Kuna wakimbizi wangapi wa Kipalestina duniani kote?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Selin Girit
- Nafasi, BBC World Service
Inaaminika kuwa kuna zaidi ya wakimbizi milioni sita wa Kipalestina, hii inawafanya kuwa miongoni mwa idadi kubwa ya wakimbizi duniani. Wanaishi zaidi katika maeneo ya Palestina na katika nchi jirani.
Aidha, karibu Wapalestina milioni 1.9 wamekimbia makazi yao ndani ya Gaza kufuatia uvamizi wa Israel mwezi Oktoba, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Ingawa wa-Palestina wamesambaa kote ulimwenguni, wengi wao wanaishi Mashariki ya Kati.
Kwa nini kuna wakimbizi wengi wa Kipalestina?
Kuhama kumekuwa na nafasi kubwa katika historia ya Palestina tangu kuundwa kwa taifa la Israel.
Mwaka 1947, muda mfupi baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia, Umoja wa Mataifa ulipitisha Azimio nambari 181 la kugawanya kile kilichoitwa Mamlaka ya Uingereza ya Palestina kuwa taifa na Kiarabu na Kiyahudi.
Palestina ilikuwa inatawaliwa na Waingereza tangu 1922 na wakati huo, wahamiaji wa Kiyahudi katika eneo hilo waliongezeka - haswa wale waliokimbia ukatili wa Nazi huko Ulaya.
.Waarabu wa Palestina walikataa Azimio la 181 (liliwapa Wayahudi eneo kubwa wakati idadi yao ni ndogo). Mivutano kati ya Waarabu na Wayahudi ilichipua na kukuwa.
Israel ilijitangazia uhuru kwa kutumia mpango huu wa mataifa mawili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika vita vya 1948, Wapalestina wapatao 750,000 walifukuzwa au kukimbia katika maeneo ambayo sasa yanajuulikana kama Israel. Wapalestina wanataja tukio hilo kama Nakba, kwa Kiarabu "janga."
Baada ya mapigano kumalizika katika vita vya 1948, Israel ilikataa kuwaruhusu wakimbizi kurudi makwao.
Israel baadaye iliteka Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza kufuatia Vita vya Siku Sita vya 1967, na karibu Wapalestina wengine 325,000 walikimbia, wengi wao waliingia Jordan, kulingana na UN.
Miaka michache iliyofuata, wastani wa Wapalestina 21,000 walihamishwa kwa mwaka katika maeneo yaliyodhibitiwa na Israel.
Israel imekataa matakwa ya Wapalestina ya kuwaruhusu wakimbizi kurudi kama sehemu ya makubaliano ya amani.
Je, kuna wakimbizi wangapi wa Kipalestina duniani?
Mwaka 1949, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutoa Misaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lilianzishwa ili kusimamia programu za misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina.
UNRWA inafafanua "wakimbizi wa Palestina ni watu ambao makazi yao yalikuwa Palestina wakati wa 1 Juni 1946 hadi 15 Mei 1948, na walipoteza nyumba na njia za kujikimu kutokana na vita vya 1948."
Vizazi vya watu hao, wakiwemo watoto walioasiliwa, pia wana sifa ya kusajiliwa kama wakimbizi.

Wakati UNRWA ilipoanza operesheni mwaka 1950, ilikuwa ikihudumia takribani wakimbizi 750,000 wa Kipalestina, shirika hilo linasema.
Leo, kuna wakimbizi milioni 5.9 wa Kipalestina wanastahiki huduma za UNRWA. Kati ya hawa, zaidi ya milioni 1.5 wanaishi katika kambi 58 za wakimbizi zinazotambuliwa na UNRWA.
Kambi hizi ziko Jordan, Lebanon, Syria, Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, pamoja na Jerusalem Mashariki.
Kwa nini kuna kambi za wakimbizi Gaza na Ukingo wa Magharibi?
“Kutokana na kuundwa taifa la Israel, Waarabu wengi wa Palestina waliokuwa wakiishi katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya taifa la Kiyahudi walikimbilia maeneo yalikusudiwa kuwa taifa la Kiarabu,” anasema Profesa Dawn Chattyn kutoka idara ya masomo kuhusu wakimbizi ya Chuo Kikuu cha Oxford.
"Walitafuta hifadhi Gaza na Ukingo wa Magharibi - wakawa wakimbizi wa 1948,” anasema.
Kambi za wakimbizi Gaza na Ukingo wa Magharibi
Zaidi ya wakimbizi 871,000 waliosajiliwa wanaishi Ukingo wa Magharibi, karibu robo yao wanaishi katika kambi 19 za wakimbizi, kulingana na UNWRA.
Huko Gaza, kuna wakimbizi wapatao milioni 1.7, karibu 620,000 kati yao wanaishi katika kambi nane zinazotambuliwa na UNRWA.
Mbali na Wapalestina milioni 3.3 wanaioshi Ukingo wa Magharibi na milioni 2.3 wanaoishi Gaza, Wapalestina wengine milioni 1.75 wanaishi Israel (karibu 20% ya idadi jumla ya Waisraeli).
Wapalestina wote walio nje ya maeneo haya wanaunda diaspora kubwa zaidi, ambayo inajumuisha wale walioondoka kabla ya 1948 (hao hawahesabiwi na Umoja wa Mataifa), vizazi vyao, na wale ambao wameondoka Palestina lakini hawakuwahi kusajiliwa kama wakimbizi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kulingana na takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina, karibu Wapalestina milioni 7.3 wanaishi ughaibuni, kuanzia Mashariki ya Kati hadi Amerika Kusini na Australia.
Hata hivyo, ofisi hiyo inahesabu tu Wapalestina ambao wana vitambulisho au waliosajiliwa kama wakimbizi, hivyo basi idadi jumla ya wanaoishi nje ya nchi inaweza kuwa kubwa zaidi.
Kwa ujumla, zaidi ya Wapalestina milioni sita wanaishi katika nchi za Kiarabu, kulingana na ofisi hiyo, na karibu nusu yao wanaishi Jordan, kwenye mpaka wa mashariki na Israel.
Wengi wa Wapalestina nchini Jordan wana uraia kamili na wana haki sawa na raia mwingine yeyote.
Lebanon, Syria na Misri zinakadiriwa kuwa na Wapalestina zaidi ya milioni moja.
Nchini Lebanon, wakimbizi wengi wa Kipalestina wanaishi katika kambi za wakimbizi tangu 1948 na hawana haki ya uraia.
Wapalestina nchini Syria, kwa upande mwingine, wanafurahia haki sawa za kiraia kama raia wa Syria. Lakini baada ya vita vya Syria kuzuka, Wapalestina wengi waliikimbia nchi hiyo.
"Wapalestina katika nchi za Ghuba ya Kiarabu wapo karibu karne moja iliyopita," anaandika Youssef Courbage na Hala Nofal katika kitabu chao Palestinians Worldwide: A Demographic Study.
"90% walikuwa nguvu katika nchi ya Saudi Arabia na Kuwait kabla ya Vita vya pili vya Ghuba [mwaka 1990], baada ya hapo walihamia zaidi Qatar na Falme za Kiarabu," wameandika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Profesa Dawn Chatty anasema sababu ya nchi za Ghuba kukumbatia wakimbizi wa Kipalestina ni uhitaji wa wafanyakazi wenye elimu ambao wanaweza kuzungumza Kiingereza na Kiarabu.
Wapalestina walikuwa na uwezo mzuri, kutokana na elimu waliyoipata katika kambi za UNRWA.
Wapalestina nje ya Mashariki ya Kati
Wengi wa Wapalestina walioko nje ya Mashariki ya Kati walihama mwisho wa Karne ya 19, wakati eneo hilo lilikuwa chini ya himaya ya Ottoman.
Ukandamizaji wa vuguvugu la kwanza wa wazalendo wa Kiarabu na mzozo wa kiuchumi - vilisababisha wafanyabiashara wengi wa Kikristo wa Kipalestina kukimbilia Amerika Kaskazini na Amerika Kusini haswa.
Mawimbi mengine ya uhamaji yalifuata, baada ya kusambaratika kwa Dola ya Ottoman, na kisha kuundwa Israel.
Katika nchi za Amerika ya Kusini, makadirio ya idadi ya Wapalestina yamegubikwa na utata, kutokana na wote wa Mashariki ya kati na Afrika Kaskazini kujuulikana kama Waarabu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Jumuiya ya Wapalestina nchini Chile inakadiriwa kuwa 500,000, na kuifanya nchi yenye idadi kubwa zaidi nje ya Mashariki ya Kati, na pia kuna idadi kubwa ya Wapalestina wanaoishi Honduras, Guatemala na Brazil.
Uhamiaji wa Wapalestina kwenda Marekani pia ulianza mwishoni mwa Karne ya 19, na kuna wastani wa Wapalestina 200,000 wanaoishi Marekani kwa sasa.
Katika Ulaya, Ujerumani ni nyumbani kwa idadi kubwa ya Wapalestina, ikifuatiwa na Uingereza, Ugiriki, Ufaransa, Denmark na Sweden.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












