Israel-Hezbollah: Kazi ya kulinda mpaka hatari zaidi Mashariki ya Kati

gf
Maelezo ya picha, Uzio wa waya na kamera katika mpaka wa mji wa Metula nchini Israel
    • Author, Jeremy Bowen
    • Nafasi, BBC

Mji wa kaskazini mwa Israel, Metula, umepakana na Lebanon katika pande zake tatu. Hiyo ina maana kwamba pia mji huo umezungukwa pande zote tatu na kundi lenye nguvu zaidi la Lebanon lenye silaha, Hezbollah.

Wanajeshi waliokuwa kwenye kizuizi cha barabarani katika mji wa Metula wote ni watu wa eneo hili, wengi wao ni askari wa akiba ambao wanaelewa vyema kuhusu kundi lililo upande wa pili wa mpaka.

Mvua ilipokuwa ikinyesha usiku na ukungu, mmoja wao ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alitumia kidole chake kutuonyesha mpaka na eneo la Hezbollah.

"Robo maili, upande wa magharibi, nusu maili kaskazini na nusu maili nyingine mashariki. Tumezungukwa kwa digrii 300 na Hezbollah,'' alisema.

Vita vya Gaza vilivyoanza baada ya Hamas kushambulia tarehe 7 Oktoba, na kuua zaidi ya Waisraeli 1,200, wengi wao wakiwa raia, vimekuwa vya uharibifu. Mashambulizi ya Israel yaliyofuata, hadi sasa, yameua zaidi ya Wapalestina 27,000, wengi wao wakiwa raia, na kusababisha uharibifu mkubwa Gaza.

Mzozo wa mpaka kati ya Israel na Hezbollah umeongezeka kwa kasi, lakini pande zote zinajua hatari ya mlipuko wa vita kamili. Hilo liko wazi hata kwa wanaume wanaolinda mji wa Metula.

Askari wa akiba wa Israel aliendelea: "Vinaweza kugeuka kuwa vita vikubwa. Na Hezbollah si kama Hamas, ni jeshi la kweli, lililofunzwa sana, lina vifaa vya kutosha na wana uzoefu mkubwa, uzoefu wa kweli nchini Syria."

Hezbollah iliingilia kati vita nchini Syria, ikipigania utawala wa Rais Bashar al-Assad.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, hana mpango wa kuzuru Metula katika ziara yake ya sasa ya Mashariki ya Kati, lakini safari ndefu ya ndege kutoka Washington kwenda miji mikuu tofauti ya Mashariki ya Kati, ni lazima sasa anaufahamu mji huo. Amerudi Mashariki ya Kati, kwa mara ya tano tangu tarehe 7 Oktoba.

Blinken hajajaribu kupunguza ukubwa wa mgogoro katika Mashariki ya Kati. Mwishoni mwa Januari, akiwa amesimama karibu na katibu mkuu wa Nato, alisema "hali tete sana ...hatujaona hali ya hatari kama hii tunayoikabili sasa katika eneo lote tangu 1973 , na bila shaka hata kabla ya hapo."

Marekani na Israel

VC
Maelezo ya picha, Askari wa akiba katika mji wa Metula, kaskazini mwa Israel, wako katika hali ya tahadhari kutokana na mashambulizi ya Hezbollah.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika safari zilizopita Katibu Blinken ameeleza mara kwa mara uungaji mkono wa Marekani kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas, lakini pia mashaka makubwa kuhusu namna Israel inavyopigana.

Marekani imeendelea kuipatia Israel silaha inazohitaji kwa ajili ya kampeni yake, licha ya kutoridhishwa kwake kuhusu namna zinavyotumika.

Marekani imekuwa na mafanikio zaidi katika kuilazimisha Israel kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu kwa zaidi ya raia milioni mbili wa Palestina ambao wamekwama katika janga hilo.

Oktoba mwaka jana, viongozi wa Israel walisema hakuna kitakachoruhusiwa kuingia. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada huko Gaza yanasema kuwa Israel haijaruhusu misaada ya kutosha.

Kipaumbele kikuu cha Blinken ni kupata usitishaji vita huko Gaza. Rais Biden anahitaji kuituliza Mashariki ya Kati, sio tu kwa sababu ya hatari mbaya ya kuendelea na kuongezeka kwa vita, lakini kwa sababu anakabiliwa na uchaguzi mwaka huu.

Kura za maoni zinaonyesha anapoteza kura huku baadhi ya Wamarekani wakilaumu uungaji mkono wake kwa Israel kwa maafa ya kibinadamu ndani ya Gaza.

Israel na Hamas

VC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Umoja wa Mataifa unasema hakuna msaada wa kutosha unaoingia Gaza kusaidia watu milioni 1.7 waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo huo

Hamas imetoa masharti yake katika mpango wa sasa wa usitishaji mapigano. Inataka mchakato wa hatua tatu kudumu kwa siku 135, ambao utaruhusu kubadilishana kwa awamu mateka kwa wafungwa wa Kipalestina katika jela za Israeli.

Imeweka orodha ndefu ya matakwa. La muhimu zaidi ni kwamba ifikapo mwisho wa siku hizo, Israel iwe imetoa majeshi yake Gaza na vita viishe.

Hayo yamekataliwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu baada ya mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje Blinken.

Tangu vita kuanza, Israel inataka kuiharibu Hamas na kurudisha mateka. Malengo hayo bado hayajafikiwa. Netanyahu alisema, vikosi vyake vinakaribia kupata "ushindi kamili." Israel pia imesema inataka kuwaua viongozi wa Hamas.

Blinken bado anaamini, mpango unawezekana. Changamoto ni kujaribu kupunguza pengo kati ya misimamo inayopingwa kwa kiasi kikubwa ya Israel na Hamas ili kupata aina fulani ya usitishaji mapigano.

V

Taarifa za ndani zinaonyesha Hamas wanajiamini kidogo kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa vita. Ukali wa mashambulizi ya Israel na mauaji ya raia wengi - inawafanya watu wa Gaza walionaswa katika vita hivyo kuanza kuichukia Hamas, na kuwafanya viongozi wake watambue kwamba wanahitaji kujaribu mazungumzo.

Nchini Israel, shinikizo linaongezeka kwa waziri mkuu na washirika wake, la kusitishwa kwa mapigano ili kuunda fursa ya mpango wa kuwarudisha mateka.