Kwanini ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance katika kambi muhimu ya Greenland imeibua utata?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Guillermo D. Olmo
- Nafasi, BBCgolmo
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Kituo cha anga cha Pituffik kilichopo kaskazini magharibi mwa Greenland kimekuwa na jukumu muhimu la kufanya upelelezi na kugundua makombora ambayo yanapaniwa kuelekezwa kwa Marekani na kutoa onyo.
Greenland imekuwa kipaumbele cha Washington tangu Rais Donald Trump aliporejea Ikulu ya White House.
Rais Trump anakiangalia kisiwa hiki kama eneo muhimu kwa ulinzi wa Marekani na kulaumu Denmark kwa kushindwa kuhakikisha usalama wa kisiwa hicho chini ya mamlaka yake.
Mivutano iliongezeka wiki hii baada ya kutangazwa kwa ziara ya kushtukizia ya ujumbe wa kiwango cha juu wa Marekani uliongozwa na Usha Vance, ambaye baadaye mume wake alijiunga naye, Makamu wa Rais JD Vance.
Serikali ya Denmark na utawala huru wa Greenland walipinga safari hiyo, hadi Washington ilipotangaza kuwa itazuru tu kwenye kambi ya Pituffik, ambayo imekuwa chini ya udhibiti wa Marekani tangu miaka ya 1950.
Kambi ya Pituffik na umuhimu Wake

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika kona hii ya mbali ya Arctic, kilomita 1,200 kutoka kwa ncha ya Kaskazini, kambi hii imekuwa sehemu muhimu tangu mwanzo wa Vita Baridi.
Ilianzishwa ili kugundua mashambulizi ya makombora kutoka kwa Umoja wa Kisovieti na kurejesha mapigo kwa haraka.
Kambi hii ya zamani, iliyojulikana kama John Thule Air Force Base, inasimamiwa na Kikundi cha 821 cha Kambi ya Anga, ambacho kinajumuisha Kikosi cha Onyo cha Anga cha 12 na Kitengo cha Operesheni cha Anga cha 23.
Kazi yake ni kufuatilia anga, kutoa onyo la mashambulizi ya makombora, na kufuatilia satelaiti za ulinzi za Marekani.
Kutokana na jukumu hili la kambi hii Makamu wa Rais wa Marekani Vance alitaja kuwa ni ulinzi wa Marekani uliyoko kaskazini ya dunia.
''Pituffik ni kambi muhimu kimkakati kwa sababu ya eneo lake la kijiografia'', Troy J. Bouffard, afisa mstaafu wa Jeshi la Marekani na mtaalamu wa usalama wa Akitiki, alisema.
"Wakati wa Vita Baridi, Akitiki ilikuwa njia fupi ya kushambulia Marekani kwa kutumia makombora ya masafa marefu, na inabaki kuwa njia muhimu kwa adui yeyote anayetaka kushambulia Marekani leo," anaiambia BBC.
Taswira unayokutana nayo ukitembelea kambi hiyo ina kuba nyeupe za Rada (chombo kitumiwacho na marubani kuonyesha vitu kwenye skrini vitu vinavyokaribia eneo lao).
Ni mifumo inayogundua pindi makombora ya kimaabara na makombora Yanayozinduliwa kwa Bahari (ICBMs na SLBM, mtawalia) yanapozinduliwa.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kulingana na data iliyochapishwa na Idara ya Ulinzi ya Marekani, kikosi hicho kina takriban watu 650.
Mia mbili ni wanachama wa Jeshi la Anga la Marekani na Jeshi la wanahewa.
Wengine ni wakandarasi wa kiraia wa Kanada, Denmark, na Greenland wanaoishi na kufanya kazi kwenye kambi.
Maisha katika kambi hii ni magumu.
Theluji inafunika sehemu kubwa ya kambi kila mara, joto linashuka hadi -34°C, na katika majira ya baridi, jua linatoweka kwa wiki kadhaa.
Mji ulio karibu na kambi hiyo, Qaanaaq, uko zaidi ya kilomita 100 kwa umbali na ni makazi madogo ambapo wakazi wanajimudu kwa uwindaji wa muhuri, nyangumi, na dubu wa ncha za dunia.
Kambi ya Pituffik inategemea uwanja wa ndege ambao unafanya kazi mwaka mzima ili kuunganishwa na dunia ya nje.
Jeshi la Uhandisi la Marekani mara nyingi linahusika na kukarabati miundombinu katika mazingira magumu ya Akitiki.
Utafiti wa kisayansi pia hufanywa katika kambi ya Pituffik.
Tangu kuundwa kwake, Jeshi la Marekani limesoma mazingira ili kuwezesha shughuli zake, na NASA imechunguza upotevu wa barafu katika Akitiki kutoka huko.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwanini Marekani ina kambi ya kijeshi Greenland?
Marekani ni nchi pekee, kando na Denmark, inayokuwa na kambi ya kijeshi ya kudumu huko Greenland.
Uwepo wake wa kijeshi ulianza wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, wakati Denmark ilipoanguka na kudhibitiwa na majeshi ya Kijerumani ya Hitler.
Marekani ilituma wanajeshi Greenland na kuanza kujenga viwanja vya ndege na miundombinu mingine ili kufuatilia shughuli za meli za kivita za Kijerumani.
Baada ya vita, na ushindani mkubwa kati ya Marekani na Sovieti, Marekani na Denmark walitia saini makubaliano yanayotambua haki ya Marekani kudumisha wanajeshi na vituo huko Greenland.
Kuundwa kwa NATO mnamo 1949, ambayo Marekani na Denmark ni wanachama wake, kulithibitisha ushirikiano mkubwa wa ulinzi kati ya nchi hizi mbili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika muktadha wa Vita Baridi, kambi ya wakati huo wa Thule ukawa hatua muhimu kwenye njia ya ncha za dunia, njia fupi zaidi ya shambulio la moja kwa moja linaloweza kutokea kati ya mataifa mawili yanayopigana kwa kutumia nyuklia.
Tangu hapo, walipuaji wa mabomu wa Marekani waliweza kufikia eneo la Soviet, na mifumo mikubwa ya rada ambayo Makao Makuu ya jeshi la Marekani ilimtazama adui wa Soviet ilijengwa hapo.
Wakazi wa asili waliokuwa wakiishi katika eneo hilo kabla ya kuwasili kwa wanajeshi wa Marekani ndio wahasiriwa.
Takriban 150 kati yao walihamishwa kutoka nchi za mababu zao na kulazimika kuhamia eneo ambalo uwindaji, msingi wa maisha yao ya kitamaduni, ulikuwa mgumu zaidi.
Ilichukua miongo kadhaa Denmark kutambua haki yake ya fidia ya kifedha.
Kukerwa na vitendo kama hivi kunaonekana kuwa mojawapo ya sababu zinazowafanya Greenland kukataa kwa wingi mamlaka ya Denmark na uanachama wake nchini Marekani katika kura za maoni.
Mnamo 2023, kituo hicho kilibadilisha jina lake rasmi kutoka Kituo cha Jeshi la Anga la John Thule hadi kambi ya anga ya Pituffik.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ulinzi wakati huo, mabadiliko hayo yalitaka "kutambua wenyeji wa eneo hilo na msaada wao kwa kituo cha usalama cha taifa cha Marekani."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pituffik na umuhimu wa Greenland
Greenland imekuwa mojawapo ya vipaumbele vya sera za kigeni za utawala wa Trump, na Pituffik imepata tena umaarufu ambao ziara ya Vance inasisitiza.
Trump amesema anataka kisiwa hicho kiwe mali ya Marekani, akisisitiza mara kwa mara kwamba usalama wake ni muhimu kwa Washington na kwamba Denmark haiwezi kuihakikishia.
Ikiwa wakati wa Vita Baridi kambi hiyo ilikuwa ufunguo wa kugundua au kuzuia makombora ya balestiki ya maabara, ushindani kati ya Urusi na Uchina kuunda silaha zenye kasi inathibitisha umuhimu ambao wachambuzi wa ulinzi wanahusisha nayo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pituffik ni kambi pekee ya kijeshi ya Marekani huko Greenland, na umuhimu wake umeongezeka kutokana na tishio la makombora yenye kasi.
Hivi sasa, silaha zenye kasi, ambazo zinaweza kusafiri kwa kasi kubwa na kwa urefu mdogo, ni tishio kubwa kwa usalama wa kimataifa.
Makombora haya ni vigumu kuzuia, na hivyo, kambi ya Pituffik inakuwa muhimu zaidi katika ulinzi wa Marekani.
Bouffard anasema, "Kwa teknolojia inayopatikana, hakuna kifaa cha ulinzi kinachofanya kazi dhidi ya silaha hii, kwa hivyo ulinzi unalenga kuzuia adui kutumia silaha za nyuklia."
Kwa hivyo, Pituffik ni sehemu muhimu kwa usalama wa Marekani, na inabaki kuwa suluhisho la kijiografia kwa changamoto za usalama za leo.
imetafsiriwa na Mariam Mjahid












