Je, ni kweli ajali za ndege zimeongezeka?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Joshua Cheetham, Yi Ma & Matt Murphy
- Nafasi, BBC Verify
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakidai kuwa ajali za ndege zimekuwa zikitokea mara kwa mara kufuatia msururu wa majanga yanayotokana na ajali kama hiyo.
Mnamo Desemba 29 2024, 179 walifariki baada ya ndege ya shirika la ndege la Jeju kuanguka alipokuwa ikielekea kutua nchini Korea Kusini. Mwezi mmoja baadaye, helikopta ya kijeshi na ndege ya abiria ziligongana huko Washington, DC, na kusababisha vifo vya watu 67.
Hivi maajuzi, ndege ya shirika la India alianguka muda mfupi baada ya kuanza safari kutoka uwanja wa Ahmedabad, kuwaua watu 261 huku mmmoja akinusurika kifo.
Ingawa hakuna maelezo ya kina kuhusiana na suala hili, uchunguzi wa shirika la habari la Associated Press mwezi wa Februari uliashiria kuwa picha za kushangaza za ajali ya ndege zinazowekwa mitandaoni zimewaathiri baadhi ya wateja wa Marekani mbao wanatilia shaka usalama wa usafiri wa ndege.
Lakini BBC Verify imechambua data nchini Marekani na duniani kote na kubaini kwamba katika miongo miwili iliyopita kumekuwa na mwelekeo wa kushuka kwa ajali za ndege.
Kwa Marekani, takwimu za ajali za ndege zimekusanywa na Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) hadi mwisho wa Januari mwaka huu.
Data hii ya NTSB inaonyesha kupungua kwa jumla kwa ajali za ndege nchini Marekani kutoka 2005 hadi 2024 licha ya ongezeko kubwa la idadi jumla ya safari za ndege katika kipindi hicho. Pia inaonyesha kuwa takwimu za Januari 2025 (52), zilikuwa chini ikilinganishwa na hali ilivyokuwa Januari mwaka jana (58) na Januari 2023 (70).
Takwimu kutoka Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), shirika la Umoja wa Mataifa linalofuatilia matukio ya anga duniani, zinaonyesha kuwa idadi ya ajali duniani kote kwa kila safari milioni moja za ndege pia imeonekana kushuka kwa wazi kati ya 2005 na 2023.
Ufafanuzi wa ICAO wa ajali ya ndege ni pana sana na haujumuishi zile ajali ambazo abiria au wafanyakazi wanajeruhiwa vibaya au kufa, lakini pia matukio ambapo ndege imeharibika na inahitaji kutengenezwa, au inapotea.
Takwimu za idadi ya vifo katika ajali za ndege dunaini pia zinaonyesha kupungua kwa kipindi kama hicho, ingawa kuongezeka kwa miaka kadhaa kunaashiria majanga makubwa ya ajali anga.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwaka 2014, matukio mawili kama haya yalichangia kuongezeka kwa kasi.
Mwezi Machi, ndege ya Malaysia MH370 ailitoweka ilipokuwa safarini kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing aikiwa na abiria 239. Mwezi Julay, ndege nyingine ya er shirika la ndege la Malaysia, MH17, ilidungulia na kombora la Urusi kaskazini mwa Ukraine , na kuwaua watu 300.
Data kama hizi zinatoa mwelekeo unaoashiria mabadiliko makubwa ya ghafla, Prof Sir David Spiegelhalter, Profesa Mstaafu wa Takwimu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, aliiambia BBC Verify.
"Ukihesabu idadi ya vifo badala ya ajali kwa ujumla inakuwa vigumu kupata taswira kamili," alisema.
Kuhusu ajali za kiwango cha juu katika miezi michache iliyopita, Ismo Aaltonen, mkuu wa zamani wa uchunguzi wa maafa yanayotokana na ajali ya ndege nchini Finland, aliiambia BBC Veryfy kuwa sio ishara ya kushuka kwa usalama usafiri wa anga.
"Ilikuwa bahati mbaya tu kwamba kipindi hicho kulishuhudiwa aina nyingi za ajali, lakini watu hawapaswi kuchukulia kuwa ajali zimeongezeka kwa kuzingatia matukio tofauti," alisema.
Alibainisha kuwa baadhi ya matukio katika kipindi cha miezi michache iliyopita yalikuwa yasiyotabirika, akitolea mfano ndege ya Shirika la Ndege la Azerbaijan ambayo ilianguka Kazakhstan mwezi Disemba baada ya kulengwa na kombora la Urusi la kudungua ndege.
Marco Chan, rubani wa zamani na mhadhiri mkuu katika Chuo Kikuu Kipya cha Buckinghamshire, aliiambia BBC Verify kwamba kuongezeka kwa ufahamu wa majanga ya anga kunachochewa ukuaji wa teknolojia ambapo watu wanauwezo wa kuonyesha "ajali ya ndege katika mitandao ya kijamii".
Video moja inayosambaa kwenye mtandao wa TikTok - ambayo imetolewa kutoka kwenye filamu ya Superman - inaonyesha shujaa huyo akizuia ndege kugonga uwanja. Kuna klipu ya maelezo mafupi: "Pete Buttigieg kila siku katika miaka minne iliyopita, kwa kuzingatia matukio ya sasa." Klipu hiyo inaashiria kuwa ajali za ndege anga zimeongezeka tangu waziri wa zamani wa uchukuzi wa Marekani alipoondoka madarakani mwezi Januari.
Msururu wa matukio katika miaka ya hivi karibuni yanayohusu ndege ya Boeing 737 Max pia yamevutia hisia kubwa kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii, haswa baada ya mlango kulipuka katikati ya safari ya ndege mnamo Januari 2024.
Wasiwasi uliotokana na hali hiyo na matukio mengine yalisababisha baadhi ya wateja wakisusia ndege zinazotengenezwa na Boeing na kuporomoka kwa bei ya hisa za kampuni hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wataalam waliambia BBC Veryfy kwamba matukio kama haya na ajali kubwa huchunguzwa kwa kina na mamlaka. Maelezo na data mpya kutoka kwa ajali hutolewa kupitia vifaa vya maigizo kwa marubani ili viweze kujiandaa kwa matukio kama hayo katika siku zijazo.
"Ukiangalia vifaa hivyo, utaona jinsi vilivyo na ubora wa hali ya juu, zina muonekano kama wa ndege ya kweli," alisema Ismo Aaltonen. "Hali ni tofauti kabisa nikilinganisha na vile nilivyotumia miaka 40 iliyopita."
Licha ya matukio kadhaa ya hivi majuzi, usafiri wa anga unasalia kuwa njia salama zaidi ya usafiri.
Bila shaka, barabara katika baadhi ya nchi ni hatari zaidi kuliko nyingine.
Shirika la Afya Duniani limekadiria viwango cha vifo vya ajali ya barabarani katika mataifao yote duniani kulingana na data kutoka 2021.
Ilibaini kuwa nchi inayoongoza duniani kwa ajali za barabarani ni Guinea (vifo 37.4 kwa kila watu 100,000), Libya (34.0) na Haiti (31.3).
Lakini bila kuzingatia mahali unapoishi, ushauri wa Ismo Aaltonen kwa wasafiri wote ni wazi.
"Kuwa mwangalifu wakati unapoelekea katika uwanja wa ndege," alisema. "Hiyo ndiyo sehemu hatari zaidi ya safari ikilinganishwa na safari halisi ya ndege."














