Walowezi wa Israel wananyakua ardhi za Wapalestina wakati huu wa vita

Katika kijiji cha Wapalestina cha Battir, ambapo mabonde ya kale yanamwagiliwa maji na chemchemi ya asili, maisha yanaendelea kama yalivyokuwa kwa karne nyingi.
Kijiji hiki ni sehemu ya Urithi wa Dunia wa Unesco, Battir inajulikana kwa mashamba yake ya mizeituni na mizabibu. Lakini sasa eneo hilo limeingia katika mvutano na makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Israel imeidhinisha makazi mapya ya Wayahudi hapa, ikichukua ardhi inayomilikiwa na watu binafsi kwa ajili ya makazi mapya ya walowezi.
"Wanaiba ardhi yetu ili kujenga makazi yao," anasema Ghassan Olyan, ambaye ardhi yake ni miongoni mwa zinazoshikiliwa.
Unesco inasema ina wasiwasi na mipango ya walowezi huko Battir, lakini kijiji hicho si mfano pekee. Makazi yote ya walowezi ni kinyume cha sheria za kimataifa, ingawa Israel haikubaliani na hilo.
"Hawajali sheria za kimataifa, au sheria za nchi, na hata sheria ya Mungu," anasema Olyan.
Hali inazidi kuwa mbaya

Wiki iliyopita, mkuu wa upelelezi wa ndani wa Israel Ronen Bar aliwaandikia mawaziri akionya kwamba Wayahudi wenye itikadi kali katika Ukingo wa Magharibi wanatekeleza vitendo vya ugaidi dhidi ya Wapalestina na kusababisha kuchafua jina la nchi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tangu kuanza kwa vita huko Gaza, kumekuwa na kasi ya ukuaji wa makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi.
Watu wenye misimamo mikali katika serikali ya Israel wanajigamba kuwa mabadiliko haya yatazuia taifa huru la Palestina kuundwa. Kuna hofu pia kwamba wanataka kurefusha vita huko Gaza ili kutimiza malengo yao.
Yonatan Mizrahi kutoka Peace Now, shirika la Israel linalofuatilia ukuaji wa makaazi ya walowezi, linasema Wayahudi wenye itikadi kali katika Ukingo wa Magharibi wanazidisha hali ya wasiwasi, na kufanya kuwa vigumu kuliko wakati mwingine wowote kumaliza mzozo kati ya Israel na Palestina.
Anaamini "mchanganyiko wa hasira na hofu" katika jamii ya Israel baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, ambapo watu 1,200 waliuawa, inawafanya walowezi kunyakua ardhi zaidi, na wala hawaulizwi.
Utafiti wa mwezi Juni uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew unaeleza kuwa 40% ya Waisraeli wanaamini makazi ya walowezi yanaifanya nchi hiyo kuwa salama zaidi, kutoka 27% ya mwaka 2013. Na 35% ya watu waliohojiwa walisema makazi hayo yanaathiri usalama wa Israel, kutoka 42%.
Tangu kuzuka kwa vita vya Gaza, ghasia za walowezi dhidi ya raia wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi zimeongezeka. Katika miezi 10 iliyopita Umoja wa Mataifa umerikodi karibu mashambulizi 1,270, ikilinganishwa na 856 katika mwaka wote wa 2022.
Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Israel, B'Tselem, katika kipindi hicho vurugu za walowezi wa Israel zimewalazimisha Wapalestina wa vijiji 18 kuondoka katika Ukingo wa Magharibi, eneo la Palestina kati ya Israel na Jordan ambalo lilitekwa na Israel katika vita vya Mashariki ya Kati mwaka 1967 na limekuwa likikaliwa kwa nguvu tangu wakati huo.
Kati ya Oktoba 7 na Agosti 2024, Wapalestina 589 wameuliwa katika Ukingo wa Magharibi - 570 na vikosi vya Israel na 11 na walowezi, kwa mujibu wa UN.
Idadi hiyo inajumuisha wale wanaotajwa kuwa walikuwa wakipanga mashambulizi na raia wasio na silaha. Katika kipindi hicho pia, Wapalestina wamewauwa walowezi watano na maafisa tisa wa vikosi vya usalama vya Israel.
Wiki hii, mwanaume Mpalestina mwenye umri wa miaka 40 aliripotiwa kupigwa risasi na kufa baada ya walowezi na wanajeshi wa Israel kuingia eneo la Wadi al-Rahhel, karibu na Bethlehem. Jeshi la Israel limesema ni baada ya mawe kurushwa.
Mwezi uliopita, kijana wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 22 aliuawa wakati walowezi kadhaa walipovamia kijiji cha Jit, na kulaaniwa kimataifa. Vikosi vya usalama vya Israel vimewakamata watu wanne na vimeelezea tukio hilo kama "tukio kubwa la kigaidi."
Kundi la kutetea haki za kiraia la Israel Yesh Din linasema, kati ya 2005 na 2023, ni asilimia 3 tu ya uchunguzi rasmi kuhusu ghasia za walowezi huishia kwa kutiwa hatiani.
Katika barua hiyo ya Ronen Bar, ambayo ilifichuliwa kwa vyombo vya habari vya Israel, mkuu huyo wa ujasusi wa ndani wa Shin Bet, anasema walowezi wenye itikadi kali wanapata nguvu kutokana na utekelezwaji dhaifu wa sheria.
Mipango ya Walowezi
Makazi mengi ya walowezi yanaungwa mkono kisheria na serikali ya Israel. Mwezi Julai, wakati mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa iliposema kwa mara ya kwanza kwamba ukaliaji wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, ni kinyume cha sheria, na kusema nchi hiyo inapaswa kusitisha shughuli zote za makazi na kujiondoa haraka iwezekanavyo.
Washirika wa Magharibi wa Israel wameeleza mara kwa mara kuwa makazi ya walowezi ni kikwazo cha amani. Israel iliipinga mahakama hiyo na kusema: “Wayahudi si wanyakuzi katika nchi yao wenyewe.”
Walowezi wanaendelea kuchukua maeneo ya Wapalestina na wanaungwa mkono na serikali yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia. Wanaendeleza mipango ya kutwaa Ukingo wa Magharibi na pia kutoa wito wa kuikalia Gaza mara vita vitakapokwisha. Walowezi sasa wanahudumu katika serikali ya Israei, katika wizara muhimu.
Wakati huo huo viongozi wa dunia wanaopinga makaazi ya walowezi wanaonyesha shauku mpya ya kupatikana kwa suluhu ya mataifa mawili – lakini Waisrael wenye itikadi kali za kidini, wanaoamini kuwa ardhi yote ni mali ya Israel wanaapa kufanya ndoto ya taifa huru la Palestina isiwezekane.
Wadadisi wa mambo wanafikiri hii ndiyo sababu baadhi ya wanasiasa wa Israel wanakataa kukubali mpango wowote wa kusitisha mapigano.
"Sababu ya kutotaka kumaliza mzozo au kuingia katika makubaliano ya kurudishwa mateka, wanaamini Israel inapaswa kuendelea na mapigano hadi ifikie mahali ambapo inaweza kukaa ndani ya Gaza," anasema Tal Schneider, mwandishi wa habari za siasa wa The Times of Israel.
"Wanafikiri kuwa itikadi yao ni ya haki zaidi," anaongeza.
Serikali ya Israel, wakati huo huo, imetangaza mipango ya makazi mapya katika maeneo matano, ikiwa ni pamoja na neo la Battir, na kutangaza eneo la kilomita za mraba 23, kwa ajili ya serikali. Hii ina maana Israel inajimilikisha ardhi, bila kujali ikiwa ni ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, au inamilikiwa na Wapalestina binafsi, na Wapalestina wanazuiwa kuitumia.
Walowezi wanatumai kuwaweka Waisraeli wengi kwenye ardhi hiyo na kujenga vya kutosha ili kufanya uwepo wao kutowezekana kuondolewa. Matumaini yao ya muda mrefu ni kwamba Israel itatwaa rasmi nchi yote.
Nje ya unyakuzi wa ardhi ulioidhinishwa na serikali, watu wenye msimamo mkali pia wananyakua ardhi na kujenga makazi kwa haraka.
Eneo la al-Qanoub, kaskazini mwa Hebron, picha za satelaiti zinaonyesha misafara na barabara mpya - zimeiubuka tangu kuanza kwa vita. Wakati huo huo, jamii nzima ya Wapalestina imelazimika kuondoka katika ardhi hiyo.
Tuliendesha gari hadi al-Qanoub tukiwa na Ibrahim Shalalda, 50, na mjomba wake Mohammed mwenye umri wa miaka 80, ambaye alituambia nyumba zao ziliharibiwa na walowezi Novemba mwaka jana.
Tulipokaribia, mlowezi mmoja mwenye msimamo mkali alifunga barabara kwa gari lake. Na Waisraeli wenye silaha wakaja. Baadhi yao ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), na mmoja ni afisa wa usalama wa makazi ya walowezi - walitusimamisha kwa ukaguzi.
Mlinzi wa makazi hayo aliwalazimisha wakulima wawili wa Kipalestina kutoka kwenye gari na kuwapekua. Baada ya saa mbili, askari wa IDF waliwatawanya walowezi na kuruhusu gari la BBC kuondoka.
Kuzuia taifa la Palestina

Israel ilianza kuweka makazi ya Walowezi katika Ukingo wa Magharibi mara baada ya kuuteka kutoka Jordan na kuukalia kwa mabavu zaidi ya miongo mitano iliyopita. Serikali zilizofuata tangu wakati huo zimeruhusu upanuzi wa makazi ya walowezi.
Kwa sasa takribani Wapalestina milioni tatu wanaishi katika ardhi hiyo - ukiondoa Jerusalem Mashariki inayoshikiliwa na Israel - pamoja nusu milioni ya Waisraeli katika zaidi ya makazi 130.
Bezaleli Smotrich kutoka serikali ya mrengo mkali wa kulia ambaye ni Waziri wa Fedha tangu mwaka 2022, anaahidi kuongeza mara mbili idadi ya walowezi.
Smotrich anaamini Wayahudi wana haki waliyopewa na Mungu kwa nchi hii. Anaongoza mojawapo ya vyama viwili vya siasa kali za mrengo wa kulia, vinavyounga mkono walowezi, ambavyo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alivileta katika muungano wake wa serikali baada ya uchaguzi wa 2022.
Smotrich anahudumu kama waziri wa fedha lakini pia ana wadhifa katika wizara ya ulinzi, ambao umemruhusu kufanya mabadiliko makubwa kwa sera za Israel katika Ukingo wa Magharibi.
Amewekeza kwa kiasi kikubwa fedha za serikali katika makazi ya walowezi, ikiwa ni pamoja na barabara mpya na miundombinu. Lakini pia amechukua mamlaka kutoka kwa jeshi, ili kuharakisha ujenzi wa makazi ya walowezi.
Katika matamshi yaliyorekodiwa kwa siri akiwaambia wafuasi wake, Smotrich alijigamba kuwa anafanya kazi kubadilisha DNA ya mfumo juu ya utanuzi wa makazi, na itakuwa rahisi kueleweka katika sheria na muktadha ya kimataifa.
Wazalendo wa kidini walikuwa pembeni mwa siasa za Israel kwa miongo kadhaa. Lakini itikadi yao polepole imekuwa maarufu zaidi. Katika uchaguzi wa 2022, vyama hivi vilichukua viti 13 katika bunge la Israel lenye viti 120 na kuwa katika muungano wa mrengo wa kulia wa Netanyahu.
Wakati wa vita, Bezalel Smotrich na mwenzake mwenye itikadi kali Itamar Ben-Gvir, ambaye sasa ni waziri wa usalama wa taifa wa Israel, wametoa maoni yanayochochea mgawanyiko wa kijamii mara kwa mara na kuwachokoza washirika wa nchi za Magharibi wa Israel.
Baada ya jeshi la Israel kuwakamata askari wa akiba wanaotuhumiwa kumnyanyasa kingono mfungwa wa Kipalestina, Ben Gvir alisema ni "aibu kwa Israel kuwakamata mashujaa wetu bora." Mwezi huu, Smotrich alisema inaweza kuwa "halali na ndani ya maadili kuwanyima chakula watu wa Gaza.”
"Hili ni kundi la Waisraeli ambao wanapinga aina yoyote ya maelewano na Wapalestina au majirani wengine (Waarabu) wa Israel," anasema Anshel Pfeffer, mwanahabari mkongwe kutoka Israel na mwandishi wa The Economist.
Kwa sababu ya vita huko Gaza, upande huo umeona fursa mpya. Smotrich ametoa wito kwa wakaazi wa Palestina kuondoka, na kutoa nafasi kwa Waisraeli ambao wanaweza "kufanya jangwa kuchanua."
Ingawa Netanyahu amefutilia mbali uwezekano wa kurejeshwa kwa makaazi ya Wayahudi huko Gaza, bado ana deni kwa vyama vya mrengo wa kulia vinavyotishia kusambaratisha muungano wake ikiwa atatia saini makubaliano ya "kizembe" ya kusitisha mapigano ili kuwarudisha nyumbani mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas kwa sasa.
Mawazo ya watu wenye msimamo mkali yaweza kuwa ya wachache miongoni mwa Waisraeli. Lakini yanasaidia kurefusha vita, na kubadilisha kwa kiasi kikubwa mazingira ya Ukingo wa Magharibi - na kusababisha uharibifu wa muda mrefu kwa mpango wa amani.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuchapishwa na Seif Abdalla








