Maafisa wa Israel wanataka kuiangamiza Gaza- Mahakama ya ICJ yafahamishwa

Polisi wakiwatawanya waandamanaji nje ya mahakama ya ICJ mjini The Hague

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Polisi wakiwatawanya waandamanaji nje ya mahakama ya ICJ mjini The Hague

Mpango wa Israel wa "kuisambaratisha" Gaza unatoka kwa " nchi ya ngazi ya juu kabisa", mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa imearifiwa.

Madai hayo yalitolewa na mawakili wa Afrika Kusini walipokuwa wakiwasilisha kesi yao ya kuishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki( ICJ.

Afrika Kusini pia iliitaka mahakama kuamuru Israel kusitisha operesheni za kijeshi huko Gaza.

Israel - ambayo itatoa utetezi wake siku ya Ijumaa - imekanusha vikali shutuma hizo kuwa "hazina msingi".

Mahakama itatoa uamuzi kuhusu madai ya mauaji ya halaiki, ingawa yanafuatiliwa kwa karibu.

Tembeka Ngcukaitobi, wakili wa Mahakama Kuu ya Afrika Kusini, aliiambia ICJ "nia ya mauaji ya kimbari" ya Israeli ilikuwa dhahiri "kutokana na jinsi shambulio hili la kijeshi linavyoendeshwa".

"Nia ya kuharibu Gaza imekuzwa katika ngazi ya juu ya serikali," alisema.

"Kila siku kunaongezeka, upotezaji usioweza kurekebishwa wa maisha, mali, utu na ubinadamu kwa watu wa Palestina," Adila Hassim, ambaye pia anawakilisha Afrika Kusini, aliiambia mahakama.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Hakuna kitakachozuia mateso, isipokuwa amri kutoka kwa mahakama hii."

Katika ushahidi wake uliowasilishwa kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, Afrika Kusini ilisema hatua za Israel "zina nia ya kuleta uharibifu wa sehemu kubwa ya kundi la taifa la Palestina, rangi na kabila".

Israel itatoa utetezi wake siku ya Ijumaa, lakini hapo awali imesema hatua zake katika Ukanda wa Gaza ni za haki kwa sababu inajibu mashambulizi mabaya ya Hamas tarehe 7 Oktoba.

Lakini akizungumza mahakamani siku ya Alhamisi, Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini Ronald Lamola alisema kuwa hakuna shambulio lolote "linaweza kutoa uhalali au kutetea ukiukaji wa Mkataba wa [Mauaji ya Kimbari]".

Israel imetia saini Mkataba wa kuzuia Mauaji ya Kimbari wa 1948, ambao unafafanua mauaji ya halaiki na kufanya mataifa kuyazuia.

ICJ ndiyo mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa, iliyoko The Hague nchini Uholanzi. Maamuzi yake kinadhamiria kuwabana kisheria pande zinazohusika na ICJ - ambazo ni pamoja na Israel na Afrika Kusini - lakini hazitekelezeki.

Mnamo 2022, mahakama iliamuru Urusi "kusitisha mara moja operesheni za kijeshi" nchini Ukraine, agizo ambalo lilipuuzwa.

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Afrika Kusini iliwasilisha kesi yake ikiishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki huko Gaza katika mahakama ya ICJ

Chini ya sheria ya kimataifa, mauaji ya halaiki yanafafanuliwa kama kufanya kitendo kimoja au zaidi kwa nia ya kusambaratisha, kwa ujumla au kwa sehemu, kikundi cha kitaifa, kikabila, rangi au kidini.

Kulikuwa na matukio ya maandamano ya jengo la ICJ, wakati polisi wa Uholanzi wakijitahidi kutenganisha makundi ya wafuasi wa Palestina na Israel tofauti.

Mamia ya watu wakipeperusha bendera za Palestina walikusanyika nje ya mahakama ya ICJ, wakitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano. Wafuasi wa Israel waliweka skrini inayoonyesha picha za baadhi ya mateka ambao bado wanazuiliwa mjini Gaza.

Kanda nyekundu na nyeupe za polisi zimewekwa nje ya ICJ katika juhudi za kuleta hali ya utulivu nje ya mahakama hiyo.

Ilikuwa ni tofauti na utaratibu uliokuwepo ndani ya mahakama hiyo, ambapo ujumbe wa Israel unasikiliza mawakili wa Afrika Kusini wakiyatuhumu majeshi ya nchi hiyo kufanya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Ujumbe wa Israel unatarajiwa kuangazia haki yake ya kujilinda chini ya sheria za kimataifa - wiki hii, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema Israel haina nia ya kuwafukuza katika ardhi ya watu wa Gaza, au kukalia kwa mabavu eneo hilo.

Tofauti na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ICJ haiwezi kuwashtaki watu binafsi kwa uhalifu kama vile mauaji ya halaiki, lakini maoni yake yana uzito na Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa.

Makundi yote yanayounga mkono Palestina na Israel yaliandamana nje ya mahakama siku ya Alhamisi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Makundi yote yanayounga mkono Palestina na Israel yaliandamana nje ya mahakama siku ya Alhamisi

Siku ya Jumatano, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema: "Tunachokipinga ni mauaji yanayoendelea dhidi ya watu wa Gaza ndio maana tumewasilisha kesi kwa ICJ."

Rais wa Israel Isaac Herzog alizitaja tuhuma hizo kuwa za kikatili na za kipuuzi.

"Tutakuwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki na tutawasilisha hoja yetu ya kujilinda ... chini ya sheria za kibinadamu," alisema.

Aliongeza kuwa jeshi la Israel "linafanya kila liwezalo chini ya hali ngumu sana kuhakikisha kwamba raia wanalindwa".

Caroline Glick, mshauri wa zamani wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, alisema kesi hiyo "ni dhihaka kwa msingi ya maadili".

Zane Dangor, mkurugenzi mkuu wa idara ya uhusiano wa kimataifa na ushirikiano wa Afrika Kusini, aliambia kipindi cha BBC cha Africa Daily kwamba madai ya mauaji ya halaiki dhidi ya Israel ni "tuhuma kali" lakini "sio jambo lisilo na msingi".

Alielezea kesi ya Afrika Kusini kama "ya uangalifu sana". Wakati akilaani mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba, haikusema chochote "kinachoweza kuhalalisha kiwango cha mauaji" yanayotokea Gaza.

Mahakama ya ICJ inaweza kutoa uamuzi wa haraka kuhusu ombi la Afrika Kusini la kutaka Israel isitishe kampeni yake ya kijeshi - lakini uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo Israel inatekeleza mauaji ya kimbari unaweza kuchukua miaka.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi