Je, walowezi wa Israel wenye itikadi kali wanaolengwa na vikwazo vya Marekani na Uingereza ni akina nani?

Wapalestina katika Jiji la Kale la Hebroni walifunga madirisha ili kujikinga na ghasia

Chanzo cha picha, Getty Images

Uingereza ilitangaza Jumatatu kwamba itawawekea vikwazo raia wanne wa Israel, wanaochukuliwa kuwa walowezi wenye itikadi kali ambao wanadaiwa kutekeleza mashambulizi makali dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.

Hatua hiyo ya Uingereza imekuja baada ya hatua sawa na ya Marekani mapema mwezi huu.

Kwa mujibu wa serikali ya Uingereza, vikwazo hivyo ni pamoja na vikwazo vikali vya kifedha na usafiri vilivyowekwa kwa watu hao wanne, ambao wanadaiwa kufanya "ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu".

"Walowezi wa Israel wenye itikadi kali wanawatishia Wapalestina, mara nyingi kwa kuwanyooshea bunduki, na kuwafukuza kutoka katika ardhi ambayo ni mali yao," alisema Waziri Mkuu wa zamani David Cameron, ambaye sasa ni waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Uingereza, katika taarifa yake.

​"Tabia hii ni kinyume cha sheria na haikubaliki," waziri huyo aliongeza.

Waisraeli wanne ambao watakabiliwa na zuio la mali, marufuku ya kusafiri na kughairiwa kwa visa nchini Uingereza ni Moshe Sharvit, Yinon Levy, Zvi Bar Yosef na Ely Federman.

Cameron

Chanzo cha picha, Getty Images

Vikwazo vya Marekani

Mapema mwezi huu, Rais wa Marekani Joe Biden pia aliidhinisha vikwazo dhidi ya walowezi wanne wa Israel wanaotuhumiwa kuwashambulia Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Biden alitia saini akitangaza kwamba ghasia katika Ukingo wa Magharibi zimefikia "viwango visivyovumilika."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Vikwazo huzuia watu hawa kufikia mali na mfumo wa kifedha wa Marekani.

Uamuzi wa Marekani, ambao sasa unafuatwa na Uingereza, uliangazia kuongezeka kwa ghasia katika Ukingo wa Magharibi tangu Hamas ilipoanzisha shambulio dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, hadi mwanzoni mwa Februari, Wapalestina 370 walikuwa wameuawa katika Ukingo wa Magharibi. Wengi wao waliuawa na vikosi vya Israeli, lakini takribani wanane waliuawa na walowezi wa Israeli, kwa mujibu wa UN.

Amri hiyo mpya ya utendaji ina maana kwamba serikali ya Marekani ina mamlaka ya kuweka vikwazo kwa mgeni yeyote anayeshambulia, kutisha au kunyakua mali ya Wapalestina.

Idara ya Hazina ya Marekani iliwataja Waisraeli wanne waliowekewa vikwazo kuwa ni David Chai Chasdai, 29; Yinon Lévi, umri wa miaka 31; Einan Tanjil, umri wa miaka 21; na Shalom Zicherman, 32.

Watatu kati yao waliishi katika makazi katika Ukingo wa Magharibi na mmoja aliishi karibu na mpaka wa eneo linalokaliwa, kama Hazina ilivyoripoti.

Rais Biden alisema ghasia katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa ni "tishio kubwa kwa amani, usalama na utulivu."

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda mfupi baada ya Biden kutia saini amri hiyo ya utendaji, Israel ilionesha kutofurahishwa, ikiwaita walowezi wengi wa Ukingo wa Magharibi "wanaofuata sheria."

Taarifa hiyo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imesisitiza kuwa Israel inachukua hatua dhidi ya wakosaji wote popote walipo, ikisema kwamba hatua za ajabu si za lazima.

Kutokubaliana huku hadharani kunaonesha mgawanyiko unaokua kati ya Marekani na Israel. Ingawa viongozi hao wawili wamekuwa washirika wa muda mrefu, kutofautiana kumeibuka hivi karibuni kuhusu wazo la kuunda taifa huru la Palestina.

Marekani inatetea suluhisho la "serikali mbili", ikizingatiwa kuwa ni muhimu kwa utulivu wa muda mrefu katika eneo hilo, wakati Netanyahu amekataa mara kwa mara pendekezo hilo.

Mwezi uliopita, Ikulu ya White House ilikubali kwamba serikali za Marekani na Israel "zinaona mambo kwa uwazi", na hivyo kufifisha matumaini ya kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya kidiplomasia na kukwama kwa mchakato wa amani kati ya Israel na Palestina.

Jinsi ghasia hizo zilivyoathiri wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi

Tangu kuanza kwa vita huko Gaza, ghasia dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi zimeongezeka sana. Mbali na Wapalestina wanane waliouawa, wengine 84 walijeruhiwa na walowezi, kulingana na UN.

Kufikia mapema 2024, idadi ya watu wanaoishi katika makazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki ilizidi 700,000.

Makazi haya ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa, ingawa Israel inapinga ufafanuzi huu.

Baadhi ya wakazi wao ni sehemu ya vuguvugu la walowezi wa Kiyahudi lenye itikadi kali na la kidini. Wanaamini kuwa wanarudisha ardhi ya kibiblia ya Yudea na Samaria, Ukingo wa Magharibi wa leo, kwa Israeli.

Mtazamo huu wa wito wa kimungu unawatofautisha na jumuiya nyingine za walowezi wanaohamia maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kwa sababu za kiuchumi au kusaidia kuimarisha usalama wa Israeli katika eneo hilo.

Lakini kinachowaunganisha wote ni imani kwamba wanayo haki, iwe Mungu amewapa au la, kudai ardhi katika Ukingo wa Magharibi.

Rabi wa Kizayuni Moshe Levinger (kushoto) akisherehekea makazi mapya katika Ukingo wa Magharibi katika miaka ya 1970.

Chanzo cha picha, Getty Images

Zamani karika eneo hilo

Imeandikwa sana kwamba familia za Wayahudi na Waarabu ziliishi pamoja katika Yerusalemu. Hata hivyo, mji huo ulipogawanywa kati ya Israel na Jordan kufuatia Vita vya Waarabu na Waisraeli vya 1948, familia za Kiyahudi zilikimbia makazi yao huko Jerusalem Mashariki, huku Waarabu wakikimbia makazi yao magharibi mwa Jerusalem.

Harakati za kisasa za makazi zilianza katika miongo iliyofuata, baada ya Vita vya Siku Sita mnamo 1967, wakati Israeli iliposhinda Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki kutoka kwa Jordan na washirika wake wa Kiarabu.

Katika miezi iliyofuata vita, makao ya kwanza ya kidini, Kfar Etzion, yalianzishwa. Leo, karibu watu 40,000 wanaishi katika makazi haya, yaliyoko katika mpaka kati ya Israeli na Ukingo wa Magharibi.

Mwaka mmoja baadaye, Rabi wa Kidini wa Kizayuni Moshe Levinger na wafuasi wake waliingia Hebroni kusherehekea sikukuu ya Kiyahudi ya Pasaka, lakini hawakuondoka. Huko, kwenye viunga vya mji, yeye na wafuasi wake walianzisha Kiryat Arba.

Tofauti na Kfar Etzion, ambaye alinufaika na usaidizi wa serikali, Rabbi Levinger na wafuasi wake walikaa Hebron kwa kudharau serikali, anaelezea mwandishi na profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha Montreal, Yakov Rabkin. Wanahistoria na wataalam kwa upana wanaichukulia hii ya mwisho kuwa sehemu ya mabadiliko katika harakati za ukoloni wa kidini.

“Wao [walowezi wa kidini] wameenda kwenye vilima na sehemu mbalimbali zinazotajwa katika Biblia na kujaribu kukaa huko, kwa sababu wanachotaka ni kuwa na maeneo yote ya Biblia,” Rabkin aeleza.

Leo, idadi ya jumuiya za walowezi ni zaidi ya 300 katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, kulingana na NGO ya Israel Paz Agora. Inasema kuwa kuna makoloni 146 na vituo 154 vya nje. Licha ya sheria za kimataifa, Israel inachukulia makazi kuwa halali lakini inafafanua vituo vya nje kuwa haramu.

Neve Gordon, profesa wa sheria za kimataifa na haki za binadamu katika Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London, anadokeza kwamba jumuiya zinazoanza kama vituo vya nje mara nyingi huishia kuhalalishwa na taifa la Israeli.

"Wataleta aina moja ya msafara, kisha msafara mwingine. Na kidogo kidogo, watapata ardhi zaidi na familia nyingine itakaa huko. Kesho yake, jeshi linakuja na kuweka askari wanne au watano huko kulinda ardhi."

Muonekano wa makazi ya Kiyahudi ya Kiryat Arba huko Hebroni, miaka 12 baada ya kuanzishwa kwake

Chanzo cha picha, Getty Images

Leo, Uzayuni wa kidini ni sehemu ya wigo wa kisiasa katika Israeli.

Hili linaungwa mkono na msukumo wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia kuingia katika shukurani kuu kwa serikali ya mseto ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

“Wana tabia ya kutoa kauli za uchochezi zaidi. Ni rahisi kutambuliwa kama ishara za mkondo huu wa itikadi kali wa Israeli ambao unaenea katika serikali nzima," anaelezea Natasha Roth-Rowland, mtafiti wa Kiyahudi.

Kiongozi wa Chama cha Settler na Mzayuni wa kidini Bezalel Smotrich amekuwa akitetea ujenzi wa makazi zaidi katika Ukingo wa Magharibi na, katika chapisho kwenye X, ambalo zamani lilijulikana kama Twitter, alitumia lugha ya uchochezi akiwaita Wapalestina Wanazi.

Mnamo Novemba, kama waziri wa fedha, alipendekeza kuongezeka kwa uwepo wa jeshi la Israeli na kutoa wito wa kupiga marufuku uchumaji wa mizeituni ya Wapalestina karibu na makazi ya Israeli.

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir ni jina lingine linalohusishwa sana na harakati za ukoloni wa kidini. Anaishi katika makazi ya Kiryat Arba na anasimamia polisi wa ndani wa Israeli na vile vile vikosi vya mpaka vya nchi hiyo katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.

Alikuwa mwanachama wa vuguvugu la Kach lenye msimamo mkali, lililoanzishwa na Rabbi wa Marekani Meir Kahane, ambalo sasa limepigwa marufuku nchini Israel chini ya sheria za kupambana na ugaidi. Ben-Gvir amewahi kuhukumiwa kwa kuchochea ubaguzi wa rangi na kuunga mkono ugaidi.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga