhudi hizo, hunamaanisha matumizi zaidi ya mafuta na kuongeza uzalishaji wa hewa chafu.
Kampuni ya Turbulence Solution, ilioko Baden, Austria, imetengeneza "mabamba" madogo ambayo huongezwa kwenye mabamba makubwa kwenye mabawa ya ndege. Mabamba haya yaliyopo katika kingo za mbawa, husaidia kuleta utulivu wa ndege, kama jinsi ndege wanavyotumia manyoya yao madogo wanaporuka.
Kampuni hiyo inasema teknolojia yake inaweza kupunguza misukosuko kwa zaidi ya 80%. Kufikia sasa teknolojia hiyo imejaribiwa tu kwenye ndege ndogo, lakini lengo ni kutumika pia katika ndege kubwa.
Mwaka jana, timu kutoka kampuni ya teknolojia ya Caltech and Nvidia ilitumia mtikisiko wa upepo ili kufanya majaribio mfumo wa akili mnemba wa kutambua na kutabiri mabadiliko ya hali ya hewa kwa ndege zisizo na rubani. Na matokeo yalikuwa mazuri.
Nao watafiti katika Kituo cha Utafiti cha Langley cha Nasa walifanyia majaribio maikrofoni iliyoundwa kunasa frekwensi zinazotokana na hali mbaya ya hewa kutoka umbali wa hadi maili 300 (480km).
Mbinu nyingine ambayo imekuwa ikiendelezwa tangu 2010 inahusisha matumizi ya ramani ya anga ya 3D kuzunguka ndege, kama vile magari yanayojiendesha ambayo yanaunda ramani ya vitu au magari yaliyo karibu, ili kukwepa kuvigonga.
Hali ya sasa

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Muunganiko wa akili mnemba, vinasa hisia na ubunifu mwingine -yanaweza kubadilisha safari za anga katika nusu ya pili ya Karne ya 21. Lakini ni nini kinachotokea leo?
Kabla ya kupaa, marubani huangalia muhtasari wa utabiri wa hali ya hewa na njia ya ndege. Wanatumia programu ya kupanga safari za ndege na kuangalia utabiri.
“Takriban miaka 20 iliyopita tumeweza kutabiri karibu 60% ya misukosuko, leo ni kama 75%,” anasema Williams.
Kwa hesabu ya hali ya juu, AI na setilaiti zinazoendelea zaidi, utabiri wa hali ya hewa unaboreka, lakini kuna ukosefu jumla wa vipimo vya upepo juu ya uso wa Dunia.
Tunachojua kwa sasa hutoka katika puto 1,300 za hali ya hewa zinazozunguka sayari na taarifa kutoka takriban ndege 100,000 za kibiashara zinazoingia angani kila siku.
Turbulence Aware kutoka Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IATA) husambaza data juu ya hali mbaya ya hewa na sasa data hizo zinatumiwa na mashirika ya ndege yakiwemo Air France, EasyJet na Aer Lingus.
Kwa abiria, kuna idadi inayoongezeka ya programu zinazotoa data ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zinaonekana tu na marubani na watoa huduma, mojawapo ikiwa ni Turbli.















