Tanzania yathibitisha kuzuka kwa virusi vya Marburg baada ya kukanusha hapo awali

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Mtu mmoja ambaye alikuwa akigua ugonjwa wa Marburg amegunduliwa nchini Tanzania.
Akizungumza katika mkutano na katibu mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwamba serikiali yake ilichukua hatua kufuatia uvumi uliokuwa ukiendelea katika eneo la Kagera.
Amesema kwamba sampuli zilizopimwa katika hospitali moja mjini Kagera na kuthibitishwa mjini Dar es Salaam zilimtambua mtu huyo aliyekuwa na virusi vya maradhi hayo.
Hata hivyo sampuli za washukiwa wengine wa maradhi hayo hazikupatikana na ugonjwa huo hatari.
Bi Samia amesema kuwa hii ni mara ya pili kwa virusi vya maradhi hayo kugunduliwa nchini Tanzania mara ya kwanza vikigunduliwa mnamo mwezi Machi 2023 katika eneo hilohilo la Kagera wilayani Bukoba.
Ameongezea kwamba kufikia sasa kumekuwepo na visa 25 vya washukiwa wa maradhi hayo ambapo sampuli zao zimepatikana hazina ugonjwa huo na kwamba serikali inawafuatilia kwa karibu.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Tanzania
Amesema kwamba uvumi uliokuwa ukiendelea katika eneo hilo kwamba kuna baadhi ya watu waliofariki haujathibitishwa na kwamba serikali yake inafanya kila juhudi kubaini chanzo cha vifo hivyo.
Alilishukuru shirika la WHO kwa kuchukua hatua za dharura akisema kwamba serikali yake itachukua hatua kama zile zilizochukuliwa mwaka 2023 kudhibiti maradhi hayo.
Kwa upande wake katibu mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa ufadhili wa $3m kwa taifa hilo ili kusaidia kudhibiti maradhi hayo, ikiwa ni pamoja na $50,000 ambazo shirika hilo lilitoa kwa Tanzania kusaidia katika uchunguzi.
Bwana Adhanom amesema kufikia sasa hakuna chanjo wala tiba iliothibitishwa kukabiliana na virusi vya Marburg licha ya kwamba kuna mipango ya kuafikia hayo.
Hatahivyo aliongezea kuwa milipuko inaweza kudhibtiwa kupitia mikakati ya kuzuia maambukizi na kuokoa maisha kama ilivyofanya Tanzania.
Ugonjwa wa Marburg ni nini?
Kulingana na Umoja wa Mataifa, virusi vya Marburg, ambavyo ni sawa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa, saba kati yao walikufa, mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt. Ujerumani na Belgrade huko Serbia.
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya viungo, kuhara na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu katika mwili.
Nchi kadhaa za Afrika zimewahi kuripoti mlipiko wa virusi ikiwa ni pamoja:
- Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
- Kenya
- Afrika Kusini
- Uganda
- Zimbabwe
Mlipuko wa mwaka 2005 nchini Angola ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 300. Lakini barani Ulaya, ni mtu mmoja tu amefariki katika kipindi cha miaka 40, na mmoja nchini Marekani,baada ya kurejea kutoka katika safari ya kuzuru mapango nchini Uganda.
Milipuko mikubwa:
- 2017, Uganda: visa vitatu, watu watatu walifariki
- 2012, Uganda: vis 15, watu wanne walifariki
- 2005, Angola: visa 374, watu 329 walifariki
- 1998-2000, DR Congo: visa 154 cases, watu 128 walifariki
- 1967, Ujerumani: visa 29, watu saba walifariki
Chanzo: WHO

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, hueneaje?
Popo wa matunda wa rousette wa Misri ndiye mbebaji mkuu wa virusi
Chanzo cha picha,Getty Images
Popo wa matunda aina ya rousette wa Misri mara nyingi huwa na virusi. Nyani wa kijani kibichi na nguruwe wanaweza pia kubeba.
Miongoni mwa wanadamu, huenea kupitia maji ya mwili na malazi yaliyochafuliwa nao.
Na hata watu wakipona, damu au mbegu zao za kiume, kwa mfano, zinaweza kuwaambukiza wengine kwa miezi mingi baadaye.
Je, Marburg inaweza kutibiwa?
Hakuna chanjo maalum au matibabu ya virusi.
Lakini aina mbalimbali za bidhaa za damu, madawa ya kulevya na matibabu ya kinga yanatengenezwa, WHO inasema.
Na madaktari wanaweza kupunguza dalili kwa kuwapa wagonjwa waliofika hospitali maji mengi ili kuchukua nafasi ya damu iliyopotea.
Vinawezaje kudhibitiwa?
Watu barani Afrika wanapaswa kuepuka kula au kushika nyama ya porini, Gavi, shirika la kimataifa linalokuza upatikanaji wa chanjo, linasema.
Watu pia wanapaswa kuepuka kuwa karibu na nguruwe katika maeneo yenye mlipuko, WHO inasema.
Wanaume ambao wamekuwa na virusi wanapaswa kutumia kondomu kwa mwaka mmoja baada ya kupata dalili au hadi mbegu zao za kiume zitakapothibitishwa mara mbili kuwa hazina virusi.
Na wale wanaozika watu ambao wamekufa kutokana na virusi wanapaswa kuepuka kugusa mwili.














