Agizo la Trump kusitisha usambazaji wa dawa za HIV ,TB na Malaria, ina athari gani Afrika?

Chanzo cha picha, ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kusaini agizo la kuiondoa nchi hiyo katika Shirika la Afya Duniani (WHO) siku chache zilizopita imeanza kuleta athari kadhaa hususan barani Afrika kama ilivyotarajiwa.
Licha ya kuwa kuna sheria zinazohitajika kufuatwa kwa taifa linalotaka kundoa ufadhili wake, Utawala wa kiongozi huyo mpya tayari umechukua hatua ya kusitisha usambazaji wa dawa za kuokoa maisha za HIV, Malaria na Kifua kikuu mbali na dawa za watoto wachanga katika mataifa yote yanayosaidiwa na shirika la USAID duniani, kulingana na barua iliopatikana na vyombo vya habari.
Athari hizo zinatokana na Marekani kuwa mchangiaji mkubwa wa kifedha wa WHO na programu mbali mbali zilizopo chini ya shirika hilo na taasisi nyingine kubwa za kiafya duniani.
Siku ya Jumanne, wakandarasi na washirika wanaofanya kazi na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) nchini Tanzania na Kenya walianza kupokea barua hizo ili kusitisha ufadhili huo mara moja, kulingana na vyanzo.
Hatua hiyo ni sehemu ya kusitishwa kwa misaada kwa Marekani na ufadhili uliowekwa tangu Trump aingie madarakani Januari 20, huku programu zikikaguliwa.
Afisa mkuu wa kituo cha kudhibti magonjwa barani Africa CDC Ngashi Ng'ongo amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema nchi nyingi zimekuwa zikitegemea uwekezaji wa Marekani kupitia WHO kufadhili shughuli za afya ya umma.
"Tunajua jukumu ambalo WHO imecheza katika bara... kuboresha utoaji wa programu za afya," Ng'ongo aliambia mkutano na wanahabari.
"Kupunguzwa au kukatwa kwa ufadhili wa (Marekani) bila shaka kutaathiri mwitikio.
"Ni wakati kwa baadhi ya nchi wanachama wa Afrika kufikiria upya ufadhili wa afya ya umma." Alisema
Nchini Kenya na Tanzania tayari shirika la misaada ya kimataifa la Marakani (USAID) limetangaza kupunguza au kufuta shughuli kadhaa katika programu zake.
Katika taarifa zilizotumwa na USAID, Shirika hilo lilisema kuwa linakatiza huduma zote zilizokuwa zikitolewa na USAID kufuatia agizo la Rais Trump la kuiondoa nchi hiyo katika WHO.
USAID imeyataka mashirika yanayopokea ufadhili huo kufuata agizo hilo ili kuhakikisha kwamba hayagharamiki na huduma zozote zilizokatizwa.
Je, uamuzi huo una athari gani za moja kwa moja barani Afrika?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeelezea wasiwasi wake kuhusu athari za kusitishwa kwa ufadhili wa mara moja wa programu za VVU katika nchi za kipato cha chini na cha kati.
Kupitia taarifa iliotumwa katika vyombo vya habari , shirika hilo limesema kwamba kusitishwa kwa ufadhili wa programu za VVU kunaweza kuwaweka watu wanaoishi na VVU katika hatari ya mara moja ya magonjwa, kifo na kudhoofisha juhudi za kuzuia maambukizi katika jamii na nchi.
WHO imesema kwamba hatua kama hizo, zikiendelea, zinaweza kusababisha kuongezeka kwa maambukizi mapya na vifo, kurudisha nyuma miongo kadhaa ya maendeleo na uwezekano wa kurudisha ulimwengu kwenye miaka ya 1980 na 1990 wakati mamilioni ya watu walikufa kwa VVU kila mwaka duniani.
Kwa mujibu wa Daktari Allen Malache wa Shirika la Kelan nchini Kenya, athari miongoni mwa wahudumu wa afya zitashuhudiwa iwapo agizo hilo la Trump litaendelea kwa takriban miezi mitatu.
'Iwapo hakutapatikana huduma za Kiafya kwa wale wanaozihitaji hususan katika kliniki zinazosimamiwa na mashirika kama vile Pepfar, wale wanaotoa huduma hizo watafanya kazi gani'',? alihoji bwana Allen.
''Wale wanaopokea huduma wataenda kupata huduma upande gani iwapo kiliniki zinazosimamiwa na fedha zinazotoka kwa Pepfar zitakuwa zimefungwa. Kwa mfano vituo vinavyosimamia Ukatili wa Kijinsia vikifungwa watu watapata shida – kwasababu watu watahitaji kupata ushauri nasaha na matibabu''.
Aliongezea kusema kwamba ni muhimu Wamarekani kutathmini upya uamuzi huo ili kuona jinsi watu watakavyotatizika kutokana na hatua hiyo.
Akizungumza katika kipindi cha alfajiri cha BBC Amka na BBC, Daktari kutoka nchini Tanzania Lawi Mwenda amesema kuwa madhara makubwa yatapatikana katika huduma kama vile za Malaria, Kifua Kikuu na HIV ambapo wagonjwa wengi wanatumia dawa za maradhi hayo.
Dkt. Lawi vilevile ameongezea kuwa changamoto itakuwa katika utafiti wa dawa mpya na hela ambayo inatumika katika mikakati ya kuzuia maambukizi mapya
Je, Afrika inaweza kujisimamia yenyewe?

Chanzo cha picha, Ikulu ya Tanzania
Kwa mujibu wa Daktari Lawi Mwenda, hela nyingi zinazotolewa na mashirika ya misaada ya kiafya kama vile USAID na Global Fund ni hela ambazo asilimia kubwa zinatumika kwa utafiti.
''Hizi dawa mpya ndizo zinazokula hela nyingi zaidi kuliko dawa zinazogawanywa hospitalini. Baadhi ya tafiti zinazofanywa hata Wamarekani wanazihitaji
Daktari huyo hatahivyo anasema kwamba wizara nyingi za Afya barani Afrika hazitaathirika pakubwa kwa kuwa kuna dawa nyingi na kwamba mataifa mengi ya Afrika yana uwezo wa kuzalisha dawa hizo barani na kugharamikia ARVs.
Alisema: Kuna nchi nyingi zinazoweza kutengeneza dawa kama vile Afrika Kusini ambayo ina uwezo wa kuzalisha dawa za ARVs, Uganda kuna kampuni ya Shippler, Kenya kuna Universal Cooperation Limited, Zambia , Ethiopia na hata Tanzania kuna viwanda vilivyo na uwezo wa kuzalisha dawa.
Amesema kwamba licha ya kuwa kuna dawa zinazotoka India zinatozotumiwa na baadhi ya wagonjwa kuna aina hiyohiyo ya dawa zinazozalishwa Afrika.
''Marekani wanaweza kuwa wamesitisha lakini sio wao ambao wanazalisha au kufadhili asilimia 100, baadhi ya serikali za Afrika zinagharamia dawa hizi asilimia 20 na nyengine asilimia 40, kwa hivyo ninaamini kwamba serikali zetu za Afrika zina uwezo wa kugharamia.
Amesema kwamba gharama ambazo zinatokana na dawa za HIV ni gharama ambazo serikali nyingi barani Afrika zinaweza kumudu.
Hatahivyo Dkt. Allen anasema kwamba ni wakati ambapo mataifa ya Afrika yanapaswa kujiuliza iwapo yanaweza kugharamikia hudumu hizi kupitia utengaji wa fedha au zitaendelea kufanya mambo mengine yasio na muhimu mkubwa wa Kiafya?
''Serikali zetu zimejikokota sana ili kuafikia kiwango ambacho zinaweza kusimamia matibabu. Kenya tuna katiba inayosema kwamba serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa kila Mkenya anapata haki yake ya Afya. Kutokana na sheria hiyo – basi jukumu sio la Uingereza au Marekani , jukumu ni letu sisi wenyewe'', alihitimisha.















