Shambulizi la Milima ya Golan lasambaratisha 'kanuni za kimya' za vita vya mpakani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, BBC International editor
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kwamba kundi la Hezbollah lenye makao yake nchini Lebanon litalipia "gharama kubwa" shambulizi lililosababisha vifo vya watoto 12 katika uwanja wa mpira wa miguu huko la Majdal Shams katika Milima ya Golan inayokaliwa na Israel siku ya Jumamosi.
Hatua hiyo inajiri huku kiongozi mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh akiuawa nchini Iran.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano, Hamas ilisema Haniyeh aliuawa katika uvamizi wa Israel kwenye makazi yake mjini Tehran.
Kwa mujibu wa kundi hilo, Haniyeh alifariki baada ya kushiriki sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Iran Masoud Pezeshkian aliyeapishwa siku ya Jumanne.
Hakuna aliyekiri kuwajibika na mauaji hayo
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Irani (The Iranian Revolutionary Guard Corps) lilisema chanzo cha "tukio" hakijafahamika mara moja lakini "kinachunguzwa", shirika la habari la AFP liliripoti.
Kundi la Wapalestina linalodhibiti Gaza lilisema Haniyeh "aliuawa katika uvamizi wa kihaini wa Wazayuni"
Vita vya mpaka kati ya Israel na Hezbollah vilianza siku moja baada ya Hamas kushambulia Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana, wakati Hezbollah iliporusha makombora ndani ya Israel kama hatua ya kuwaunga mkono Wapalestina.
Tangu wakati huo, pande hizo mbili zimekuwa zikipigana katika mazingira ya uelewa ambao haujawekwa wazi. Israel na Hezbollah zimeshambulia zaidi ngome za kijeshi, lakini raia wameuawa katika matukio hayo.
Matokeo yake ni vita, ingawa sio vikubwa sana, vimeendelea kudhibitiwa. Hata hivyo, maelfu ya watu wa pande zote za mpaka wameyakimbia makazi yao. Miji yenye shughuli nyingi imesalia mahame.
Hofu tangu mwanzo imekuwa kwamba shambulio kubwa la raia wa pande zote mbili lingesababisha kuongezeka kwa mapigano ambayo yanaweza kusababisha vita vikali, kwani Israel na Hezbollah watatumia uwezo wao wote.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mashambulio dhidi ya Hezbollah katika maeneo yasio na wakazi wengi kusini mwa Lebanon yanaweza kuepusha kuongezeka kwa mzozo. Kuwaua raia wa Lebanon mjini Beirut au kuharibu miundombinu kama madaraja au vituo vya umeme ni jambo ambalo haingewezekana.
Hezbollah inadai, bila ya kuwa na ushahidi, kwamba haikuhusika na shambulio la Majdal Shams. Hata hivyo, ni vigumu kuelewa kwa nini ililenga watoto wa jamii ya Druze waliokuwa wakicheza mpira uwanjani.
Hezbollah imezingatia zaidi kanuni kimya kimya katika mzozo huo, ikijaribu kukabiliana na wanajeshi, sio raia tangu ilipoanzisha vita vya mpakani tarehe 8 Oktoba.
Huenda ilikuwa inalenga vituo vya tahadhari ya mapema ya Israel kwenye ngome za kijeshi katika Mlima Hermoni.
Hezbollah ni adui mkubwa wa Israeli kuliko Hamas. Ina nguvu zaidi kuliko Lebanon na inafanya kazi bila kushauriana nayo.
Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah ni mwandani wa karibu wa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei. Wapiganaji wa Hezbollah wana nidhamu na mafunzo ya kutosha, na Iran imewapa silaha kubwa na makombora ambayo yanaweza kushambulia miji ya Israel.
Hezbollah ilipigana na Israel katika vita vyao vikubwa vya mwisho mwaka 2006. Wapiganaji wake wana uzoefu mkubwa wa vita baada ya kupigana kwa miaka mingi nchini Syria kuunga mkono utawala wa Rais Bashar al-Assad.
Uongozi wa Israel unajua yote hayo. Pia wanajua pia kwamba licha ya uwezo wao mkubwa wa silaha hawajaitiisha Hamas huko Gaza, na askari wa akiba wanaowategemea jeshi lao wanahisi uchovu wa vita hivyo.
Israel pia iko chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa washirika wake, ikiwa ni pamoja na Marekani - kutochukua hatua ambayo inaweza kugeuza mzozo vita huo kuwa vita kamili.
Wamarekani na Wafaransa wamejaribu kujadili njia ya kumaliza vita vya mpaka kati ya Israel na Hezbollah. Kutofikiwa kwa mkataba wa usitishaji vita huko Gaza kunadidimiza matumaini ya kupatikana kwa mwafaka.
Mpaka kati ya Israel na Lebanon unakabiliwa na tishio la kuwa chanzo cha vita vya Mashariki ya Kati kushika kasi.
Hata kama mgogoro uliosababishwa na mauaji ya watoto waliokuwa wakicheza mpira huko Majdal Shams utapita bila makabiliano makaliano makali, "sheria" za vita vya mpaka zimesambaratishwa.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na seif Abdalla












