Vita vya Arctic? Kwa nini Norway na Denmark zinainasaidia Ukraine katika vita na Urusi

w

Na Georgy Erman

BBC News Ukraine

Baada ya kuzuka kwa vita kamili kati ya Urusi na Ukraine , Norway na Denmark zilikuwa wafadhili wakuu katika sekta ya usalama ya Ukraine. Norway ilitoa mifumo muhimu ya ulinzi wa anga ya NASAMS, na Denmark ikawa moja ya nchi za kwanza za NATO kuamua kuipatia Ukraine silaha za wa F-16.

Mataifa yote mawili yametuma mabilioni ya dola kwa Ukraine. Kulingana na taasisi ya ufuatiliaji wa misaada ya Ukraine, iliyoundwa na Taasisi ya Ujerumani ya Kiel ya Uchumi wa Dunia, Norway na Denmark zilichukua nafasi ya tano na sita baada ya Marekani, Ujerumani, Uingereza na EU katika suala la usaidizi wa kijeshi tangu mwanzo wa uvamizi wa Urusi.

Ikiwa tunazungumzia juu ya msaada wa nchi nyingine mbili za Scandinavia - Uswidi na Finland - kila kitu ni wazi zaidi. Zote mbili zina historia ndefu ya migogoro na Urusi; Ufini ilitetea uhuru wake katika vita vikali na USSR.

Nchi hizi zimeteseka mara kwa mara kutokana na vitendo vya Urusi, kwa mfano, ndege za kijeshi za Urusi zimepita kinyume cha sheria mara kwa mara anga la Uswidi.

Lakini kwa nini Norway na Denmark, ambazo hazina historia ya migogoro na Urusi, zikajitolea hata kabla ya majirani zao katika kanda katika suala la misaada kwa Ukraine?

Idhaa ya BBC ya Ukraine ilichunguza sababu kuu ni nini na mapambano ya Arctic, ambayo yameongezeka katika miaka 20 iliyopita, yana uhusiano gani nayo.

Kwa nini Oslo na Copenhagen wanaunga mkono Ukraine

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Denmark na Norway zote zina maeneo makubwa, lakini kila nchi ina wakazi milioni 5-6 tu. Uchokozi wa Urusi, ambao ni mkubwa katika eneo na idadi ya watu, dhidi ya Ukraine ndogo zaidi, ambayo inaambatana na uhalifu wa kivita, inaonekana kwao kama jaribio la kurejea katika hali ambayo "mataifa makubwa " yatalazimisha tena nchi ndogo kutekeleza utashi wao.

Kwa asili, tunazungumza juu ya uharibifu wa utaratibu wa ulimwengu, ambao umeruhusu nchi za Scandinavia kuishi kwa amani kwa miaka 80 iliyopita na kuwa mojawapo ya nchi zilizoendelea zaidi ulimwenguni.

"Kwa Norway, ambayo ina idadi ndogo ya watu, ni muhimu sana kudumisha heshima ya sheria za kimataifa na uhuru wa mataifa," anabainisha afisa wa mambo ya kigeni wa Ukraine nchini Norway Igor Golovchenko.

Kwa hiyo, Norway ina nia ya kushinda tisho la kijeshi la Kirusi sasa, na muhimu zaidi, ina rasilimali muhimu kwa ajili ya jeshi la Ukraine.

"Norway imetengeneza viwanda vya hali ya juu vya zana za kijeshi, kwa hivyo sio tu inajitahidi kuisaidia Ukraine, lakini pia ina fursa ya kufanya hivyo. Nchi hii ni mtengenezaji mkubwa wa vifaa vya mifumo ya ulinzi wa anga na makombora , "anasema mwanadiplomasia wa Kiukreni.

Norway iliipatia Ukraine mifumo ya ulinzi wa anga ya NASAMS, rada za kisasa za Arthur, makombora ya kukinga vifaru , makombora ya kuzuia ndege ya Mistral na aina zingine nyingi za silaha.

Ikishirikiana na Uingereza, Norway imeunda muungano wa ulinzi wa baharini wa Ukraine, na mamia ya wakufunzi wa Norway wanatoa mafunzo kwa jeshi la Ukraine.

Mnamo mwezi wa Februari 2023 Norway ilikuwa nchi ya kwanza kuidhinisha "mpango wa Nansen" wa miaka mingi wa msaada kwa Ukraine katika kipindi cha kuanzia mwaka 2023 hadi 2027 wa kiasi cha zaidi ya dola bilioni 7.

Kwa upande wa asilimia ya pato la Taifa lililotengwa kuisaidia Ukraine, Norway kwa ujumla imekuwa ikiongoza mataifa mengine ulimwengu, huku ikitumia 1.6% ya oato la ndani ya taifa (GDP) .

Denmark pia ilituma 1.6% ya ya mapato ya taifa lake kuisaidia Ukraine, lakini sio tu kwa msingi wa nchi mbili, lakini pia kupitia fedha za Ulaya.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mfumo wa ulinzi wa anga wa NASAMS Ulinzi ukiwa katika kiwanda Kongsberg, Norway

Mtafiti mkuu katika Taasisi ya Nansen ya Norway Andreas Osthagen anabainisha kuwa sera ya Norway inasukumwa na kuunga mkono haki za binadamu na utawala wa sheria, pamoja na uwepo wa mpaka na Urusi.

"Wanorway waliona jinsi serikali kubwa na yenye nguvu zaidi kuliko nchi yetu inavyoshambulia jirani yake, hii iliwatia wasiwasi. Kuiunga mkono Ukraine, bila shaka, ni kuwaunga mkono Waukraine, lakini kwa ujumla ni kuyasaidia mataifa madogo katika uhusiano wao na mataifa makubwa kama vile Urusi," Osthagen anafafanua.

Kura ya maoni ya mwezi Februari mwaka 2023 ya Taasisi ya Utafiti wa Miji na Mikoa ya Norway (NIBR) iligundua kuwa Wanorway 7 kati ya 10 walichukulia uvamizi wa Urusi kuwa tukio ambalo liliharibu uhusiano wa Norway na Urusi kwa kizazi kimoja.

Ni zaidi ya 10% tu ya waliohojiwa walioamini kwamba Norway inapaswa kuacha kulipatia silaha jeshi la Ukraine, na Ukraine inapaswa kutoa sehemu ya maeneo yake kwa ajili ya amani.

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maandamano ya kuonyesha mshikamano na Ukraine mbele ya Bunge la Denmark wakati wa ziara ya Vladimir Zelensky, Agosti 2023

Katika Denmark, msaada kwa ajili ya Ukraine pia sasa inaonekana kuimarika. Kulingana na uchunguzi wa Eurobarometer, 76% ya Wadenmark mnamo Agosti 2023 waliunga mkono usaidizi wa kijeshi kwa Ukraine na utoaji wa mafunzo ya jeshi la Ukraine. Ni 19% tu ndio waliopinga.

"Watu wa Denmark wana hulka yao ya kutaka kurekebisha mambo: ikiwa kitu kibaya kimetokea ulimwenguni, wanataka kurekebisha, kufanya kila juhudi kumsaidia muathiriwa wa uchokozi usio na msingi kujilinda. Huruma inasikika kila mahali hapa,” Balozi wa Ukraine nchini Denmark Andriy Yanevsky anaelezea uungwaji mkono huo mkubwa na kuongeza kuwa nchini Denmark, tofauti na baadhi ya nchi nyingine za Magharibi, mtu hawasikii wanasiasa wanaohoji kufaa kwa msaada kwa Ukraine.

"Kwa mtazamo wa serikali, kila mtu hapa anaelewa kwamba ikiwa, Mungu apishe mbali, tunaruhusu Urusi kushinda vita vyetu, itakuwa kuanguka kwa utaratibu wa ulimwengu ambao sisi sote tumezoea wa kuishi. Wanaelewa kuwa ustawi wao unategemea, kati ya mambo mengine, juu ya matokeo ya vita hivi, "anabainisha Andrei Yanevsky.

Kulingana na serikali ya Denmark, Copenhagen iliipatia Ukraine msaada wa kijeshi wa euro bilioni 4.3 na msaada wa kifedha wa euro milioni 408 kwa madhumuni ya kiraia.

Wakufunzi wa kijeshi wa Denmark wanawafunza wanajeshi wa Ukreni kama sehemu ya programu ya Interflex. Denmark ilitoa mizinga, risasi, na ndege zisizo na rubani kwa Ukraine—Andrei Yanevsky abainisha kwamba nchi hiyo haitengenezi silaha hizo nyingi bali inazinunua nje ya nchi.

Denmark ilikuwa mojawapo ya nchi za kwanza kuwekeza katika kurejea kwa hali thabiti ya Ukraine, ikiwekeza dola milioni 180 katika miradi ya miundombinu katika eneo la Mykolaiv.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vladimir Zelensky na Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen katika ndege ya F-16, Agosti 2023

Mchambuzi wa kijeshi katika Chuo cha Ulinzi cha Royal Danish Anders Pak Nielsen anabainisha kuwa Denmark pia inalinda maslahi yake kwa njia hii.

"Serikali ya Denmark inaelewa uharibifu utakaotokea kwa usalama wa Ulaya ikiwa Urusi itashinda vita hivi," anabainisha.

Sababu nyingine ni wajibu ambao uanachama wa NATO unailazimu Denmark.

"Urusi haitoi tisho la moja kwa moja kwa Denmark kwa maana kwamba watavaimia sehemu yoyote ya taifa hilo, lakini hatari ya vita bado ipo. Denmark ni nchi ya NATO, na ikiwa nchi nyingine yoyote ya NATO itashambuliwa na Urusi, Denmark nayo italazimika kuingia vitani, na miji ya Denmark ingekuwa viwanja vya mapambano ya vita,” anaeleza Anders Park Nielsen.

Mnamo Mei 2023, Denmark ilizindua mkakati mpya wa usalama na sera ya kigeni ambapo ilikiri kwamba haikulichukulia tisho la Urusi kwa uzito wa kutosha.

"Sasa watu nchini Denmark wanazingatia zaidi kila kitu kinachotokea karibu na Ukraine, nchi za Baltic, na Ufini.

Vita vya mseto na makabiliano ya NATO vinazidi kuzungumziwa kwenye vyombo vya habari na katika mazungumzo. Lakini kuna watu ambao wana wasiwasi lakini hawaoni jinsi hali hii inavyoathiri maisha yao, "anasema Lin Alexandra Mortensgaard, mtafiti katika Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Denmark.

Migogoro katika Arctic

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kituo cha kijeshi cha Urusi "Arctic Trefoil" kwenye kisiwa cha Alexandra Land kilijengwa mnamo 2016

Lakini kuna jambo lingine ambalo halikumbukwi sana nchini Ukraine - mahusiano yanayokinzana ya watu wa Scandinavia na Urusi katika Arctic.

Baada ya Vita Baridi, kulikuwa na hali ya ushirikiano katika eneo hilo kwa muda. Mnamo 1996, mataifa manane (USA, Canada, Russia, Finland, Sweden, Norway, Denmark, Iceland) yaliunda Baraza la Arctic, ambalo, haswa, lilipaswa kukuza ulinzi wa mazingira, ushirikiano wa kitamaduni na utafiti wa kisayansi.

Lakini tangu miaka ya 2000, ushindani katika kanda hiyo ulianza kuongezeka sana. Arctic imejikuta katika kitovu cha siasa za kimataifa kutokana na ongezeko la joto duniani na kupungua kwa barafu, na kuruhusu kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kama vile usafirishaji wa kibiashara na uchimbaji madini.

Chini ya Vladimir Putin, matarajio ya Urusi katika Arctic yamechukua mwelekeo mpya. Ishara ya kurudi kwa siasa hai ilikuwa kutua kwa mkurugenzi wa FSB wa wakati huo Nikolai Patrushev kwenye Ncha ya Kaskazini mnamo 2004. Mnamo miaka ya 2010, Urusi ilijenga besi kadhaa mpya za kijeshi na viwanja vya ndege katika Arctic.

Moscow inapanga kuendeleza Njia ya Bahari ya Kaskazini, ambayo inapita kupitia Bahari ya Arctic, kama njia ya biashara kati ya Ulaya na Asia.

Ikilinganishwa na njia ya asili ya kupitia Mfereji wa Suez, njia hii itapunguza kwa kiasi kikubwa njia ya kutoka China na nchi nyingine za Asia Mashariki hadi Ulaya Kaskazini na Magharibi.

Meli zinazosafiri kutoka Shanghai hadi bandari ya Uholanzi ya Rotterdam kupitia Mfereji wa Suez husafiri zaidi ya kilomita elfu 20, na kutoka Shanghai hadi Rotterdam kupitia Njia ya Bahari ya Kaskazini - zaidi ya kilomita elfu 14.

Matarajio ya Urusi yanaweza kufadhiliwa na Uchina, ambayo mnamo 2018 ilijitangazia kuwa "eneo la karibu na Arctic," lilitangaza uundaji barabara “Polar Silk Road” kando ya Bahari ya Arctic na kuanza kununua meli za kuvunja barafu.

Baada ya kunyakuliwa kwa Crimea, ushirikiano kati ya washiriki wa Baraza la Arctic ulipungua, na uvamizi kamili wa Urusi ulilemaza kwa muda.

"Ushirikiano wote wa kijeshi kati ya Urusi na mmataifa mengine ndani ya Baraza la Arctic ulisimamishwa, miradi ya kiuchumi, uhusiano wa kitamaduni, nk. Sasa tunaweza kuzungumza juu ya uwepo wa Arcticmbili," anasema Lin Alexandra Mortensgaard, mtafiti katika Taasisi ya Mambo ya Kimataifa ya Denmark.

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kadiri barafu zinavyopungua katika Aktiki, ndivyo ushindani wa rasilimali utakavyoongezeka huko.

Denmark ina jukumu muhimu katika Arctic kupitia Greenland inayojitegemea.

"Denmark inazingatia sana Arctic na kiasili inajiona kuwa sehemu ya Kaskazini na eneo la Aktiki. Hawaweki kando uwezekano wa mapigano ya kijeshi kwa muda mrefu, pamoja na Arctic. Lakini sasa tunazungumzia mashambulizi ya mseto, operesheni za ushawishi kutoka Urusi,” anasema Balozi wa Ukraine nchini Denmark Andrey Yanevsky.

Haya yote yamewekwa juu ya migogoro ya muda mrefu ya eneo ambayo ipo, haswa, kati ya Denmark na Urusi.

Mnamo Desemba 2014, Denmark na Greenland ziliwasilisha ombi kwa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Seabed wakidai umiliki wao wa mita za mraba 895,000. katika Bahari ya Arctic.

Hata hivyo, pamoja na Denmark, chini ya maji ya Lomonosov Ridge na Ncha ya Kaskazini pia inadaiwa na Urusi , ambayo inazungumzia uunganisho wa ridge na eneo la urusi na Canada - Hii ni sababu nyingine kwa nini vita vya Urusi dhidi ya Ukraine na majaribio yake ya kujenga miundombinu ya kijeshi katika Arctic jambo linaloitia wasi wasi Copenhagen.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Greenland ina jukumu muhimu katika sera ya Arctic ya Denmark

Vita vya Urusi dhidi ya Ukraine vimebadili mitazamo kuihusu Urusi nchini Norway, nchi ambayo ina mpaka wa ardhi wa kilomita 219 nayo.

Wakati wa Vita Baridi, ilikuwa mpaka pekee wa moja kwa moja kati ya USSR na nchi za NATO, na Arctic ilionekana kama uwanja unaowezekana wa mapambano kati ya kambi za uhasama. Hata hivyo, tangu kumalizika kwa Vita Baridi, hali ya wasiwasi katika eneo hilo imepungua. Mnamo 2010, nchi ziliweza hata kuweka mipaka ya bahari - eneo la maji lililokuwa na mzozo liligawanywa kwa usawa .

Hali ilianza kuzorota mwaka 2014 na kuingizwa kwa Crimea. Norway imejiunga na vikwazo dhidi ya Urusi. Urusi ilijibu kwa vikwazo dhidi ya bidhaa za Norway, na Naibu Waziri Mkuu wa Urusi aliyeidhinishwa Dmitry Rogozin alitembelea visiwa vya Svalbard vya Norway kwa helikopta mnamo Aprili 2015, akitumia hadhi yake maalum ya kisheria. Kisha Wizara ya Mambo ya Nje ya Norway ikamwita balozi wa Urusi.

Ombi la mara kwa mara la Urusi linapokelewa kwa baridi na majirani zake wa Aktiki

Na bado, hata baada ya 2014, Norway haikukataa ushirikiano na Urusi katika Arctic.

"Mpaka Februari 2022, serikali ya Norway ilisema kwamba iliona juhudi za kijeshi za Urusi katika Arctic, lakini haikuona kama tisho. Lakini baada ya Februari 2022, mtazamo wa Urusi umebadilika, kuna tathmini kwamba uelewa wake haukuwa sahihi na, labda, Urusi iko tayari kuingia katika mzozo fulani na Norway, "anabainisha Andreas Osthagen.

Kwa maoni yake, katika miaka ya hivi karibuni, Urusi katika Arctic imekuwa ikivutia mbinu za Vita Baridi. Wanorwe walidharau tishio kutoka kwa Urusi, anasema, kwa sababu walikuwa na hakika kwamba Moscow ilikuwa na nia ya maendeleo ya kiuchumi ya eneo hilo, na kwa hiyo kudumisha utulivu huko.

"Baada ya 2022, makadirio yamebadilika. Hii haihusu zaidi migogoro ya moja kwa moja katika Aktiki na zaidi kuhusu hofu ya matukio madogo—kwamba Urusi inaweza kutumia udhaifu fulani kuichokoza NATO, ambayo inaweza kusababisha mvutano zaidi katika Aktiki,” anaelezea Otshagen.

Mahali pa hatari zaidi nchini Norway ni visiwa vya Spitsbergen, ambavyo vina hadhi maalum ya kisheria.

Mkataba wa 1920 unatambua uhuru wa Norway juu ya visiwa, lakini pia huanzisha hali yake maalum. Nchi zilizotia saini zinaweza kutoa rasilimali kutoka kwa visiwa, lakini shughuli za kijeshi - kujenga vituo vya kijeshi au kutumia eneo hilo kwa vita - zimepigwa marufuku.

Hata hivyo, kati ya nchi zaidi ya 40 zilizotia saini makubaliano hayo, ni Urusi pekee inayochimba makaa ya mawe huko Spitsbergen, na kijiji cha Barentsburg, chenye wakazi 500, wengi wao wakiwa raia wa Urusi, ndiyo imekuwa kituo cha Urusi.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kijiji cha Barentsburg huko Svalbard, ambapo kampuni ya Urusi inachimba makaa ya mawe, inakaliwa na Warusi mia kadhaa.

Mnamo Mei 2023, Warusi wa eneo hilo, kwa mpango wa Mkuu wa Ubalozi wa Urusi, walifanya gwaride la magari yaliyopambwa kwa alama za Urusi, na mnamo Julai 2023, "gwaride la bahari" na ushiriki wa meli za raia, lililofanyika wakati wa Siku ya Jeshi la Wanamaji la Urusi. .

"Wakati mwingine inaonekana kwamba Urusi inaweza kuichochea serikali ya Norway, na wakati mwingine inaonekana kwamba kampuni ya Kirusi Arktikugol, ambayo inawakilisha maslahi ya Kirusi, inataka kuonyesha watazamaji wa ndani kwamba Urusi iko katika Arctic, ili kuthibitisha madai yake," anasema Osthagen.

Kwa maoni yake, tishio la mzozo wa moja kwa moja na Urusi kwa Norway, ambayo ilikuwa mwanzilishi mwenza wa NATO na ina uhusiano mkubwa wa kijeshi na Merika, haiwezekani.

"Mazoezi ya kijeshi yanafanyika katika ardhi ya Norway ili kuonyesha Urusi kuwa ni bora kutocheza na moto. Norway inaashiria kuwa iko tayari kujilinda na inaungwa mkono na washirika wake. Nadhani viongozi wa Urusi wanajua kwamba ikiwa mzozo wa kijeshi utazuka, hii itasababisha jibu kutoka kwa washirika wa NATO wa Norway, "anasema mtafiti huyo wa Norway.

Norway inajali zaidi kuhusu matukio ya uchochezi wa mseto.

"Kuna hali ya wasi wasi kidogo kufuatia makosa ya hesabu au operesheni za kijasusi zinazoiusisha meli za uvuvi za Urusi au raia. Katika hali hii, Norway inaingilia kati na inajaribu kuizuia, na Urusi inatuma kikosi chake cha Kaskazini kulinda wavuvi wa Urusi. Na hapa ni vigumu kuelewa jinsi ya kuondokana na mvutano huu, "anaelezea Andreas Osthagen.

Migogoro katika Arctic imechangia ukweli kwamba kwa watu wa nchi za Scandinavia kuishi na hali ya kufuatilia maendeleo ya vita vya Ukraine, inakuwa sehemu muhimu ya usalama wao wenyewe, kama ilivyo kwa nchi za Baltic au Poland.

Kwa Ukraine, hii inaelezea matarajio ya ushirikiano wa siku zijazo na nchi za Arctic katika ulinzi na utafiti wa eneo hilo, ambazo hadi sasa zimekuwa mbali na matarajio ya Ukraine

imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi