Israel na Marekani wataamuaje wameshinda vita dhidi ya Iran?

Chanzo cha picha, Atta Kenare/AFP
Kulingana na kauli za viongozi wa Marekani na Israel, vita dhidi ya Iran vina malengo kadhaa ya kisiasa, muhimu zaidi yakiwa ni kubadilisha utawala wa Iran na kuharibu mipango yake ya nyuklia na makombora. Hata hivyo, bado haijulikani ni lini wataweza kujua kama malengo hayo yameafikiwa.
Kuwa na lengo la kisiasa lililo wazi ni jambo muhimu kwa sababu kufanikiwa kwake kunamaanisha mwisho wa vita.
Lengo hilo husaidia kutathmini muda ambao vita vinaweza kuchukua na mwelekeo wake, lakini muhimu zaidi linawapa fursa wanaoshiriki vita hivyo kuelewa ni hatua gani zinapaswa kuchukuliwa ili kufikia mwisho wa mgogoro huo au wameshinda vita hivyo.
Israel na Marekani bado hawajatangaza nia ya kutuma wanajeshi wao ndani ya Iran, taifa ambalo ukubwa wake ni Zaidi ya mataifa ya Ulaya isipokuwa Urusi.
Aidha maeneo mengi ya Iran, yamejaa milima, ambayo inafanya kuwa vigumu kupigana vita eneo hilo.
Makombora ya Iran
Hakuna takwimu za wazi zinazoonyesha idadi ya makombora inayozalishwa nchini Iran au idadi ya vifaa vya kurusha makombora walivyonavyo.
Mtaalam wa masuala ya usalama kutoka Israel David Gendelman aliambia BBC idhaa ya Urusi, kuwa kulingana na ripoti ya ujasusi ya Israel, Iran inamiliki takriban makombora 2500 hadi 3000 mwaka wa 2025. Makombora hayo yanaweza kuenda umbali wa kilomita 1000 hadi 3000.
Taasisi ya kiyahudi ya The American think tank, walidhiitisha idadi hiyo katika ripoti yao iliyochapishwa mwezi Februari mwaka wa 2026. Kulingana na taasisi hiyo, Iran haina makombora yanayoweza kuenda umbali wa Zaidi ya kilomita 2000.
Kulingana na Gendelman, ujasusi wa Israel unaamini kuwa Iran inaweza kuongeza makombora yake yenye umbali wa wastan hadi kufikia 8000 kwa kipindi cha miaka miwili, nah ii ilichochea kuanza kwa vita vilivyotokea mwezi Juni mwaka wa 2025.
Kando na makombora yenye umbali wa wastan, Iran pia ina makombora yanayoweza kurushwa kwa umbali mfupi wa kilomita 500 hadi 1000.
Makombora haya si tishio kwa usalama wa Israel, ila ni tishio kwa mataifa ya Ghuba. Kulingana na mtaalam huyo, Iran ina makombora haya kwa wingi.
Kando na makombora ya kibalistiki, Iran pia ina makombora ya majini na droni za Shahed, ambazo Urusi inatumia kutekeleza mashambulizi nchini Ukraine. Hizi zina hatari yake kivyake. Kujikinga dhidi yake kunahitaji mfumo tofauti wa ulinzi wa anga.

Chanzo cha picha, Win McNamee/Getty Images
Kushambulia na kuharibu makombora ya Iran ilikuwa lengo kuu la Israel katika vita walizoanzisha mwaka wa 2025.
Kulingana na David Gendelman, ingawa mpango wa makombora wa Iran uliathirika pakubwa wakati wa vita na Israel, waliweza kurejelea uzalishaji wa makombora hayo mwaka wa 2026.
Miezi kadhaa iliyopita, Iran imeonyesha kustahimili mashambulizi baada ya vituo vyao vya makombora kulengwa.
Mashambulizi ya chini ya ardhi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Taasisi ya utafiti ya Marekani, ya Jewish Institute for National Security Affairs, imechapisha katika ripoti yake kwamba makombora ya Iran yanahifadhiwa katika vituo vingi, vikiwemo vile vinavyojulikana kama "miji ya makombora" vilivyo chini ya ardhi.
Kabla ya operesheni ya kijeshi iliyofanywa na Israel na Marekani, kulikuwa na vituo 24 vya aina hiyo vilivyoko karibu na mji wa Kermanshah magharibi mwa Iran, katika jimbo la milimani la Lorestan, na katika milima ya Zagros.
Ripoti hiyo pia inasema kwamba makombora ya kibalistiki ya masafa mafupi huenda yamehifadhiwa magharibi mwa Iran kwa sababu yakulenga mataifa ya Ghuba.
Makombora ya cruise yapo katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ili yaweze kushambulia maeneo yaliyoko magharibi na kusini mwa Iran. Miundombinu ya ndege zisizo na rubani pia inajumuisha vituo vya chini ya ardhi, viwanja vya ndege, na vituo vya uzalishaji vilivyoenea katika maeneo ya kati, magharibi na kusini mwa Iran.

Chanzo cha picha, EPA
Maeneo haya mengi yana njia ya chini ya ardhi ambayo hutumika kurusha makombora na wakati huo huo hutumika kama maeneo ya kujificha baada ya kutekeleza shambulizi.
Ila katika mfumo huu ni vigumu sana kujua athari ya shambulio lililotekelezwa, Gendelman anasema ni kwa mashirika ya kijasusi kutangaza athari iliyotokea.
Ila kufikia sasa hakuna udhibitisho kuwa handaki za Iran zimeharibiwa.
Mradi wa Nyuklia
Ingawa mpango wa makombora wa Tehran ni tishio duniani, mpango wake wa nyuklia unawapa wasiwasi mataifa ya magharibi.
Waziri wa ulinzi wa Israel Benjamin Netanyahu,alisema vita dhidi ya Iran inafaa kuanza sasa, ili kuzuia Iran kumaliza kutengeneza mpango wake wa nyuklia na kuwa na nguvu na huenda ikawa vigumu kuishambulia.
Msemaji wa ikulu ya White House Carolyn Leavitt, alisema lengo kuu la kuishambulia Iran ni kulemaza azma yao ya kumiliki silaha za nyuklia.
Tofauti na mpango wa makombora wa Iran, mpango wao wa nyuklia una vituo tofauti za utafiti na kuzalisha silaha hizo, na imekuwa vigumu kujua ni wapi haswa uzalishaji wa silaha hizo unafanyika.
Vituo hivi vililengwa mwaka uliopita. Ndege za Marekani na Israel zililenga kituo cha utafiti wa nyuklia cha Isfahan, pamoja na vituo vya kuzalisha urani vya Natanz na Fordow.
David Gendelman anaelezea kuwa hakuna taarifa, kuhusu mpango wa nyuklia unaoendelea nchini Iran kwani shughuli nyingi zinafanyika chini ya ardhi.
Pia kuna swala la madini ya urani, haijulikani Iran ina kiwango gani cha madini haya ambayo imehifadhi chini ya ardhi.
Kulingana na Andrea Stricker, naibu mkurugenzi katika shirika la Foundation for Defense democracies, aliambia BBC idhaa ya Urusi kuwa, Israel na Marekani wako na wasiwasi kuhusu Iran kurejelea kutengeneza silaha za nyuklia.
Mtaalamu huyo anasema kuwa kituo cha chini ya ardhi katika eneo la Koh Kalang Ghazla ambacho Wamarekani wanakiita Mount Kirk ni eneo moja ambalo silaha za nyuklia huenda zinatengenezwa. Eneo hilo liko karibu na Natanz, mahali palipokuwa kituo kikuu cha Iran cha kutengeneza urani. Kituo cha Natanz kilikuwa mojawapo ya maeneo yaliylengwa katika operesheni ya Marekani na Israel katika mashambulizi ya mwaka 2025.
Orodha ya maeneo ambayo Andrea Stricker anasema shughuli zake zimevutia umakini wa Israel na Marekani pia inajumuisha Taleghan-2 na Isfahan, ambapo ni vigumu kutathmini hali ilivyo baada ya mashambulizi ya mwaka 2025.
Pia kuna kituo cha mabomu ya ardhini kilicholengwa na ndege za Israel katika vita vya sasa.
"Hakuna uhakika kwamba utawala huo hautarejelea uwezo wao wa kupata silaha za nyuklia siku zijazo, isipokuwa kama Marekani na Israel wataweza kuwashawishi viongozi waliobaki kuachana na wazo hilo, au utawala huo pamoja na viongozi wenye mawazo kama yao wataondolewa madarakani," anasema Andrea Stricker.
Mashambulizi ya anga yanaweza kutumika kushinda vita hivi?
Mark Urban, mchambuzi wa masuala ya kijeshi kutoka Uingereza na mwandishi wa zamani wa BBC, ameandika kwenye blogu yake kwamba Marekani inaweza kutangaza ushindi wakati wowote, lakini nini kitatokea ikiwa Iran haitasitisha vita?
Anasema:
"Huenda Iran, ikakataa kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano. Kiongozi wao anayeheshimika ameuawa na sehemu kubwa ya uongozi wa Islamic Revolutionary Guard Corps imeondolewa. Hisia zimepanda sana na hamu ya kulipiza kisasi ni kubwa."
Mark Urban anaendelea kuandika kwamba:
"Iran itajipa muda, itaendelea kuhifadhi na kulinda maeneo yake ya kurusha makombora, na itajaribu kuongeza uzalishaji wa ndege zisizo na rubani."
Anaongeza kuwa yote haya yatafanywa kwa matumaini ya kuwachosha Wamarekani kupitia mambo kadhaa: shinikizo kutoka kwa washirika wao kutokana na madhara makubwa ya kiuchumi ya vita vinavyoendelea, kukosa subira kwa Donald Trump, pamoja na kupungua kwa akiba ya silaha za ulinzi na mashambulizi za Marekani.
Kwa maneno mengine, mkakati huo unamaanisha kuendeleza vita kwa muda mrefu ili kujaribu kupunguza uwezo na uvumilivu wa United States na washirika wake.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa kijeshi, Iran pia imekuwa ikitegemea zaidi droni za bei nafuu na kuhifadhi makombora yake, ili kuweza kuendeleza mashambulizi kwa muda mrefu licha ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya maeneo ya kurusha makombora ya Iran.

Chanzo cha picha, Majid Saeedi/Getty Images
Ili kuyumbisha eneo la Mashariki ya Kati, Iran haitahitaji hazina kubwa ya silaha za kurusha makombora vinavyoweza kurusha makombora kadhaa kwa wakati mmoja. Hata kurusha kombora moja moja kunaweza kutosha. Hili linaweza lisionekane kama ushindi kwa Iran, lakini litazuia Israel na Marekani kutangaza ushindi.
David Gendelman anasema:
"Kadri tu utawala huu unavyoendelea kuwepo, utajenga upya kila kitu kilichoharibiwa, hata kama italazimika kuanza kutoka mwanzo kabisa. Kwa hiyo hata sasa, mradi tu utawala huu upo, utajenga upya mpango wa makombora, mpango wa nyuklia, na kadhalika."















