Israel-Palestine: Mvutano usio wa kawaida kati ya Marekani na Israel wazuka

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Mark Lowen
- Nafasi, BBC
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alisema siku ya Ijumaa kuwa ameionya Marekani kuhusu kuanzishwa kwa taifa la Palestina mara baada ya mzozo wa Gaza kumalizika.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Netanyahu aliunga mkono mashambulizi yanayofanyika Gaza na kuahidi yataendelea hadi ushindi kamili. Ikiwemo kuiharibu Hamas na kuwarudisha nyumbani watu waliotekwa nyara katika mashambulizi ya Oktoba 7.
"Inaweza kuchukua miezi mingi," alisema.
Takribani Wapalestina 25,000 wameuawa katika Ukanda huo, kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayoratibiwa na Hamas, karibu 85% ya watu wamekimbia makazi yao kutokana na vita hivyo.
Israel iko chini ya shinikizo kubwa la kuacha mashambulizi yake na kuanza mazungumzo ya kumaliza vita.
Washirika wa Israel, ikiwa ni pamoja na Marekani wanatoa wito wa kufufuliwa mazungumo ya kuanzishwa suluhisho la mataifa mawili, la Palestina na taifa la Israel.
Mzozo wa sasa unaweza kulazimisha pande zote mbili kuketi kwenye meza ya mazungumzo, labda ndio chaguo pekee la kumaliza ghasia zisizokwisha katika eneo hilo.
Lakini nia ya Netanyahu Ijumaa hii, iko kinyume kabisa na hilo.
Msemaji wa Baraza la Usalama la Marekani, John Kirby, alikiri kwamba Israel inaona mambo tofauti.
Siku ya Jumanne, Netanyahu alisema Israel inapaswa kuwa na udhibiti wa ardhi yote kutoka Mto Jordan hadi baharini, ambapo inajumuisha eneo la taifa la baadaye la Palestina.
"Hilo ni lazima na linakwenda kinyume na wazo la taifa (la Palestina). "Nitasema ukweli kwa marafiki zetu wa Marekani - nitazuia jaribio lolote ambalo litatishia usalama wa Israeli," waziri mkuu alisema.
Mvutano na Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Netanyahu ametumia muda mwingi wa maisha yake ya kisiasa kupinga wazo la taifa la Palestina. Mwezi uliopita alisema anajivunia kuzuia hilo kutokea.
Lakini kukataa hadharani mpango wa kidiplomasia wa Washington na azma ya kuendelea na kampeni ya kijeshi, kunaonyesha jinsi pengo kati ya Israel na washirika wake wa kimataifa linavyozidi kupanuka.
Tangu shambulio la Hamas katika eneo la Israel Oktoba 7 na kusababisha vifo vya watu 1,300 na kuchukua mateka 240, Marekani iliunga mkono Israel na haki yake ya kujilinda.
Huku idadi ya wanaofariki Gaza ikiongezeka na matukio ya kutisha yakiongezeka, serikali za Magharibi zimeitaka Israel kupunguza mashambulizi yake.
Ikulu ya White House imejaribu kushawishi sera ya kijeshi ya Israel; imehimiza matumizi ya silaha zinazolenga shabaha kwa usahihi zaidi badala ya mashambulizi ya anga yasiyo na utaratibu.
Ilipinga uvamizi wa ardhini na inaendelea kutoa wito wa suluhisho la mataifa mawili, na kuipa jukumu Mamlaka ya Palestina kusimamia Gaza vita vitakapomalizika.
Kirby alieleza Marekani imekuwa "wazi kabisa" kuhusu mpango wa Gaza baada ya vita.
"Tunataka serikali Gaza ambayo ni mwakilishi wa matarajio ya watu wa Palestina, ambayo ina usemi katika kile wanachotaka kwa eneo lao na isikaliwe kwa mabavu," alisema.
Ushauri kutoka Washington umepuuzwa na wakati mwingine umekataliwa moja kwa moja na Israel, tena hadharani, wakati wa ziara za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.
Hilo limezidisha mfadhaiko kwa baadhi ya wanasiasa na maafisa huko Washington - juu ya uungaji mkono wa wazi wa utawala wa Biden kwa Israel, na kutolewa wito wa kuwekwa masharti ya msaada wa Marekani kwa mshirika wake huyo wa Mashariki ya Kati.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












