Kwa nini Iran inataka vita vyake dhidi ya Israel na Marekani viendelee?

Chanzo cha picha, Reuters

Chanzo cha picha, Atta KENARE / AFP via Getty Images
Maafisa wa Iran wamekuwa wakitoa ujumbe kuwa wako tayari "kwa vita vya muda mrefu"
Ali Larijani, katibu wa baraza la usalama la Iran, alisema tarehe 2 mwezi Machi kuwa wako tayari kwa vita vya muda mrefu.
"Iran, tofauti na Marekani, tumejiandaa kwa vita vya muda mrefu" alisema.
Pia alipuuzilia uwezekano wa kufanya mazungumzo, na kusema hakuna muda sahihi wakusitisha kulipiza mashambulio ya Israel na Marekani.
Hii inamaanisha vita hivyo vinaweza kudumu kwa miezi kadhaa au zaidi.
Tarehe 8 mwezi Machi, spika wa bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf alisema "hatutaki mazungumzo ya kusitisha vita, lazima tumuadhibu adui."
Pia aliongozea kuwa taifa lake linapigana kushinda dhidi ya Israel.
Msemaji wa wizara ya ulinzi Brigedia Reza Talay-Nik alisema "Iran inaweza kujilinda kwa muda mrefu kuliko adui wetu"
Aliongezea kuwa Iran inadhibiti jinsi inatumia silaha zake, na kuhifadhi silaha za kisasa zaidi.
Mkakati wao ni upi?

Chanzo cha picha, Morteza Nikoubazl/NurPhoto via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wachambuzi wengi wanasema mkakati wa Iran ni kutegemea "uchovu wa vita."
Iran bado inaendelea kuishambulia Israel, na kambi za kijeshi za Marekani katika mataifa ya Ghuba kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani.
Mashambulio hayo yana malengo tofauti.
Kwanza, mkakati huo unahitaji mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani na Israel kubaki ikiwa inafanya kazi muda wote ili kuzuia makombora na ndege zisizo na rubani za Iran.
Mifumo ya Marekani ya ulinzi wa anga na makombora, kama vile Patriot missile system na Terminal High Altitude Area Defense (THAAD), ni ya teknolojia ya hali ya juu sana, lakini ni ghali mno na pia idadi ya vifaa hivyo ni ndogo.
Mara nyingi, kombora au droni wanayoidungua huwa na thamani ndogo sana ikilinganishwa na silaha wanayotumia kuidungua.
Hii ina maana kwamba droni za bei nafuu za Iran zinaharibiwa kwa kutumia silaha za bei ghali.
Pili, mashambulizi yanayoendelea yanaweza kuweka shinikizo kubwa kwenye akiba ya makombora ya kuzuia mashambulizi, mitandao ya usafirishaji na usambazaji wa vifaa vya kijeshi, pamoja na utayari wa kijeshi.
Kulingana na ripoti ya The Washington Post, katika wiki ya kwanza ya operesheni, vikosi vya Marekani vilikuwa vinatumia silaha za hali ya juu pamoja na makombora ya ulinzi wa anga.
Baadhi ya wachambuzi wanasema matumizi haya makubwa ya silaha yanaonyesha udhaifu katika mfumo wa usambazaji wa vifaa vya kijeshi.
Maafisa wa Iran wanasema kuwa akiba yao ya silaha ni endelevu zaidi, na kwamba majeshi yao "yanaweza kuendeleza vita hivyo kwa kasi hii kwa angalau miezi sita."
Makomanda wa Iran wanasema kuwa uzalishaji wa makombora unafanywa ndani ya nchi hiyo, huku wakiwa na vituo vingi vya uzalishaji, na akiba kubwa ya silaha ambayo inaiwezesha Iran kuendelea na mashambulizi kwa muda mrefu.
Iran pia inaonekana kueneza mashambulizi yake kwa muda mrefu, na hivyo kuwalazimisha washambulizi wake kuendelea kujilinda kila wakati.
Mkakati huu ni sehemu ya mafunzo pana ya kijeshi ambayo Iran imeendeleza kwa miongo kadhaa ili kukabiliana na maendeleo ya kijeshi ya mataifa makubwa na yenye nguvu zaidi.
Baada ya vita vya Iran-Iraq ya miaka ya 1980, mkakati wa vita wa Iran ulilenga kupambana na majeshi yenye nguvu zaidi bila wao kuwa na nguvu sawa za kijeshi.
Lengo halikuwa kumshinda adui moja kwa moja, bali kufanya vita viwe vigumu, virefu, na visivyotabirika.
Athari za kiuchumi

Chanzo cha picha, Fadel SENNA / AFP via Getty Images
Mzozo wa muda mrefu unaweza kuwa na athari kubwa za kiuchumi ndani ya Iran na pia duniani kote.
Kuna hatari ya kusambaratika kwa mfumo wa usambazaji wa nishati kutoka eneo hilo, jambo ambalo linaweza kusababisha kupanda kwa bei ya nishati na biashara duniani.
Takribani asilimia 20 ya mafuta ya dunia hupitia eneo la bahari la Strait of Hormuz, lakini zaidi ya wiki moja baada ya vita kuanza, usafiri katika njia hii nyembamba ya baharini imesitishwa.
Njia za biashara za kikanda pia zimeathiriwa na wasiwasi wa kiusalama pamoja na kufungwa kwa anga ya baadhi ya mataifa muhimu kibiashara tangu mzozo huo uanze.
Iran pia iko chini ya shinikizo la kiuchumi. Uchumi wake tayari umedhoofishwa na vikwazo vya kimataifa, na katika hali ya vita, shinikizo hilo linaweza kuongezeka zaidi kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya kijeshi, kuyumba kwa thamani ya sarafu ya Iran, pamoja na kuathirika kwa sekta za biashara na utoaji huduma.
Wachambuzi wanasema kwamba ikiwa mzozo huu utaendelea kwa muda mrefu, unaweza kusababisha kudorora kwa uchumi kwa kiwango kikubwa na kulemaza shughuli nyingi.
Maafisa wa Iran wameendelea kusisitiza kuwa kulinda raia na kushiriki katika maandalizi ya vita ni wajibu wa kitaifa. Serikali ya Iran inaendelea kuhakikisha inapata uungwaji mkono wa wananchi ndani ya nchi.
Hatari za kisiasa ni zipi?

Chanzo cha picha, Arezoo / Middle East Images / AFP via Getty Images
Kadri mzozo unavyoendelea kwa muda mrefu, ndivyo hatari za kisiasa zinavyoongezeka kwa pande zote zinazohusika.
Nchi nyingi katika eneo la Ghuba zimeelezea hofu ya kupata hasara za kiuchumi ikiwa vita vitaendelea kwa muda mrefu.
Katika baadhi ya nchi hizi, ambako Iran inashambulia kambi za kijeshi za Marekani, Iran imekuwa ikiita mashambulizi hayo kuwa ni kulenga "mali na kambi za mshambuliaji."
Baadhi ya nchi hizo pia zimeomba mazungumzo ya kidiplomasia yarejelewe ili kusitisha mapigano.
Aidha, mapigano yanayoendelea yanaweza kubadilisha miungano ya kikanda na hata kuyageuza mataifa jirani kuwa wapinzani wa Iran.
Changamoto kwa Iran ni kusawazisha mkakati wake wa kijeshi na nguvu ya kiuchumi pamoja na kudhibiti hali ndani ya nchi hiyo.
Changamoto inayoikabili Marekani na Israel inaweza kuwa jinsi ya kudhibiti gharama za kimataifa za kiuchumi, kisiasa na athari za vita vya muda mrefu huku wakiendelea na operesheni za kijeshi.















