Sababu zilizofanya Somalia iwe na ghadhabu kali dhidi ya UAE

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa wiki kadhaa, Somalia imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kidiplomasia kuhamasisha uungwaji mkono wa kimataifa baada ya Israel kulitambua eneo lake lililojitenga la Somaliland kama taifa huru.
Kupitia juhudi za kidiplomasia na mawasiliano ya ngazi za juu kwa njia ya simu, serikali ya Somalia imefanikiwa kupata uungwaji mkono wa nchi nyingi barani Afrika na Mashariki ya Kati, zikikusanyika kupinga hatua hiyo ya utambuzi. Hata hivyo, uhusiano mmoja umeharibika kwa kiasi kikubwa, ushirikiano wa muda mrefu wa Somalia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kwa miaka mingi, taifa hilo tajiri kwa mafuta limekuwa likionekana kama mdau muhimu katika masuala ya usalama, uchumi na siasa za Somalia, hasa ikizingatiwa kuwa Somalia ina ufukwe wa zaidi ya kilomita 3,000 (maili 1,864) kando ya Ghuba ya Aden na Bahari ya Hindi, eneo la kimkakati la baharini lililoathiriwa na uharamia na usafirishaji haramu wa silaha, mambo ambayo yamechangia kukosekana kwa utulivu barani Afrika na Mashariki ya Kati.
UAE ilijenga uhusiano wa ngazi nyingi na serikali ya shirikisho ya Somalia pamoja na maeneo yake ya kikanda, na imehusika katika uendeshaji wa bandari za Bosaso huko Puntland na Kismayo huko Jubaland, pamoja na Bandari ya Berbera huko Somaliland.
Lakini siku ya Jumatatu, serikali ya shirikisho ya Somalia ilitangaza kufuta mikataba yote ya ushirikiano wa usimamizi wa bandari na usalama na UAE, ikiituhumu kwa kudhoofisha mamlaka ya nchi hiyo.
"Tulikuwa na uhusiano mzuri na UAE, lakini kwa bahati mbaya hawakutuhusisha kama taifa huru na lenye mamlaka kamili. Baada ya tathmini ya kina, tulilazimika kuchukua uamuzi tuliouchukua," Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema katika hotuba ya televisheni baada ya kikao cha dharura cha baraza la mawaziri.
Hadi sasa, UAE haijatoa majibu kuhusu kauli zake.
Omar Mahmoud, mtafiti mwandamizi katika taasisi ya utafiti ya International Crisis Group, aliiambia BBC kuwa utambuzi wa Somaliland na Israel ndio uliokuwa msingi wa uamuzi huo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Somalia inaona hili kama uvunjaji wa uadilifu wa mipaka yake ya eneo na inaamini kuwa UAE ilichukua jukumu la siri katika kuunga mkono matokeo hayo," Mahmoud anasema.
Mwishoni mwa Desemba, Israel ikawa nchi ya kwanza duniani kuitambua Somaliland kama taifa huru. Hatua hiyo ilisababisha shangwe kubwa katika mji mkuu wa Somaliland, Hargeisa, kwani Israel ilikuwa imetoa utambuzi ambao eneo hilo limekuwa likiuota kwa muda mrefu tangu lilipojitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita, likaunda serikali yake, na kupitisha pasi ya kusafiria na sarafu yake yenyewe.
Kwa upande wake, Somaliland ilisema itajiunga na Mikataba ya Abraham ya mwaka 2020, ambayo hadi sasa imeshuhudia UAE, Bahrain na Morocco zikianzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia na Israel, jambo lililoipa serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu msukumo wakati ambapo imekuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kuhusu vita vya Gaza.
"Eneo hili linazidi kufafanuliwa na miungano ya kijiografia na kisiasa inayotofautiana, ambapo UAE na Israel wako upande mmoja, na Saudi Arabia, Uturuki na wengine wako upande mwingine," Mahmoud anasema.
Siku ya Jumatatu, tovuti ya habari ya Middle East Eye iliripoti kuwa athari za mtafaruku wa kidiplomasia zimesababisha UAE kuwaondoa wafanyakazi wake wa usalama pamoja na vifaa vizito vya kijeshi kutoka kambi ya anga ya Bosaso.
Mahmoud anasema kuwa uhusiano kati ya Somalia na UAE umekuwa ukizorota taratibu tangu mwaka 2024, wakati Ethiopia, mshirika mkubwa wa UAE katika eneo la Pembe ya Afrika ilipoonesha kuwa iko tayari kuitambua Somaliland kama taifa huru, kama sehemu ya makubaliano ambayo yangeiruhusu kuanzisha kambi ya kijeshi ya majini katika pwani ya eneo hilo lililojitenga.
"Shaka ya Somalia dhidi ya UAE iliongezeka kufuatia hati ya makubaliano ya mwaka 2024 kati ya Ethiopia na Somaliland ya kubadilishana upatikanaji wa bahari na utambuzi, kwani Somalia iliiona UAE kama ilikuwa ikiunga mkono makubaliano ambayo iliupinga vikali.
"Lakini Ethiopia iliahidi tu kutoa utambuzi. Israel ilitekeleza ahadi hiyo, na hilo linaongeza uzito wa mgogoro," Mahmoud anaongeza.
Mchambuzi huyo pia anabainisha kuwa Somalia imeituhumu UAE kwa kutumia ardhi yake kumsaidia kiongozi wa waasi wa kujitenga wa Yemen, Aidarous al-Zubaidi, kuondoka nchini humo, hatua ambayo inaelezwa kuwa huenda ilikuwa "tone la mwisho" lililosababisha kuvunjika kwa uhusiano wao.
"Kutumia anga ya Somalia na viwanja vyake vya ndege kumsafirisha mtu anayekimbia sheria si jambo ambalo Somalia inalikubali," Ali Omar, waziri wa nchi wa Somalia anayeshughulikia masuala ya mambo ya nje, aliiambia Al Jazeera.
Wiki iliyopita, muungano unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen ulitoa tuhuma kama hizo, ukidai kuwa al-Zubaidi, ambaye anaongoza Baraza la Mpito la Kusini (Southern Transitional Council) la waasi wa kujitenga wa Yemen, alivuka hadi Berbera kwa njia ya bahari, kisha akasafirishwa kwa ndege ya mizigo hadi Abu Dhabi kupitia Mogadishu chini ya "usimamizi" wa maafisa wa UAE. UAE inakanusha kuunga mkono waasi wa vuguvugu la kujitenga nchini Yemen.
Hii si mara ya kwanza kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Somalia na UAE kuzorota. Mwaka 2018, Somalia chini ya Rais wa wakati huo Mohamed Abdullahi Farmajo ilikata uhusiano na UAE, ikiituhumu kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Wakati huo, rais wa sasa alikuwa kiongozi wa upinzani na alitetea kwa nguvu ushiriki wa UAE nchini Somalia, lakini sasa amekuwa na msimamo tofauti kabisa, akijaribu kutumia tofauti zilizopo kati ya UAE na Saudi Arabia kuhusu vita vya Yemen kwa manufaa yake.
"Maendeleo ya kikanda, ikiwemo utambuzi wa Somaliland na Israel na mabadiliko ya kisiasa nchini Yemen yanayohusisha Saudi Arabia na Baraza la Mpito la Kusini, yaliweka shinikizo la kutosha kwa serikali kuchukua hatua za haraka na za uamuzi," Samira Gaid, mchambuzi katika taasisi ya utafiti ya Balqiis Insight, aliiambia BBC.

Chanzo cha picha, Reuters
Hata hivyo, Mahmoud anasema serikali ya shirikisho ya Somalia haina uwezo wa kutekeleza uamuzi wake wa kufuta mikataba ya bandari na UAE, kwa kuwa haina mamlaka juu ya jimbo lililojitenga la Somaliland.
Vilevile, haina udhibiti mkubwa juu ya bandari zilizoko Puntland na Jubaland, maeneo mawili yenye mamlaka ya nusu uhuru ndani ya Somalia.
"Serikali ya Somalia ina uwepo mdogo sana katika maeneo haya na iko katika ushindani wa kisiasa na tawala hizi kuhusu mgawanyo wa madaraka ndani ya mfumo wa shirikisho wa Somalia," Mahmoud anasema.
Kampuni ya usafirishaji na vifaa ya DP World yenye makao yake Dubai inaonekana kutotikiswa na tangazo la serikali ya shirikisho, ikisema shughuli zake katika bandari ya Berbera huko Somaliland zitaendelea kama kawaida.
"DP World inaendelea kujikita katika uendeshaji salama na wenye ufanisi wa bandari, pamoja na kuwezesha biashara na kuleta manufaa ya kiuchumi kwa Somaliland na eneo lote la Pembe ya Afrika," kampuni hiyo ilisema katika taarifa kwa Reuters, ikiongeza kuwa maswali kuhusu "maamuzi ya kisiasa, mazungumzo ya kiserikali, au misimamo ya kidiplomasia yanapaswa kuelekezwa kwa mamlaka husika."
Kauli hiyo haikushangaza, kwani Somaliland ilisema kuwa mikataba yake yote na UAE "inaendelea kuwa halali na yenye nguvu kisheria."
Kwa upande wa Jubaland, ilisema inaona uamuzi wa serikali ya shirikisho kuwa "batili na hauna nguvu yoyote ya kisheria," huku Puntland ikilaani uamuzi huo ikisema "hauendani na misingi ya utawala wa kikatiba."
Hata hivyo, Mahmoud anasema Somalia bado ina njia za kuishinikiza UAE na washirika wake, licha ya changamoto zilizopo.
"Mogadishu inadhibiti anga ya nchi na inaweza kutumia uwezo huo, pamoja na shinikizo la kidiplomasia, kushinikiza UAE na tawala za kikanda.
"Somalia pia ina uwezekano wa kuhamasisha washirika wake kama Uturuki na Saudi Arabia kuunga mkono msimamo wake," anaongeza.
Mahmoud haoni uhusiano kati ya Somalia na UAE ukiimarika katika siku za usoni, kwani "imani tayari imepotea."
"Itahitaji juhudi kubwa za kidiplomasia na hatua za vitendo kurekebisha hali hiyo," anasema.















