Afrika Kusini yahofu wakati Marekani ikipunguza msaada wa tiba ya HIV

A glove-wearing nurse takes a blood sample from a child for an HIV test while the child's mother looks on at a clinic in Diepsloot, north of Johannesburg, South Africa, 12 March2025

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Mayeni Jones
    • Nafasi, BBC News, Johannesburg
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Gugu alikuwa akipokea dawa zake za kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa kliniki moja inayofadhiliwa na USAID mjini Johannesburg.

Lakini wakati Rais Trump alipotangaza hatua ya kusitisha ufadhili wa misaada ya Marekani mapema mwaka huu, anasema hatima ya maelfu ya wagonjwa wengine wanaoishi na VVU kote nchini Afrika Kusini sasa haijulikani.

Gugu alikuwa na bahati, kliniki iliyokuwa ikimsaidia kukabiliana na magonjwa nyemelezi iliwasiliana naye kabla haijafunga milango yake.

"Nilikuwa mmoja wa watu waliofanikiwa kupata dawa zao kwa mkupuo mmoja. Nilikuwa nikichukuwa dawa za miezi mitatu, Lakini kabla ya kliniki yangu kufungwa, walinipatia dawa ya miezi tisa."

Dawa zake zitakapoisha mwezi Septemba anapanga kwenda kwa hospitali ya umma kutafuta dawa zingine.

Mfanyabisahara huyo wa ngono wa zamani aliye na umri wa miaka 54, alipata virusi baada ya kuachana na kazi hiyo.

Miaka kumi iliyopita alijipata akikohoa, mwanzoni alifikiri amaeambukizwa maradhi ya kifua kikuu. Alipoenda hospitali daktari alimwamwambia kuwa amepata maambukizi ya kifua na kupatia dawa.

Lakini tiba hiyo ilipofeli, alienda kliniki kufanyiwa vipimo vya HIV.

"Kufikia wakati huo tayari nilihis kuwa nina virusi na hata nikamgusia nesi juu ya hilo."

Hakukosea alikuwa sahihi, na kutokea wakati huo amekuwa akitumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi. Ameomba tusitaje jina lake.

Kwa sasa anahudumu kama mshirikishi wa mradi katika shirika moja lisilo la kiserekali.

"Tunawasaidia wafanyabiashara ya ngono wajawazito kupata dawa zao za ARV, kuhakikisha watoto wao watakapozaliwa hawana VVU. Pia tunawatembelea nyumbani ili kuhakikisha kuwa kina mama wanatumia dawa kwa wakati, na kuwatunza watoto wao wanapoenda kwa uchunguzi wa kimatibabu wa kila mwezi."

Wafanyabiashara wengi wa ngono wenye VVU nchini Afrika Kusini walitegemea kliniki za kibinafsi ambazo zilikuwa zikifadhiliwa na shirika la misaada la Marekani USAID, kupata maagizo na matibabu yao.

Lakini vituo kadhaa vya afya vilifungwa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusitisha misaada mingi ya kigeni mapema mwaka huu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Gugu anaamini kuwa wafanyabiashara wengi wa ngono huenda wakakatishwa tamaa kwenda katika hospitali za umma kutafuta dawa zao wakishindwa kuzipata katika kliniki zilizo karibu nao.

"Changamoto ya kuenda katika hospitali za umma ni suala la muda. Ili kuhudumiwa kwa wakati wanasahahili kufika hapo mwendo wa saa kumi au kumi na moja alfajiri, na huenda wakasubiri siku nzima kupata dawa zao. Kwa wafanyabishara wa ngono, muda ni pesa," Gugu anasema.

Anaongeza kuwa hivi majuzi alienda hospitalini akiwa na baadhi ya marafiki zake ili kupeana maelezo yake na kujenga uhusiano na wafanyikazi.

"Muuguzi aliyetuhudumia alikuwa mkorofi sana. Alituambia hakuna kitu maalum kuhusu wafanyabiashara ya ngono."

Anadhani hii inaweza kusababisha wafanyabiashara wengi wa ngono kukataa kutumia dawa zao, "hasa ​​kwa sababu faili zao za hospitali zina taarifa nyingi za kibinafsi, na wasiwasi ni kwamba wakati mwingine wauguzi katika kliniki hizi za mitaa sio makini sana wanaposhulikia taarifa za aina hii".

Standing at a podium, George W. Bush, in a suit, turns his head as South Africa's Thandazile Darby and Dr Helga Holst, both seated with children, applaud on 1 December 2005 as World Aids Day is commemorated in the Eisenhower Executive Office Building in Washington, DC.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Marekani George W Bush alipongezwa sana kwa kujitolea kwake kukabiliana na HIV/Aids

Katika ripoti iliyotolewa siku ya Alhamisi, chombo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na kupambana na VVU/UKIMWI hakijaitaja Marekani moja kwa moja, lakini kinasema kuwa kupunguzwa kwa kiwango kikubwa cha wafadhili kumeyatikisa mataifa kote ulimwenguni, ikizingatiwa "hatua kubwa" iliyopigwa katika kukabiliana na hatari ya ugonjwa.

"Maambukizi mapya ya VVU yamepungua kwa 40% tangu mwaka 2010, na watoto milioni 4.4 wamekingwa kutokana na maambukizi ya VVU tangu 2000. Zaidi ya watu milioni 26 wameokolewa," UNAids inasema, ikionya kwamba ikiwa ulimwengu hautachukua hatua, kunaweza kuwa na maambukizi mapya ya VVU milioni sita na vifo milioni nne vinavyohusiana na Ukimwi ifikapo mwaka 2029.

UNAIDS ilisema kuwa, kabla ya kupunguzwa kwa ufadhili, idadi ya kila mwaka ya maambukizo mapya ya VVU na vifo vinavyohusiana na Ukimwi vimeshuka hadi viwango vya chini zaidi katika zaidi ya miaka 30.

Data zote zilizochapishwa katika ripoti hiyo ni za kabla ya Marekani na wafadhili wengine kupunguza ufadhili mapema mwaka huu. Lakini inaangazia ni kwango gani cha hatua iliyopigwa inaweza kurudi nyuma kutokana na gatua hiyo.

Eneo la Kusini mwa Jangwa Sahara limeshuhudia kupungua kwa asilimia 56 kwa idadi ya maambukizi mapya. Kanda hiyo bado ndio kitovu cha janga hilo - nusu ya maambukizo mapya mwaka jana yalirekodiwa barani Afrika. Lakini nchi nne za Kiafrika - Lesotho, Malawi, Rwanda na Zimbabwe - zilikuwa kwenye njia ya kufikia kupungua kwa 90% ya maambukizi mapya ifikapo 2030 ikilinganishwa na 2010.

Hatua zingine za mafanikio katika kukabilia na VVU Afrika imekuwa utendaji kazi wa dawa za kurefusha maisha, ambazo husaidia kukandamiza dalili za VVU. Pamoja na maendeleo mengine ya kimatibabu katika nyanja hiyo, yalisaidia kuongeza maisha katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kutoka miaka 56 mwaka 2010 hadi miaka 62 mwaka 2024.

Mabadiliko yalianza wakati Rais wa Marekani George W Bush alipozindua mpango kabambe wa kupambana na VVU/UKIMWI mwaka 2003, akisema utasaidia "maslahi ya kimkakati na maadili" ya Marekani.

Mkakati huo unaojulikana kama Mpango wa Dharura wa Rais wa Kusaidia Ukimwi (Pepfar), ulichangia uwekezaji wa zaidi ya $100bn (£74bn) katika juhudi za kukabiliana na VVU/UKIMWI duniani - dhamira kubwa zaidi ya taifa lolote kushughulikia ugonjwa mmoja duniani.

Afrika Kusini ina takriban watu milioni 7.7 wanaoishi na VVU, idadi kubwa zaidi duniani, kulingana na UNAIDS.

Takriban milioni 5.9 kati yao wanapokea matibabu ya kurefusha maisha, na hivyo kuchangia kupungua kwa asilimia 66 kwa vifo vinavyohusiana na Ukimwi tangu 2010, shirika la Umoja wa Mataifa linaongeza.

Serikali ya Afrika Kusini inasema ufadhili wa Pepfar ulichangia takriban 17% katika mpango wake wa VVU/UKIMWI. Fedha hizo zilitumika katika miradi mbalimbali ikiwamo kuendesha kliniki tamba ili kurahisisha matibabu kwa wagonjwa.

Hatua ya utawala wa Trump kupunguza ufadhili huo kumeibua wasiwasi kwamba viwango vya maambukizi vinaweza kuongezeka tena.

"Nadhani tutaanza kushuhudia ongezeko la idadi ya maambukizi ya VVU, idadi ya wagonjwa wa TB, idadi ya magonjwa mengine ya kuambukiza," Prof Lynn Morris, Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Wits cha Johannesburg, anaambia BBC.

"Na tutaanza kuona mabadiliko ya kile ambacho kimsingi kilikuwa hadithi ya mafanikio. Tulikuwa tumekabiliana vilivyo na baadhi ya mambo haya."

Gugu anabainisha kuwa matibabu ni suala la maisha na kifo, hasa kwa watu walio katika mazingira magumu kama vile wafanyabiashara ya ngono.

"Sio kwamba watu hawataki kutumia dawa zao za ARV. Wanahofia kwamba watakufa ikiwa hawatazipata.

Kupunguzwa kwa ufadhili pia kumeathiri utafiti unaolenga kupata chanjo ya VVU na tiba ya Ukimwi.

"Kuna athari za muda mrefu, ambazo ni kwamba hatutapata chanjo mpya za VVU," Prof Morris anaongeza.

"Hatutaweza kuendelea na juhudi za kudhibiti virusi wala kukabiliana na maambukizi ya virusi vipya, hatutakuwa na miundombinu ya ufuatiliaji ambayo tulikuwa nayo hapo awali."

Afrika Kusini imekuwa mstari wa mbele kimataifa katika utafiti wa VVU. Dawa nyingi zinazosaidia kuzuia virusi, na ambazo zimenufaisha watu kote ulimwenguni, zilifanyiwa majaribio nchini Afrika Kusini.

Hii ni pamoja na Prep (pre-exposure prophylaxis), dawa ambayo huwakinga watu wasio na VVU kupata maambukizi.

Dawa nyingine ya ufanisi ya kuzuia iliyotolewa mwaka huu, Lenacapavir, sindano ambayo mtu huchomwa mara mbili kwa mwaka na ambayo inatoa kinga kamili dhidi ya VVU, ilijaribiwa pia nchini Afrika Kusini.

Prof Abdullah Ely ikiwa katika maabara
Maelezo ya picha, Msomi wa Afrika Kusini Prof Abdullah Ely ana wasiwasi kwamba utafiti utaathiriwa na kupunguzwa kwa ufadhili wa Marekani

Katika maabara ya Sayansi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Wits, kundi dogo la wanasayansi bado wanafanyia kazi chanjo ya VVU.

Wao ni sehemu ya Brilliant Consortium, kikundi cha maabara kinachofanya kazi katika nchi nane za Kiafrika kutengeneza chanjo ya kukabiliana na virusi.

"Tulikuwa tukitengeneza kipimo cha chanjo ili kuona jinsi inavyofanya kazi vizuri, na baadaye tungeifanyia majaribio kwa wanadamu," Abdullah Ely, Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Wits, anaiambia BBC katika maabara yake.

"Mpango ulikuwa wa kuendesha majaribio barani Afrika kulingana na utafiti uliofanywa na Waafrika kwa sababu tunataka utafiti huo kufaidisha jamii yetu."

Lakini kupunguzwa kwa ufadhili wa Marekani kumeiweka kazi yao shakani.

"Agizo la kusitisha ufadhili, lilimaanisha kwamba tulipaswa kuachana na kila kitu. Ni wachache miongoni mwetu wameweza kupata ufadhili wa ziada wa kuendelea na kazi yetu. Iliturudisha nyuma kwa miezi kadhaa, pengine inaweza kuwa mwaka," Prof Ely anasema.

Maabara haina ufadhili wa kufanya majaribio ya kimatibabu yaliyopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

"Hiyo ni hasara kubwa sana kwa Afrika Kusini na bara zima. Ina maana kwamba utafiti wowote unaofanyika Afrika utalazimika kujaribiwa Ulaya, au Marekani," Prof Ely anasema.

Dr Phethiwe Matutu
BBC
We are pleading for support because South Africa is leading in HIV research, but it's not leading for itself"
Dr Phethiwe Matutu
Universities South Africa

Mwezi Juni, vyuo vikuu viliiomba serikali ruzuku ya randi 4.6bn sawa na ($260m; £190m) katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kufidia baadhi ya ufadhili uliokatizwa kutoka Marekani.

"Tunaomba kuungwa mkono kwa sababu Afrika Kusini inaongoza katika utafiti wa VVU, lakini haijielekezi yenyewe. Hii ina athari katika utendaji na sera za dunia nzima," anasema Dk Phethiwe Matutu, mkuu wa Vyuo Vikuu Afrika Kusini.

Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Aaron Motsoaledi alitangaza Jumatano kwamba ufadhili mbadala wa utafiti umepatikana.

Wakfu wa Bill na Melinda Gates na Wellcome Trust umekubali kuchangia randi 100m kila moja, huku serikali ikitarajiwa kutoa randi 400m katika miaka mitatu ijayo, alisema.

Gugu, alikuwa na matumaini kwamba akiwa mzee, dawa ya VVU/UKIMWI ingekuwa imepatikana, lakini matumaini sasa yamefifia.

"Ninamtunza mtoto wa miaka tisa. Nataka kuishi kadri niwezavyo ili kuendelea kumtunza," aliambia BBC.

"Hili sio tatizo tu kwa sasa, inabidi tufikirie jinsi litakavyoathiri kizazi kijacho cha wanawake na vijana."

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi