Mzozo wa Israel na Palestina: Netanyahu aapa kuendelea na mashambulizi Gaza

Excavators worked to clear rubble in Gaza City after the new air strikes

Chanzo cha picha, Reuters

Jeshi la Israeli linasema limeilipua kwa bomu nyumba ya kiongozi wa kisiasa wa kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas katika msururu wa mashambulio ya angani kwenye Ukanda wa Gaza.

Ilitoa video ya bomu lililokuwa likilipuka ambalo ilisema liligonga nyumba ya Yahya Sinwar, kiongozi mkuu wa kikundi hicho katika eneo hilo.

Mashambulio ya anga ya Israeli huko Gaza yaliwauwa watu wasiopungua 26 mapema Jumapili, maafisa huko walisema.

Wanamgambo walirusha roketi zaidi nchini Israeli, na kupelekea watu kutafuta hifadhi kwingine .

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa "kuendelea kujibu kwa nguvu" mashambulio ya roketi, wakati wito ukitolewa na jamii ya kimataifa kumaliza mzozo huo unaozidi.

Mkutano wa Baraza la Usalama la umoja wa mataifa unatarajiwa kufanyika baadaye Jumapili.

Rais wa Marekani Joe Biden alimpigia simu Bwana Netanyahu na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kuelezea wasiwasi juu ya hali hiyo Jumamosi.

Tangu mapigano yalipoanza Jumatatu watu wasiopungua 174 wameuawa huko Gaza, wakiwemo watoto 47 na wanawake 29, na 1,200 wamejeruhiwa, kulingana na wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas. Israel inasema makumi ya wanamgambo ni miongoni mwa waliokufa.

Watu kumi, pamoja na watoto wawili, wameuawa na mashambulio ya wanamgambo dhidi ya Israeli, maafisa wa Israeli wanasema.

Kuibuka kwa ghasia kwa siku sita zilizopita kulitokea baada ya wiki kadhaa za kuongezeka kwa mvutano wa Israeli na Wapalestina huko Jerusalem Mashariki, ambao ulisababisha mapigano kwenye eneo takatifu linaloheshimiwa na Waislamu na Wayahudi. Hamas - kundi la wanamgambo wa Kipalestina linalosimamia Gaza - lilianza kufyatua roketi baada ya kuionya Israeli ijiondoe kwenye eneo hilo , na kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa Israel

Mashambulizi yameendelea usiku kucha

Wanajeshi wa Israeli walisema kuwa walishambulia nyumba za Yahya Sinwar na kaka yake Muhammad Sinwar, ambaye ilimtaja kama mkuu wa vifaa na nguvu kazi wa Hamas.

Makazi hayo yote yalikuwa, "ilisema" kama ngome ya miundombinu ya kijeshi "kwa Hamas.

Yahya Sinwar (file photo)

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Yahya Sinwar (Maktaba)

Vyanzo vya ndani vilithibitisha kwa vyombo vya habari kwamba nyumba ya kiongozi wa Hamas ilikuwa imepigwa bomu. Hakukuwa na ripoti kuhusu hatima ya ndugu hao wawili.

Mashambulio mengi ya angani yalitikisa Jiji la Gaza wakati wa usiku, na watu wengi waliripotiwa kupotea chini ya vifusi vya nyumba, Rushdi Abualouf wa BBC alisema.

"Sijawahi kuripoti kuhusu mashambulizi makali ya anga kama haya , milipuko iko kila mahali huko Gaza, kuna ugumu wa kuwasiliana na maafisa ili mashambulizi yako wapi," alisema kwenye Twitter.

"Jengo ambalo ninaishi katika [magharibi] ya jiji lilitikiswa kama tetemeko la ardhi," alisema. "Hali ya wasiwasi na machafuko, watoto na wanawake katika jengo hilo ambalo lina zaidi ya watu 200 wakipiga kelele."

Kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas, watu 26 waliuawa na 50 walijeruhiwa katika Mtaa wa al-Wehda katikati mwa Jiji la Gaza usiku kucha , na watoto wanane na wanawake 10 kati ya waliokufa. Shughuli ya kuwatafuta watu chini ya vifusi inaendelea

Makombora takriban 120 yalirushwa na wanamgambo huko Gaza kwenda kusini na katikati mwa Israeli mara moja, jeshi la Israeli lilisema. Hakukuwa na ripoti za majeraha mabaya.

Je,Kuna uwezekano wa mapigano kusitishwa?

Akiwalaumu wanamgambo kwa mzozo huo. Bw Netanyahu alisema mashambulizi yataendelea kwa "muda mrefu kadri itakavyohitajika" na kila linalowezekana lilikuwa likifanywa ili kupunguza vifo vya raia.

Jumamosi, jeshi la Israeli lililipua Jengo la ghorofa katika Jiji la Gaza linalotumiwa na vyombo vya habari vya kimataifa baada ya kutoa ilani kwa waliokuwemo kuondoka .

Rais Biden alimwambia Bw Netanyahu aliendelea kuunga mkono haki ya Israeli ya kujilinda. Alielezea wasiwasi wake juu ya vifo kwa pande zote mbili na akataka waandishi wa habari walindwe.

Akizungumza na Rais Abbas, kiongozi huyo wa Marekani alisema amejitolea "kuimarisha ushirikiano wa Marekani na Palestina". Alisema pia mashambulizi ya roketi kutoka kwa Hamas ndani ya Israeli yanafaa kukomeshwa mara moja .

Rais Abbas, ambaye yuko katika Ukingo wa Magharibi, ana nguvu kidogo huko Gaza lakini Marekani imekataa kuzungumza na Hamas, ambayo inaiona kama kundi la kigaidi.

ramani

Bwana Biden aliwaambia viongozi wote aliendelea kujitolea kutafuta suluhisho la kuwepo nchi mbili ili kumaliza mzozo huo.

Mjumbe wa Marekani Hady Amr yuko Tel Aviv kushiriki katika mazungumzo na maafisa wa Israeli, Palestina na UN, na kuimarisha kile wanadiplomasia wa Marekani walisema ni umuhimu wa kurejesha "utulivu wa kudumu'.

Kabla ya mkutano wa Baraza la Usalama, Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres alizikumbusha pande zote "kwamba kuwalenga raia na vyombo vya habari kunakiuka sheria za kimataifa na lazima iepukwe kwa gharama yoyote".

Maandamano yanayounga mkono Wapalestina yalifanyika ulimwenguni siku ya Jumamosi, kutoka Ulaya hadi Marekani. Katikati mwa Paris, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi na maji kutawanya maandamano yasio halali ilhali huko London, maafisa tisa wa polisi walijeruhiwa wakati wa makabiliano na waandamanaji nje ya ubalozi wa Israeli.