Fahamu mambo Matano muhimu kumhusu mtuhumiwa mkuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda

Kibuga

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Laillah Mohammed
    • Nafasi, BBC Swahili, Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Taarifa za kifo cha mtuhumiwa mkuu wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, Felicien Kabuga zimepokelewa nchini humo na kote duniani huku wengi wakijuliza maswali kuhusu haki ambayo waathiriwa wa vitendo vyake walikuwa wanaitafuta kwa zaidi ya miongo mitatu sasa.

Félicien Kabuga, ambaye alishtakiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini Rwanda mwaka 1994, alifariki dunia mjini The Hague, Uholanzi, Jumamosi akiwa na umri wa miaka 91, katika hospitali ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (IRMCT), mahakama ya zamani yenye makao yake makuu mjini Arusha, mahakama hiyo ilitangaza.

Daktari wa magereza wa mahakama alifahamishwa mara moja na mamlaka ya Uholanzi "imeanzisha taratibu na uchunguzi wa kawaida unaohitajika na sheria ya taifa ya Uholanzi," taarifa hiyo ilisema.

Kwa mujibu wa sheria za mahakama na kanuni za uchumba, rais wa mahakama hiyo, raia wa Uruguay Graciela Gatti Santana, aliamuru "uchunguzi kamili" kuhusu kifo cha Kabuga, na kumteua jaji wa Uholanzi Alphons Orie kuongoza uchunguzi huo.

Kwa sasa mawakili wanapojiandaa kupokea taarifa za ni wapi kesi hiyo inakwenda baada ya sasa.

Kwa jamaa za waliouawa kikatili katika mauaji hayo yaliyoanza Aprili 7 1994 na kudumu kwa mwezi mzima, taarifa hii inafunga ukurasa muhimu katika historia ngumu sana ya taifa hilo la Afrika Mashariki ambapo takriban watu laki nane waliuawa baada ya kushambuliwa na Kundi la jamii ya WaHutu iliyofahamika kama INTERAHAMWE ambao ilichochewa kumaliza watu kutoka jamii ya Watutsi ambao walitajwa kama INYENZI {mende kwa lugha ya Kinyanrwanda.}

Kabuga alikuwa mfanyabiashara maarufu nchini Rwanda aliyekuwa na ushawishi mkubwa vile vile katika siasa za chi hiyo.

Kwa miongo miwiili Kabuga alikuwa mafichoni.

Ufuatao ni utaratibu wa mambo yalivyotokea kabla na baada ya kukamatwa kwake;

Aprili 29, 2013: 'Hati ya kukamatwa ilitolewa na iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR/TPIR. )

Mei 16, 2020: Alikamatwa nchini Ufaransa.

Oktoba 26, 2020: Alihamishiwa Mahakama ya The Hague.

Septemba 29, 2022 : Kesi yake ilianza kusikizwa.

Lakini Felicien Kabuga ana umuhimu gani katika historia ya Rwanda?

Haya hapa ni mambo Matano kumhusu mzee huyo aliyefariki akiwa mwenye umri wa miaka 91, jijini The Hague ambapo alikuwa ana zuiliwa na mamlaka za usalama na ambapo pia kesi yake ilikuwa imeanza kusikilizwa lakini ikasimamishwa kwa muda usiojulikana katika mahakama ya umoja wa mataifa ya International Residual Mechanism for Criminal Tribunals (IRMCT)

1: Alikuwa Tajiri na ushawishi mkubwa

Hata kabla ya mauaji ya kimbari, Kabuga, Mhutu, alikuwa mmoja wa wafadhili wenye nguvu zaidi wa Rwanda ya 1994.

Kabuga alikuwa akitambuliwa kama mtu mwenye utajiri mkubwa zaidi nchini Rwanda. Mali yake ilitokana na biashara ya kahawa na majani chai. Pia alikuwa mwendani wa karibu wa kisiasa na shemeji wa Rais wa zamani Juvenal Habyarimana.

2: Alitumia mali yake kufadhili mauaji

Upande wa mashtaka ulimfungulia kesi Kabuga katika mahakama ya ICC, akituhumiwa kwa mauaji ya kimbari na vile vile mashtaka ya ukiukaji wa haki za kibinadamu. Kabuga anashutumiwa kwa kutumia mali yake kufadhili na kununua silaha zilizotumiwa na Kundi la Interahamwe na kuchangia kubuniwa kwa hazina iliyofahamika kama NATIONAL DEFENCE FUND kwa ajili ya kunuwa silaha.

3: Alitumia kituo chake redio kusambaza chuki

Kabuga alimiliki kituo cha redio na televisheni cha RADIO TELEVISION LIBRE DES MILLE COLLINES (RTLM). Kituo hicho kilikuwa na umuhimu mkubwa katika kampeni ya kuwamaliza WaTutsi nchini Rwanda kwa muda huo ambapo mauaji yalipangwa na kutekelezwa. Watangazaji wake walitakiwa kutangaza taarifa za uchochezi na propaganda ya chuki dhidi ya jamii ya WaTutsi kutoka kwa jamii ya WaHutu.

4: Alikwepa kukamatwa kwa miaka 26

Kwa wakati mmoja vyombo vya habari nchini Kenya viliripoti kwamba Kabuga alikuwa anaishi mafichoni nchini Kenya n ahata baadhi yao yakafanya uchunguzi kutafuta ukweli kuhusu madai hayo.

Kenya ilikanusha madai hayo mara kwa mara ikisema kwamba Kabuga hayupo nchini humo na wala serikali haiwezi kushirikiana na mtu ambaye alikuwa ni mshukiwa wa uhalifu na aliyekuwa akitafutwa na mamlaka za usalama za kimataifa.

Kutokana na uwezo wake mkubwa kifedha, mfanyabiashara huyo alitumia fedha na kushirkiana na marafiki wake na washirika wake katika mataifa mbali mbali duniani kujificha kwa takriban miaka 26, kabla ya kukamatwa.

Marekani ilikuwa imetoa Zawadi ya Dola Milioni 5 kwa yeyote atakaye toa taarifa muhimu kumhusu Kabuga. Lakini ujanja wake ulifikia ukingoni mnamo May 2020 alipokamatwa na maafisa wa usalama Jijini Paris , Ufaransa.

5: Kesi yake ilisimamishwa kwa sababu ya hali mbaya ya afya yake

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya kukamatwa nchini Ufaransa, ilichukuwa muda kabla shughuli rasmi za mahakama ya kimataifa ya jinai ICC kuanza. Alipelekwa mbele ya mahakama maalum ya kimataifa ya Umoja wa mataifa ya {International Residual mechanism for Criminal Tribunals -IRMCT) iliyopo mjini The Hague, mnamo 2022.

Hata hivyo miezi michache baadaye mwaka wa 2023, Majajji waliosimamia kesi hiyo walitangaza kwamba Kabuga hangeweza tena na kesi hiyo kutokana na afya yake ya akili kwani alithibitishwa na daktari kwamba anauguwa ugonjwa wa DEMENTIA ambao huathiri uwezo wa ubongo kuhifadhi kumbukumbu muhimu.

Kutokana na hali hiyo, kesi ilisimama kwa muda huo wote, mahakama ikisubiri kupata taarifa muhimu kutoka kwa Kundi la wataalamu waliokuwa wakimpa huduma ya matibabu.

Kabuga amefariki kabla ya kesi hiyo kurejelewa, huku wengi wakihofia kwamba huenda haki walioitamani itazikwa naye kaburini.

Serikali ya Rwanda haijatoa taarifa kuhusu kifo chake Kabuga.

Kabuga amefariki kabla ya kesi hiyo kurejelewa, huku wengi wakihofia kwamba huenda haki walioitamani itazikwa naye kaburini.

Nyaraka za mahakama zinaonyesha alizaliwa mwaka wa 1935 – na kumfanya kuwa na umri wa miaka 91, katika wilaya ya zamani ya Mukarange katika jimbo la zamani la Byumba, ambalo sasa ni wilaya ya Gicumbi katika jimbo la kaskazini mwa Rwanda.

Hata kabla ya mauaji ya kimbari, Kabuga, Mhutu, alikuwa mmoja wa wafadhili wenye nguvu zaidi wa Rwanda.

Mbele ya mahakama, Kabuga alitaja mashtaka dhidi yake kuwa "uongo"

Mnamo Juni 6, 2023, mahakama iliamua kwamba Kabuga asingeweza kuendelea na kesi yake kutokana na afya yake kuwa mbaya.

Wakati wa kifo chake, Kabuga alikuwa bado anasubiri kuachiliwa kwa muda kwa nchi ambayo ingekuwa tayari kumpokea katika eneo lake.

Mnamo 2025, Mahakama ilihitimisha kuwa "Bwana Kabuga hawezi kusafiri hadi Rwanda" kutokana na afya yake mbaya.

Ilisema kwamba kurejeshwa kwake Rwanda "kungeweka hatari ya wazi na kubwa kwa afya yake" na kwamba "kuamuru kuachiliwa kwake kwenda Rwanda" itakuwa kinyume na jukumu la Mahakama ya kumtunza, "angalau bila idhini yake".

Waendesha mashtaka na serikali ya Rwanda walikuwa wakitaka Kabuga arejeshwe Rwanda, nchi pekee iliyomkubali baada ya mahakama kuamuru aachiliwe kwa dhamana kutokana na hali yake mbaya ya kiafya. Familia ya Kabuga na mawakili walikuwa wakibishana kwamba kumtuma Rwanda kungekiuka haki zake na kuibua wasiwasi kuhusu usalama wake.