"Kuwaandaa Wakurdi kwa vita kuna hatari ya kuchochea hisia za kizalendo Iran" - Wall Street Journal

[

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maandamano katika Uwanja wa Trafalgar jijini London, yaliyoandaliwa na Wakurdi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mwishoni mwa Februari.
Muda wa kusoma: Dakika 6

Tunaanza ziara yetu ya magazeti katika gazeti la Wall Street Journal la Marekani, na makala iliyoandikwa na bodi ya wahariri ya gazeti hilo yenye kichwa cha habari "Hatari za Kuwapa Wakurdi Silaha Nchini Iran. "

Gazeti hilo linazungumzia mateso ya Wakurdi kwa miongo kadhaa chini ya tawala dhalimu za kikanda, na msaada wao wa kijeshi kwa Marekani zaidi ya mara moja - lakini hata hivyo, "si busara kuwahamasisha na kuwapa silaha Wakurdi kukabiliana na utawala nchini Iran."

Jarida la Wall Street linabainisha Trump alitoa taarifa kwa waandishi wa habari wiki iliyopita kwamba atawaunga mkono Wakurdi ikiwa watakabiliana na jeshi la Iran, lakini Jumamosi pia aliwaambia waandishi wa habari amefikiria upya uzito wa jambo hilo kwa sababu "vita ni vigumu" - na gazeti hilo linaona kwamba maoni ya mwisho ya Trump ndio sahihi.

Jarida la Wall Street linabainisha kwamba Wakurdi wanawakilisha asilimia 10 ya idadi ya watu wa Iran na kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta uhuru wa kisiasa, wanajua jinsi ya kupigana kwa njia ambayo wataweza "kinadharia" kugeuza sehemu ya jeshi la Iran kuwa dhaifu - ili lisiweze kutumika tena kuwaua au kuwakamata waandamanaji wanaopinga utawala.

Lakini jambo hilo si rahisi hivyo, kulingana na gazeti hilo, kuna hatari kubwa katika kuwahamasisha Wakurdi kukabiliana na utawala nchini Iran na uwezekano wa utawala huu kutumia vibaya uzalendo wa Iran, ikibainisha kwamba kabila la Waajemi linawakilisha karibu nusu ya idadi ya watu nchini humo, na hata wale wanaochukia utawala wa mullah hawataki kuigawanya nchi yao au kuiona ikiingia kwenye dimbwi la vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Jarida la Wall Street pia linaonya kuhusu athari za mzozo kati ya Wakurdi na utawala nchini Iran kwenye uhuru wa eneo lao kaskazini mwa Iraq. Wakurdi wa Iraq wana uhusiano mzuri na Uturuki na mazungumzo ya kupanua taifa la Wakurdi yataathiri vibaya uhusiano huo.

Gazeti hilo pia linaonya dhidi ya kuwasukuma vitani Wakurdi na kisha kuwaacha baadaye, sawa na kile ambacho Marekani ilikifanya kwa makundi mengine - kama vile Washia wa Iraq katika miaka ya 1990 - na "kuwatelekeza na hilo limeigharimu Marekani sifa yake na maisha ya watu wake."

Mwisho wa wazo la taifa la Palestina"

k

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour

Tunageukia gazeti la Times, ambalo limechapisha makala yenye kichwa cha habari "Vita hivi vitaangamiza taifa la Palestina," na mwandishi na mwanahistoria wa masuala ya kijeshi Max Hastings.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hastings anasema mashambulizi ya walowezi Wayahudi dhidi ya Wapalestina mwaka jana yalizidi, kwa mara ya kwanza, mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Wapalestina dhidi ya walowezi, akibainisha kuwa vurugu za walowezi mara nyingi haziadhibiwi.

Mwandishi pia anabainisha ongezeko kubwa la utoaji wa leseni kutoka serikali ya Israel kwa ajili ya upanuzi wa makazi, jambo ambalo linaweza kusababisha mgawanyiko katika Ukingo wa Magharibi, na kauli za Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich ambaye amesema serikali yake inalenga "kuua" wazo la taifa la Palestina.

Ameongeza kuwa tawala za awali za Marekani ziliweka vikwazo kwenye sera hizo, lakini utawala wa sasa wa Washington, unashiriki kwa kunyamaza kimya.

Hastings anaamini vita ambavyo Donald Trump anapigana sasa katika Mashariki ya Kati vinamnufaisha mtu mmoja zaidi kuliko mtu mwingine yeyote katika eneo hilo, yaani Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye miaka miwili iliyopita alikuwa akikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa.

Mwandishi anasema Netanyahu anaweza kutoa wito wa kuahirisha tarehe ya uchaguzi na ana uhakika wa kushinda, kwani ndiye mtu ambaye ametimiza ndoto ya zamani ambayo amekuwa nayo katika taaluma yake yote ya kisiasa, yaani kumshawishi Trump kushiriki katika vita dhidi ya Iran.

Kulingana na Hastings, Wayahudi wa Israel wameonyesha kiwango cha nadra cha makubaliano katika historia ya Israel, huku asilimia 93 kati yao wakiunga mkono uamuzi wa kwenda vitani, kulingana na kura ya maoni.

Hata hivyo, mwandishi anaamini uungwaji mkono wa sera ya mkono wa chuma kwa Wapalestina umeenea hata kabla ya vita dhidi ya Iran, akibainisha kuwa kura za maoni zinaonyesha wapiga kura wengi ambao hawakumpigia kura Netanyahu, wanakubaliana mbinu yake dhidi ya Wapalestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Hastings anaamini tangu shambulio la Oktoba 7, 2023, Waisraeli wengi wanaamini kuishi kwa amani na watu wanaotaka kuwaangamiza haiwezekani.

Hata hivyo, mwandishi anabainisha kwamba kuna Waisraeli wanaoamini kuwepo kwa Wapalestina wapatao milioni 4.4 hakuwezi kupuuzwa, lakini pia wanatambua kwamba haiwezekani kwa serikali yoyote ya Israel, hasa ile inayoongozwa na Netanyahu, kutoa haki kamili za kiraia na kisiasa kwa wasio Wayahudi wanaoishi Israel.

Hastings anaongeza kuwa ushirikiano wa Marekani na Israel katika vita dhidi ya Iran umeimarisha ushawishi wake hadi kufikia hatua ambapo anaweza kuweka sera yoyote anayoona inafaa kwa ajili ya kuwatawala Wapalestina.

Mwandishi anaamini Trump amemwezesha Netanyahu hatua kwa hatua kuelekea kuunyakua Ukingo wa Magharibi, ili kutimiza kile anachokieleza kama ndoto ya "Israel Kubwa," na inaonekana hakuna mtu yeyote anayeweza kumzuia.

Hastings anahitimisha kwa kusema, msiba wa Wapalestina, kwa maoni yake, upo katika ukosefu wao wa washirika wa kweli, hata katika kiwango cha maoni ya umma katika nchi za kiarabu, pamoja na kutokuwepo kwa viongozi waaminifu au wanaoheshimika, iwe miongoni mwa marafiki au wapinzani.

Kuchagua kukaidi

p

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mwanamke akiwa na picha ya Kiongozi Mkuu mpya wa Iran, Ayatollah Mojtaba Khamenei.

Ziara hii inahitimishwa na jarida la The Economist na makala yenye kichwa cha habari "Utawala wa Irani waonyesha ukaidi kwa kumchagua Mojtaba Khamenei kama Kiongozi Mkuu mpya."

Jarida hilo linasema kumchagua Mojtaba Khamenei kama mrithi wa baba yake, ambaye aliuawa siku kumi zilizopita, kunatuma ujumbe wa ukaidi kwamba utawala huo bado upo, na kudokeza kwamba Mojtaba ni "kiongozi" tu kwa sasa, tofauti na baba yake ambaye alikuwa na uamuzi wa mwisho.

Jarida linasema chaguo hili linaonyesha kiwango cha udhibiti cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran juu ya madaraka nchini Iran.

Jarida hilo linasema kumchagua Mojtaba kunaweza kuwakatisha tamaa wanamageuzi waliokuwa wanatumai kwamba mmoja wao angechaguliwa.

Mchakato wa kumchagua kiongozi mpya umechukua muda mrefu, Mojtaba huenda akabaki mbali na watu na katika maeneo ya chini ya ardhi yenye ngome, kwa hofu kwamba atakumbana na hatima sawa na ya baba yake, baada ya Israel kumtishia kiongozi huyo mpya, na yeyote yule.

Jarida hilo linabainisha kuwa Mojtaba Khamenei hajaonekana hadharani tangu mwanzo wa vita, baada ya mauaji ya jamaa zake kadhaa wa karibu, jambo ambalo limezua uvumi kuhusu hali yake ya kiafya.

Kulingana na jarida hilo, baadhi ya wanaharakati wa mageuzi wanamwona Mojtaba Khamenei kama mtu mwenye msimamo mkali, kwani anashutumiwa kwa kuwafuatilia wanaharakati wa mageuzi na kushiriki katika kuchakachua matokeo ya uchaguzi wa rais wa 2009, pamoja na jukumu lake katika kubadilisha utawala wa Iran kutoka mfumo wa "mseto" unaochanganya dini na baadhi ya vipengele vya uwakilishi kupitia uchaguzi hadi kuwa taifa lenye msimamo mkali katika kukabiliana na upinzani.

Jarida hilo linaamini kiongozi mpya anaweza kukabiliwa na ugumu katika kutekeleza mamlaka yake, likibainisha kwamba baba yake alikuwa amewapa viongozi wa eneo hilo mamlaka fulani ikiwa atashambuliwa na mapigano kuendelea.

Jarida hilo linahusisha ugumu huo na kile kilichoelezwa kama ukosefu wa uratibu kati ya kauli za Rais wa Iran Masoud Pezeshkian na viongozi wa Walinzi wa Mapinduzi, ambao walirusha makombora kuelekea nchi za Kiarabu katika Ghuba yapata nusu saa baada ya rais kuomba msamaha.

Jarida hilo linasema baadhi ya waangalizi, kabla ya kuzuka kwa vita, walidhani Mojtaba Khamenei anaweza kuwa mfano wa Mohammed bin Salman nchini Saudi Arabia, kwa kupunguza ushawishi wa viongozi wa kidini na kupunguza mvutano na Israel, lakini mauaji ya wanafamilia wake yanaweza kuwa yameondoa dhana hizo.