Kwa nini uhusiano wa Putin na Trump unadorora?

- Author, Steve Rosenberg
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Tuanze na vita vya Urusi nchini Ukraine. Rais wa Urusi, Vladimir Putin hajaonyesha nia ya kutaka kumaliza mapigano wala kutangaza kusitisha vita hivyo vya muda mrefu.
Wakati huo huo, rais wa Marekani, Donald Trump anaharakisha juhudi za kuishinikiza Moscow kukomesha mapigano: kwa kutangaza makataa, matakwa, vitisho vya vikwazo vya ziada dhidi ya Urusi na ushuru mkubwa kwa washirika wa kibiashara wa Urusi, kama India na China.
Ongeza juu ya hayo yote, nyambizi mbili za nyuklia za Marekani ambazo Rais Trump anadai ameziweka tena karibu na Urusi.
Je, hayo yote yanamaanisha kuwa Ikulu ya Marekani inaelekea kwenye mzozo mkubwa zaidi na Kremlin juu ya Ukraine?
Au ziara ya mjumbe maalum wa Donald Trump, Steve Witkoff wiki hii huko Moscow, ni ishara kwamba makubaliano kati ya Urusi na Marekani kumaliza mapigano bado yanawezekana?
Kurudi kwa Trump

Chanzo cha picha, WILL OLIVER/EPA/Shutterstock
Katika wiki za mwanzo za muhula wa pili wa urais wa Trump, Moscow na Washington zilionekana kuanzisha upya uhusiano wao wa nchi mbili.
Wakati fulani ilionekana kana kwamba Vladimir Putin na Donald Trump walikuwa kwenye njia moja, wakielekea upande uleule. Mwezi Februari Marekani iliegemea upande wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, kwa kupinga azimio lililoandaliwa na Ulaya la kulaani "uvamizi" wa Urusi nchini Ukraine.
Katika mazungumzo ya simu mwezi huo marais hao wawili walizungumza kuhusu kutembeleana. Ilionekana kana kwamba mkutano kati ya Putin na Trump unaweza kutokea siku yoyote.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati huo huo utawala wa Trump ulikuwa ukitoa shinikizo kwa Kyiv, Ukraine na si kwa Moscow, na kuwashambulia washirika wa jadi wa Marekani, kama vile Canada na Denmark. Katika hotuba na mahojiano ya televisheni, maafisa wa Marekani waliikosoa vikali NATO na viongozi wa Ulaya.
Yote haya yalikuwa ni muziki wa kupendeza kwenye masikio ya Kremlin.
"Marekani sasa inakubaliana zaidi na Urusi kuliko Washington inavyokubaliana na Brussels au Kyiv," mchambuzi wa siasa Konstantin Blokhin kutoka Taasisi ya Urusi ya Masuala ya Usalama aliliambia gazeti la Izvestia mwezi Machi.
Wakati huo mjumbe wa Donald Trump, Steve Witkoff, alikuwa mgeni wa kawaida nchini Urusi. Alifanya safari nne ndani ya miezi miwili, akitumia saa kadhaa katika mazungumzo na Vladimir Putin. Baada ya mkutano mmoja, kiongozi wa Kremlin alimpa mchoro wa picha ya Donald Trump ili aipeleke White House.
Rais Trump alisemekana "kuguswa wazi" na zawadi hiyo.
Lakini Rais Trump alikuwa akitafuta zaidi ya mchoro kutoka Moscow. Alitaka Rais Putin kutia saini makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine bila masharti.
Trump anazidi kuchanganyikiwa

Chanzo cha picha, Chris Kleponis - Dimbwi kupitia CNP/POOL/EPA-EFE/Shutterstock
Akiwa na imani kuwa Urusi bado ina nguvu kwenye uwanja wa vita, Vladimir Putin anasitasita kusitisha mapigano, licha ya madai yake kwamba Moscow imejitolea kutatua mzozo huo kidiplomasia.
Ndio maana Donald Trump amekua akifadhaika zaidi na Kremlin.
Katika wiki za hivi karibuni amelaani mashambulizi ya Urusi dhidi ya miji ya Ukraine kuwa "ya kuchukiza", "ya fedheha" na kumshutumu Rais Putin kwa kuzungumza "ujinga mwingi" juu ya Ukraine.
Mwezi uliopita, Donald Trump alitangaza makataa ya siku 50 kwa Rais Putin kumaliza vita, na kutishia vikwazo na ushuru. Baadaye alipunguza hadi siku kumi. Tarehe ya mwisho itakuwa ni mwishoni mwa wiki hii. Hadi sasa, hakuna dalili kwamba Vladimir Putin atakubali shinikizo kutoka Washington la kusitisha vita.
Kwani Vladimir Putin anahisi yuko chini ya shinikizo?
"Kwa sababu Donald Trump amebadilisha muda wa makataa yake mara nyingi na anaweza kubadilika kwa namna moja au nyingine, sidhani kama Putin anamchukulia kwa uzito," anasema Nina Khrushcheva, profesa wa siasa za kimataifa katika kitivo cha The New School, cha chuo kikuu cha New York City.
"Putin atapigana kwa muda mrefu awezavyo, au Ukraine iseme, 'Tumechoka, tuko tayari kukubali masharti yako.'
Amani bado inawezekana

Chanzo cha picha, REUTERS/Kevin Lamarque
Kwa mtazamo mpana ambao nimeueleza hadi sasa, inaweza kuonekana kana kwamba mzozo mkubwa kati ya Putin na Trump hauepukiki.
Lakini unaweza kuepukika.
Donald Trump anajiona kama mpatanishi mkubwa na, kwa mtazamo wa mambo, hajakata tamaa kujaribu kupata mkataba wa amani na Vladimir Putin.
Steve Witkoff anatarajiwa kurejea Urusi wiki hii kwa mazungumzo na kiongozi huyo wa Kremlin. Hatujui ni ofa ya aina gani anaweza kuja nayo. Lakini wachambuzi huko Moscow wanatabiri kutakuwa na mambo chanya zaidi kuliko hasi.
Usisahau kuwa siku ya Jumapili Rais Trump alisema Urusi "inaonekana iko vizuri sana katika kuepuka vikwazo."
Siku ya Jumatatu, Ivan Loshkarev, profesa wa masuala ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha MGIMO, Moscow aliiambia Izvestia kwamba ili kuwezesha mazungumzo, Bw Witkoff anaweza kuwasilisha "ofa za manufaa katika ushirikiano [na Urusi] ambazo zitapatikana baada ya makubaliano ya amani ya Ukraine."
Je, hiyo inaweza kutosha kuishawishi Kremlin kukubalia makubaliano ya amani baada ya miaka mitatu na nusu ya vita?
Hakuna uhakika.
Baada ya yote, hadi sasa Vladimir Putin bado hajaachana na madai yake ya kutaka kuyakalia maeneo ya Ukraine, na kuitaka Ukraine kutoegemea upande wowote na anazungumzia ukubwa wa jeshi la Ukraine.
Donald Trump anataka makubaliano ya amani. Vladimir Putin anataka ushindi.












