Matokeo ya uchaguzi Uganda 2026: Bobi Wine yuko wapi?

Bobi Wine

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Na Laillah Mohammed
  • Muda wa kusoma: Dakika 2

Polisi nchini Uganda wamekanusha madai kwamba mgombea kiti cha urais nchini humo kwa tiketi ya chama cha National Unity (NUP) Robert Ssentamu Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine Pamoja na mke wake Barbara Kyagulanyi wamekamatwa, na kusisitiza kwamba wapo nyumbani kwao mjini Kampala.

Lakini kiongozi huyo wa upinzani ametoa taarifa akisema alifanikiwa kutoroka wakati wa uvamizi wa vikosi vya usalama Ijumaa usiku, na kwamba hakuwepo tena nyumbani kwake. Hata hivyo alisema mkewe na jamaa wengine bado wako nyumbani chini ya kizuizi cha vikosi vya usalama nyumbani.

Kupitia ujumbe kwenye ukurasa wake wa Facebook siku ya Jumamosi, Wine amesema kwamba jeshi na polisi walivamia nyumbani kwake Magere, ambapo 'walizima umeme na baadhi ya kamera za CCTV', huku helikopta zikizunguka juu ya nyumba yake.

"Nataka kuthibitisha kwamba nilifanikiwa kuwatoroka. Kwa sasa, siko nyumbani, ingawa mke wangu na wanafamilia wengine bado wako chini ya kizuizi cha nyumbani. Najua kuwa wahalifu hawa wananitafuta kila mahali, na ninajaribu niwezavyo kuwa salama," alisema Wine katika taarifa hiyo.

Awali, msemaji wa polisi nchini humo Kituuma Rusoke alisema kwamba maafisa wa usalama wameyazingira makazi ya Bobi Wine kwa sababu ya kisheria kwa kuwa yeye ni mgombea Urais na inawalazimu kuhakikisha usalama wake.

Bobi Wine na wafuasi wake

Chanzo cha picha, Getty Images

Polisi: Madai ya Wine kukamatwa hayana msingi

Polisi wamesisitiza kwamba madai hayo hayana msingi wowote na kwamba Wine yupo nyumbani kwake, mtaani Magere, wilayani Wakiso.

Mapema Jumamosi, Msemaji wa Polisi Kituuma Rusoke alipuuzilia mbali madai hayo na kuyataja kama taarifa za kughushi akisisitiza kwamba japo zimechapishwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, hakuna aliyethibitisha madai hayo kwamba Wine amekamatwa na wala ana zuiliwa na polisi wala jeshi la nchi.

Mtandao wa intaneti umeminywa

Kwa kuwa mtandao wa intaneti umeminywa kabisa nchini Uganda, imekuwa vigumu kuthibitisha madai hayo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hapo awali, Wine alisema kuwa amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani, huku vikosi vya usalama vikizingira makazi yake.

Katika hatua hiyo, msemaji wa polisi Kituuma Rusoke aliliambia shirika la utangazaji la ndani NBS kwamba kama mgombea urais, Wine alikuwa "mtu wa kuangaliwa", na akaongeza kuwa uwepo mkubwa wa usalama kuzunguka nyumba yake ulikuwa kwa usalama wake mwenyewe.

Baadhi ya waandishi wa habari wa ndani walisema kuwa vikosi vya usalama vilikuwa vimewazuia kufika nyumbani kwa kiongozi huyo wa upinzani katika eneo la Magere, jijini Kampala.

Tume ya uchaguzi nchini Uganda inatarajiwa kutangaza matokeo rasmi ya kinyangayiro cha Urais leo Jumamosi.

Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Rais Yoweri Kaguta ameongoza kwa kishindo katika uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi, akiwa mbali mbele ya mpinzani wake mkuu Bobi Wine, ambaye chama chake tayari kimeanza kuhoji uhalali wa matokeo.

Wine pia aliwaambia wafuasi wake wapuuze "matokeo ya uongo" yaliyotangazwa, akisema kuwa mamlaka "zinaiba kura". Hakutoa ushahidi wowote kuhusu madai yake, na mamlaka husika hazijajibu tuhuma hizo.