Somalia yakatiza uhusiano wa kidiplomasia na UAE

Somalia imetangaza kukatiza uhusiano na Umoja wa Falme za Kiarabu, na kufuta makubaliano yote ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya kikao cha baraza la mawaziri siku ya Jumatatu, Baraza la Mawaziri limesema kuwa limebatilisha mikataba yote iliyofikiwa na UAE, ikiwa ni pamoja na ile inayohusiana na bandari, usalama na ushirikiano wa ulinzi.
Uamuzi huo unajumuisha mipango yote inayohusisha bandari za Berbera, Bosaso, na Kismayo, pamoja na makubaliano na taasisi za serikali, mashirika tanzu na tawala za mikoa.
Miongoni mwa mikataba iliyoathiriwa ni mkataba wa bandari ya Berbera, ambapo utawala wa Somaliland ulitia saini mkataba wa usimamizi mwaka 2016 na DP World.
Serikali ya Somalia kwa muda mrefu imekuwa ikipinga makubaliano hayo, ikisema yalifikiwa bila idhini yake.
Serikali ilisema hatua hiyo ilichukuliwa ili kulinda mamlaka ya Somalia, umoja wa eneo na utaratibu wa kikatiba.
Ilisema uamuzi huo ulifuata kile ilichotaja kama ripoti za kuaminika na ushahidi wa vitendo vinavyodhoofisha uhuru wa Somalia, umoja wa kitaifa na mamlaka ya kisiasa.
Baraza la Mawaziri lilisema vitendo hivyo vinakiuka kanuni za kimataifa za kujitawala na kutoingilia kati, kama ilivyoainishwa katika mikataba ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.
Wizara ya Mambo ya Nje imeagizwa kuiarifu rasmi Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu uamuzi huo na kuratibu utekelezaji wake.
Wizara hiyo pia itawafahamisha washirika wa kimataifa na kikanda, ikiwemo Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Serikali ya Somalia ilisema bado iko wazi kwa ushirikiano wa kimataifa unaozingatia kuheshimiana, kutambua mamlaka ya Somalia, na kuzingatia kanuni za kikatiba na kimataifa.


















