Je, Urusi inaijaribu NATO kupitia shambilio la ndege isiyo na rubani nchini Poland?

Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya Kaja Kallas alisema kuwa "kuna dalili" kwamba ukiukaji wa Urusi wa anga ya Poland "ilikuwa ya kukusudia, sio bahati mbaya."

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 5

Vikosi vya Poland na NATO vilidungua ndege zisizo na rubani katika anga ya Poland siku ya Jumatano wakati wa shambulizi la anga la Urusi dhidi ya Ukraine, nchi ambayo inapakana nayo.

Mamlaka ya Poland ilielezea uvamizi huo kama "ukiukaji usio na kifani" wa eneo lao na ulianzisha Kifungu cha 4 cha NATO, ambacho kinaruhusu mashauriano rasmi na muungano wakati uadilifu wa eneo la nchi wanachama unatishiwa.

Rais wa Poland Donald Tusk alionya kwamba hali ni "ya hatari zaidi kuliko hali yoyote iliyopita" na akabainisha kuwa matarajio ya mzozo mkubwa wa kijeshi "yamekaribia kuliko wakati wowote tangu ''Vita vya pili vya Dunia ."

Pavel Muravyeika, naibu waziri wa ulinzi wa Belarus, mshirika wa Urusi, alisema ndege zisizo na rubani ziliingia katika anga ya Poland kwa bahati mbaya baada ya mifumo yao ya urambazaji kuzuiwa.

Unaweza kusoma

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alikataa kutoa maoni yake juu ya suala hilo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari Jumatano asubuhi. "Si sisi wa kufanya hivyo. Ni suala la Wizara ya Ulinzi."

Baadaye kidogo, wizara hiyo ilitoa taarifa ikisema imefanya "shambulio kubwa dhidi ya maeneo ya kijeshi na viwanda magharibi mwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani," lakini ikaongeza kuwa "hakukuwa na mipango ya kushambulia vituo kwenye eneo la Poland."

Wakati huo huo, Shirika la Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) lilisema kuwa "limejitolea kulinda kila kilomita ya eneo la nchi wanachama wake, ikiwa ni pamoja na anga yetu."

Poland ni miongoni mwa wanachama 32 wa NATO, muungano wa kiusalama ulioanzishwa mwaka 1949 ukiwa na lengo kuu la kuzuia Umoja wa Kisovieti kujitanua hadi Ulaya.

Mojawapo ya kanuni zake za msingi inategemea Kifungu chake cha 5, ambacho kinasema kwamba shambulio dhidi ya mwanachama mmoja au zaidi litachukuliwa kuwa shambulio dhidi ya wote.

Uvamizi huu, ambao umelaaniwa na idadi kubwa ya nchi za Ulaya, unazua swali kuu.

Ilikuwa "ajali" kama mamlaka ya Belarus inavyosema, au ilikuwa ni hatua ya makusudi iliyoamriwa na Putin?

"Ni vigumu kuamini"

Mwanajeshi wa Poland akikagua nyumba iliyoharibika baada ya ndege zisizo na rubani za Urusi kukiuka anga ya Poland.

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tusk alibainisha kuwa usiku kucha jeshi la Poland lilirekodi mashambulizi 19 ya ndege zisizo na rubani katika anga ya Poland.

Akizungumza mbele ya Bunge, alisema kuwa ndege zisizo na rubani "tatu au nne" zilidunguliwa na ndege za Poland na NATO.

Pia alisema kuwa idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani ziliingia nchini kutoka Belarus.

Kaja Kallas, makamu wa rais wa Tume ya Ulaya, alitaja uvamizi huo kuwa "ukiukaji mkubwa zaidi wa anga ya Ulaya na Urusi tangu mwanzo wa vita" na Ukraine.

"Kuna dalili kwamba ilikuwa ya kukusudia, sio bahati mbaya," aliandika katika X.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Czech Petr Fiala alisema ni "vigumu kuamini" shambulio hilo lilikuwa sadfa na akaishutumu Urusi kwa "kuchunguza kwa utaratibu jinsi inavyoweza kufikia."

Mykhailo Podolyak, mshauri wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, pia alidai kwenye mitandao ya kijamii kwamba shambulio hilo lilipangwa.

"Urusi ilishambulia Poland na ndege zisizo na rubani kwa nia maalum, kwa makusudi na kwa kufikiria," aliandika.

Uvamizi unaoonekana wa makusudi

Mwandishi wa masuala ya usalama wa BBC Frank Gardner anaeleza kuwa kupotea kwa ndege moja isiyo na rubani katika anga ya Poland kumetokea hapo awali na kunaweza kuamuliwa kuwa ajali.

Lakini "uvamizi wa droni kadhaa unaonekana kuwa wa makusudi zaidi."

Gardner anafafanua kuwa ndege zisizo na rubani zinazozungumziwa hazikuwa zile quadcopter ndogo ambazo huwawinda askari kwenye mahandaki wakiwa na guruneti au kombora.

Donald Tusk alionya kwamba mzozo mkubwa wa kijeshi "uko karibu kuliko wakati wowote tangu Vita vya pili vya dunia."

Chanzo cha picha, Reuters

Anabainisha kuwa zilikuwa ndege kubwa zaidi, zenye urefu wa karibu 3.5 m na upana wa 2.5 m, zisizo na rubani na zilizojaa vilipuzi vikali.

"Kila mazungumzo ambayo nimekuwa nayo hivi karibuni na maafisa wa kijeshi wa NATO au wataalam wa kitaaluma kuhusu hatua zinazofuata za Urusi yanahitimisha kwamba Moscow itataka kulijaribu azimio la NATO kwa njia fulani," mtaalam wa usalama wa BBC anabainisha.

"Kwa kuzingatia huruma ya Donald Trump kwa Vladimir Putin, kuna shaka kama utawala wake utamsaidia mwanachama wa NATO ikiwa angeshambuliwa karibu na mipaka yake."

Kwa upande wake, Sarah Rainsford, mwandishi wa BBC wa Ulaya Mashariki, alibainisha kuwa "hii inaonekana kama uchokozi wa Moscow, kupima jinsi Magharibi itakavyojibu."

Kwa wachambuzi wa kikanda, inaonekana wazi kwamba mashambulizi yote mawili kwenye makao makuu ya serikali ya Ukraine mjini Kyiv Jumapili iliyopita na uvamizi huu wa ndege zisizo katika ardhi ya Poland ni sehemu ya mkakati wa Moscow wa kupima hisia za NATO na Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani.

"Majibu ya Magharibi hayajatosha"

Kwa Vitaliy Shevchenko, mhariri wa Urusi wa BBC Monitoring, uvamizi wa Urusi katika eneo la Poland ni "mfano mwingine wa kushindwa kwa sera ya Magharibi" katika kukabiliana na tishio la Urusi na vita vyake nchini Ukraine.

"Kwa miaka mingi, majibu ya nchi za Magharibi kwa mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine yamekuwa yakizuiliwa kwa hofu ya kuibua jibu kali zaidi na la vurugu kutoka Moscow," Shevchenko alisema.

"Hofu hizi, pamoja na vikwazo vya kifedha, vimezuia washirika wa Ukraine kuipatia silaha nyingi na bora zaidi, achilia mbali kupeleka wanajeshi ardhini," anaendelea.

Mtaalamu huyo wa Kirusi anaongeza kuwa Moscow haina wasiwasi kuhusu hilo na haiogopi kuzidisha hali hiyo, iwe kwa kuzidisha mashambulizi ya anga dhidi ya Ukraine, kuwalenga raia, au kuwahusisha wanajeshi wa Korea Kaskazini.

"Majibu ambayo tumeona kutoka Magharibi hadi sasa hayajatosha kumfanya Putin kuogopa matokeo ikiwa ataamua kutuma ndege zisizo na rubani nchini Poland."