Je, Hezbollah ina uwezo gani wa kijeshi na inaweza kuanzisha vita vikubwa dhidi ya Israel?

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Israel lilisema kuwa ndege yake ilishambulia kwa ghafla maelfu ya mitambo ya kurusha roketi za Hezbollah kusini mwa Lebanon siku ya Jumapili, baada ya kupata taarifa kwamba kundi hilo la wanamgambo lilikuwa linajiandaa kushambulia Israel hivi karibuni.
Hezbollah ilithibitisha kuwa vikosi vyake vilirusha mamia ya roketi na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel baada ya hapo, kujibu mauaji ya mmoja wa viongozi wake wakuu mwezi uliopita, na kuashiria kwamba mipango yake haikutatizika kama inavyodai Israel.
Hatua hii inajiri huku kukiwa uwezekano wa vita vya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili baada ya miezi kumi ya kushambuliana katika mpaka kati ya Israel na lebanon huku vita hivyo vikitoa hofu ya kuzuka kwa mapigano makali .
Hezbollah ni nini?
Hezbollah ni shirika la Waislamu wa madhehebu ya Shia ambalo lina ushawishi wa kisiasa na linadhibiti kundi lenye nguvu zaidi nchini Lebanon.
Shirika hilo lilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 na mamlaka kuu ya Shiite katika eneo hilo - Iran - ili kukabiliana na Israeli.
Wakati huo, wanajeshi wa Israel waliteka eneo la kusini mwa Lebanon wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo
Hezbollah limeshiriki katika chaguzi za kitaifa tangu 1992 na limekuwa sehemu kuu ya kisiasa nchini.
Mrengo ulio na wapiganaji wa vuguvugu hilo pia ulifanya mashambulizi mabaya dhidi ya wanajeshi wa Israel na Marekani nchini Lebanon. Wakati majeshi ya Israel yalipoondoka Lebanon mwaka 2000, Hezbollah ilidai kuwa ilifanikiwa kuwafukuza.
Tangu wakati huo, Hezbollah imedumisha maelfu ya wapiganaji na idadi kubwa ya makombora kusini mwa Lebanon, na inaendelea kupinga uwepo wa Israeli katika maeneo ya mpaka yanayozozaniwa.
Kundi hilo limetajwa kuwa shirika la kigaidi na nchi za Magharibi, Israel, nchi za eneo la Ghuba, na Jumuiya ya Kiarabu.
Vita vikali vilizuka kati ya Hezbollah na Israel mwaka 2006 baada ya Hezbollah kufanya mashambulizi makali ya kuvuka mpaka.
Vikosi vya Israel vilivamia kusini mwa Lebanon katika jaribio la kuondoa tishio la Hezbollah. Hatahivyo , hawakuweza kuiangamiza harakati hiyo, ambayo iliweza kuongeza idadi ya wapiganaji na kupata silaha mpya na za kisasa zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah ni nani?
Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hezbollah tangu 1992, anatoka katika madhehebu ya Kiislamu ya Kishia nchini Lebanon.
Alichukua jukumu kubwa katika kubadilisha vuguvugu hilo kuwa la kisiasa pamoja na kuwa jeshi la nchi.
Pia ana uhusiano mkubwa na Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.
Nasrallah anafurahia heshima kubwa kutoka kwa Hezbollah kama kiongozi wa vuguvugu hilo, na anatoa hotuba kwenye televisheni kila wiki.
Hezbollah ina nguvu kiasi gani?
Hezbollah ni mojawapo ya vikosi vya kijeshi visivyo vya serikali vilivyo na silaha nyingi zaidi duniani, na hupokea ufadhili na zana za kijeshi kutoka Iran.
Nasrallah anadai kuwa na wapiganaji 100,000, lakini makadirio huru yanaweka idadi ya wapiganaji wa Hezbollah kati ya 20,000 na 50,000.
Wanachama wa vuguvugu hilo walipata mafunzo mazuri na uzoefu wa hali ya juu wa mapigano, na pia walishiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria.
Hezbollah ina wastani wa roketi na makombora 120,000 hadi 200,000, kulingana na Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa.
Sehemu kubwa ya zana za kivita za vuguvugu hilo la Lebanon ni roketi ndogo.
Lakini pia inaaminika kuwa na makombora ya kukinga ndege na kushambulia meli, pamoja na makombora ya kuongozwa yenye uwezo wa kulenga ndani kabisa ya Israel.
Kundi hili lina silaha hatari zaidi kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza
Je, vita kamili vinaweza kuzuka kati ya Israel na Hezbollah?

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mapigano ya hapa na pale yaliongezeka Oktoba 8 - siku moja baada ya wanamgambo wa Hamas kufanya shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa nchini Israeli kutoka Gaza - wakati Hezbollah ilipofyatua makombora dhidi ya Israeli kwa mshikamano na Wapalestina.
Tangu wakati huo, vuguvugu hilo limerusha zaidi ya makombora 8,000 katika maeneo ya kaskazini mwa Israel na katika milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu, kurusha makombora ya kivita dhidi ya magari ya kivita, na kushambulia maeneo ya kijeshi kwa kutumia ndege zisizo na rubani zenye vilipuzi.
Jeshi la Israel lilijibu mashambulizi ya anga, kwa kurusha makombora dhidi ya maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon.
Wizara ya afya ya Lebanon ilisema zaidi ya watu 560 wameuawa katika muda wa miezi 10 iliyopita, wengi wao wakiwa wapiganaji wa Hezbollah.
Lakini takriban raia 133 walikuwa miongoni mwa waathiriwa wa mashambulizi ya Israel, wizara hiyo ilisema.
Nchini Israel, mamlaka zilithibitisha kuwa takriban raia 26 na wanajeshi 23 waliuawa katika mashambulizi ya Hezbollah.
Takriban watu 200,000 pia wamekimbia makazi yao pande zote mbili za mpaka
Licha ya mapigano hayo, waangalizi wa mambo wanasema pande hizo mbili hadi sasa zimelenga kuzuia uhasama bila kuvuka mipaka katika vita vya pande zote.
Lakini kuna wasiwasi kwamba hali inaweza kushindwa kudhibitika.
Wasiwasi huu uliongezeka baada ya watoto 12 kuuawa katika shambulio la roketi kwenye eneo milima ya Golan Heights inayokaliwa na Israel mnamo Julai 27.
Israel ilidai kuwa Hezbollah ndio waliotekeleza shambulio hilo, lakini kundi hilo lilikana kuhusika.
Tarehe 30 Julai, jeshi la Israel lilitangaza kuwa limemuua kamanda mkuu wa jeshi la Hezbollah, Fouad Shukr, katika shambulio la anga kwenye viunga vya kusini mwa Beirut.
Siku iliyofuata, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh aliuawa katika mji mkuu wa Iran, Tehran.
Israel haijathibitisha wala kukanusha kuhusika kwake na operesheni hiyo.
Tangu wakati huo, eneo hilo limekuwa likisubiri majibu kutoka kwa Hezbollah na Iran, ambao wote wameapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel.
Marekani inatarajia kupunguza mvutano kwa kupatanisha usitishaji mapigano na kuwaachilia mateka huko Gaza, na Washington inaweka shinikizo kwa Israel na Hamas.
Hezbollah imesema haitasimamisha uhasama hadi mapigano ya Gaza yatakapomalizika
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












