Makumi waripotiwa kuuawa katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia huko Gaza

Shirika la habari la Ufaransa AFP limekuwa katika eneo la tukio huko Jabalia baada ya mlipuko katika kambi ya wakimbizi iliyojaa watu.

Moja kwa moja

Yusuf Jumah and Ambia Hirsi

  1. Habari za hivi punde, Wahouthi nchini Yemen: Tumeishambulia Israeli mara tatu, na zaidi yanakuja

    .

    Chanzo cha picha, Telegram/Yahya Saree

    Kama tunavyoripoti kwamba kuna vurugu katika eneo lote la Ukanda wa Gaza, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, kwenye mpaka wa Israeli na Lebanoni, na mahali kwengine.

    Sasa, Wahouthi nchini Yemen - mamia ya maili kusini-mashariki mwa Israeli - wanathibitisha kuwa tayari wamerusha "idadi kubwa" ya makombora ya balestiki na drones kuelekea Israeli.

    Kama tulivyoripoti hapo awali, ving'ora vya mashambulizi ya anga vilisikika katika mji wa Eilat kusini mwa Israel siku ya Jumanne baada ya "uvamizi mkali wa ndege", ambao Israel ilidungua kwenye Bahari Nyekundu.

    Msemaji wa jeshi la Houthis Yahya Saree alisema katika taarifa yake kwa njia ya televisheni kuwa ni operesheni yao ya tatu inayolenga Israel - na kwamba zaidi yatafuata.Vikosi vya Houthi "vitaendelea kufanya operesheni maalum hadi uvamizi wa Israel utakapomalizika," Saree alisema.

    Wiki iliyopita, Israel ilishutumu kundi la waasi la Yemen wanaoungwa mkono na Iran kwa kutuma ndege zisizo na rubani ambazo zilisababisha milipuko katika miji miwili ya Misri - ikisema zilinuiwa kuishambulia Israel.

  2. Habari za hivi punde, Vifo vyaripotiwa katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia huko Gaza

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Vifo vingi na majeruhi vimeripotiwa katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza.

    Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, na mkurugenzi wa hospitali iliyo karibu ya Indonesia, wanasema takriban watu 50 wameuawa.

    Wizara hiyo imesema mlipuko huo ulisababishwa na shambulio la anga la Israel.

    Jeshi la Israel bado halijazungumzia kuhusu mlipuko huo

    Picha zilizowasilishwa na mpiga picha wa Reuters katika eneo la tukio zinaonyesha majengo na miili ikitolewa nje ya vifusi.

    BBC inajitahidi kuthibitisha maelezo ya tukio hilo.

    Maelezo ya video, Video inaonyesha uharibifu baada ya mlipuko katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia.
  3. Tanzania, Ujerumani kujadiliana kuhusu urejeshaji wa mabaki yaliyo Ujerumani

    Rais Samia na Rais wa Ujerumani Frank Walter Stainmeier

    Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaanzisha majadiliano kuhusu yaliyotokea kwenye utawala wa Ujerumani nchini, ambapo mojawapo ni urejeshaji wa mabaki yaliyo kwenye makumbusho mbalimbali za Ujerumani kwa familia zao.

    Amesema hayo baada ya kumpokea na kuzungumza na Rais wa Ujerumani Frank Walter Stainmeier aliye nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi

    Rais Samia amesema anatambua juhudi za pamoja zinazofanywa na taasisi za serikali hizo mbili ili kufanikisha lengo hilo.

    Jumatano Rais huyo wa Ujerumani anatarajiwa kutembelea mji wa Songea mkoa wa Ruvuma, Kusini wa Tanzania katika kumbukumbu ya vita vya Majimaji vilivyopiganwa 1905-1907 kupinga utawala wa kikoloni wa Ujerumani,ambapo maelfu ya watu walikufa.

    Awali, Ujerumani ilisema iko tayari kuomba msamaha kwa kunyongwa kwa wanaume 19 katika eneo ambalo sasa ni kaskazini mwa Tanzania miaka 123 iliyopita.

    Maiti nyingi zilikatwa vichwa na mafuvu yalitumwa Berlin.

    Vizazi vyao wametumia miongo kadhaa kutafuta mabaki hayo na hivi karibuni, katika kile kinachoitwa ugunduzi wa miujiza, mafuvu mawili ya watu waliouawa yametambuliwa kati ya mkusanyiko wa maelfu ya vitu vya kale.

    Soma zaidi;

  4. Tazama Video: Wanajeshi wa Israel waingia Gaza tayari kwa operesheni ya kuangamiza Hamas

    Maelezo ya video, Wanajeshi wa Israel waingia Gaza tayari kwa operesheni ya kuangamiza Hamas
  5. Vinicius Jr: Mshambulizi wa Brazil aongeza mkataba wake na Real Madrid

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Vinicius Jrt

    Mshambulizi wa Real Madrid Vinicius Jr ameongeza mkataba wake na klabu hiyo ya Uhispania hadi Juni 2027.

    Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 23 tayari ameshacheza mechi 235 akiwa na Real, akifunga mabao 63 tangu ajiunge nayo mwaka 2018.

    Ametwaa mataji tisa likiwemo taji la Ligi ya Mabingwa 2022, akifunga bao la ushindi mjini Paris dhidi ya Liverpool.

    Hata hivyo, pia amekuwa akikabiliwa na dhulma za ubaguzi wa rangi na mashabiki wa upinzani mara kadhaa.

  6. Watoto wako kwenye hatari ya kifo kutokana na upungufu wa maji Gaza - Unicef

    Watu wakichota maji kutoka kwenye bomba huko Khan Younis

    Chanzo cha picha, EPA

    WHO imesema kuna hatari ya "janga la afya ya umma" huko Gaza.

    Shirika jingine la Umoja wa Mataifa - Unicef, ambalo linaangazia watoto, linasema vifo vya watoto wachanga vinavyosababishwa na upungufu wa maji mwilini ni "tishio linaloongezeka".

    Gaza ina asilimia 5 pekee ya pato lake la kawaida la maji kwa siku, msemaji James Elder alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko Geneva.

    Aliongeza kuwa watoto walikuwa wakiugua kwa kunywa maji yenye chumvi na ambayo hayajawekwa dawa.

  7. Waziri Mkuu wa Misri akataa wito wa wakimbizi wa Kipalestina kwenda Sinai

    Uharibifu Gaza

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Misri amekataa mpango wowote wa watu waliohamishwa kutoka Gaza kuhamishwa kwa wingi katika rasi ya Sinai nchini Misri.

    Vyombo vya habari nchini Israel vimeripoti kuwa baadhi ya maafisa wa Israel wanataka kuwahamisha raia kutoka Gaza hadi kaskazini mashariki mwa Misri.

    Lakini, katika ziara yake Kaskazini mwa Sinai, Mostafa Madbouly anasema hakuna mzozo wa kikanda unapaswa kutatuliwa kwa gharama ya Misri.

    Kama ukumbusho, vivuko vya Israel kuingia Gaza vimefungwa, kivuko cha Rafah kinachodhibitiwa na Misri ndiyo njia pekee inayoweza kuwawezesha raia kuondoka Gaza.

    Unaweza kusoma;

  8. Tazama video: Onyo - Ina baadhi ya matukio ya kukasirisha. Msichana mwenye umri wa miaka 5, aliyejeruhiwa akutana na dada mdogo ambaye yuko hai

    Maelezo ya video, Msichana mwenye umri wa miaka 5, aliyejeruhiwa akutana na dadake mdogo ambaye yuko hai

    Dada wawili wa Kipalestina wameunganishwa tena huko Rafah, kusini mwa Gaza.

    Julia, mtoto mchanga mwenye umri wa miezi 18, alitolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo lililoharibiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya El-Najar.

    Dada yake, Joury mwenye umri wa miaka mitano, naye aliokolewa kutoka kwenye vifusi na tayari alikuwa hapo, akitibiwa majeraha yake.

    "Dada yangu, mpenzi wangu," Joury alilia mara tu alipogundua kuwa dada yake amenusurika.

    Wawili hao walikuwa na familia yao wakila chakula cha mchana wakati jengo lililo karibu na lao lililipuliwa na kuharibu nyumba waliyokuwamo, mjomba wa wasichana hao alisema.

    Wasichana hao walitibiwa majeraha ya kichwa na waliachwa wakiwa na hofu , mjomba wao aliongeza. Baadaye waliondoka hospitalini na familia yao.

  9. Mabingwa wa Kombe la Dunia la Raga wa Afrika Kusini wakaribishwa kishujaa

    Nahodha Siya Kolisi akiwasalimia wafuasi wake wakati akishikilia Kombe la Webb Ellis Cup wakati timu ya raga ya Afrika Kusini ikiwasili.

    Chanzo cha picha, AFP

    Timu ya raga ya Afrika Kusini imerejea nyumbani kutoka Ufaransa baada ya kushinda kombe la dunia.

    Wachezaji hao walikutana kwenye Uwanja wa Ndege wa OR Tambo mjini Johannesburg na umati mkubwa wa watu wenye furaha siku ya Jumanne.

    Afrika Kusini ndiyo timu iliyofanikiwa zaidi katika Kombe la Dunia baada ya kushinda mataji manne katika mechi nane.

    Nahodha Siya Kolisi

    Chanzo cha picha, Reuters

    Nahodha Siya Kolisi alisalimiana na wafuasi katika uwanja wa ndege na Kombe la Webb Ellis, lililoshinda Jumamosi baada ya mchuano mkali dhidi ya New Zealand.

    Mashabiki

    Chanzo cha picha, Reuters

    Aliuambia mkutano na waandishi wa habari mnamo Jumanne huko Johannesburg: "Tulifanya uamuzi kwamba tayari tuna Kombe la Dunia moja mnamo 2019. "Tulitaka kuhakikisha kuwa hii ni ya watu wa Afrika Kusini. Hii ni ya kila mtu wa Afrika Kusini. Tajiri, maskini... haijalishi unatoka wapi.

  10. Mahakama ya DR Congo yaondoa zuio dhidi ya Moïse Katumbi kuwania urais

    Moïse Katumbi aliondoka DR Congo mwaka 2016 baada ya kutuhumiwa kuajiri mamluki - mashtaka yalifutwa baadaye.

    Chanzo cha picha, AFP

    Mahakama ya juu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetupilia mbali kesi iliyokuwa ikitaka kumzuia kiongozi wa upinzani Moïse Katumbi kushiriki uchaguzi wa urais kwa kuhoji uraia wake.

    Bw Katumbi, ambaye baba yake Muitaliano, anaonekana kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa Félix Tshisekedi katika uchaguzi wa Desemba.

    Uraia pacha hauruhusiwi chini ya sheria za Congo. Mahakama iliamua Jumatatu kwamba shauri hilo "halikuwa na msingi".

    Mvutano wa kisiasa unaongezeka nchini humo kabla ya uchaguzi wa Disemba 20 ambapo Rais Tshisekedi atakuwa anawania muhula wa pili.

    Bw Tshisekedi pia atashindana na Martin Fayulu, ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita, Waziri Mkuu wa zamani Adolphe Muzito na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake aliyeshinda Tuzo ya Nobel Denis Mukwege.

    Zaidi ya wagombea 20 wamejiandikisha kuwania urais lakini bodi ya uchaguzi nchini humo inatarajiwa kuchapisha orodha ya mwisho tarehe 18 Novemba baada ya kuwachuja wagombeaji wote.

    Noel Tshiani, ambaye pia ni miongoni mwa wanaotarajia kuwa rais, alikuwa amewasilisha ombi kwa mahakama kumfutilia mbali Bw Katumbi kuwania urais kwa madai kuwa yeye si raia wa Congo. Baba yake Bw Katumbi alikuwa na asili ya Ugiriki na Italia, ripoti zinasema.

    Mahakama ya Kikatiba mnamo Jumatatu ilitupilia mbali kesi dhidi ya Bw Katumbi kutokana na "kukosa msimamo". Wakili wa Bw Katumbi, Herve Diakiese, alisema kwamba hakuna uthibitisho kwamba mteja wake alikuwa na uraia mwingine zaidi ya Congo. "Hii ni kilele cha mapambano ya muda mrefu dhidi ya ukosefu wa haki, uwongo, udanganyifu na upotoshaji," Bw Diakiese aliambia shirika la habari la AFP.

    Wafuasi wa Bw Katumbi walionekana wakisherehekea nje ya mahakama katika mji mkuu, Kinshasa, baada ya uamuzi huo. Bw Tshiani pia amependekeza rasimu ya sheria ambayo inalenga kuruhusu tu raia ambao wazazi wao wote walikuwa Wacongo kushikilia nyadhifa za juu za kisiasa, ikiwa ni pamoja na urais.

  11. Habari za hivi punde, Idadi ya waliouawa huko Gaza yaongezeka kwa zaidi ya 200

    Takribani watu 8,525 wameuawa huko Gaza tangu tarehe 7 Oktoba, wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas huko imetangaza hivi punde.

    Watoto 3,542 na wanawake 2,187 ni miongoni mwa Wapalestina waliouawa, pamoja na wahudumu wa afya 130, wizara hiyo inasema.

  12. Kombe la Dunia la 2034: Saudi Arabia yatarajiwa kuandaa dimba hilo baada ya Australia kujiondoa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Timu ya Argentina ndio mabingwa wa sasa wa kombe la dunia

    Saudi Arabia iko tayari kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la 2034 baada ya Australia kuamua kutowasilisha ombi la kutaka kuandaa mashindano hayo.

    Shirikisho la Kandanda Australia ilithibitisha uamuzi wake saa chache kabla ya tarehe ya mwisho ya Fifa kutangaza ombi hilo Jumanne.

    Saudi Arabia ndio taifa la pekee lililowasilisha ombi

    "Tumefikia hitimisho la kutofanya hivyo kwa mashindano ya 2034," ilisoma taarifa kutoka kwa Soka Australia.

    Kombe la Dunia la 2026 litafanyika Marekani, Mexico na Canada.

    Morocco, Ureno na Uhispania zitakuwa mwenyeji wa dimba la 2030, na mechi pia zitachezwa nchini Argentina, Paraguay na Uruguay.

    Saudi Arabia imekuwa mwenyeji wa hafla kadhaa kuu za michezo tangu 2018, zinazohusisha mpira wa miguu, mashindano ya magari ya Formula One , mchezo wa gofu na ndondi.

    Mwanamfalme Abdulaziz bin Turki bin Faisal, waziri wa michezo wa Saudi Arabia, alisema ombi la Kombe la Dunia "ni hatua muhimu na ya asili katika safari yetu kama nchi inayopenda soka".

    Ufalme wa Ghuba umeshutumiwa kwa kuwekeza katika michezo na kutumia matukio ya hali ya juu ili kuboresha sifa yake ya kimataifa - mchakato unaojulikana kama kuosha ‘uchafu’ kwa kutumia michezo.

  13. Mazishi huko Gaza huku mashambulizi ya Israel yakiendelea

    Umekuwa usiku mwingine wa mashambulizi makubwa ya mabomu katika Ukanda wa Gaza - Israel inasema kuwa ililenga shabaha 300 kwa jumla usiku mmoja.

    Picha zilizochukuliwa kutoka kusini mwa Israeli zinaonyesha moshi mwingi ukipanda juu ya vitongoji vilivyotandazwa na mashambulizi hayo.

    Na ndani ya Gaza asubuhi ya leo, mazishi yanaendelea kufanywa kwa maelfu ya waliouawa tangu tarehe 7 Oktoba.

    TH

    Chanzo cha picha, Reuters

    TH

    Chanzo cha picha, Reuters

    TH

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza

  14. Marekani kuiondoa Uganda na nchi nyingine tatu za Afrika katika mkataba wa Agoa

    Serikali ya Marekani iliziondoa Burkina Faso, Mali na Guinea kutoka Agoa mwaka jana, baada ya zote kufanyiwa mapinduzi.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Serikali ya Marekani iliziondoa Burkina Faso, Mali na Guinea kutoka Agoa mwaka jana, baada ya zote kufanyiwa mapinduzi.

    Rais wa Marekani Joe Biden amefichua mipango ya kuzifukuza Uganda, Gabon, Niger na Jamhuri ya Afrika ya Kati kutoka kwa mpango maalum wa kibiashara wa Marekani na Afrika.

    Nchi hizo ima zilihusika katika "ukiukaji mkubwa" wa haki za binadamu au kutopiga hatua kuelekea utawala wa kidemokrasia, rais alisema. Marekani ilianzisha Sheria ya Ukuaji na Fursa Afrika (Agoa) mwaka 2000.

    Inazipa nchi zinazostahiki za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na ufikiaji bila ushuru wa Marekani kwa zaidi ya bidhaa 1,800.

    Rais Biden alisema kuwa Niger na Gabon - zote mbili kwa sasa ziko chini ya utawala wa kijeshi kufuatia mapinduzi ya mwaka huu - hazistahiki Agoa kwa sababu "hazijaanzisha, au hazifanyi maendeleo endelevu katika kuanzisha ulinzi wa vyama vingi vya kisiasa na utawala wa sheria. ".

    Pia alisema kuwa kuondolewa kwa CAR na Uganda kutoka kwa mpango huo kulitokana na "ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu zinazotambulika kimataifa" na serikali zao.

    Mwezi Mei, serikali ya Marekani ilisema inafikiria kuiondoa Uganda kutoka Agoa na kuiwekea vikwazo nchi hiyo baada ya kupitisha sheria yenye utata dhidi ya mapenzi ya jinsia moja.

  15. Jiji la Nairobi lajiunga na Ushirikiano wa Miji yenye afya kwa lengo la kupunguza magonjwa yasiyoambukiza

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jiji kuu la Kenya Nairobi ni miongoni mwa majiji matatu ambayo yamejiunga na Ushirikiano wa Miji yenye Afya Ambayo Inashughulikia Kupunguza Magonjwa yasio ya kuambukizana na Kuzuia Majeraha.

    Hatua hiyo ni muhimu kwa sababu itaipa Nairobi uwezo wa kupata rasilimali na utaalam kusaidia kuboresha afya ya umma.

    Mtandao huu, ambao sasa unajumuisha miji 73, unaunga mkono mameya kutekeleza jitihada za hali yajuu na za matokeo yaliyothibitishwa nkatika hatua ya kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukizana (NCDs) na majeraha - ambayo yanayosababisha zaidi ya 80% ya maafa yote katika jamii zao.

    Magonjwa yasiyo ya kuambukizana ni pamoja na magonjwa ya moyo, kisukari, magonjwa ya kupumua, na saratani.

    "WHO inakaribisha Nairobi, New York City na Osaka - miji mitatu mikubwa zaidi duniani - kwa ushirikiano unaozidi kupanuka na inawapongeza mameya wao kwa kujitolea kwao kujenga mazingira ya mijini ambayo yanakuza afya," Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

    Mpango wa Uhisani wa Bloomberg wa kuunda mazingira bora ya mijini sasa unajumuisha miji 73

    "Kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukizana kwa ufanisi kunahitaji mchango wa sekta mbali mbali na wa fani nyingi," alisema. Sakaja Arthur Johnson, Gavana wa Kaunti ya Jiji la Nairobi.

    Ilizinduliwa mwaka wa 2017 kama sehemu ya jukumu la Michael R. Bloomberg kama Balozi wa Kimataifa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya Magonjwa yasio ya kuambukizana na Majeraha ,Ushirikiano wa Bloomberg Philanthropies kwa Miji yenye Afya ni ushirikiano na WHO na Vital Strategies, shirika la afya duniani.

    Ushirikiano huu unasaidia miji katika kuimarisha sera za afya ya umma katika maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa tumbaku, sera ya chakula, usalama barabarani, ufuatiliaji wa data na kuzuia matumizi ya kupindukia ya dawa.

    Ulimwengu leo unaadhimisha Siku ya Miji Duniani.

    Unaweza pia kusoma

  16. IDF: 'Tunashambulia maeneo yote ya ukanda wa Gaza'

    TH

    Chanzo cha picha, IDF

    Jeshi la Israel "linashambulia maeneo yote ya ukanda wa Gaza", msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Lt Kanali Jonathan Conricus alisema katika maelezo ya hivi punde kuhusu operesheni siku ya Jumanne.

    "Tutaelekeza shughuli zetu katika sehemu ya kaskazini ya Gaza, ambayo ni kitovu cha Hamas ... lakini tunaendelea kushambulia katika maeneo mengine ya Gaza.Tunawawinda makamanda wao, tunashambulia miundombinu yao na kila inapotokea lengo muhimu tunalipiga.”

    Conricus pia alikariri kwamba Israel ilikuwa inafanya kila iwezalo kuzuia mauaji ya raia, kabla ya kuishutumu Hamas kwa kutumia hospitali kuu ya Gaza City, Al Shifa, kama mahali pa "magaidi kujificha".

    Wiki mbili zilizopita, Israel ilitoa wito kwa raia waliokwama katika eneo hilo kuelekea kusini mwa mto Wadi Gaza kwa usalama wao, huku ikiendelea na mashambulizi yake ya kulipiza kisasi.

    Siku ya Jumatatu, vikosi vya IDF vilisonga mbele zaidi kaskazini mwa Gaza - ambapo inaaminika watu 600,000 wamesalia - na vifaru vikikata kwa muda njia ya uokoaji kuelekea kusini katika mchakato huo, kulingana na mashahidi wa Palestina.

    Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza

  17. Israel-Gaza:Matukio ya hivi punde

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Umekuwa usiku mwingine wa mapigano makali huko Gaza Ikiwa unajiunga nasi tu, haya ndiyo mapya zaidi:

    • Israel imeendelea kushambulia kwa mabomu Ukanda wa Gaza huku Umoja wa Mataifa ukitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu na kutoa onyo kali kuhusu hali ndani ya eneo hilo.
    • Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amepuuzilia mbali wito wa kusitisha mapigano mara moja huko Gaza, akisema Israel itasonga mbele na mipango ya kuliangamiza Hamas.
    • Hapo awali Shirika la Red Crescend la Palestina liliripoti kuwa eneo karibu na Hospitali ya Al-Quds na Mji wa Gaza lilikuwa chini ya mashambulizi makubwa ya wanajeshi wa Israel.
    • Wakati huo huo idadi ya vifo katika eneo hilo imeongezeka hadi watu 8,306 - ikiwa ni pamoja na watoto 3,457 - kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, ambayo inasimamiwa na Hamas.
    • Marekani imesema inatarajia kutakuwa na ongezeko kubwa la misaada kwenda Gaza katika siku zijazo
    • Tangazo hilo linakuja huku kukiwa na onyo kutoka kwa Umoja wa Mataifa kwamba watoto wengi sasa wanakunywa maji ya chumvi pekee.
    • Zaidi ya mateka 200 bado wanashikiliwa na Hamas huko Gaza, lakini siku ya Jumatatu Jeshi la Ulinzi la Israel lilisema kuwa limefanikiwa kumuokoa mmoja wa wanajeshi wake - Private Ori Megidish - kutoka kwa kundi hilo la wanamgambo.

    Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza

  18. Vita vya Ukraine: Familia nzima yauawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Ukraine unaokaliwa na Urusi

    th

    Chanzo cha picha, OFISI YA MWENDESHA MASHITAKA WA MKOA WA DONETSK

    Watu tisa wakiwemo watoto wawili wamepatikana wameuawa kwa kupigwa risasi ndani ya nyumba yao katika mji wa Volnovakha mashariki mwa Ukraine unaokaliwa na Urusi.

    Maafisa wa Ukraine wanasema wanaamini kuwa wanajeshi wa Urusi waliua familia nzima ya Kapkanet tarehe 27 Oktoba kwa kukataa kuwapa nyumba yao.

    Wachunguzi wa Urusi wanasema washukiwa wawili wanaume wameshikiliwa, wakisema ni wanajeshi wa Urusi kutoka Mashariki ya Mbali.

    Ukraine na Urusi zimeanza uchunguzi tofauti kuhusu shambulio hilo.

    Picha zimeibuka kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha miili iliyotapakaa damu na risasi ikiwa vitandani, baadhi yao wakiwa bado wamefungwa wakikumbatiana.

    Mwendesha Mashtaka wa Ukraine Dmytro Lubinets alisema Jumatatu kwamba "mikono ya Warusi yenye damu ilihusika" katika mauaji ya Volnovakha.

    "Kulingana na habari za awali, wakaaji hao wameua familia nzima ya Kapkanets, ambao walikuwa wakisherehekea siku ya kuzaliwa na ambao walikuwa wamekataa kukabidhi nyumba yao wenyewe kwa wakaaji kutoka Chechnya," alisema kwenye Telegraph.

    Ofisi ya mwendesha mashitaka wa Donetsk inayodhibitiwa na Ukraine, ikitoa taarifa za awali, ilisema washambuliaji waliovalia sare za jeshi waliipiga risasi familia hiyo baada ya ombi lao la kutaka kuondoka katika nyumba hiyo kukataliwa.

    Watoto wawili, waliozaliwa mwaka wa 2014 na 2018, walikuwa miongoni mwa waathiriwa, ofisi hiyo iliongeza.

    Kamati rasmi ya Uchunguzi ya Urusi iliwataja waliokamatwa kuwa wanajeshi wa Urusi kutoka Mashariki ya Mbali ya nchi hiyo, ambao walikuwa wametia saini kandarasi na jeshi la Urusi.

    "Kwa mujibu wa taarifa za awali, sababu ya uhalifu huo ilikuwa migogoro ya ndani," kamati ilisema katika taarifa yake.

  19. Waandishi 31 wameuawa katika vita vya Israel na Hamas - CPJ

    Takriban waandishi wa habari 31 wameuawa wakiripoti mzozo kati ya Israel na Hamas, kulingana na hesabu ya hivi punde kutoka kwa Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ).

    Kati ya waliopoteza maisha, 26 walikuwa Wapalestina, 4 Waisraeli, na 1 wa Lebanon.Waandishi wengine 8 wameripotiwa kujeruhiwa, huku 9 wakizingatiwa kutoweka au kuzuiliwa, CPJ inasema.

    "Waandishi wa habari huko Gaza wanakabiliwa na hatari kubwa sana wanapojaribu kuangazia mzozo huo katika kukabiliana na shambulio la ardhini la Israel... mashambulizi ya anga ya Israel, kukatika kwa mawasiliano na kukatika kwa umeme," shirika hilo lilisema katika taarifa yake Jumatatu.

    Miongoni mwa waliofariki ni Roshdi Sarraj - mtayarishaji filamu maarufu wa Kipalestina - na Issam Abdallah, mpiga picha wa video kutoka Beirut wa Reuters, ambaye aliuawa karibu na mpaka wa Lebanon kwa kupigwa makombora kutoka upande wa Israeli, kulingana na CPJ.IDF ilisema inachunguza madai hayo.

    IDF pia iliambia Reuters na mashirika ya habari ya Agence France Press kwamba haiwezi kuwahakikishia usalama waandishi wao wa habari wanaofanya kazi katika Ukanda wa Gaza, baada ya kutafuta hakikisho kwamba wafanyikazi wao hawatadhuriwa na mashambulizi ya Israeli, kulingana na Reuters.

    Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza

    • Afrika Kusini yatangaza likizo ya umma kwa ushindi wa Kombe la Dunia

      th

      Chanzo cha picha, YOAN VALAT/EPA-EFE/REX/SHUTTERSTOCK

      Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza siku ya mapumziko baada ya nchi hiyo kushinda Kombe la Dunia la Raga la 2023 mjini Paris siku ya Jumamosi.

      Springboks walishinda kwa mara ya nne Kombe la Dunia la Raga wikendi, wakiwashinda New Zealand kwa pointi moja, 12-11.

      Rais alisema amefanya uamuzi huo "katika kusherehekea mafanikio makubwa ya Springboks" katika hotuba ya kitaifa Jumatatu.

      Itafanyika tarehe 15 Disemba.

      Bw Ramaphosa alisema serikali ilitaka siku hiyo iwe "siku ya matumaini, siku ya sherehe na umoja. Wanamichezo wetu na wametuonyesha kile kinachowezekana".

      Ushindi huo umepongezwa na rais huyo kuwa ni ishara ya matumaini, huku nchi hiyo ikikabiliwa na kiwango cha juu zaidi cha ukosefu wa ajira duniani kwa asilimia 42, pamoja na matatizo mengine ya kiuchumi yakiwemo viwango vya juu vya umaskini na kukatika kwa umeme mara kwa mara.

      Kufuatia ushindi wa timu hiyo katika Kombe la Dunia huko Stade de France, Bw Ramaphosa alisema anataka umoja wa timu hiyo uwe sifa kuu ya jamii.

      "Tunahitaji zaidi ya haya, na sio tu katika uwanja wa mafanikio ya michezo," alisema, akionyesha kwamba idadi ya wachezaji weusi kwenye kikosi imepanda kutoka mmoja mwaka 1995 hadi karibu nusu ya wachezaji wa Afrika Kusini katika fainali ya 2023. .