Lebanon yataka kufanya mazungumzo na Israel kumaliza mzozo wa Hezbollah

Rais Aoun apendekeza mpango kuelekea "usalama na utulivu wa kudumu", huku mashambulizi ya Israel dhidi ya Hezbollah yakiendelea.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Kufikia hapo tunakamilisha taarifa zetu za moja kwa moja

  2. Mfanyabiashara Mtanzania Rostam Aziz anunua shirika la habari la NMG

    .

    Chanzo cha picha, NMG

    Mfuko wa maendeleo wa Aga Khan (AKFED) umetangaza kuuza asilimia 100% ya hisa zake katika shirika la habari la Nation Media Group (NMG) kwa kampuni ya Taarifa Ltd, inayomilikiwa na mfanyabiashara Mtanzania Rostam Aziz.

    Hatua hii inamaanisha kwamba Aga Khan inajiondoa rasmi kwenye shirika hilo la habari baada ya miaka 66.

    Shirika la habari la NMG linahudumu katika mataifa ya Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda, na linamiliki magazeti kama vile Daily Nation, Sunday Nation, The EastAfrican, Daily Monitor (Uganda),Mwananchi, The Citizen (Tanzania), pamoja na NTV Kenya, Nation FM miongoni mwa vituo vingine.

    Lilianzishwa na marehemu Prince Karim Aga Khan IV mwaka wa 1959.

    Mnunuzi wake ni Taarifa Ltd, kampuni inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa Afrika Mashariki Rostam Aziz, ambaye amewekeza katika sekta kadhaa ikiwemo vyombo vya habari, madini, mawasiliano, kilimo, bandari, nishati na ujenzi.

    Aga Khan ni mwanahisa mkuu wa NMG kwa kumiliki asilimia 54.08% ya kampuni hiyo kupitia kampuni ya NPRT Holdings Africa Limited.

    Shirika hilo limesajiliwa katika masoko ya hisa ya Nairobi, Dar Es Salaam, Uganda na Rwanda.

    Katika taarifa, Aziz amesema ‘Ni furaha yetu kuwa mwanahisa mkuu wa Nation Media Group’, akiongeza kuwa ‘tutajitolea kusimamia uhuru wake wa habari huku tukiwekeza katika kuendeleza mafanikio yake kama shirika linaloongoza kwa uhuru wa vyombo vya habari.’

    Uuzaji wa shirika la NMG unatarajiwa kufanyika ndani ya miezi mitatu au minne ijayo, kwa kuzingatia idhini ya mamlaka husika.

  3. British Airways yaahirisha safari zaidi Mashariki ya Kati

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la ndege la Uingereza, British Airways, limeahirisha safari za ndege kuelekea Mashariki ya Kati.

    British Airways imetangaza kusitisha safari za kuelekea Amman, Bahrain, Doha, Dubai, Tel Aviv hadi tarehe 28 Machi.

    Safari ya Abu Dhabi hata hivyo haitarejelewa tena hadi Oktoba, kwa sababu ndio njia pekee ya ndege hiyo msimu wa baridi.

    Shirika hilo la ndege lilisema kuwa litatoa maelezo zaidi kwa abiria kadiri ya uwezo wake.

    Ndege hiyo bado ina safari mbili zaidi za kuwarejesha nyumbani raia wa Uingereza kutoka Oman wiki hii, na tikiti bado zinauzwa.

    Shirika hilo la ndege hata hivyo linaendelea kutoa huduma ya safari hadi Larnaca, Cyprus.

  4. Mashambulizi ya leo ya Marekani dhidi ya Iran yatakuwa 'makali zaidi' - Hegseth

    ..

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amesema leo itakuwa siku "kali zaidi" ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran kufikia sasa.

    Ameongeza kuwa Iran imerusha idadi ndogo zaidi ya makombora katika kipindi cha saa 24 tangu vita kuanza,

    Akiunga mkono kauli iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Marekani Jenerali Dan Caine alisema: "Mashambulizi makombora ya balistiki ya Iran yamepungua kwa asilimia 90 tangu yalipoanza na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani pia yamepungua kwa asiliamia 83 tangu yalipoanza."

    Wakati huo huo, Marekani "inatathmini hatua" ambazo zitawezesha jeshi kusindikiza meli kupitia Mlango wa Hormuz, Caine alisema.

    Hegseth alisema Kiongozi Mkuu mpya wa Iran, Mojtaba Khamenei, "ingelifanya jambo la busara" kutii ujumbe wa Donald Trump wa kuachana na silaha za nyuklia.

    Alipoulizwa kuhusu hatua ambazo Pentagon inachukua kupunguza vifo vya raia, Waziri huyo wa ulinzi alisema watachunguza madai yoyote ambayo yanahitaji kuchunguzwa, lakini alidai hakuna taifa "linachukua tahadhari zaidi kuhakikisha usalama wa raia."

    Maelezo zaidi:

  5. Lebanon yataka kufanya mazungumzo na Israel kumaliza mzozo wa Hezbollah

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Lebanon ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na Israel kama sehemu ya pendekezo la kumaliza mzozo unaozidi kuongezeka na Hezbollah, huku akilikosoa vikali kundi linaloungwa mkono na Iran kwa kuiingiza nchi hiyo katika vita vikubwa zaidi vya kieneo.

    Msemaji wa Rais Joseph Aoun aliambia BBC kuwa Lebanon iko tayari kufanya mazungumzo, lakini sio wakati nchi hiyo ikiwa chini ya mashambulizi ya Israeli.

    Akizungumza wakati wa mkutano na maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya siku ya Jumatatu, Aoun alielezea kile alichokitaja kama njia kuelekea "mipango ya kudumu ya usalama na utulivu kwenye mipaka yetu".

    Maafisa wa Israel wameonyesha dalili ndogo ya kuunga mkono mazungumzo, na serikali haijatoa kauli ya moja kwa moja kuhusiana na hilo.

    Aoun alisema vita hivyo vimesababisha madhara makubwa nchini Lebanon, ambapo zaidi ya watu 700,000 wameyakimbia makazi yao, wakiwemo watoto 200,000, na mamia ya watu kuuawa katika mashambulizi ya Israel katika muda wa siku tisa zilizopita, kulingana na Umoja wa Mataifa.

    "Baadhi yao wako barabarani. Hawana makazi wala mahitaji muhimu ya kimsingi," alisema.

    Soma pia:

  6. Mauzo ya China yaongezeka licha ya ushuru wa Trump

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mauzo ya bidhaa za China nje ya nchi yaliongezeka katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka huu licha ya mgogoro wa kibiashara kati ya taifa hilo na Marekani.

    Takwimu rasmi zinaonyesha kwamba bidhaa zinazotumwa nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 20 mwezi Januari na Februari. Hii ni zaidi ya mara tatu ya makadirio ya wanauchumi.

    Ongezeko hili linaiweka taifa hilo katika nafasi nzuri ya kuvunja rekodi yake iliyoweka mwaka 2025 ambapo kiwango cha bidhaa zilizouzwa nje ya nchi kilipita kiwango cha bidhaa zilizoagizwa kuingia nchini humo.

    Tangazo hilo linakuja huku Rais wa Marekani Donald Trump akitarajiwa kuzuru China mapema mwezi Aprili kukutana na mwenzake wa China Xi Jinping.

    Uchumi wa China ambao ni wa pili kwa ukubwa duniani unategemea sana mauzo ya nje huku ikikabiliwa na masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na matumizi duni ya walaji, kupungua kwa idadi ya watu na mgogoro wa soko la bidhaa.

    Soma pia:

  7. Kenya kufanya mkutano wa dharura na wauzaji mafuta

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Waziri wa Kawi wa Kenya, Opiyo Wanyayi, ameitisha mkutano wa dharura na wauzaji mafuta, saa chache baada ya kufanya mazungumzo na makampuni yanayosambaza mafuta nchini chini ya makubaliano ya ya serikali kwa serikali maarufu G-2-G.

    Wandayi amesema atafanya mkutano huo leo huku akiondoa wasiwasi wa uhaba wa mafuta.

    Waziri huyo pia amedokeza kuwa serikali inajadiliana na mataifa yanayozalisha mafuta ambayo Kenya ilifikia mkataba wa G-2-G nayo, kama vile ARAMCO ya Saudi Arabia, ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha kwa muda mrefu iwezekanavyo kwa kuzingatia mipango ya dharura.

    "Tunaendelea kushirikiana kwa karibu sana na wasambazaji wetu wa mafuta kama vile Saudi Aramco, ADNOC na ENOC katika suala la mipango ya dharura," Wandayi alisema.

    Haya yanajiri kufuatia mgogoro uliozuka Mashariki ya Kati baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran na kumuua Kiongozi Mkuu wake Ayatollah Ali Khamenei wiki iliyopita.

    Iran imekuwa ikilipiza kisasi hatua hiyo kwa kuyashambulia mataifa jirani ya Ghuba ambayo ni mshirika wa Marekani na kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, njia inayotumika kwa usambazaji wa asilimia 21 ya mafuta duniani.

    Maelezo zaidi:

  8. Video: Tazama kombora la Marekani la Tomahawk likishambulia kambi ya kijeshi ya Iran karibu na shule

    Maelezo ya video, Tazama: Kombora la Tomahawk likishambulia kambi ya kijeshi ilio karibu na shule .
  9. Kiongozi wa kijeshi nchini Madagascar avunja serikali

    Kanali Michael Randrianirina
    Maelezo ya picha, Kiongozi wa kijeshi wa Madagascar Kanali Michael Randrianirina

    Kiongozi wa kijeshi wa Madagascar Kanali Michael Randrianirina amevunja serikali katika hatua ambayo haikutarajiwa, na kumfukuza waziri mkuu na baraza zima la mawaziri, kulingana na taarifa kutoka kwa msemaji wake.

    "Serikali imesitisha majukumu yake," ilisema, na kuongeza kuwa Randrianirina atamteua waziri mkuu mpya "kulingana na vifungu vilivyoainishwa na katiba".Hakuna sababu iliyotolewa kufuatua hatua hiyo.

    Randrianirina alichukua mamlaka Oktoba iliyopita kutoka kwa Andry Rajoelina, kufuatia wiki kadhaa za maandamano yaliyoongozwa na vijana katika taifa hilo la kisiwa cha Bahari ya Hindi.

    Rajoelina alichaguliwa kuwa rais kwa muhula wa tatu kufuatia kura ya maoni iliyokumbwa na utata mwaka 2023.

    Maandamano hayo yalichochewa na uhaba wa stima na maji, lakini baadaye yakageuka wito wa kutaka mabadiliko serikalini. Hatimaye jeshi likaungana na waandamanaji na kuchukua uongozi..

    Randrianirina ameahidi kuitisha uchaguzi mpya ndani ya miaka miwili.

    Maelezo zaidi:

  10. Putin aweka masharti magumu kusitishaji mapigano

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani kuhusu mazungumzo ya Trump na Putin inaonyesha kuwa amekataa ombi la kusitisha mapigano haraka ya ardhini, angani na baharini, badala yake, Putin amekubali kusimamisha mashambulizi ya makombora ya masafa marefu kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine.

    Hili lilikuwa pendekezo la Ukraine ambalo Wamarekani walilipuuza wiki moja iliyopita.

    Trump na Putin pia wameonekana kukubaliana kufanya mazungumzo ya haraka kupata suluhu ya muda mrefu.

    Vladmir Putin amemthibitishia Trump "ahadi yake ya msingi" ya makubaliano ya azimio la amani lakini kwa masharti yafuatayo:

    • Taarifa ya Urusi inasema Putin alimwambia Trump "sharti muhimu" la kuzuia kuongezeka kwa mzozo "linapaswa kuwa kukomesha kabisa misaada ya kijeshi ya kigeni na kushirikishana taarifa za kijasusi na Ukraine"
    • Putin pia alizungumzia kuhusu "hitaji la kukomesha usajili wa wanajeshi wa kulazimishwa nchini Ukraine na upangaji upya wa Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine"
    • Makubaliano yoyote "yanapaswa kuwa magumu, thabiti na ya muda mrefu" na lazima "yazingatie hitaji kamili la kuondoa sababu kuu za mgogoro", taarifa hiyo ilisema.
    • Pia lazima izingatie "madai halali ya Urusi"

    Pia unaweza kusoma:

  11. Ndugu maarufu wahukumiwa kwa kosa la biashara haramu ya ngono

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ndugu wawili maarufu waliokuwa wakifanya kazi kama madalali wa majengo wamehukumiwa kwa kuwawekea wanawake kadhaa dawa za kulevya na kuwabaka kwa miongo kadhaa.

    Tal Alexander, 39, na Oren Alexander, 38, walijipatia umaarufu kutokana na mauzo yao ya mali isiyohamishika ya kifahari huko New York na Miami.

    Pamoja na kaka wa tatu Alon, 38, lopo la majaji huko New York liliwakuta wote watatu na hatia ya biashara haramu ya ngono.

    Waendesha mashtaka walikuwa wamewashtaki ndugu hao kwa kutumia utajiri wao kuwavutia wanawake kwenye sherehe na nyumba za kifahari, kisha kuwatumia vibaya. Lakini mawakili wao walidai kuwa wanawake hao walikuwa tayari kushiriki vitendo hivyo.

    Walipatikana na hatia katika makosa yote 10 ya jinai, ikiwa ni pamoja na biashara ya usafirishaji haramu na kushiriki ngono na mtoto mdogo.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Putin anataka 'kusaidia' Mashariki ya Kati - Trump

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais Donald Trump amezungumzia mazungumzo aliyofanya awali na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kusema kuwa anataka 'kusaidia' Mashariki ya Kati.

    Akifafanua mazungumzo yake ya simu na Putin wakati akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari, Trump alisema, "Tulikuwa tunazungumzia kuhusu Ukraine, ambayo imekumbwa na mapigano yasiyoisha".

    "Kuna chuki kubwa kati ya Putin na Zelensky na inaonekana hawawezi kupatana. Lakini nadhani ilikuwa wito mzuri juu ya mada hii."

    Aliongeza kwamba pia walizungumzia kuhusu Mashariki ya Kati, na Putin "anataka kusaidia."

    "Nilimwambia, 'unaweza kuwa msaada zaidi kwa kumaliza vita ya Ukraine. Hilo litakuwa msaada mkubwa.' Lakini tulikuwa na mazungumzo mazuri sana."

    Pia siku ya Jumatatu, Putin alimpongeza Mojtaba Khamenei kwa kuwa kiongozi mkuu mpya wa Iran na akathibitisha tena uungaji mkono wa Moscow kwa Tehran, kulingana na ujumbe uliochapishwa kwenye tovuti ya Urusi.

    Mwishoni mwa wiki, vyombo kadhaa vya habari vya Marekani, ikiwa ni pamoja na The Washington Post, The New York Times, na Associated Press, viliwanukuu maafisa wasiojulikana wakidai kwamba Urusi ilikuwa ikiipa Iran taarifa za kijasusi zilizosaidia kulenga wanajeshi na mali Mashariki ya Kati.

    Hata hivyo, Urusi haijathibitisha rasmi kwamba inaisaidia Iran.

    Lakini imelaani mashambulizi hayo dhidi ya Iran, ikiyaita "hatua ya kizembe".

    Kinadharia, kuisaidia Iran kushambulia maeneo ya kimkakati ya Marekani kunaweza kuathiri uhusiano wa Urusi na utawala wa Trump.

    Marekani na Urusi zilikutana mara kadhaa mwaka huu kwa mazungumzo yenye lengo la kukomesha vita nchini Ukraine — mazungumzo ambayo Urusi imekuwa ikitumai Marekani itashinikiza Ukraine.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Waandamanaji wazuia basi lililobeba timu ya soka ya wanawake ya Iran waliopewa hifadhi Australia

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Wanaharakati wa Iran nchini Australia walilala barabarani nje ya hoteli ya Gold Coast kuzuia njia ya basi lililokuwa limewabeba wachezaji wa Iran.

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Wachezaji watano wa timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Iran wamepewa viza zenye kuhusisha na masuala ya kibinadamu nchini Australia baada ya kuondolewa katika Kombe la Asia.

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Siku ya Jumatatu, Trump aliitaka Australia "itoe hifadhi" kwa timu ya mpira wa miguu ya wanawake. "Marekani itawachukua ikiwa hamtakubali," aliongeza.

    Karibu saa moja baadaye, Trump alichapisha tena ujumbe akisema alikuwa amezungumza na Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese na "watano hao tayari walikuwa wanaendelea kupewa huduma huku wengine wakiwa njiani".

    Ujumbe wa Trump ulionekana pia kuashiria baadhi yao walihofia usalama wa familia zao huko Iran na hivyo walihisi lazima "warudi".

    Pia unaweza kusoma:

  14. Jeshi la Iran lamjibu Trump

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kikosi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC ) limejibu matamshi ya Trump kwamba vita nchini Iran vitaisha hivi karibuni, kikisema kwamba wao ndiyo "watakaoamua kumalizika kwa vita".

    Iran haitaruhusu "lita moja ya mafuta" kusafirishwa nje ya eneo hilo ikiwa mashambulizi ya Marekani na Israel yataendelea, IRGC imesema, kulingana na Reuters.

    Bei ya mafuta imekuwa ikibadilika badilika kutokana na kuongezeka kwa mvutano kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao ni muhimu kwa soko la mafuta duniani huku karibu moja ya tano ya mafuta duniani yakipita kwenye njia nyembamba ya maji.

    Soma zaidi:

  15. Trump asema vita 'vitaisha hivi karibuni'

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais Donald Trump amehudhuria mkutano wa Wabunge wa Republican huko Miami na kusema kuwa "vitaisha hivi karibuni".

    "Ndani ya wiki moja wangetushambulia kwa 100%. Walikuwa tayari. Walikuwa na makombora mengi zaidi ya mtu yeyote angefikiria, na wangetushambulia, lakini pia wangeshambulia Mashariki ya Kati na Israel yote."

    "Na kama wangekuwa na silaha za nyuklia, wangeitumia dhidi ya Israeli. Na hili lingekuwa shambulizi kubwa. Ninajua walikuwa na maeneo yote ya makombora na vifyatuaji vyote ambavyo tumeviharibu, karibu 80% kufikia sasa, tumeharibu sehemu kubwa ya makombora. Wana kidogo sana waliobaki nayo."

    Trump aliendelea kusema jeshi limefanya "kazi nzuri".

    "Na makombora yamepunguzwa kwa kiasi kikubwa. Ndege zisizo na rubani zimedondoshwa, na tunashambulia mahali wanapotengeneza ndege zisizo na rubani," Trump alisema.

    "Tunawajua wote, na tunawamaliza kabisa. Pale, wanapotengeneza ndege zisizo na rubani. Kazi kubwa inaendelea. Lakini tutakuwa na ulimwengu salama zaidi mara tu itakapokamilika, na itakamilika hivi karibuni."

    Vita havitaisha wiki hii, lakini 'hivi karibuni' - Trump

    Akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari kuhusu muda ambao "operesheni" ya kijeshi ya Marekani itachukua nchini Iran, Trump alirejelea alichosema awali, operesheni hiyo itaisha "hivi karibuni" - lakini si wiki hii.

    "Nafkiri hivi karibuni. Kila kitu Iran iko nacho kimemalizwa, ikiwa ni pamoja na uongozi wao," alisema.

    "Watu wengi hata hawajasikia kuhusu kiongozi wanayemzungumzia (kuchukua nafasi ya ayatollah)," Trump alisema.

    Soma zaidi:

  16. Trump aonya 'kushambulia' Iran mara ishirini zaidi ikiwa itavuruga njia ya mafuta duniani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais Donald Trump ametoa onyo lingine kwa Iran kuhusu kuvuruga usafirishaji wa njia ya meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

    "Ikiwa Iran itafanya chochote kinachozuia usafirishaji wa mafuta ndani ya Mlango-Bahari wa Hormuz, itashambuliwa na Marekani mara ISHIRINI ZAIDI kuliko ilivyoshambuliwa hadi kufikia sasa," Trump alisema katika ujumbe wa mtandaoni.

    Takriban 20% ya mafuta duniani hupita kwenye mlango bahari huo na vita hivyo vimepunguza sana safari za usafirishaji mafuta baharini na kusababisha bei ya mafuta duniani kupanda.

    "Kama haitoshi, tutataja maeneo ya kuyalenga kwa urahisi na kuharibiwa kiasi kwamba itakuwa vigumu kwa Iran kujengwa tena, kama Taifa — Vifo, matukio ya Moto, na Ghadhabu vitatawala — Lakini natumaini, na kuomba, kwamba isitokee!" alisema.

    Bei ya mafuta yashuka baada ya Trump kuashiria kwamba vita vitaisha hivi karibuni

    Wakati huo huo, bei ya mafuta duniani ilishuka mapema Jumanne asubuhi barani Asia.

    Bei ilishuka kwa takriban 8.5% kwa pipa la $92.50 (£68.85). Mafuta yaliyouzwa Marekani pia yalishuka kwa takriban 9%, hadi $88.60 kwa pipa.

    Bei bado ziko juu kwa takriban 30% kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa mzozo.

    Kushuka huko kunafuatia matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump Jumatatu kwamba vita vitaisha "hivi karibuni".

    Soma zaidi:

  17. Hujambo msomaji wetu. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 10/03/2026.