Jinsi uchumi wa Israel unavyoathiriwa na vita vya Gaza

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Athari za vita huko Gaza tayari zinaonekana kwenye uchumi wa Israel.

Kulingana na data rasmi iliyotolewa na Ofisi Kuu ya Takwimu ya Israeli mnamo Februari 19, mapato ya kitaifa yalipungua sana katika miezi ya mwisho ya 2023.

Pato la Taifa (GDP), kiashiria muhimu cha utajiri wa nchi, lilipungua kwa karibu asilimia 5 katika robo ya nne ya mwaka jana, mwanzoni mwa mzozo na Hamas, ikilinganishwa na miezi mitatu iliyotanguliwa.

Takwimu hiyo iliwashangaza wataalam, ambao walisema matokeo yalikuwa "mabaya zaidi" kuliko ilivyotarajiwa. Timu ya wachambuzi wa Bloomberg ilikadiria kupungua kwa wastani kwa mwaka kwa kwa kiwango kisichozidi asilimia 10.5.

Kilichoongezwa kwa hili ni uamuzi wa wakala wa mikopo wa Moody's kupunguza viwango vya Israel mapema Februari, ikitaja hatari za kisiasa na kibajeti, pamoja na kuongezeka kwa madai ya udhaifu wa taasisi zilizo na vita huko Gaza.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Moody's kushusha viwango vya Israel, jambo ambalo lilionekana kuwa pigo kwa sura ya kimataifa ya nchi hiyo, kwani wawekezaji wanatumia ukadiriaji huo kubaini hatari ya kuwekeza katika maeneo fulani.

Uamuzi huo wa wakala wa mikopo ulitiliwa shaka na mamlaka ya Israeli.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema uchumi wa nchi yake "uko imara" na kwamba ukadiriaji "hauhusiani na uchumi, lakini unatokana na ukweli kwamba tuko vitani."

"Ukadiriaji utapanda tena mara tu tutakaposhinda vita, na tutashinda," aliongeza.

Vita kati ya Israel na Hamas vilianza tarehe 7 Oktoba, wakati kundi hilo la Kiislamu lenye itikadi kali lilipofanya shambulizi ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel na kuua watu 1,200. Zaidi ya watu 30,000 wameuawa katika mashambulizi yaliyofuata ya Israel huko Gaza.

Licha ya kushuka kwa kasi kwa Pato la Taifa kati ya Oktoba na Desemba, uchumi wa Israeli ulikua kwa asilimia 2 mnamo 2023.

Kabla ya mashambulizi ya Oktoba 7, ulitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 3.5.

Kwa hivyo, kwa kuzingatia hali ya sasa, wachambuzi wengine wanaonya juu ya kile kinachoweza kutokea mnamo 2024.

Liam Peach, mchumi wa masoko yanayoibukia katika Capital Economics, anasema inaonekana kuna uwezekano kwamba mtazamo wa ukuaji wa Isreal kwa mwaka huu utafikia "moja ya viwango vya chini kabisa kwenye rekodi."

Netanyahu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Kushuka kwa matumizi

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Ofisi Kuu ya Takwimu ya Israeli, kushuka kwa Pato la Taifa kulitokana hasa na kushuka kwa matumizi ya ndani, ambayo yalipungua kwa asilimia 26.9.

Kulingana na Eran Yashiv, profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv na mtafiti katika Kituo cha Uchumi, London School of Economics (LSE), hii ni kwa sababu ya upotezaji wa imani ya umma wakati wa vita.

“Watu wana mwelekeo wa kutumia pesa kidogo kwa matumizi ya kawaida; wanaokoa zaidi. Pia hawanunui bidhaa za kudumu wakati wa shida kama hii, kama vile magari, samani au vifaa,” Yashiv aliiambia BBC.

Ofisi Kuu ya Takwimu ilieleza kuwa kushuka kwa Pato la Taifa kulitokea wakati ambapo karibu watu 250,000 waliitwa kupigana vita, wakiacha kazi zao na biashara.

"Kuna mamia ya maelfu ya watu ambao hawafanyi kazi na hawawezi kuchangia katika uzalishaji wa nchi," alisema Josep Comajuncosa Ferrer, profesa wa uchumi katika taasisi ya chuo kikuu cha Esade.

Hii ilisababisha uhaba wa wafanyikazi.

"Soko la ajira nchini Israel limepitia mabadiliko mengi tangu kuanza kwa mzozo na Hamas. Baadhi ya maeneo yanakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi kwani watu wengi hasa vijana wamejiunga na jeshi,” Yashiv alisema.

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

"Pia kuna watu waliohamishwa kaskazini, kwenye mpaka na Lebanoni, na kusini, katika Ukanda wa Gaza. Wengi wamepoteza kazi zao, angalau kwa muda, na hawawezi tena kuendelea kufanya kazi mahali walipo. "anaongeza.

Zaidi ya hayo, wafanyakazi wengi wa Palestina hawaendi tena Israeli.

"Wakati wa amani, Wapalestina wengi kutoka Ukingo wa Magharibi wanavuka mpaka kufanya kazi nchini Israel. Na kwa sasa, kwa sababu za usalama, kuna vikwazo vingi. Matokeo yake, shughuli za kitaaluma zinapungua,” kulingana na Josep Comajuncosa Ferrer.

Ripoti iliyochapishwa na Taasisi ya Taub Center ya Israeli inadai kwamba, kulingana na habari kutoka kwa taasisi kadhaa rasmi, karibu asilimia 20 ya wafanyikazi hawakuhudhuria kazi zao kwa muda mnamo Oktoba 2023.

Sekta ya uwekezaji na mali isiyohamishika

Uwekezaji katika bidhaa za mtaji ni eneo jingine lililoathiriwa sana na vita, na kushuka kwa asilimia 67.8 katika robo ya nne, kulingana na data kutoka Ofisi Kuu ya Takwimu.

Kushuka kwa kiwango kikubwa kulionekana katika uwekezaji wa makazi, kama vile ununuzi wa nyumba au vyumba, ambayo ulichochea mgogoro katika sekta ya mali isiyohamishika, kulingana na wataalam.

“Kwa nini uwekezaji unashuka? Kwa sababu kuna kutokuwa na uhakika mkubwa. Wakati wa vita, hakuna anayetaka kununua nyumba,” anaeleza msomi huyo.

Hali ni mbaya zaidi ikizingatiwa kuwa ukosefu wa vibarua pia umeathiri eneo la ujenzi.

"Soko la mali isiyohamishika linapitia mgogoro mkubwa. Na watu wengi wanaathirika, wauzaji na wanunuzi, makampuni ya ujenzi, wamiliki wa biashara na benki ambao mikopo yao inaweza kuathirika. Hii ni sekta muhimu sana ya uchumi," anasema Eran Yashiv.

zz

Chanzo cha picha, Getty Images

Makampuni ya teknolojia: Chachu ya ukuaji wa Israeli

Uchumi wa Israel hata hivyo umeweza kuonyesha dalili chanya katika miezi ya hivi karibuni.

Benki kuu ya nchi hiyo, kwa mfano, ilisema kuwa ununuzi wa kadi za mkopo, ambao ulipungua kwa kiasi kikubwa katika wiki za kwanza za vita, tayari unaonyesha dalili za unafuu, ikionyesha kwamba matumizi yanaonyesha dalili za uboreshaji.

Kitu kama hicho kinafanyika katika soko la ajira, huku askari wa akiba wakirejea kazini.

Lakini moja ya wasiwasi mkubwa kwa sekta ya biashara ya Israeli ni sekta ya teknolojia, ambayo inachukua asilimia 17 ya Pato la Taifa na ni injini yenye nguvu ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

Mnamo 2023, ufadhili wa kampuni za teknolojia umepungua sana ikilinganishwa na mwaka 2022, anaelezea Eran Yashiv.

Kwa wataalam wengine, vita vinaweza kuendelea kuimarisha hali hii.

"Ikiwa Israeli iko vitani au katika machafuko ya kijiografia mwaka huu na mwaka ujao, ninashuku kuwa wawekezaji wengi wa kigeni wataiacha Israeli na kuhimiza makampuni ya teknolojia kuondoka nchini," Eran Yashiv alisema.

xx

Chanzo cha picha, Getty Images

Kipi cha kutarajia

Hata hivyo Benki ya Israel imesisitiza kuwa uchumi wa nchi hiyo wenye thamani ya dola bilioni 500 uko "imara vya kutosha" kustahimili athari zilizoachwa na vita.

"Kiwango cha juu cha akiba ya fedha za kigeni ya Benki ya Israeli, ambayo ilifikia karibu dola bilioni 200 kabla ya vita, inatupa nafasi kudumisha utulivu wa uchumi na, wakati huo huo, kupunguza kutokuwa na uhakika," Gavana alisema. Amir Yaron. .

Eran Yashiv, hata hivyo, anasisitiza kwamba kila kitu kinategemea kile kinachotokea katika miezi ijayo. "Kama vita vingemalizika sasa, nadhani kwamba katika muda mrefu matatizo kwa uchumi hayatazingatiwa kuwa makubwa sana. Lakini ikiwa itaendelea au kuzidi katika nyanja zingine, inaweza kupata uharibifu mkubwa," alisema.

Msomi Josep Comajuncosa Ferrer anaonya kwamba "ikiwa mzozo utaendelea, itakuwa vigumu sana kwa Israeli kuweka uchumi wake kufanya kazi."

Hata hivyo, serikali ya Benjamin Netanyahu imedhamiria kuendeleza mashambulizi huko Gaza, bila kujali gharama ya kiuchumi.

Imetafsiriwa na Jason Nyakundi