Madereva wa malori wauawa na wanajihadi Mali

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Shirikisho la Kimataifa la Wafanyakazi wa Uchukuzi (ITF) limeitaka serikali ya Mali kuchukua hatua baada ya wimbi la mashambulizi mabaya ya msafara kuwalenga madereva wa malori ya usafirishaji mafuta.
'Wafanyikazi wa usafiri ni muhimu ili jamii zihudumiwe - haistahili waachwe bila ulinzi', ITF ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Nchini Mali, kikundi chenye silaha chenye uhusiano na Al Qaeda kimewaua madereva kadhaa wa malori ya usafiri wa masafa marefu na vijana wawili waliokuwa wanafunzwa kazi ya udereva kusini magharibi mwa nchi hiyo, kulingana na ripoti iliyochapishwa Jumatatu Machi 9 na shirika la Human Rights Watch.
Kwa mujibu wa HRW, mauaji hayo yalifanyika Januari 29, wakati wapiganaji kutoka Jama'at Nusrat al-Islam wa al-Muslimeen (JNIM) waliposhambulia msafara wa takriban malori 40 ya mafuta yaliyosindikizwa na jeshi kuelekea mji wa Kayes.
Kuchapishwa kwa ripoti hii kuliibua hisia nyingi mtandaoni kwani inaonyesha jinsi hali imekuwa hatari kwa madereva wa malori.
Miili ya waathiriwa iligunduliwa wiki mbili baadaye, huku wakiwa wamezibwa macho, mikono ikiwa imefungwa migongoni mwao na kukatwa koo, katika kile ambacho Human Rights Watch ilikielezea kuwa uhalifu wa kivita wa wazi.
Mamlaka ya Mali bado haijatoa maoni yoyote kuhusu madai mahsusi katika ripoti ya Human Rights Watch. Serikali pia mara kwa mara inashutumu mashirika yasiyo ya kiserikali kwa upendeleo au kutegemea taarifa ambazo hazijathibitishwa.
Na hivi majuzi zaidi, wanajeshi wa Mali na mamluki wa jeshi la Urusi barani Afrika waliripotiwa kuwaua raia saba karibu na mpaka wa Mauritania kwa madai ya kuwa na uhusiano na vikundi vya kijihadi.
Waathiriwa hao waliripotiwa kusafiri kutoka Fassala kusini-mashariki mwa Mauritania kuelekea soko la kila wiki karibu na Tenenkou katika eneo la Mopti nchini Mali walipozuiwa na doria ya jeshi la Mali na wapiganaji wa Urusi.
Abiria walijaribu kukimbia na sita "walipigwa risasi papo hapo, na wa saba akakatwa koo", ripoti hiyo ilisema.
Wanajeshi wa Mali na mamluki wa Urusi mara nyingi wamekuwa wakishutumiwa kufanya ukatili dhidi ya raia, madai ambayo yamekanushwa mara kwa mara na utawala wa kijeshi, ikisisitiza kuwa operesheni zao zinalenga makundi ya kijihadi pekee.
Pia unaweza kusoma:




