Mauaji ya kimbari ya Rwanda: Dunia ilitupa kisogo mwaka wa 1994, Rais Paul Kagame asema
Na Wedaeli Chibelushi ,
BBC News

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Rwanda alisema jumuiya ya kimataifa "ilitufeli sisi sote", alipokuwa akiadhimisha miaka 30 tangu mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 yaliyoua takriban watu 800,000.
Rais Paul Kagame alihutubia viongozi wa dunia waliokuwa wamekusanyika katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, kuadhimisha tukio hilo la umwagaji damu.
"Rwanda ilifedheheshwa kabisa na ukubwa wa maafa yetu," alisema.
"Mafunzo yameandikwa katika damu."
Siku kama ya jana (Tarehe 7 Aprili) mwaka wa 1994, watu wenye msimamo mkali kutoka kabila la Wahutu walianzisha mauaji ya siku 100, ambapo watu wa kabila la Watutsi walio wachache na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa.
Vikosi hasa vya Watutsi vilivyochukua mamlaka kufuatia mauaji ya halaiki vilidaiwa kuwaua maelfu ya Wahutu nchini Rwanda kwa kulipiza kisasi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Siku ya Jumapili, Bw Kagame na kundi la watu mashuhuri waliweka shada la maua kwenye makaburi ya halaiki kwenye Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari ya Kigali - ambapo zaidi ya waathiriwa 250,000 wanaaminika kuzikwa. Rais pia aliwasha mwenge wa kumbukumbu.
Katika hotuba yake baadaye, Bw Kagame alizishukuru nchi za Afrika zikiwemo Uganda, Ethiopia na Tanzania kwa usaidizi wao wa kuwapokea wakimbizi wa Kitutsi na kukomesha mauaji ya kimbari.
"Nchi nyingi zinazowakilishwa hapa pia zilituma watoto wao wa kiume na wa kike kuhudumu kama askari wa kulinda amani nchini Rwanda," alisema.
"Wanajeshi hao hawakuifelisha Rwanda. Ilikuwa ni jumuiya ya kimataifa ambayo ilitufelisha sisi sote. Iwe kwa dharau au woga."
Kushindwa kwa mataifa mengine kuingilia kati kumekuwa sababu ya aibu inayozidi kujadiliwa .
Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi waliozuru waliohudhuria, maadhimisho hayo ameyataja mauaji ya halaiki kuwa kufeli zaidi kwa utawala wake.
Katika ujumbe wa video uliorekodiwa kwa ajili ya kumbukumbu hiyo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikiri kwamba nchi yake na washirika wake wangeweza kukomesha mauaji ya halaiki lakini hawakuwa na nia ya kufanya hivyo.
Ufaransa, chini ya rais wa wakati huo François Mitterrand, ilikuwa mshirika wa karibu wa serikali inayoongozwa na Wahutu ya Juvenal Habyarimana kabla ya mauaji hayo, na Rwanda imeishutumu Ufaransa kwa kupuuza au kukosa ishara za onyo na kutoa mafunzo kwa wanamgambo waliofanya mashambulizi hayo.
Ufaransa imekuwa ikikana kuhusika, lakini ripoti iliyoidhinishwa na Macron miaka mitatu iliyopita ilihitimisha kwamba Ufaransa ina "majukumu mazito ya kuwajibikia maafa hayo" .

Chanzo cha picha, Picha za Getty
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Stéphane Séjourné alihudhuria hafla hiyo mjini Kigali kumwakilisha Bw Macron siku ya Jumapili. Viongozi wengine waliozuru ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, na Rais wa Israel Isaac Herzog.
Matukio ya Jumapili yanaashiria mwanzo wa kipindi cha maombolezo cha wiki nzima kote nchini Rwanda. Muziki, michezo na filamu zimepigwa marufuku kutangazwa kwenye redio au TV na bendera za taifa zitapeperushwa nusu mlingoti.
Barabara za Kigali zimekuwa tulivu isivyo kawaida, kulingana na timu ya BBC huko, bila magari mengi , maduka mengi yamefungwa, na watembea kwa miguu ni wachache.
Mauaji ya halaiki yalichochewa usiku wa tarehe 6 Aprili 1994, wakati Rais wa Kihutu Juvenal Habyarimana alipouawa - ndege aliyokuwa amepanda ilidunguliwa.
Wahutu wenye msimamo mkali walilaumu kundi la waasi la Watutsi la RPF, na kuanzisha kampeni iliyoandaliwa vyema ya mauaji .
Waathiriwa wao walipigwa risasi, kupigwa au kukatwakatwa hadi kufa katika mauaji yaliyochochewa na propaganda za kupinga Watutsi zilizoenezwa kwenye TV na redio.
Maelfu ya wanawake wa Kitutsi walitekwa nyara na kuwekwa kama watumwa wa ngono.
Baada ya siku 100 za ghasia, wanamgambo wa waasi wa RPF, wakiongozwa na Bw Kagame, walifanikiwa kupindua mamlaka ya Wahutu na kukomesha mauaji ya halaiki.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema wapiganaji wa RPF waliwaua maelfu ya raia wa Kihutu walipokuwa wakichukua madaraka - na zaidi baada ya kuwafuata wanamgambo wa Kihutu waliokimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. RPF inakanusha hili.
Makovu kutokana na ghasia hizo bado yangalipo,na makaburi mapya ya halaiki bado yanafichuliwa kote nchini.
Katika miezi iliyofuata mauaji ya halaiki, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Rwanda iliundwa nchini Tanzania .
Makumi ya maafisa wakuu katika utawala wa zamani walipatikana na hatia ya mauaji ya halaiki - wote wakiwa Wahutu.
Ndani ya Rwanda, mahakama za jamii, zinazojulikana kama gacaca, ziliundwa ili kuharakisha mashtaka ya mamia kwa maelfu ya washukiwa wa mauaji ya halaiki yanaosubiri kusikilizwa.
Kulingana na Rwanda, mamia ya washukiwa wamesalia huru ikiwa ni pamoja na katika mataifa jirani kama vile DR Congo na Uganda.
Rais Kagame amesifiwa kwa kuibadilisha nchi hiyo ndogo na iliyoharibiwa aliyochukua usukani kupitia sera ambazo zilihimiza ukuaji wa haraka wa uchumi.
Lakini wakosoaji wake wanasema hakubali upinzani na wapinzani kadhaa wamekumbana na vifo visivyoeleweka, nchini na nje ya nchi.

Chanzo cha picha, BBC/Jean Claude Mwambusa
Mauaji ya kimbari bado ni suala nyeti sana nchini Rwanda, na ni kinyume cha sheria kuzungumzia ukabila.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












