Lipa fidia ama ufe: Simulizi za 'kutisha' kutoka kwa jamaa za wafungwa wa RSF El Fasher

Chanzo cha picha, Getty Images
Waasi wa Rapid Support Forces (RSF) wamekuwa wakiwazuilia makumi ya wakaazi wa El Fasher kaskazini mwa Darfur nchini Sudan tangu walipochukua udhibiti wa mji huo, kulingana na ushahidi uliokusanywa na BBC kutoka kwa familia ambazo zinaishi kwa hofu ya kushambuliwa na vikosi hivyo.
Kijana ambaye hakutaka kutaja jina lake halisi alizungumza na BBC.
Mohammed Ahmed (sio jina lake) amekuwa akitunza familia yake tangu vita vilipozuka Sudan japo alikuwa ikiishi nje ya nchi.
Anasema amekuwa akifuatilia habari na video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu wapiganaji wa RSF walipouteka mji wa El Fasher, kusaka mtu yeyote wa wanafamilia yake ambaye amekwama ndani ya jiji hilo kwa zaidi ya miezi 16.
"Nilishindwa kulala kwa siku mbili, nilikuwa nikitazama video hizo nikitarajia kumtambua mmoja wao, hadi nikamuona mjomba na jirani yangu kwenye moja ya video wakiwa wamekaa chini huku wakihojiwa na RSF,''alisema.
''Nilidhani wameuawa, hasa baada ya matukio ya mauaji ya watu wengi kuenea katika video hizo mitandaoni."
Lakini Aalipigwa na mshangao alipopokea simu kupitia App ya Messenger kutoka kwa mjomba wake siku mbili baada ya video hizo kutolewa.
Mjomba wake alimwambia kuwa bado yuko hai lakini anashikiliwa na askari wa RSF, ambao walikuwa wakidai fidia ya pauni milioni 10 za Sudan, au takriban dola 3,00 za Kimarekani.
''Mmoja wa askari wa RSF kilizungumza nami na kunipa saa moja tu ya kutuma pesa, vinginevyo mjomba wangu angeuawa. Nililazimika kukopa pesa hizo na kuwatumia kwa wakati kwa kuhofia mjomba angeuawa," alisema Mohammed.
Hatimaye mjomba wake aliachiliwa baada ya fidia kulipwa, na aliweza kufika mji wa Tawila, ulioko takriban kilomita sita magharibi mwa El Fasher.
Hakuna hakikisho hata fidia ikilipwa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hali ilikuwa ngumu kwa zaidi kwa Ibrahim Qasim (sio jina lake halisi). Kikosi cha RSF kilikua kinawashikilia watu watano wa familia yake.
Anasema alifanikiwa kumkomboa kaka yake baada ya kulipa fidia ya pauni milioni kumi za Sudan, lakini kundi hilo lilidai kiasi sawai ana hicho cha fedha ili kuwaachilia huru binamu zake wawili, pamoja na pauni milioni 25 za ziada ili kuwaachilia ndugu wa mama yake.
Ibrahim anasema: "Katika simu ya kwanza, walinipa dakika kumi tu kutuma pesa kupitia huduma ya (Bankak), na walitishia kumuua kaka yangu. Pia walinipa saa moja kulipa fidia ya mjomba wangu ambaye alijeruhiwa wakati wa vita vya Al-Fasher.
Na mpaka sasa, sijafanikiwa kukamilisha fedha zinazohitajika ili kuwaachilia ndugu zangu wengine."
Jamaa wa wafungwa hao ameiambia BBC kuwa hakuna hakikisho la kweli kwamba ndugu zao wataachiliwa baada ya fidia kulipwa, akibainisha kuwa baadhi ya walioachiliwa wanakamatwa tena wakati wakijaribu kuondoka jijini, na anaeleza kinachoendelea kuwa ni "msururu wa unyang'anyi".
Baadhi ya familia za mateka zimeishiwa kabisa na akiba baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu, Wale walio nche ya nchi wamekuwa wakituma pesa kwa jamaa zao ili wawanunue chakula, ambacho bei ilikuwa imepanda. Sasa, fidia zinakusanywa kupitia michango, mikopo, au usaidizi kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada na ya kibinadamu.
Hali ya inazidi kuzorota

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Novemba 4, 2025, Madaktari Wasio na Mipaka walisema kuwa vikosi vya RSF vinawashikilia maelfu ya raia ndani ya jiji la El Fasher, kuwazuia kuondoka baada ya kuchukua vyombo vyote vya usafiri vilivyotumika kuwahamisha waliokimbia makazi yao.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa baadhi ya waliokimbia walirudishwa mjini kwa nguvu wakiwemo waliopigwa risasi wakati wakijaribu kutoroka na wengine kukabiliwa na utapiamlo.
Taarifa hiyo aidha ilionya kwamba kuendelea kuzuiliwa kwa idadi kubwa ya raia katika mazingira magumu, kukiwa na uhaba mkubwa wa dawa na ukosefu wa na huduma za matibabu - kunazidisha janga la kibinadamu linalozidi kuwa mbaya.
Pia iliongeza kuwa miili ya watu waliouawa ambayo imetapakaa viungani mwa jiji hilo ni tishio kubwa kwa mazingira.
Mtandao huo uliomba kuachiliwa mara moja kwa raia, kufunguliwa kwa njia salama ili kuwawezesha raia waliokwama kuondoka, kuruhusi mashirika ya kibinadamu kufikia maeneo yaliyoathiriwa, na kuhifadhiwa kwa miili uliyotapakaa mitaani ili kuzuia maafa ya mengine ya kimazingira.

Chanzo cha picha, Getty Images
GHada Abdel Rahman, mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu, anaelezea hali ya sasa ya raia wanaozuiliwa El Fasher kuwa ya kusikitisha, na anadai kuwa ni "ukiukwaji mkubwa" wa sheria za kimataifa na za kibinadamu, akiongeza kuwa kushikiliwa kwa raia katika maeneo yenye migogoro kama mateka, jinsi wanavyofanywa wanamgambo RSF, ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na za kibinadamu.
Abdel Rahman anabainisha kwamba kuna ukiukwaji wa wazi wa haki dhidi ya raia huko El Fasher, akiongeza kuwa vikosi vya RSF vinafanya uhalifu wa kifedha kwa kuwaweka kizuizini raia na kudai fidia kutoka kwa familia zao ili waachilie huru.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












