Vita vya kielektroniki': Mbinu ya kuharibu silaha ya Urusi inayoishangaza NATO

Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu kuanza kwa vita vya Urusi na Ukraine mnamo Februari 2022, nchi hizo mbili zimefanya mashambulizi mengi zaidi ya ndege zisizo na rubani katika siku za hivi karibuni.
Kwamujibu wa ripoti, Ukraine imefanya mashambulizi zaidi ya 80 ya ndege zisizokuwa na rubani dhidi ya Urusi, baadhi zikilenga mji mkuu Moscow, huku Urusi imeilenga Ukraine kwa mashambulizi zaidi ya 140 ya ndege zisizokuwa na rubani.
Kuenea kwa matumizi ya ndege zisizo na rubani kama silaha kumeleta mapinduzi katika vita hivi. Silaha za kisasa, silaha nzito pamoja na ndege zisizo na rubani zimeonekana kuwa silaha zenye ufanisi sana katika kufukuza vikosi vya adui kwenye uwanja
Droni ndio 'macho' kwenye uwanja wa vita

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa Phillips O'Brien, profesa wa masomo ya vita katika Chuo Kikuu cha St. Andrews Uskochi, droni zimekuwa silaha muhimu katika vita vya Ukraine na zimeathiri sana jinsi vita vinapiganwa.
Ndege zisizo na rubani za uchunguzi zinaweza kufuatilia harakati za askari kwenye mstari wa mbele kwenye uwanja wa vita, au maandalizi yao ya shambulio.
Wakati droni hizi zinaona lengo la kushambulia wakati wa ufuatiliaji, zinaweza kutuma habari kuhusu eneo linalochunguzwa kwenye kituo cha amri cha jeshi, ambacho kinaweza kuagiza silaha kushambulia kulingana na habari hiyo.
Profesa O'Brien anasema kuwa katika usawa wa kijeshi, mchakato wa kulenga shabaha kwa kuiona kwa kutumia ndege isiyo na rubani unaitwa 'mnyororo wa kuua' na matumizi ya ndege zisizo na rubani yameshuhudia ongezeko la haraka katika mchakato huu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Karibu malengo yote yanaweza kuonekana kwa kutumia ndege zisizo na rubani kwa muda mrefu kama hazijafichwa vizuri," anasema. Hii ina maana huwezi kujilinda dhidi ya shambulio kwa mizinga mikubwa na silaha nyingine."
Wakati ndege zisizo na rubani zinatumiwa kwa silaha kushambulia adui. Jeshi la Ukraine limeweza kuzuia harakati za vikosi vya vifaru vya Urusi kwa kuvilenga kwa ndege zisizo na rubani.
Mwanzoni mwa vita hivi, Ukraine ilitumia ndege zisizo na rubani za TB2 Beriktar zilizotengenezwa na Uturuki. Ndege hizi za kijeshi zina uwezo wa kurusha makombora na kudungua mabomu.
Hata hivyo, Urusi na Ukraine sasa zimeanza kutumia ndege zisizo na rubani za bei nafuu za 'kamikaze'.
Kwa kawaida hizi ni ndege zisizo na rubani za kibiashara ambazo husafirishwa na vilipuzi vilivyounganishwa nazo. Zinaweza kudhibitiwa kutoka umbali wa kilomita kadhaa na zinaweza hata kuelea juu ya eneo kabla ya kulipiga.
Urusi pia inatumia maelfu ya ndege zisizo na rubani za kamikaze, ikiwemo Shahid 136 iliyotengenezwa na Iran, kulenga maeneo ya kijeshi na ya kiraia nchini Ukraine.
Mizinga 'hutumika kama maji'

Chanzo cha picha, Getty Images
Silaha inayotumika zaidi katika vita vya Ukraine ni mizinga.
Kwa mujibu wa taasisi ya Royal United Services Institute (RUSI) yenye makao yake nchini Uingereza, Urusi inarusha makombora 10,000 kwa Ukraine kila siku, huku Ukraine ikirusha makombora kati ya 2,000 na 2,500 dhidi ya Urusi.
Mizinga hutumiwa kila wakati kuzuia harakati za askari wa adui na kuharibu magari ya silaha, na vifaa vya ulinzi.
Kanali Petro Pyatakov, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa BBC, anasema kuwa "mizinga hutumiwa katika vita kama maji au kama petroli kwenye gari."
Nchi zote mbili hadi sasa zimetumia mamilioni ya makombora ya kuagiza kutoka nje ya nchi. Marekani na nchi za Ulaya zinatoa silaha kwa Ukraine, huku Urusi ikipokea risasi kutoka Korea Kaskazini.
Kwa mujibu wa Justin Crump, afisa mkuu mtendaji wa Sabine, kampuni ya mchambuzi wa masuala ya ulinzi yenye makao yake nchini Uingereza, nchi za magharibi zimekuwa zikihangaika kuipatia Ukraine silaha inazohitaji.
"Kampuni za silaha za Magharibi sasa zinazalisha idadi ndogo ya silaha zinazoongozwa kwa usahihi," anasema. Hata hivyo, sasa hawana uwezo wa kutosha kuzalisha idadi kubwa ya risasi.
Urusi na Ukraine pia zinatumia silaha zinazoongozwa kwa usahihi. Ukraine inatumia makombora yanayoongozwa na satelaiti ya Magharibi 'Excalibur', huku Urusi ikitumia makombora yanayoongozwa na yanayoitwa 'Krasnopol'.
Marekani na nchi nyingine za Magharibi pia zinaipatia Ukraine makombora ya masafa marefu ya Hammars. Makombora haya yameyawezesha majeshi ya Ukraine kushambulia vituo vya silaha vya Urusi na vituo muhimu vya amri nyuma
Mabomu ya glide ni vigumu kuepukika

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni mabomu ya bei rahisi lakini ya hatari ambayo yanatumiwa na Urusi wakati wa vita nchini Ukraine. Tangu mapema mwaka 2023, vikosi vya Urusi vimetumia maelfu ya 'mabomu ya glide' kulipua maeneo ya Ukraine kwenye uwanja wa vita na kulenga maeneo ya makazi na miundombinu.
Mabomu haya yamewekwa na 'mbawa za kufyatuka' ambazo hufunguliwa baada ya bomu kuangushwa, na kuruhusu mabomu kugonga umbali mkubwa.
Kwa msaada wa 'mfumo wa mwongozo wa nyota' uliowekwa katika mabomu haya, yanaweza kulengwa kwa lengo lolote kwa urahisi.
Urusi hutumia mabomu haya ya glide. Uzito wake ni kati ya kilo 200 hadi kilo 3000 au zaidi.
"Mabomu ya Glide yamekuwa na ufanisi mkubwa katika kuvunja mitambo muhimu ya kijeshi na mistari ya mbele na kulenga majengo," anasema Profesa Justin Bronk, mtaalam wa vita vya anga katika Taasisi ya Royal United Services (Urusi).
Anasema Urusi imezitumia sana kuharibu ulinzi wa Ukraine karibu na mji muhimu wa kimkakati wa Udevoka mashariki mwa Ukraine. Urusi iliuteka mji huo mwezi Februari 2024.
Kwa mujibu wa Prof. Bronk, bomu hilo la glide ni la bei rahisi na linagharimu kati ya dola 20,000 na 30,000 kwa kulitengeneza. Linaweza kuzinduliwa maili kadhaa kutoka kwenye eneo lake na ni vigumu kulidungua.
Ukraine pia imetumia mabomu ya glide yaliyotolewa na Marekani na Ufaransa katika vita hivi. Ukraine imejitengenezea yenyewe, pamoja na mabomu madogo yaliyotengenezwa na Marekani yenye uwezo wa kubeba takriban kilo 200 za milipuko.
Hata hivyo, kuna mabomu machache ya glide kuliko Urusi.
Vita vya kielektroniki: Njia ya bei rahisi ya kuzuia silaha za gharama kubwa
Vita vya Urusi na Ukraine vimetumia vita vya elektroniki zaidi kuliko zamani.
Katika njia hii, mafundi wanajaribu kudhibiti makombora ya adui au silaha kwa kutumia njia za elektroniki.
Katika vita kati ya Urusi na Ukraine, maelfu ya wanajeshi wa kila upande wanafanya kazi katika vitengo maalum kuzima ndege zisizo na rubani za adui na mifumo ya mawasiliano, na kuondoa makombora ya adui kwenye maeneo yao.
Jeshi la Urusi lina mifumo ya kielektroniki kama vile Zhatel ambayo inaweza kuzima au kuzuia mawasiliano yote ya satelaiti, mawasiliano ya redio za mawasiliano, na ishara za simu za mkononi ndani ya eneo la zaidi ya kilomita 10.
Mfumo huu hutoa mawimbi makubwa ya nishati ya 'electromagnetic' ambayo huzima mawimbi ya redio.
Vile vile, kwa msaada wa mfumo unaoitwa Shipovnik Aero Unit, vikosi vya Urusi vinaweza kuangusha ndege zisizo na rubani kutoka umbali wa kilomita 10. Mfumo huu sio tu kwamba una uwezo wa kuangusha ndege zisizo na rubani, lakini pia unaweza kubainisha eneo la marubani wa ndege zisizo na rubani na pia kuripoti eneo lake kwa silaha.
Kulingana na Dkt Marina Miron wa Idara ya Mafunzo ya Vita katika Chuo cha King's London, nchi za Magharibi zilishangaa kuona jinsi Urusi ilivyotumia mifumo hii kuzuia makombora ya hali ya juu kama vile Hamars nchini Ukraine.
"Ni mkakati wa vita usio wa kawaida au usio na usawa," anasema. wanaweza kuyalipua."
Duncan McCrory wa taasisi ya vita vya anga Freeman katika chuo cha King's College London anasema wakuu wa jeshi la NATO wanahitaji kujifunza jinsi Urusi inavyoendesha vita vyake vya kielektroniki nchini Ukraine.
"Wanahitaji kuwafundisha askari wao jinsi ya kupigana wakati wa kulengwa na ndege zisizo na rubani na jinsi adui alivyo na uwezo wa kusikiliza kila ujumbe uliotumwa," anasema.
"Vita vya kielekroniki sio tena mawazo ya baadaye au mawazo yajayo" aliongeza. Hii inahitaji kuzingatiwa wakati unaunda mkakati wako wa vita, kutoa mafunzo kwa vikosi vyako au kutengeneza silaha za hali ya juu."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla












