Kiongozi wa Iran akiri maelfu ya watu kuuawa wakati wa maandamano

Chanzo cha picha, Iranian leader press office via Getty Images
Kiongozi mkuu wa Iran kwa mara ya kwanza amekiri hadharani kwamba maelfu ya watu waliuawa, “baadhi yao kwa njia isiyo ya kibinadamu na ya kikatili,” wakati wa maandamano ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa shirika la Iran Human Rights Activists News Agency (HRANA) lenye makao yake Marekani, ukatili dhidi ya maandamano nchini Iran umesababisha vifo vya watu 3,090.
Machafuko hayo yalianza tarehe 28 Desemba kutokana na hali ya uchumi. Kuzimwa kwa mtandao kumeifanya iwe vigumu sana kupata taarifa sahihi.
Katika hotuba yake siku ya Jumamosi, Ayatollah Ali Khamenei alisema maelfu ya watu waliuawa wakati wa machafuko hayo, akiwalaumu waliowaita “wachochezi wa ghasia.”
Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni aliwahimiza waandamanaji wanaopinga serikali ya Iran “waendelee kuandamana” na akatishia kuingilia kijeshi endapo vikosi vya usalama vitawaua.
Tangu wakati huo, maandamano hayo yamegeuka kuwa wito wa kumaliza utawala wa kiongozi mkuu wa Iran.
Serikali ya Iran imeyataja maandamano hayo kama “ghasia” zinazodaiwa kuungwa mkono na maadui wa Iran.
Waandamanaji wamekabiliwa na nguvu za kikatili zilizosababisha vifo, na video zinazoonesha vikosi vya usalama vikifyatua risasi kwa waandamanaji zimethibitishwa na BBC Persian pamoja na BBC Verify.
Kumekuwa pia na kuzimwa karibu kabisa kwa huduma za mtandao na mawasiliano nchini Iran. Siku ya Jumamosi, muunganisho wa mtandao kwa ujumla ulibaki takriban asilimia 2 tu ya kiwango cha kawaida, kulingana na shirika la ufuatiliaji wa mtandao NetBlocks.
Unaweza kusoma;





