'Hatuuzwi': Wakaazi wa Greenland waelezea hofu yao huku Trump akipanga kulitwaa eneo hilo

    • Author, Abdou Aziz Diédhiou
    • Nafasi, BBC News Afrique
  • Muda wa kusoma: Dakika 5
Mia Chemnitz

Chanzo cha picha, Mia Chemnitz

Maelezo ya picha, Mia Chemnitz anasema "Wakaazi wa Greenland hawataki kuwa Wamarekani"

"Sisi wa wakaazi wa Greenland hatutaki kuwa Wamarekani," Mia Chemnitz aliiambia BBC, "Hatuuzwi."

Mwanabiashara huyo mwenye umri wa miaka 32 katika jiji kuu la Nuuk huko Greenland inaunga mkono msimamo wa baadhi wa wakaazi waliozungumza na BBC kuhusu jinsi walivyohisi kuhusu matamshi ya hivi punde ya utawala wa Trump.

Ikulu ya White House imesema kwamba "inajadili" mpango wa kununua eneo ambalo kwa karne nyingi limekuwa la Denmark. Rais wa Marekani Donald Trump na maafisa wake hapo awali walikuwa wamedokeza nia ya kuichukua kwa nguvu ikiwa wakilazimika kufanya hivyo.

Kauli hiyo imeibua hofu miongoni mwa watu wa Greenland - nani na nje ya kisiwa hicho kikubwa zaidi duniani na kwingineko.

Wasiwasi huu umeongezeka tangu Marekani ilipomkamata Rais wa Venezuela Nicolas Maduro kutoka makao yake huko Caracas na kumsafirisha hadi New York kwa mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya na ugaidi katika operesheni ya kijeshi ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Mara baada ya hapo, mke wa afisa mkuu wa watumishi wa Ikulu ya White House aliashiria kuwa Greenland inayofuata.

"Hapo ndipo nilipigwa na butawaa," anasema Tupaarnaq Kopeck, 40, ambaye alihamia Canada - eneo lingine ambalo Trump ametishia kulinyakua - kwa familia na kazi.

"Kwa mara ya kwanza, niliwasiliana na dada yangu anayeishi Greenland na kumwambia kwamba ikiwa jambo hili la kushangaza linaweza kufanyika, wana mahali pa kuishi nasi."

Aaja Chemnitz, mmoja wa wabunge wawili katika bunge la Denmark anayeiwakilisha Greenland, anasema maoni kutoka kwa utawala wa Trump ni "tishio la wazi" ambalo "alichukizwa" nalo.

"Jaribio la Marekani kutaka kunyakua eneo lilipo ndani ya nchi yetu ni dharau kubwa kutoka kwa mshirika mwingine wa Nato," anasema.

Tupaarnaq Kopeck

Chanzo cha picha, Tupaarnaq Kopeck

Maelezo ya picha, Tupaarnaq Kopeck anasema uingiliaji wa kijeshi nchini Venezuela imenifanya nihisi tishio hilo kuwa la kweli
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Greenland ni eneo lenye watu wachache zaidi ulimwenguni. Kwa kuwa sehemu kubwa ya kisiwa hicho cha Aktiki kimefunikwa na barafu, wakazi wengi wanaishi Nuuk na ukanda wa pwani wa kusini-magharibi unaozunguka.

Lakini ni muhimu kimkakati kwa Marekani - ndiyo maana imekuwa na uwepo wa kijeshi katika eneo hilo tangu wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

"Inasikitisha kuwa miongoni mwa watu 56,000 wanaokabiliwa na vitisho hivi - kama unaweza kusema - kutoka kwa nchi kubwa kama Marekani," anasema Masaana Egede, Mhariri wa gazeti la Greenland linaloitwa Sermitsiaq.

Eneo la Greenland liko kati ya Amerika Kaskazini na Arctic jambo ambalo hulifanya liwe mahali pazuri pa kuweka mifumo ya tahadhari ya mapema iwapo kuna mashambulizi ya makombora.

Hivi majuzi, pia kumeongezeka hamu ya maliasili ya Greenland, ikiwa ni pamoja na madini adimu, ambayo yanapatikana kwa urahisi barafu yake inapoyeyuka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Raia wa Greenland wana hofu juu ya hili, kwa sababu hili sio jambo ambalo tunalichukulia kirahisi."

Wataalamu kwa ujumla wanakubali kwamba kuichukua Greenland kijeshi itakuwa ni jambo rahisi kwa Marekani - lakini mzozo huo wa kisiasa wa kijiografia ungemaliza kabisa muungano wa Nato.

Baada ya suala la umiliki wa Greenland kuibuliwa upya na Ikulu ya Marekani, washirika sita wa Ulaya walitoa taarifa wakisema mustakabali wake unapaswa kuamuliwa na watu wake - jambo ambalo Mia anasema anashukuru.

Lakini ana wasiwasi kwamba hii haitakuwa na umuhimu kwa Marekani "ikiwa haijaungwa mkono kwa vitendo".

"Kama mkazi, ninajiuliza: thamani yetu kwa washirika hawa ni ipi? Je, wako tayari kutulinda kwa kiwango gani?"

Tupaarnaq anasema: "Heshima ya miungano inaishia kwenye karatasi. Wakati mataifa yenye nguvu yanapozungumza kukuhusubadala ya kusema na wewe, heshima hiyo haidumu."

Aleqatsiaq Peary, a 42-year-old Inuit hunter, infront of a boat

Chanzo cha picha, Aleqatsiaq Peary

Maelezo ya picha, Aleqatsiaq Peary, mwindaji wa Inuit aliye na umri wa miaka 42 anasema kuwa Marekani itatwaa tu "mkaaji mmoja badala ya mwingine"

Utawala wa Trump umesisitiza nia yake ya kuinunua Greenland kutoka kwa Denmark - licha ya Copenhagen kuilia mkazo kuwa eneo hilo haliuzwi- huku ikibakiza uingiliaji wa kijeshi kama chaguo.

Aaja anaona unyakuzi kwa nguvu hauwezekani - badala yake, "tunachoona ni kwamba watatuwekea shinikizo ili kuhakikisha kwamba wataichukua Greenland baada ya muda".

Kura ya maoni mara kwa mara inaonyesha kuwa wakazi wa Greenland kwa ujumla wanapendelea kuwa na uhuru kutoka kwa Denmark lakini wanapinga kumilikiwa na Marekani. Eneo hilo kwa kiasi kikubwa linajitawala, huku udhibiti wa mambo ya nje na ulinzi ukisalia Copenhagen.

Labda hii ndiyo sababu Aleqatsiaq Peary, mwindaji wa Inuit aliye na umri wa miaka 42 anayeishi katika mji wa kaskazini wa Qaanaaq, alionekana kutoshtushwa na matarajio ya umiliki wa Marekani.

"Itakuwa sawa na kubadili kutoka kwa bwana mmoja hadi mwingine, kutoka kwa mwenyeji mmoja hadi mwingine," anasema. "Sisi ni koloni chini ya Denmark. Tayari tunapoteza mengi kutokana na kuwa chini ya serikali ya Denmark."

Lakini anasema: "Sina muda wa Trump. Watu wetu wana uhitaji," akieleza wawindaji kama yeye huwinda na mbwa kwenye barafu na kuvua samaki baharini, "lakini barafu ya bahari inayeyuka na wawindaji hawawezi kujikimu tena".

Kwa mhariri wa Sermitsiaq Masaana, tamko la Marekani linashiniza chaguo mbili ngumu na hakuna iliyo sahali.

"Kwa kweli lazima tujaribu kuzuia suala hali ambapo Greenland italazimika kuamua kati ya Marekani na Denmark, kwa sababu hiyo sio chaguo ambalo watu wa Greenland wanataka."

Christian Keldsen

Chanzo cha picha, Christian Keldsen

Maelezo ya picha, Christian Keldsen anasema "watu huko Greenland wanakerwa sana na hili"

Kwa wengine, ambao wanaona uhusiano uliopo sasa kati ya Greenland na Marekani kuwa mbaya, bila shaka wanaghabishwa na yale yanayoendelea.

"Watu wa Greenland wanakerwa sana na hili," anasema Christian Keldsen wa Chama cha Biashara cha Greenland.

"Wakazi wa Greenland ni wakarimu na wenye moyo mkunjufu, ni jambo muhimu sana kwa nchi. Lakini sasa kwa hili, baadhi ya watu wana hofu."

Greenland iko wazi kufanya biashara na Marekani, Christian anasisitiza, akibainisha kuwa kuna safari mpya za ndege za moja kwa moja kutoka Greenland hadi New York - ishara ya uhakika "hawana haja ya kutuchukua".

"Sisi ni demokrasia inayofanya kazi vyema na serikali yetu ina mamlaka madhubuti," Mia anasema. "Sisi ni mshirika wa Nato na Marekani imekuwa na kambi za kijeshi huko Greenland kwa zaidi ya miaka 70 - na bado ina haki ya kuanzisha na kuendesha mpya na zaidi.

"Kama ilivyosemwa kutoka Greenland hapo awali: hatuuzwi, lakini tuko wazi kwa biashara."