Hamas: Lifahamu kundi la wapiganaji wa Palestina lililoivamia Israel kupitia angani, baharini na nchi kavu

Ushindi wa uchaguzi wa kundi la hamas 2006 ulilipatia kundi hilo nguvu katika malengo yao

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ushindi wa uchaguzi wa kundi la hamas 2006 ulilipatia kundi hilo nguvu katika malengo yao

Miaka hamsini baada ya Vita vya Yom Kippur, vilivyoanza kwa shambulio la ghafla dhidi ya Israel na Misri pamoja na Syria, wapiganaji wa Kipalestina wamefanya mashambulizi mengine makubwa.

Hili pia halikutarajiwa, kwenye sherehe nyingine ya Kiyahudi.

Mvutano ulikuwa umeongezeka hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza, lakini hekima iliyozoeleka ni kwamba si Hamas, kundi la Kiislamu linalotawala huko, wala Israel waliotaka vita.

Badala yake, Hamas imekuwa ikipanga operesheni kali dhidi ya taifa hilo la Kiyahudi .

Wapiganaji wa Kipalestina waliingia kusini mwa Israel kwa njia ya bahari, nchi kavu na angani.

Kwasasa wanashikilia miji na vituo vya jeshi la Israeli chini ya mzingiro kwa saa kadhaa na wameua watu wengi na kuteka idadi isiyojulikana ya raia na wanajeshi wa Israeli huko Gaza.

Lakini Hamas ni kundi la aina gani?

Kundi la wapiganaji wa Hamas `ni mojawapo ya makundi kadhaa ya wapiganaji wa Kipalestina ambayo yanadhibiti ukanda wa Gaza, eneo ambalo mara kwa mara hulitumia kukabiliana na Israel, taifa ambalo halilitambui.

Ghasia mbaya zaidi zilizuka mwezi Mei 2021 huku mamia ya roketi yakirushwa kutoka Gaza kuelekea Israel kwa siku kadhaa huku Israel ikijibu mashambulizi hayo katika eneo hilo hatua ambayo imesababisha uharibifu huku ikiwacha makumi ya watu wakiwa wameuawa katika pande zote mbili.

Jina lake kwa Kiarabu humaanisha Vuguvu la Kiislamu na chanzo chake kilianzia siku za kwanza za Intifada au mapinduzi ya Palestina 1987 dhidi ya maeneo yanayokaliwa na Israel katika eneo la West Bank na ukanda wa Gaza.Hii leo kundi hilo ndilo kubwa la kiislamu miongoni mwa raia wa Palestina.

Shughuli zake za kisiasa

Tangu lilipoanzishwa , kundi hilo lina matawi mawili yenye malengo yasiofanana: Mojawapo, Kundi la wapiganaji wa Qassam, linalosimamia mapambano ya kivita dhidi ya Israel ambao uwepo wake haujatumbuliwa na Hamas , na upande mwengine kuna wingi ya kisiasa, ambayo lengo lake ni kujenga shule, hospitali na kuisaidia jamii katika masuala ya kisiasa na kidini.

Lakini tangu 2005, upande wa Kiislamu ulichukua mwelekeo tofauti , ikiwa ni kuwashirikisha kisiasa watu wa Palestina .

Mwaka 2006, Hamas lilichukua utawala baada ya kupata ushindi katika uchaguzi wa bunge la Palestina lakini ushindi wake haukudumu kwa muda mrefu.

Hofu ya kisiasa na kundi jingine la Fatah, ilipelekea kuingia katika mapambano ya kivita.

Mwezi Juni 2007, makundi hayo mawili yalikabiliana katika vita vikali ndani ya ukanda wa Gaza kabla ya vita hivyo kukamilika huku Hamas likichukua utawala wa ukanda wa Gaza huku mpinzani wake wa kisiasa Fatah likitawala kutoka West Bank.

Kwa Marekani, Canada, Japan na Muungnao wa Ulaya kundi hilo la Kiislamu ni kundi la kigaidi kutokana na historia yake ya mashambulizi dhidi ya Israel na lengo lake la kutaka kuliangamizia taifa hilo kitu ambacho imeandika katika sheria yake.

Lakini kwa wafuasi wake ni vuguvugu halali la kupigania haki za Wapalestina.

Wapiganaji wa al Qassam katika mkutano na vyombo vya habari

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wapiganaji wa al Qassam katika mkutano na vyombo vya habari

Mwezi Mei 2017, kwa mara ya kwanza tangu lilipoanzishwa , kundi hilo lilichapisha sera mpya ambapo lilitangaza kukubali taifa la muda la Palestina kabla ya mipaka ya 1967 , wakati Israel ilipochukua udhibiti wa Jerusalem yote na eneo la West Bank katika vita vya siku sita.

Hatahivyo , liliendelea kutoitambua Israel , ijapokuwa haikurejelea matamshi yake dhidi ya makubaliano yao na Wayahudi.

Tamko hilo lilichukuliwa kama juhudi za Hamas kuonyesha kupunguza msimamo wake mkali , ijapokuwa kundi hilo lilitangaza wazi kwamba halijabadilisha sera yake inayosema kwamba ardhi ya Wapalestina ni takatifu kwa Waislamu, haiwezi kubadilika na ikaitisha jihad - vita vitakatifu.

Ngome ya Gaza

Madai hayo kwa mara nyengine ndio yaliosababisha uadui mwengine mwezi Mei 2021 , huku kundi hilo likirusha mamia ya makombora ya roketi kutoka Gaza , kufuatia ghasia kati ya vikosi vya usalama vya Israel na waumini wa Kiislamu katika msikiti wa Al-Aqsa, Mjini Jerusalem , na mipango ya kuzifurusha família za Kipalestina kutoka katika makazi yao ili kutoa nafasi kwa walowezi wa Kiyahudi..

Israel ilijibu kwa mashambulizi makali , ikiharibu majumba na kuwaua baadhi ya viongozi wa makomando wa jeshi la Hamas..

Wanajeshi wa Israel wakijiandaa katika mpaka na Ukanda wa Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israel wakijiandaa katika mpaka na Ukanda wa Gaza

Israel mara tatau imetekeleza mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Hamas mnamo mwezi Disemba 2008, Novemba 2012 na Julai 2014.

Kampeni mbili za kwanza za Israeli ziliathiri uwezo wa jeshi la Hamas , lakini kundi hilo lilipata uungwaji mkono katika ukanda wa Gaza na eneo la West Bank kwa kusimama kidete dhidi ya Israel na kuendelea kustawi.

Vyanzo vya Palestina vinasema kwamba kundi hilo la kiislamu lilijaribu kunyamaza baada ya operesheni ya pili ambayo ilisababisha vifo vya Wapalestina 170 wengi wao wakiwa raia pamoja na raia sita wa Israel katika siku nane ya mapigano na kwamba wapiganaji wa Qassam waliwacha kurusha makombora ya roketi Israel.

Lakini kundi hilo halikufanya chochote kuzuia makundi mengine ya Gaza kutekeleza mashambulizi yao , kwa kuwa halikutaka kuonekana kwamba halikupendelea vita dhidi ya Israel badala ya wapiganaji wengine hususan kutoka Islamic Jihad.

Kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal (kushoto) na yule wa kundi la Fatah Mahmoud Abbas, mwaka 2014

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal (kushoto) na yule wa kundi la Fatah Mahmoud Abbas, mwaka 2014

.Walipuaji wa kujitolea muhanga

Baada ya Intifada ya kwanza nchini Palestina, Kundi la Hamas lilijitokeza kama upinzani mkuu wa makubaliano ya amani ya Oslo kati ya Israel na shirika la ukombozi wa Kipalestina la (PLO).

Licha ya opersheni kadhaa za Israel na hatua kali zilizochukuliwa na mamlaka ya Palestina PNA dhidi yao, kundi hilo lilijibu majadiliano hayo ya amani kwa kutekeleza mashambulizi ya kujitolea muhanga.

Kati ya Februari na Machi 1996, mashambulizi hayo yaliwaua takriban Waisraeli 60 - mashambulizi hayo ya kulipa kisasi baada ya mauaji ya mwanachama wake Yahya Ayyash.

Mamlaka ya Israel ikichunguza mabaki ya basi kufuatia shambulio la bomu 2001 mjini haifa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mamlaka ya Israel ikichunguza mabaki ya basi kufuatia shambulio la bomu 2001 mjini Haifa

Msururu wa mashambulizi ulichukuliwa na wengi kama sababu kuu ya Israel kupuuza mchakato wa amani na uchaguzi wa Benjamin Netanyahu ambaye amekuwa mpinzani mkuu wa makubaliano hayo ya Oslo.

Kutokana na kufeli kwa mazungumzo ya Camp David , Marekani , ikiwa kati ya PNA na Israel 2000 na mlipuko wa Intifada ya pili, Hamas iliendelea kupata uungwaji mkono wa kisiasa.

Katikati ya intifada, mshambulizi ya walipuaji wa kujitoa muhanga ya wapiganaji wa Hamas yalionekana na wengi kama njia mahsusi ya kukabiliana na uvamizi wa Israel katika ardhi yao.

Na kufautia kifo cha Yasser Araft 2004, kiongozi mkuu wa Palestina na mmoja ya waanzilishi wa Fatah , kulisababisha ushindi wao mwaka 2006.

Mwanzilishi wa kundi la Hamas 2002 Ahmed Yassin aliyeuwa na Israel

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanzilishi wa kundi la Hamas 2002 Ahmed Yassin aliyeuwa na Israel

Lakini Fatah sio kundi la pekee ambalo lilimpoteza kiongozi wake 2004. Mwezi Machi mwaka huohuo Sheikh Ahmed Yassin , mwanzilishi wa kundi hilo na kiongozi wake wa kidini aliuawa katika shambulio la kombora la Israel.

Viongozi wengine wa Hamas waliouawa na Israel ni pamoja na Qassam Brigade Salah Shehada mwezi Julai 2002; Abdul Aziz al-Rantissi, kiongozi wa viguvugu la Gaza, mnamo mwezi Aprili 2004; Ismail Abu Shanab mwezi Agosti 2003; Said Siyamin mwezi Januari 2009 na Ahmed Jabariin mwezi Novemba 2012.

Hamas imejitolea kusitisha vita kwa miaka 10 iwapo Israel itaondoka katika maeneo ya PaLestina iliyoyateka 1967 : Eneo la West Bank, Ukanda wa Gaza na Mashariki mwa Jerusalem.

Lakini kundi hilo linasisitiza kuwa mamilioni ya Wakimbizi wa Palestina walioondoka makazi yao 1948 , mwaka ambao taifa la Israel lilibuniwa , lazima warudi nyumbani, kitu ambacho Israel inakiona kama tisho la uwepo wake kama taifa.

Kutokana na sababu hizo licha ya kuchaguliwa kidemokrasia serikali ya Hamas ililengwa na vikwazo vya kiuchumi na kidiplomasia kutoka kwa Israel na washirika wake wa magharibi.