'Mke wangu anahofia unyumba, mimi naogopa kufa' - Athari za kufungiwa USAID

Mike Elvis Tusubira .

Chanzo cha picha, Mike Elvis Tusubira

    • Author, Dorcas Wangira
    • Nafasi, Mwandishi wa habari za afya Afrika,BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Maisha ya Mike Elvis Tusubira, mwendesha pikipiki anayeishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini Uganda, yamebadilika ghafla tangu Rais wa Marekani Donald Trump alipotangaza mpango wake wa kusitisha misaada ya kigeni mwezi uliopita .

Kando na kuhofia maisha yake anapotumia dawa za kuokoa maisha za kupunguza makali ya VVU (ARV) mtu huyo mwenye umri wa miaka 35 anakabiliwa na tisho la kutengana na mke wake -anasema itabidi aachane naye kwa sababu hawawezi tena kupata haki ya unyumba kwa njia salama.

Mwenza wake hana virusi vya HIVna anategemia PrEP, dawa za kupunguza hatari ya kupata maambukizi HIV.

"Inamaanisha kwamba hata ndoa yangu itavunjika, kwa sababu bila ya hatua za kuzuia, atakuwa hana budi kubiacha," aliiambia BBC.

"Hatuna mipira ya kondomu, wala dawa za PrEP, yaani hatuna kinga yoyote. Hatuwezi kuisha katika ndoa bila unyumba. Inamaanisha nitabaki mwenyewe."

Dawa zote za wanandoa hao ilikuwa inatokana na fedha za msaada kutoka kwa serikali ya Marekani kupitia shirikala lake la misaada ya kimataifa USAID.

Tangu shughuli za USAID zilipositishwa ghafla, jambo ambalo walijulia kwenye mitandao ya kijamii, hawajaweza kuongeza dawa zao. Mke wake ameishiwa kabisa na PrEP na wote sasa wanahofia kutegemea kondomu pekee kama njia ya kinga - zimesalia chache - ni hatari sana.

Pia unaweza kusoma:

Trump aliamuru misaada ya kigeni kusitishwa kwa siku 90 aliporejea ofisini, na baada ya hapo amri za kusitisha shughuli zikaanza kutolewa kwa mashirika yanayofadhiliwa na USAID.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baadaye, msamaha ulitolewa kwa ajili ya miradi ya kiutu, lakini kufikia wakati huo mpango wa VVU Bw. Tusubira ulikuwa sehemu ya shughuli za Kliniki ya Marpi iliyofungwa kaskazini mwa mji mkuu, Kampala.

Alimpigia simu mshauri wake wa Kituo cha Afya cha Kiswa III mjini ili kujua kinachoendelea.

"Mshauri wangu alikuwa vijijini. Aliniambia kuwa hahudumu tena kwenye kliniki."

Tangu wakati huo baba huyo aliye na mtoto mmoja, ambaye alipatikana na VVU mnamo 2022, hajafanyiwa kipimo cha kubaini kiwango cha virusi kwenye damu yake na uwezo wa mfumo wake wa kinga.

"Ninaelekea gizani. Sijui kama virusi vyangu vimekandamizwa. Nimeingiwa na kiwewe."

Haoni kama kazi yake ya kuendesha teksi ya pikipiki - inayojulikana nchini kama "boda-boda" - itamuwezesha kukimu familia yake kukabiliana na vikwazo vinavyowakabili sasa.

"Baadhi ya watu wanasema kuwa dawa hizo zitakuwa katika maduka ya dawa ya kibinafsi... kama mwendesha boda-boda sijui kama nitaweza kumudu gharama ya kuendeleza matibabu yangu."

Pia wameathiriwa na ukosefu wa huduma zinazotolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ambayo yalipata ufadhili kutoka USAID, anasema.

Mkewe alikuwa akipata PrEP yake kupitia shirika lisilo la kiserikali huko Marpi na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitano alikuwa akinufaika na mpango ambao ulitoa shule na chakula kwa watoto walio katika mazingira magumu.

"Mtoto wangu hayupo tena shuleni kwa sasa," alisema.

Dawa za kudhibiti makali ya virusi zinastahili kutumiwa kila siku - na hatua yoyote ya kuvuruga matibabu inaweza kusababisha madhara makubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Dawa za kudhibiti makali ya virusi zinastahili kutumezwa kila siku - na hatua yoyote ya kuvuruga matibabu inaweza kusababisha madhara makubwa.

Sekta ya afya ya Uganda inategemea sana ufadhili wa wafadhili, ambao unasaidia 70% ya mipango yake ya Ukimwi.

Taifa hilo la Afrika Mashariki ni miongoni mwa wapokeaji 10 bora wa fedha za USAID barani Afrika. Kulingana na takwimu za serikali ya Marekani, nchi hiyo ilipata $295m (£234m) katika ufadhili wa afya kutoka kwa shirika hilo mwaka 2023 - ikishika nafasi ya tatu baada ya Nigeria iliyopokea $368m na Tanzania $337m.

USAID pia inaunga mkono programu zake za malaria, kifua kikuu na ukoma - pamoja na kufadhili huduma za afya ya mama na mtoto na msaada wa dharura wa afya.

Maelfu ya wafanyikazi wa afya wameathiriwa na kufungia kwa ufadhili wa Amerika.

Dk Shamirah Nakitto, daktari wa Reach Out Mbuya (Rom) - shirika la kijamii la kidini linalotoa msaada wa kimatibabu na kisaikolojia kwa watu wanaoishi na VVU nchini Uganda - alikuwa na makao yake katika Kituo cha Afya cha Kisenyi IV, ambacho kinahudumia makazi duni yenye watu wengi huko Kampala.

Kwa wastani, alihudumia wagonjwa 200 wenye VVU/UKIMWI na kifua kikuu kila siku. Lakini baada ya agizo la kusimamishwa kazi, wafanyikazi wote wa afya wanaoungwa mkono na Rom waliachishwa kazi.

Kitengo chake cha kifua kikuu sasa kiko kimya na sehemu yake ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu pia imefungwa Kisenyi.

"Tunasubiri siku 90. Kwa hivyo sikuwa na budi kuondoka kwa lazima, sikuwa nimejiandaa," aliiambia BBC.

"Ilikuwa ghafla sana. Hatukuwa na makabidhiano yanayofaa kwenye kituo hicho. Tuliacha kufanya kazi."

Wizara ya afya ya Uganda inasema inachunguza njia za kudhibiti hali hiyo.

Dk Diana Atwine, mhudumu mkuu wa serikali katika wizara hiyo, aliwataka wafanyakazi "walio tayari kuendelea kufanya kazi kwa moyo wa uzalendo kama watu wa kujitolea" ili kuwasiliana.

Mkulima wa Malawi Eddah Simfukwe Banda, ambaye amekuwa akitumia ARVs kwa takriban miaka minane, anahofia amri ya kusitisha shughuli za USAID haitatenguliwa.
Maelezo ya picha, Mkulima wa Malawi Eddah Simfukwe Banda, ambaye amekuwa akitumia ARVs kwa takriban miaka minane, anahofia amri ya kusitisha shughuli za USAID haitatenguliwa.

Kwa miongo kadhaa, Marekani imekuwa mshirika muhimu zaidi wa afya ya umma barani Afrika.

Hasa kupitia mpango wake wa kimsingi wa kukabiliana na kuenea kwa VVU duniani, ambao ulizinduliwa mwaka 2003. Unaoitwa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kusaidia Ukimwi (Pepfar), umeokoa maisha zaidi ya milioni 25.

Kulingana na mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), USAID ilitoa msaada wa $8bn kwa Afrika katika mwaka uliopita.

"Asilimia sabini na tatu walikwenda kwenye huduma za afya," Jean Kaseya aliambia BBC Newsday mwezi uliopita.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa kuchukua nafasi ya ufadhili huu itakuwa vigumu sana.

Serikali za Afrika zimepiga hatua katika kupunguza utegemezi wa misaada. Kenya sasa inafadhili karibu 60% ya mwitikio wake wa VVU. Afrika Kusini inafadhili karibu 80%.

Lakini kwa mataifa mengi ya kipato cha chini, mizigo ya madeni, majanga ya hali ya hewa na misukosuko ya kiuchumi hufanya suala kujitosheleza kuwa changamoto.

Amref Health Africa, mojawapo ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya kiafya katika bara hilo, inaonya kwamba bila hatua za haraka, usalama wa afya duniani uko hatarini.

"Hii ingehitaji serikali za Afrika na Afrika CDC kuongeza ufadhili wao wenyewe, jambo ambalo haliwezekani chini ya hali ya sasa ya dhiki ya madeni," Mkurugenzi Mtendaji wake Dkt Githinji Gitahi aliiambia BBC.

"Kwa kuharakisha milipuko ya mabadiliko ya hali ya hewa na migogoro ya binadamu na mazingira, hii ingeacha dunia kuwa tete na isiyo salama - sio tu kwa Afrika lakini kwa kila mtu."

Kliniki hii - kituo kikuu cha matibabu ya VVU kaskazini mwa Malawi - kilifunga milango yake siku 18 zilizopita
Maelezo ya picha, Kliniki hii - kituo kikuu cha matibabu ya VVU kaskazini mwa Malawi - kilifunga milango yake siku 18 zilizopita

Ulimwenguni kote mnamo 2023, kulikuwa na vifo 630,000 vinavyohusiana na Ukimwi na maambukizo mapya milioni 1.5.

Ijapokuwa viwango vya maambukizi vimekuwa vikipungua katika nchi zilizoathirika zaidi, athari za kufungwa kwa USAID zinaweza kurudisha nyuma mafanikio haya.

"Ikiwa utaondoa mchango huu mkubwa wa serikali ya Marekani, tunatarajia kwamba katika miaka mitano ijayo, kutakuwa na vifo milioni 6.3 vya ziada vinavyohusiana na Ukimwi," Winnie Byanyima, mkuu wa UNAids, aliiambia BBC Africa Daily podcast wiki hii.

"Kutakuwa na maambukizi mapya milioni 8.7, yatima milioni 3.4 ya ziada ya Ukimwi. Sitaki kuonekana kama nabii wa maangamizi, lakini nina wajibu wa kutoa ukweli kama tunavyouona."

Shirika la misaada la matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) pia limeonya juu ya hatari ya kukatiza matibabu ya VVU.

"Dawa za VVU lazima zinywe kila siku au watu watakuwa katika hatari ya kupata ukinzani au matatizo hatari kiafya," Tom Ellman, kutoka MSF Kusini mwa Afrika, amesema katika taarifa yake.

Huku Uganda, Bw Tusubira anahisi huzuni kuhusu siku zijazo.

Amebakiza takriban siku 30 za dawa zake za ARV - na anaweza kuchagua kuondoka Kampala na kwenda nyumbani kijijini kwake baada ya hapo.

"Angalau itakuwa rahisi kidogo. Nikifa watanizika tu huko, badala ya kuwasumbua watu wangu hapa Kampala.

"Kwa sababu sina jinsi naweza kuishi hapa bila huduma za ARV."

Maelzo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi