Walowezi wa Kiyahudi wanaotaka kujenga makazi huko Gaza

Nani hataki nyumba eneo la pwani? Kwa baadhi ya upande wa kulia wa Israeli, ufuo unaohitajika sasa unajumuisha mchanga wa Gaza.
Muulize tu Daniella Weiss, 78, nyanya wa vuguvugu la walowezi la Israel, ambaye anasema tayari ana orodha ya familia 500 tayari za kuhamia Gaza mara moja.
"Nina marafiki huko Tel Aviv," anasema, "hivyo wanasema, 'Usisahau kuniwekea shamba karibu na pwani ya Gaza,' kwa sababu ni pwani nzuri, nzuri, mchanga mzuri wa dhahabu".
Anawaambia viwanja vilivyoko ufukweni tayari vimehifadhiwa.
Bibi Weiss anaongoza shirika la walowezi wenye itikadi kali linaloitwa Nachala, au nchi ya nyumbani.
Kwa miongo kadhaa, amekuwa akianzisha makazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israeli na Jerusalem Mashariki, kwenye ardhi ya Palestina iliyotekwa na Israeli katika vita vya Mashariki ya Kati vya 1967.
Baadhi ya vuguvugu la walowezi wamefurahia ndoto ya kurejea Gaza tangu mwaka 2005, wakati Israel ilipoamuru kuondoka, makazi 21 yalivunjwa na takribani walowezi 9,000 walihamishwa na jeshi. (Nikiripoti kutoka Gaza wakati huo, niliona wengi ambao walitolewa nje.)
Walowezi wengi waliona haya yote kama usaliti wa serikali, na kosa la kimkakati.
Kura za maoni zinaonesha kuwa Waisraeli wengi wanapinga kuwekwa upya kwa Gaza, na sio sera ya serikali, lakini tangu mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba inazungumzwa kwa sauti kubwa na baadhi ya sauti kubwa na kali zaidi katika serikali ya Israeli.
Bibi Weiss ananionesha kwa fahari ramani ya Ukingo wa Magharibi yenye vitone vya waridi vinavyoonesha makazi ya Wayahudi.
Alama zimetawanyika kwenye ramani, zi kila ardhi ambayo Wapalestina wanatumai au walitarajia kujenga nchi yao.
Kuna walowezi wa Kiyahudi wapatao 700,000 katika maeneo haya sasa na idadi ya walowezi inaongezeka kwa kasi.
Idadi kubwa ya jumuiya ya kimataifa inachukulia makazi kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa, likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Israel inapinga hili.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tunakutana na Daniella nyumbani kwake katika makazi ya Ukingo wa Magharibi wa Kedumim, ambako nyumba zilizoezekwa paa jekundu zimeenea juu ya vilima na mabonde. Anaendelea na mwendo licha ya kuwa bado anapona majeraha.
Maono yake kwa mustakabali wa Gaza, ambayo sasa ina Wapalestina milioni 2.3, wengi wao wakiwa na njaa ni kwamba itakuwa ya Kiyahudi.
"Waarabu wa Gaza hawatasalia katika Ukanda wa Gaza," anasema. "Nani atabaki? Wayahudi."
Anadai kwamba Wapalestina wanataka kuondoka Gaza na kwamba nchi nyingine zinapaswa kuwapokea, ingawa katika mahojiano marefu, mara chache hutumia neno "Palestina".
"Dunia ni pana," anasema. "Afrika ni kubwa. Canada ni kubwa. Dunia itawanyonya watu wa Gaza. Tunafanyaje? Tunahimiza. Wapalestina wa Gaza, wazuri, watawezeshwa. Sisemi kulazimishwa, nasema kuwezeshwa kwa sababu wanataka kwenda."
Hakuna ushahidi kwamba Wapalestina wanataka kuondoka katika nchi yao, ingawa wengi wanaweza sasa kuwa na ndoto ya kuondoka kwa muda, kuokoa maisha yao.
Kwa Wapalestina wengi, hakuna njia ya kutoka. Mipaka inadhibitiwa kwa nguvu na Israeli na Misri, na hakuna nchi za kigeni zimetoa kimbilio.
Nilimweleza kwamba maoni yake yanasikika kama mpango wa utakaso wa kikabila. Yeye hakatai.
“Unaweza kuuita utakaso wa kikabila, narudia tena, Waarabu hawataki, Waarabu wa kawaida hawataki kuishi Gaza, ukitaka kuita utakaso ukitaka kuuita ubaguzi wa rangi chagua tafsiri yako. Ninachagua njia ya kulinda taifa la Israeli."
Siku chache baadaye, Daniella Weiss anauza wazo la kurudi Gaza kwenye mkusanyiko mdogo, ulioandaliwa na mlowezi mwingine kwenye sebule yao.
Ana projekta, inayoonesha ramani mpya ya Gaza, kamili na makazi, na vipeperushi vyenye kichwa "Rudi Gaza".
"Watu wananiuliza kuna uwezekano gani hili litatokea?" anasema.
Wachache waliohudhuria wanaonekana kuwa tayari wameshawishika. "Nataka kurudi mara moja," anasema Sarah Manella. "Watakaponipigia simu, nitarejea Gush Katif [kambi ya zamani ya makazi ya Israel huko Gaza]."
Vipi kuhusu watu wanaoishi huko, tunauliza.
"Eneo ni tupu sasa," anajibu. "Sasa huna haja ya kufikiria mahali pa kuweka makazi, unahitaji tu kurudi na kuweka makazi mapya."

Sehemu kubwa ya Gaza imefutwa baada ya karibu miezi sita ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Israeli.
Ni "kaburi kubwa zaidi la wazi" duniani, kwa maneno ya mkuu wa sera za kigeni wa EU, Josep Borrell.
Zaidi ya Wapalestina 32,000 wameuawa, kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Shirika la Afya Ulimwenguni linachukulia data za wizara kuwa za kuaminika.
Kwa baadhi ya baraza la mawaziri la Israel, eneo la Wapalestina, ambalo sasa limejaa damu, liko tayari kwa makazi mapya. Hiyo ni pamoja na Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa mrengo mkali wa kulia wa Israel Itamar Ben Gvir, mlowezi mwenyewe.
Mwishoni mwa Januari, alipitia ukumbi wa mikutano uliojaa, akisimamishwa kwa kukumbatiana na kupeana mikono. Alikuwa miongoni mwa marafiki wapatao 1,000 wenye imani kali zaidi wakishinikiza kurejea Gaza katika tukio kauli mbiu 'Makazi Huleta Usalama'.
Bw Ben Gvir, ambaye anapendelea "kuhimiza uhamiaji", alikuwa miongoni mwa mawaziri kumi na wawili waliohudhuria.
"Ni wakati wa kurudi nyumbani," alisema kutoka jukwaani, na kupiga makofi makubwa. "Ni wakati wa kurejea katika ardhi ya Israeli. Ikiwa hatutaki Oktoba 7 nyingine, tunahitaji kurejea nyumbani na kudhibiti ardhi."
Katika kivuli cha mti unaostawi, Yehuda Shimon anacheza na wanawe wawili wachanga, walio katika machela, wakining’inia kwenye matawi.
Amewalea watoto 10 hapa katika kituo cha walowezi katika Ukingo wa Magharibi kiitwacho Havat Gilad, au Shamba la Gilad, karibu na mji wa Palestina wa Nablus.
Kote karibu naye kuna vijiji vya Wapalestina, umbali wa karibu zaidi wa mita 500. Hakuna mawasiliano kati yao, anasema.

Shimon ameishi Gaza hapo zamani na anadai haki aliyopewa na Mungu ya kurudi.
"Lazima tufanye hivyo. Ni sehemu ya eneo la Israeli," anasema. "Hii ndiyo nchi ambayo Mungu alitupa, na haungeweza kwenda kwa Mungu na kumwambia, 'Sawa ulinipa, na niliwapa watu wengine.' Hapana. Naamini mwisho tutarejea Gaza."
Nauliza hii ina maana gani kwa Wapalestina.
"Wana maeneo mengine 52 ya kwenda duniani," anasema, "nchi 52 za Kiislamu". Anasema Gaza mpya itakuwa "Tel Aviv nyingine".
Vikosi vya nje kama vyake vinaongezeka katika Ukingo wa Magharibi, pamoja na makazi makubwa, kugawanya eneo la Palestina na kuzua mvutano.
Mashambulizi ya walowezi dhidi ya Wapalestina yameongezeka tangu tarehe 7 Oktoba kulingana na Umoja wa Mataifa, ambao umelaani makazi hayo kwa muda mrefu kama "kizuizi cha amani".
Na sasa mashirika ya walowezi yameweka tena macho yao Gaza.
Je, kuna matarajio ya kweli ya walowezi kufika ufukweni mwa Gaza?
Mwandishi wa habari mahiri wa Israeli aliniambia haitafanyika. "Wito wa kuipatia Gaza makazi mapya hautatafsiriwa kuwa sera," alisema.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga














